Archive for August, 2012

DR. KAFUMU NJE

Dk. Dalali Peter Kafumu.

Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora  imetengua wadhifa wa ubunge wa Mbunge wa jimbo la Igunga kwa tiketi ya chama cha CCM, Dk. Dalali Peter Kafumu.

Uwamuzi huo umefuata kufuatia kesi iliyofunguliwa mahakamani hapo na Joseph Kashindey wa chama cha Demokrasia na maendeleo CHADEMA akiongozwa na wakili wake Profisa Abdalla Safari.

Mahakama hiyo imesema imeridhika na hoja nane kati ya 15 za upande wa malalamikaji kutoka chama cha CHADEMA.

Aidha mahakama imemtaka Dr. Kafumu kulipa gharama zote za kuedeshea kesi na kumpa nafasi ya kukata rufaa endapo hajaridhishwa na uwamuzi wa mahakama.

Dr, Kafum alifanikiwa kuwa mbunge baada ya kujiuzulu kwa aliekuwa mbunge jimbo la Igunga Rostum Aziz na kuitishwa uchaguzi mdogo wa jimbo hilo uliofanyika Octoba mosi mwaka 2011.

Kufuatia hukumu hiyo jaji aliesikiliza mamalamiko hayo Meli Shangali ameigiza tume ya taifa ya uchaguzi kufanya uchaguzi mwengine katika jimbo hilo

WATAKAO SUSIA SENSA ZANZIBAR KUKIONA

Omar Yussuf Mzee

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imesema itawachukuliwa hatua za kisheria wananchi watakaokataa kuhesabiwa katika zoezi la sense ya watu na makaazi litakaloanza Jumapili ijayo.

        Waziri wa nchi ofisi ya rais fedha na mipango Ya maendeleo Omar Yussuf Mzee ambae wizara yake ni mratibu wa sensa hiyo amesema ipo kisheria na mtu atakaekataa kutoa taarifa atachukuliwa hatua za kisheria.

        Hata hivyo amesema kazi za sensa zitafanikiwa hata kama baadhi ya wananchi watasusia sensa hiyo kutokana na viongozi wa kitaifa kutoa maelezo ya kina juu ya umuhimu wa sensa.

        Taarifa hiyo ya serikali inafuatia baada ya taasisi za kislamu kutoa tamko la kuwataka wafuasi wao kususia sensa hiyo itakayofanyika tarehe 26 mwezi huu wakidai kuwepo kipengele kinachouliza dini ya mtu.

TAASISI ZA KISLAMU ZANZIBAR ZASUSA SENSA 2012

Umoja wa taasisi na Jumuiya za kislamu Zanzbiar umetishia kususia kazi za sensa na makaazi zinazotarajiwa kufanyika Jumapili ijayo hadi pale kipengele cha dini kitapoingizwa katika madodos ya sensa hiyo.

        Akitoa tamko hilo kwa wandishi wa habari huko msikiti wa Mbuyuni Amir wa jumuiya ya Uamsho Sheikh Mselem Ali amesema jumuiya hazikatai sensa yenye malengo na maslahi, lakini hawako tayari kushiriki sensa yenye lengo la kuficha ukweli.

Amesema kuingizwa kwa kipengele cha dini katika sensa sio jambo geni katika sheria za kimataifa zinaruhusu sensa watu waulizwe dini zao bila ya kuzingatia nchi inaendeshwa kwa misingi gain.

Sheikh Mselem amesema madai yao mengine ya kutoshiriki sensa hiyo ni kutaka wazanzibari wenye sifa za kupewa vitambulisho wapatiwe na walio waliopewa kinyume na sheria wanayanganywe.

Taasisi  hizo za Kislamu zimeungana na taasisi kama hizo za Tanzania bara zilizotoa tamko wiki iliyopita kususia zoezi la Sensa litakalofanyika tarehe 26 mwezi huu Tanzania nzima.      

WANAOPANGA KUVUNJA AMANI ZANZIBAR KUKIONA

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imevitahadharisha vikundi vya watu vinavyopanga na kushabikia vitendo vya uvunjifu wa amani na utulivu kuwa watachukuliwa hatua za kisheria.

        Rais wa Zanzibar Dr. Ali Mohammed Shein amesema katika siku za karibuni Zanzibar ilikabiliwa na viashiria vya kutoweka amani na utulivu iliyomarika baada ya kuanzishwa serikali ya umoja wa kitaifa.

        Akilihutubia baraza la Edel-fitri mjini hapa amesema matukio ya ghasia na vurugu yaliotokea Mei 26, 27 na 28 na July 20 mwaka huu yameitia doa Zanzibar iliyokuwa na sifa nzuri ya amani na utulivu.

        Amefahamisha tofauti ya mawazo na mitazamo baina ya wananchi isiwe chanzo cha vitendo vya kuvunja amani na kutofuata sheria, hivyo ni vyema kutumia busara za kutatua matatizo kwa njia ya mazungumzo

Dr. Shein amesema kuvurugika kwa amani ni muda mfupi, lakini kuirejesha itachukua muda, hivyo amewaomba wananchi, wasijingize katika vitendo vya uvunjifu wa amani….

        Aidha Dr. Shein amesema katika kipindi kifupi tangu kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa Zanzibar imepiga hatua katika nyanja za kiuchumi na kijamii zikiwemo sekta ya mawasiliano, afya, elimu na kilimo.

                  Kuhusu sense ya watu na makaazi inayotarajiwa kuanza hivi karibuni, Dr. Shein amewataka wananchi kushiriki kwa kwa kukuali kuhesabiwa kwa vile sense hiyo imewekwa kisheria

        Baraza la Iddel-fitri pia limehudhuriwa na mbabalozi, makamu wa kwanza wa rais Zanzibar Malim Seif Sharif Hamad, makamu wa pili balozi Seif Ali Iddi na viongozi wengine wa chama na serikali.

11 WAKIWEMO RAIA WATATU WA KIGENI WAMEOKOLEWA KWENYA AJALI YA KUZAMA BOTI ZANZIBAR

Watu 11 waliozama jana katika chombo kilichokuwa kikitokea Tanga kuja Unguja wameokolewa wakiwa hai, na mwengine mmoja bado hawajulikani aliko.

Chombo hicho cha Saluwat kilizama jana jioni katika eneo la Kigombe wilaya ya Pangani Tanga kikiwa na abiria saba wakiwemo raia wa kigeni watatu na mabaharia watano.

Watu hao waliokolewa wamefikishwa katika hospitali ya Kivunge mkoa wa Kaskazini Unguja, lakini nahoza wa chombo hicho Ahmada Haji Gora mkaazi wa Beitras hali yake imedhofu.

Akizungumza na Zenji Fm radio mmoja wa walinusurika Talib Haji Maulid mkaazi wa Pitanazako amesema hali ya bahari ilichafuka na kusababisha mawimbi makubwa.

Amesema hali hiyo ilisababisha mashine mbili za chombo hicho kuzima na kusabisha chombo chao kujaa maji

Maulid ambae amelazwa katika hospitali ya Kivunge amesema walipata msaada wa ukozi leo majira ya saa 2.00 asubuhi, lakini abiria mmoja mwanamke hajulikani aliko

        Majina ya watu waliokolewa katika chombo hicho ni nahodha wa chombo Ahmada Haji Gora, Shaame Ali Shaame mkaazi wa Mtoni Kidatu miaka 50, Ali Iddi Haji miaka 31 mkaazi wa Mkokotoni, Khamis Dina Mtwana miaka 33 mkaazi wa Kibeni.

        Wengi ni Lebnan Ali Shaame miaka 50 mkaazi wa Magogoni, Othman Makame Othman miaka 40 mkaazi wa Mtoni Kidatu na Halid Haji Maulid mkaazi wa Pitanazako.

        Majina ya raia kigeni waliokuwemo kwenye chombo hicho ni Benjamin Liben na Joen miaka 27 mwanamke wote raia wa Ufaransa na Reed Welson Mholanzi mwenye umri wa miaka 23.

        Hata hivyo watu hao walionusurika hali zao zinaendelea vizuri baada ya kupata huduma katika hospitali ya Kivunge na taratibu za kuwasialana na balozii kwa raia wa kigeni zimeanza.

        Vyombo vya uokozi vimewaokoa watu hao wakiwa katika vikundi vya watu wawili wawili na watu wakiwa wamevaa makoti ya kuokolea maisha

Baraza la jumuiya ya taasisi za Kislamu Zanzibar kesho linatarajia kutoa tamko la kuungana na taasisi za kislamu Tanzania bara kususia kazi za sense ya watu na maakazi itakayofanyika tarehe 26 mwezi huu.

        Akizungumza na Zenji Fm radio juu ya tamko hilo mmoja wa viongozi wa taasisi hiyo Abdala Said Ali amesema taarifa zaidi zitatolewa rasmi kesho, lakini lengo ni kuungana na taasisi za Tanzania bara kususia sensa.

Amesema tamko hilo la taasisi za kislamu Zanzibar litatolewa na msemaji wa taasisi hizo Sheikh Mselem bin Ali katika mkutano na waandishi wa habari utakaofanyika msikiti wa Mburyuni mjini hapa

Akizundua kampeni za sense mjini Dar es Salaam waziri mkuu Mizengo Pinda amevitahadharisha vikundi vya kidini vinavyojaribu kuwashawishi wafuasi wao wasishiriki katika sensa kuwa kitendo hicho hakina tija kwa taifa.

Amesema suala la sensa halina uhusiano na masuala ya imani za kidini lakini takwimu zake zinatumika kwa kupanga mipango ya maendeleo

MGOGORO WA CHWAKA NA MARUMBI KUPATIWA UFUMBUZI

Rais wa Zanzibar Dr. Ali Mohammed Shein akiwahutubia wananchi wa Marumbi

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein leo amefanya mazungumzo na wananchi wa kijiji cha Marumbi na kuwataka kufungua ukurasa mpya wa kumaliza mgogoro uliodumu kwa zaidi ya miaka 30 kati yao na wanakijiji wa Chwaka na kujenga uhusiano mwema baina yao.
 
Mazungumzo hayo yalifanyika huko katika katika Skuli ya Marumbi kati ya Rasi na wananchi wakiwemo wavuvi wa kijiji hicho kiliopo, Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja, kufuatia mgogoro huo uliodumu muda mrefu juu ya suala zima la uvuvi haramu unaofanyika katika eneo la mpaka wa bahari kati ya Marumbi na Chwaka.
 
Katika maelezo yake Dk. Shein aliwaeleza wananchi hao wa kike na kiume waliojaa mbele ya viwanja vya skuli hiyo ya Marumbi wakiwa na hamu ya kumsikikiliza kiongozi huyo kama walivyoomba baada ya kukataa kuzungumza na viongozi wengine wote wa ngazi mbali mbali, wakiwemo wa Wilaya na Mkoa.
 
Dk. Shein katika mazungumzo yake na wananchi hao wa Marumbi aliwakata kujenga uhusiano mwema baina yao na ndugu zao wa Chwaka pamoja na kujenga imani na pia, kuwataka washirikiane na viongozi wao kwani wote ni wamoja huku akiahidi kwenda kuzungumza na wananchi wa Chwaka hapo baadae ili kuumaliza kabisa mgogoro huo.
 
Alieleza kuwa amefurahishwa na wananchi hao kwa kumuomba aende kuwasikila matatizo yao yanayowakabili na kueleza kuwa kweli amegundua kuwepo kwa tatizo la uvuvi haramu unaofanywa katika Ghuba hiyo ya Chwaka na kuviagiza vyombo husika kulichukulia hatua mara moja.
 
Alisema kuwa kuna haja ya kufuatwa Sheria na taratibu zilizowekwa juu ya uvuvi wa bahari, Sheria ambazo zimewekwa na Serikali kwa mashirikiano na wananchi na wavuvi wenyewe wa Unguja na Pemba.
 
“Najua mna hoja ya msingi ya kunitaka mimi kuja Marumbi leo, tumekumbushwa kuwa ni lazima tuishi vizuri na majirani… kufuata sheria na taratibu za Serikali na lazima tuelewe kuwa lengo ni kupata suluhisho, haiwezekani mwanaadamu wa karne hii wakagombana wakati wote”,alisema Dk. Shein.
 
Aidha, alieleza kusikitishwa kwake na baadhi ya watu mgogoro huo kuuhusisha na mambo ya siasa na kueleza kuwa ni ukweli usiopingika kuwa ajira hazitoshi na ndio maana wananchi waliowengi katika maeneo hayo hujishughulisha na shughuli za uvuvi, hivyo ipo haja ya kuyaezi na kuyatunza mazingira ya bahari ili yalete tija.
 
Dk. Shein alisem kuwa lengo la Serikali ni kuiimarisha sekta ya uvuvi ili iwe endelevu kwa kuwaendeleza wavuvi kwa  kuwatafutia mikopo na mitaji ili waweze kuvua zaidi hadi kufikia bahari kuu kwani ndio utaratibu unaoandaliwa na serikali na hautochukua muda pindipo kama mipango itakwenda vizuri.
 
Alisema kuwa watu wa Marumbi wanahistoria kubwa katika kujiletea maendeleo sambamba na kuwa wastaarabu hivyo aliwataka wasikubali kuchokozeka wala kuchukua sheria mikononi mwao na yale yanayohusu serikali waiachie serikali iyafanyie kazi.
 
Katika mazungumzo hayo, Dk. Shein aliwasisitiza wananchi wa Marumbi na maeneo mengine nchini kutunza mazingira kutokana na hali ya Tabia nchi inavyojitokeza hivi sasa hatua ambayo imepelekea joto kuwa kali pamoja na kupungua kwa kiwango cha maji katika ardhi na kuzidi kiwango cha maji ya bahari.
 
Kutokana na hali hiyo, Dk. Shein alisisitiza kuwa Serikali haitochelea kuchukua Sheria kwa yeyote Yule atakae ivunja na kuvitaka vyombo vya Sheria kufanya wajibu wao na kulitaka Jeshi la Polisi kuwasaidia wananchi katika kusimamia Sheria.
 
Pia, alizitaka Mahakama nazo ziendelee kufanya wajibu wao kama ilivyokawaida pamoja na kazi zao vizuri bila ya kuingiliwa huku akiutaka uongozi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kufanya kazi ipasavyo.
 
Pamoja na hayo, Dk. Shein aliwasisitiza wananchi hao wa Marumbi kushiriki kikamilifu katika zoezi la Sensa linalotarajiwa kufanyika mwezi huu na kuachana na mgomo waliokuwa wameuweka hapo kabla kwani zoezi hilo litawasaidia katika maendeleo yao.
 
Sambamba na hayo, Dk. Shein aliwaahidi wananchi hao wa Marumbi kuwa ahadi alizoziahidi Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Idd zipi pale pale ikiwa ni pamoja na kueleza kuwa kwa kushirikiana nae watawapelekea mashua mbili na vifaa vyengine vitapelekwa na Wizara husika.
 
Akitoa maelezo kwa niaba ya wananchi wa Marumbi Bwana Ufuzo Haji alitoa shukurani kwa ujio wa Dk. Shein na kumueleza kuwa  katika eneo hilo la Ghuba ya Chwaka kumekuwa na mgogoro wa siku nyingi hali ambayo ilipelekea hadi kuchomwa moto vyombo vyao vya uvuvi pamoja na vifaa vyengine.
 
Wananchi hao walieleza kuwa kutokana na kuwepo kwa mgogoro huo wa muda mrefu ndipo walipokataa kukutana na viongozi wengine wote ila Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwani yeye ndio atakaewasaidia kutatua.
 
Aidha, walieleza kuwa mbali ya hatua hiyo ya kumuomba Rais pia walikwishaanza kususia shughuli zote za chama na Serikali hadi wakabidhiwe vifaa vyao vilivyoharibiwa.
 
Bwana Ufuzo alieleza kuwa sio kweli kama alivyoambiwa Rais katika ziara zake za Mikoa hivi karibuni kuwa mgogoro huo umeshamaliza bali ulikuwa bado unaendelea huku akisisitiza kilio chao kikubwa ni kuwepo kwa uvuvi haramu unaosababishwa na watu wachache.
 
Nae Waziri husika wa Wizara hiyo alieleza juhudi za makusudi zlizozichukua tokea alipoingia katika Wizara hiyo lakini alikiri kuwa zimegonga mwamba licha ya kuahidiwa na wananchi hao kuwa suluhisho limeshapatikana.
 
Mapema Makurugenzi wa Uvuvi, Mussa Aboud Jumbe alimueleza Dk. Shein kuwa Sheria ya Uvuvi ipo na juhudi za makusudi zilichukuliwa katika kuhakikisha wavuvi wanashirikishwa katika utungaji wake sanjari na kupata maoni kutoka kwa Kamati zote za uvuvi
 
“Sheria ipo, na kwa mara ya kwanza ni mchango wa wananchi wote wa Unguja na Pemba wakiwemo wananchi wa Marumbi”,alisema Mussa.
 
Alisema kuwa suala la doria limekuwa ni gumu kufanyika kwani hujitokeza baadhi ya wananchi wa Marumbi na kuwaambia wananchi wa Chwaka siku inayokusudiwa kufanywa doria na kusababisha kutofanikiwa zoezi hilo huku akikiri kuwa uvuvi haramu kwenye Ghuba ya Chwaka umekisiri.
 
Mkurugenzi Mussa alisisitiza kuwa Sheria imepiga marufuku uvuvi wa nyavu ya kukokota,uharibifu wa nyavu za mtando, mabomu na matumizi ya umangu, matumzi ya sumu ambayo yote haya ndani ya sheria yametajwa.
 
Viongozi wengine waliotakiwa na Rais kutoa maelezo yao mbali ya hao ni Mkuu wa Wilaya na Mwakilishi wa Jimbo na Mwakilishi wa Komadoo wa KMKM ambao nao walikiri kuwepo kwa mgogoro huo na kueleza juhudi zilizochukuliwa huku mkuu wa Wizaya akisikitishwa na hatua za wananchi hao kutkataa kuzungumza na viongozi wa ngazi za chini kabla ya kumuomba Rais.
 
 Nae Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi na Kaibu Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Mhe. Abdalla Mwinyi Khamis aliusifu ustaarabu wa wananchi wa Marumbi kwa kutoa maelezo yao kwa uwazi na ukweli bila ya kuonesha ghadhabu na hasira mbele ya kiongozi wao mkuu wan chi kwa lengo la kutafuta suluhisho la mgogoro huo.