Meli ya Mv. Mapinduzi iliyokuwa inamilikiwa na SMZ, lakini kwa sasa imeuzwa na kuzama katika kisiwa cha Madagasca

RAIS  wa  Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein, ameiagiza Wizara ya Nchi Afisi ya Rais Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo kuandaa utaratibu wa kupata fedha ndani ya wiki moja kwa ajili ya kununua meli kubwa mpya ya abiria wapatao 1000 na yenye uwezo wa kuchukua mizigo ya tani 100.
 
Dk. Shein ametoa agizo hilo leo wakati alipokuwa na mazungumzo na uongozi wa Shirika la Meli pamoja na Wajumbe wa Bodi ya Shirika hilo ambapo pia kikao hicho kilihudhuriwa na uongozi wa Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano na  Wizara ya Nchi Afisi ya Rais  Fedha, Uchumi na  Mipango ya Maendeleo.
 
Katika kikao hicho maalum Dk. Shein ameiagiza Wizara hiyo kutafuta  fedha hizo kutokana na vianzio vya ndani au nje ya nchi ama kutokana na  taasisi zinazohusiana na mambo ya fedha.
 
Alieleza kuwa katika kipindi  kisichozidi miezi miwili ujumbe maalum uende kwa  Kampuni zinazotengeneza meli nchini Korea Kusini, China au Japan kwa ajili ya kuwasilisha fedha za utangulizi kwa ajili ya ujenzi wa meli hiyo.
 
Mapema uongozi wa Shirika la Meli, ulimueleza Dk. Shein  kuwa kwa kawaida ujenzi wa meli yenye ukubwa huo, huchukua mwaka  mmoja kukamilika.
 
Kikao hicho ambacho kilikuwa na lengo la kuangalia mwelekeo na Mipango ya Shirika la Meli pia, kilijadili hali halisi ya meli za Shirika la Meli na  baadae kujadili  masuala ya ununuzi wa meli mpya itokayowaondoshea usumbufu wa usafiri wa baharini wananchi wanaosafiri kati ya Unguja, Pemba na Tanzania Bara.

Advertisements