Mwakilishi wa jimbo la Kwamtipura Hamza Hassan Juma

 

TAARIFA YA KAMATI YA BARAZA LA WAWAKILISHI YA KUSIMAMIA OFISI ZA VIONGOZI WAKUU WA KITAIFA JUU YA  TUKIO LA KUZAMA KWA MELI YA SKAGIT  ILIYOTOKEA TAREHE 18.07.2012 KATIKA ENEO LA KISIWA CHA CHUMBE NJE KIDOGO YA ZANZIBAR.

UTANGULIZI

Mheshimiwa Spika, Kwanza kabisa napenda kuchukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia kukutana tena mbele ya Baraza lako tukufu tukiwa wazima wa afya ili kujadili mambo mbali mbali yanayohusu mstakbali mzima wa maendeleo ya nchi yetu. Aidha tuishukuru neema hii aliyotupa M/Mungu ya kuendelea kutupa neema ya pumzi zake ili kuweza kutekeleza majukumu yetu ambayo tulikula kiapo kwa kukamata Msahafu kuwatumikia wananchi wetu kwa ukweli, uwazi na uadilifu mkubwa na tunamuomba tene atuzidishie uzima na afya njema ili tuiokoe nchi yetu kutokana na janga la umasiskini na nnaamini kwa ukweli na uadilifu tunaoendelea nao hivi sasa basi naamini si muda mrefu nchi yetu itapiga hatua kubwa za maendeleo .

Mheshimiwa Spika, Aidha kwa niaba ya kamati nakushukuru wewe binafsi kwa kuniruhusu kusimama mbele ya Baraza lako tukufu ili niwasilishe taarifa ya kamati ya Kusimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa juu ya tukio hilo la maafa. Pia naomba  nawashukuru wananchi wangu wa jimbo la K/pura walionileta hapa kuja kuwawakilisha na nnaomba waendelee kuniamini na nnawaahidi kuwatumikia na nitajitahidi kuhakikisha kuwa nitawatumikia kwa uadilifu mkubwa na nitaishauri Serikali yetu kila ambalo nitahisi linaweza kuisaidia Serikali yetu, na wananchi kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya kamati, nachukua fursa hii kumuomba Mwenyezi Mungu awalaze mahali pema peponi wale wote waliofariki kutokana na ajali hiyo, na pia kuwataka kuwa na subra wale wote waliopoteza  ndugu na jamaa  zao. Pia na wale walionusurika katika ajali hiyo tunawatakia afya njema na inshallah Mwenyezi Mungu atawape afueni ili tuweze kujumuika nao na  kuweza kuendelea na majukumu ya kujenga Taifa letu.

Mheshimiwa Spika,Sisi Wajumbe wako wa Baraza la Wawakilishi pamoja na wewe mwenyewe binafsi tulipata mshituko mkubwa baada ya kupata tarifa ya kuzama kwa meli  mchana wa siku ya jumatano ya tarehe 18.07.2012 kwa masikitiko makubwa iliyokua ikitoka Dar-es-Salaam kuja Zanzibar,kwani ilitukumbusha machungu tuliyoyapata takriban ni Mwaka ukizingatia ni karibu Mwaka mmoja tu  uliyopita hapa nchini kwetu tuliweza kupata msiba mkubwa unaolingana na huu.

Mheshimiwa Spika,kamati yangu inasikitika sana kwa kuona kuwa visiwa vyetu vya Unguja na Pemba vimekumbwa na msukosuko mkubwa katika usafiri wa baharini ukiacha suala la kuzama kwa meli hii kwani kwa mtu yeyote aliyekuwa makini hakupigwa na mshangao kwa kutokea ajali hii kwani kulikuwa kuna kila dalili ya kutokea ajali baharini kwani kumekuwa na mfululizo wa matukio mbali mbali yakuashiria kutokea ajali baharini kwa baadhi ya meli kuzimika injini ovyo mara kwa mara huko Baharini zikiwa katika safari zake za kila siku zikiwa na abiria wengi ndani yake.

Mheshimiwa Spika,tukio la kuzama kwa meli limetupa funzo kubwa, kwani tatizo kubwa tulilokuwa nalo hapa ZNZ ni kutokuwa waaminifu na waadilifu kwa kusimamia majukumu tunayopewa au dhamana tunayopewa na wananchi wetu aidha kwa uzembe au tamaa binafsi inayopekea kutokuwajibika ipasavyo kwa umma, kwani kuna mamlaka iliyopewa jukumu la kusimamia kuhakikisha usalama wa vyombo vya baharini laikini inaonesha kuwa mamlaka hiyo imeshindwa kazi na ndio maana uzembe mkubwa unaendelea kufanyika ikiwemo kutokukagua vizuri injini za boti hizo,upakiaji abiria kiholela na ukataji wa tiketi ovyo bila kutumia vitambulisho pamoja na uuzwaji ovyo wa tiket vichochoroni bila ya kutumia Ofisi zinazotambulikana kitu ambacho kinachopelekea kupakia abiria wengi kuliko uwezo wake. Ndio maana hata takwimu zinayotolewa wakati chombo kinapopata ajali inakuwa ni tofauti na hali halisi ya idadi ya watu wanaokuwemo. Kwa hiyo, tunaitaka Serikali kuhakikisha kwamba inasimamia watendaji wake kutekeleza yale majukumu waliyopewa ili kuepusha ajali kama hizo zisitokezee tena.

Mhe Spika, jengine tunalojifunza nia kwamba Serikali yetu kutozifanyia kazi kwa haraka ripoti mbalimbali za aidha za kamati inazoziunda wao wenyewe au zile za Baraza lako tukufu au hata za taasisi mbali mbali Srikali inazopelekea kwani ukiangalia mambo mengi yanayoshauriwa basi yanakuwa ni kwa faida ya nchi yetu na pale zinapodhararauliwa basi matokeo yake wakati mwengine yakuwa na athari kubwa kwa jamii kwa ujumla.

Mhe Spika , kwa funzo hilo Serikali yetu ililolipata kama kawaida yetu tunaishauri sasa wakati umefika kuzifanyia kazi ripoti zote ilizopelekewa ukiacha zile za Baraza bali ni kwa ripoti zote zilizopelekwa Serikalini.

Mheshimiwa Spika,jambo jengine inaonesha kuna udhaifu mkubwa katika ukaguzi na usajili wa meli kutokuangalia historia ya meli hiyo kuanzia mwaka iliyotengenezwa,kazi inazoweza kuzifanya,muda wa uhai wa kutumika kwa chombo hicho,lakini pia na udhaifu wa (modification) zinazofanywa ili kuongeza nafasi za kupakilia abiria bila ya kuzingatia uwezo wa injini ya chombo hicho kwa lengo la kutengeneza faida kubwa bila kujali maisha ya watu.

Mheshimiwa Spika,imekuwa ni jambo la kawaida kwa hivi sasa mtu akitaka kusafiri kwa boti au kwa meli anawaza mara tatu tatu kwani hana uhakika wa kufika salama safari yake, hii inaonesha kuwa hakuna uhakika wa salama wa maisha yake, leo hii  imekuwa hata wanafamilia wanaposafirisha jama zao huwa presa juu juu mpaka wafike safari na kuwajuilisha kuwa wamefika salama, kwa hiyo hivi sasa Serikali imeweka rehani maisha ya wanachi wake kwani hakuonekani juhudi zozote za waliokabidhiwa majukumu ya kuwasimamia usalama wa abiria wetu kama wako makini kiasi hicho, hii ni kusema kwamba wameshindwa kazi.

Lakini kwa kuwa kwa mara ya kwanza Serikali yetu ya Mapinduzi ya Zanzibar yenye mfumo wa umoja wa kitaifa imesikia kilio cha Wawakilishi na wananchi wa Zanzibar kwa kumtaka Waziri ajiuzulu ambapo suala hili tulilipendekeza tokea ilipozama meli ya Spice Islander tulimtaka ajiuzulu ili kuonesha uwajibikaji wa kisiasa, lakini kwa bahati mbaya hakufanya hivyo lakini tunamshukuru kwa hivi sasa kwa kuwa ameamua kuwajibika ili kuonesha kuwa na yeyé ameguswa katika tukio hili kubwa la kitaifa. Na hili wala asione taabu wala aibu kwani kwa mfumo huu tuliokuwa nao hivi sasa wa Serikali ya umoja wa kitaifa wa demokrasia ya ukweli na uwazi ni jambo la kawaida sana tu na tunawaomba wengine wanaposhindwa kusimamia majukumu yao basi waamue mapema kuliko kusubiri kung’olewa kwa nguvu.

Mheshimiwa Spika, ni jambo la kusikitisha sana kwa wananchi wetu, kwani hata kuna baadhi ya wahangana waliopata ajali katika meli ya MV SPICE ISLANDER hawajapata ubani wao uliotengwa na Serikali, lakini leo hii tayari kuna msiba mwengine mkubwa ulioikumba nchi yetu, inawezekana pia miongoni mwa familia waliopata maafa hayo na katika maafa haya ikawa yamewakuta tena kama wapo watu hawa basi tunamuomba Mwenyezi Mungu awape subra kwani ni mtihani mkubwa kwao na inabidi washukuru kwani kila mtihani anaokupa Mwenyezi Mungu basi ukiwa na subra kuna kheri pia inakuja baadae nawaomba Wajumbe wenzangu wa Baraza hili pamoja na Watanzania wote kwa ujumla tuwaombee kila la kheri katika kukabiliana na mitihani hii pia tumuombe Mwenyezi Mungu awaepushe na mitihani mengine.

Mheshimiwa Spika,kwa tukio hili kuna baadhi ya maneno yanayozungumzwa na baadhi ya wanasiasa kuwa kuna kundi ndani baraza lako tukufu kwamba lina chuki za ubaguzi wa kisiasa kwa baadhi ya mawaziri tunataka kuwahakikishia wananchi wote wa Zanzibar kuwa sisi sote ni kitu kimoja na tunafanya kazi kwa pamoja kuwatumikia wananchi wetu bila ya chuki wala upendeleo wowote, bali ni kwa maslahi ya umma tu. Kwani kwa hivi sasa tumeamua kuweka kando itikadi zetu za kisiasa na kuamua kujenga nchi yetu kwa pamoja kwa maslahi ya Taifa letu na wananchi wetu, kwa hiyo tunaomba kila mmoja atimize majukumu yake aliyotumwa na wananchi wake kwa upande wa Wawakilishi ya kuisimamia ipasavyo Seriakali na kuhakikisha usalama wa maisha yao na mali zao kwa mujibu wa Katiba na Sheria zote , za hapa ZNZ na Tanzania nzima. Vile vile kusimamia uwajibikaji wa watumishi wote wa umma katika majukumu waliokabidhiwa na Serikali, lakini pia na mawaziri kwa upande wao kuhakikisha wanawasimamia walio chini yao ili kutekeleza majukumu yao ipasavyo kwa ajili ya kuimarisha ustawi wa wananchi wa Zanzibar.

Mhe Spika,  kamati yangu inaishauri Serikali kuendelea kulitumia eneo la kama kuwa ni eneo la kudumu kwa ajili kuzikia kwani eneo hilo inaonyesha eneo hilo lilitelekezwa baada kuzikwa watu waliofariki katia ajali ilyopita, lakini pia ukizingatia kuwa hivi sasa eneo la makaburi ya mwanakwerekwe limeshajaa kwa muda mrefu lakini bado linaendelea kuzikiwa maiti hadi vivi sasa jambo ambalo halipendezi hata kidogo.

Mhe Spika. Kamati yangu kutokana na funzo la ajali hii ya tatu mfululizo ndani ya miaka mitano tumeona iko haja ya kuwashauri wananchi wetu kujikatia bima za maisha ili yanapotokea majanga kama haya waweze kulipwa Bima ya maisha au ya afya kwa wale waliojeruhiwa au kupoteza uwezo wa kufanya kazi tene katika maisha yao kuliko kutegemea ubani utakaotolewa na Serikali kama utakuwepo.

Mhe Spika,  ripoti ya Serikali imeelezea kuwa wamewasaidia jamaa wa marehemu gharama za mazishi, usafirishaji wa maiti ,sanda na ubao lakini kamati yangu inaiomba Serikali pia kuwasaidia na gharama za Tahtimu kwani hali za familia zetu tunazijua kuwa nyingi zinaishi katika hali duni ya maisha na pengine hao waliofariki wengine ndio tegemeo lao katika familia, kwa hiyo kwao wao msiba unakuwa ni mara mbili. Kwa hiyo tunaamini jambo hilo litawapunguzia machungu wakati wa kuomboleza msiba.

Mhe Spika, katika ripoti ya ya Mhe Waziri ametueleza kuwa kuna baadhi ya wasamaria wema wanaendelea kufika ofisi ya Makamo wa pili wa Rais kutoa ubani wa mkono wa pole, na kwa upande fedha taslim wameziweka katika Account maalum iliyofunguliwa wakati wa ajali ya MV SPICE ISLANDER’S , lakini hadi leo Serikali yetu bado haijaanzisha mfuko wa maafa ambao utaweza kutumika au kusaidia wakati wowote maafa yatakapotokea aidha kwa upande wa Baharini ,au nchi kavu kwani ajali ziko za aina nyingi tu, kwani kuna Mafuriko, Moto, ajali za Ndege, Meli, Upepo mkali, n.k. kwa hiyo kamati yangu inaishauri Serikli kuanzisha mfuko wa maafa kwani si busara kuendelea kutumia pesa kutoka mfuko Mkuu wa Serikali, kama ilvyo hivi sasa kwani inasababisha kuwazuia wafanya biashara, Mashirika ,Makampuni au taasisi au mtu yeyote anayehitaji kuchangia mfuko huo kushindwa kufanya hivyo, lakini pia tunata kujua kuwa katia account hiyo maakum je kutakuwa na utaratibu mpya wa utoaji ubani kwa kiasi kili kile kilichotolewa katika ajali ya mwanzo?

Mhe Spika, Lakini pia tunaiuliza Serikali kupitia ahadi zilizotolewa na baadhi ya taasisi za fedha waliahidi kuwasomesha baadhi ya mayatima waliochwa na waliopoteza maisha katika ajali ya MV SPICE ISLANDER, je Serikali kupitia Ofisi yako imelifuatilia kwa kiasi gani? Na kama limetekelezwa je ni mayatima wangapi hadi sasa wanasomeshwa na taasisi hizo?.

Mhe Spika, kamati yangu inaiomba Serikali kuimarisha kikosi chetu cha KMKM pamoja na kikosi cha Zimamoto na uokozi ili kuweza kukabiliana na maafa ya ajali yoyote inayowezac kutokea aidha kwa Baharini au nchi kavu, kuwa na zana za kisasa ikwemo kuwa na Helikopta ya uokozi ambayo itakuwa na huduma za matibabu ya dharura inapokuwa angani ili kuweza kuokoa maisha ya wa wananchi wetu popote majanga yatakapokuja kutokea, vile vile tunaiomba Serikali yetu kuandaa utaratibu mzuri wa uokozi kwani tumeona udhaifu mkubwa wakati wa harakati za uokoaji pale Bandarini hapakuwa na utaratibu mzuri wa nani aliekuwa na amri ya mwisho katika kuongoza zoezi zima la uokozi, kwani tumeshuhudia hata vyombo vilivyokuwa vikitumika vilikuwa ni vikubwa kitu ambacho kilihitajika kutumika pia vyombo vidogovidogo ambavyo vingeliweza kusaidia zaidi huduma za uokozi.

Mhe Spika, katika hali iliyokuwa si ya kawaida au fadhaa tulishangaa kuona baada ya kutokea ajali chombo cha mwanzo kwenda kwenye tukio kiliwaacha wazamiaji ambao waneliweza kusaidia kuokoa maisha ya watu wengi badala yake chombo hicho walipanda viongozi wakiwemo mawaziri utadhani wanakwenda kuangalia snema huko baharini wakati wao wenyewe hawajui hata kuogelea seuze kuokoa watu waliopata ajali , hili pia ni funzo kubwa tunatakiwa tujipange vizuri, vile vile kitu chengine cha kushangaa ni kule kuona hata kuna baadhi ya boti ambazo zilikwenda kuokoa watu waliozama kusikia nazo zilizimalizika mafuta huko baharini kitu ambacho ni kibaya sana kwani kinaweza kusababisha ajali nyingine huko baharini kwa hiyo inaonyesha kuwa bado hatujakuwa na mipango mizuri ya uokozi pale majanga yanapotokea,

Mhe Spika, Kamati yangu inaiomba Serikali kufanya ukaguzi wa kina kwa vyombo vyote vya Baharini, ikiwemo Engine pamoja na uwezo wa Manahodha na Mabaharia wanofanyakazi katika vyombo hivyo na wakigundulika wasiokuwa na uwezo kuachishwa kazi na ni bora kuwa na vyombo vichache vyenye uhakika kuliko kuwa na vyombo vingi visivyokuwa na ubaora au kiwango, .

Mhe Spika, kamati yangu bado inaiomba Serikali yetu kufanya kila linalowezekana kununua Meli ya kubebea abiria na mizigo kwani ni aibu kuwa sisi tunachaguliwa na wananchi hao hao na tunalipwa mishahara kupitia kodi zao lakini tunashindwa kuwahakikishia usalama wa maisha yao.

Mhe Spika, Lakini pamoja na Serikali kununua Meli hizo kwa kuwa mzingira ya nchi yetu ni ya visiwa sio kama watu wote wataweza kusafiri kwa siku moja na kupanda Meli hizo la Serikali kwa hiyo bado ni lazima kutakuwa ulazima wa kuwa na vyombo binafsi , ndio maana tukasema kuwa suala kubwa hapa na la ulazima ni kuhakikisha ukaguzi wa kina wa usalama wa vyombo hivyo kwani hata hizo Meli za Serikali pia nazo zitahitajika kukaguliwa kila wakati kwani sio kama hizo Meli za Serikali hazitaweza kupata ajali zikiwa nazo hazitakuwa na ubora .

Mhe Spika, kwa kumalizia tunaishauri Serikali yetu kuwa sasa wakati umefika wa kuyatekeleza maoni na ushauri wa kakati zote aidha ilizoziunda wenyewe Serikali ,ripoti za washauri mbali mbali wa nje na ndani na zile za Baraza la wawakilishi kwani zina faida kubwa kwa nchi yetu kaka zitatekelezwa kwa vitendo na muda muafaka, vinginevyo hata hizo idara zilizoundwa kila wizara Idara za utafiti zitakuwa hazina maana yeyote kwani nao baada ya kufanya utafiti baadae pia hutoa ripoti kwa hiyo ripoti hizo kama hazikufanyiwa kazi yatakaua ndio hayo hayo (BUSINESS AS USSUAL)

Mhe Spika kwa mara nyingine tena naomba niwashukuru  wajumbe wa kakati yangu kwa kuwa wastahamilivu na kunipa mashirikiano makubwa kuandaa ripoti hii kwani tuliweza kuaa hadi saa sita za usiku na kuweza kuikamilisha asubuhi hii na kuiwakilisha hapa Barazani,

Mwaisho kabia naomba kuwashukuru wananchi wote wa ZNZ pamoja na wananchi wangu wa jimbo la Kwamtipura walionileta hapa ili ukwatumika nnawaahidi kuendelea kuwatumikia kwa uadilifu na moyo wangu wote.

Mhe Spika mwisho kabisa naomba kumkaribisha Mhe Hamad Masoud Hamad katika nyumba yetu ya Back Bancher ili kushirikiana nasi kuwatumikia wananchi wetu wa ZNZ kuwaletea maendeleo, tunakuombea kila la kheri katika kazi yako hii mpya ambayo kwa miaka mingi uliitumikia kwa uadilifu mkubwa, na tunamuomba M/Mungu akuepushe na shari nyengine naomba kuwasilisha .

Mhe Spika naomba kuwasislisha.

Ahsante sana.

Ahsante

 

…………………

MHE: HAMZA HASSAN JUMA

KAMATI YA KUSIMAMIA OFISI ZA VIOGOZI WAKUU WA KITAIFA

BARAZA LA WAWAKILISHI

ZANZIBAR.

 

            

Advertisements