Archive for September, 2012

JUMUIYA YA MAIMAMU WALAANI FUJO ZA BUBUBU

Viongozi wa Jumuiya ya Maimu wakiongoza moja ya maandamano yao

Jumuiya ya Maimamu Zanzibar JUMAZA imewataka Wanzazibari kuenzi amani na utulivu iliopo baada ya kipindi kirefu kuishi katika migogoro na uhasama zilizotokana na siasa za chuki.

        Tamko la JUMAZA dhidi ya vitendo vya vurugu katika uchaguzi mdogo jimbo la Bububu limesema uvunjifu wa amani uliotokea katika uchaguzi huo umeitia doa serikali ya umoja wa kitaifa iliyopatikana kwa gharama kubwa.

        JUMAZA imesema kila Mzanzibari alishuhudia maafa yaliotokana na siasa za chuki na uhasama ikiwemo kuharibu mali za watu na kususiana katika shughuli za kijamii.

        Hivyo jumuiya hiyo imewataka wanzanzibari wasikubali kurejeshwa walikotoka na kuiunga mkono serikali ya umoja wa kitaifa kwa kuendelea kudumisha amani.

Jumuia hiyo pia laani matumizi ya nguvu na vitisho katika uchaguzi huo vilivyosababisha hofu wakati wa uchaguzi na watu wengine kujeruhiwa kwa risasi za moto na asili.

        Tamko hilo la JUMAZA lililotiwa saini na naibu Amir Mkuu wake Sheikh Ali Abdala Shamte limeitaka serikali kuwachukulia hatua watu waliohusika na vurugu hizo vikiwemo vikosi vya SMZ

UAMSHO WASHINDIKIZA KUFANYA MAANDAMANO YA KUPINGA FILAM YA MAREKANI

Jumuiya ya mihadhara ya Kislam UAMSHO inaangalia taratibu za kufanya maandamano kupinga filamu iliyotengenezwa nchini Marekani na vibonzo vilivyochapisha Ufaransa vinavyomkashifu mtume Muhamad SAW.

        Naibu katibu wa UAMSHO Sheikh Azan amesema viongozi wa jumuiya hiyo wamefanya mazungumzo na waziri wa katiba na sheria Abubakr Khamis Bakar kuruhusiwa kufanya maandamano hayo.

        Hata hivyo Sheikh Azan amesema jumuiya hiyo imetoa tamko katika mkutano wa ndani wa kulaani vitendo hivyo kutokana na kuzuiliwa kufanya maandamano.

        Aidha Sheikh Azan amewataka waislamu nchini kuwa watulivu katika kipindi hichi

        Nchi kadhaa za kiarabu na kislamu leo zimefanya maandamano baada ya sala ya Ijumaa kulaani vibonzo vinavyomkashifu Mtume Muhammad SAW vilivyochorwa na jarida na jarida moja la Ufaransa.

        Ufaransa yenyewe leo imeanza kufunga balozi zake katika nchi zaidi ya 20 pamoja na sehemu zenye maslahi kwa kuhofia uharibifu wa mali baada ya kuchorwa vibonzo hivyo katikati ya wiki hii.

MALIM SEIF AIJIA JUU SERIKALI YA UMOJA WA KITAIFA ZANZIBAR

Malim Seif Sharif Hamad

Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi CUF Maalim Seif Sharif Hamad ameelezea kusikitishwa kwake na vitendo vya vurugu  vilivyotokea wakati wa uchaguzi mdogo wa Uwakilishi jimbo la Bububu wiki iliyopita ambavyo vilipelekea watu kadhaa kujeruhiwa.
Amesema vitendo hivyo vimeiletea sifa mbaya serikali ya umoja wa kitaifa ambayo iliundwa kwa ajili ya kuendeleza amani ya nchi iliyotoweka kwa kipindi kirefu.
Akizungumza na baadhi ya wahanga wa tukio hilo huko makao makuu ya chama hicho Mtendeni Zanzibar, Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar amesema haikutarajiwa kuwa vitendo hivyo vingetokea wakati huu ambao serikali inatekeleza maridhiano ya kisiasa yaliyopelekea kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Amesema pande zote mbili zina wajibu wa kuheshimu na kuyalinda maridhiano hayo katika jitihada za kuendeleza umoja wa Wazanzibari, na kuvishutumu vyombo vya ulinzi kwa kuingilia na kuharibu uchaguzi huo.
Amesema ni jambo la kusikitisha kuona kuwa vyombo vilivyohusika na vurugu hizo havijachukuliwa hatua yoyote, na kwamba bado chama chake kinasubiri kuona hatua zitakazochukuliwa dhidi ya vyombo vya ulinzi vilivyohusika na vurugu hizo.
Akizungumza kwa niaba ya wahanga wa tukio hilo, Mbunge wa Jimbo la Mtoni Unguja kutoka chama hicho Mhe. Faki Haji Makame ambaye alikamatwa kwa tuhuma za kupigana hadharani, amevitupia lawama vyombo vya ulinzi kwa kukubali kutumiwa na wanasiasa kwa maslahi ya vyama vyao.
Kwa mujibu wa taarifa za chama hicho, watu wapatao 22 wakiwemo wanawake, walijeruhiwa katika vurugu hizo za Bububu zilizotokea tarehe 16 mwezi huu kufuatia harakati za uchaguzi mdogo wa Jimbo hilo.

Hassan Hamad,

CUF KUIBURUZA TUME MAHAKAMANI KUPINGA MATOKEO YA BUBUBU

Salim Bimani

Chama cha wananchi CUF kinajiandaa kwenda mahakamani kupinga ushindi wa mgombea wa CCM Hussein Ibrahim Makungu katika uchaguzi mdogo wa jimbo la Bububu uliofanyika Jumapili iliyopita.

        Akizungumza na Zenji Fm radio mkuregenzi wa mawasiliano na haki za binadamu wa CUF Salim Bimani amesema wanasheria wa chama hicho wanaandaa taratibu za kisheria ili kufungua kesi hiyo.

        Amesema wanaushahidi wa kutosha wa kukiukwa taratibu za uchaguzi ikiwemo upandikizaji wa wapiga kura.

Bimani amesema taratibu za kisheria za kufungua madai hayo zinatarajiwa kukamilika ndani ya siku 14 tokea kutangazwa mshindi huyo

Chama cha wananchi CUF kimepinga matokeo ya uchaguzi yaliompa ushindi mgombea wa CCM Makungu kwa kupata asilimi 50.7 ya kura dhidi ya mgombea wa CUF Issa Khamis Issa aliepata asilimia 48.2 ya kura.

Wakati huo huo mbunge wa jimbo la Mtoni Faki Haji Makame amekanusha taarifa za kukamatwa na jeshi la polisi na kufikishwa mahakamani akidaiwa kupigana hadharani siku ya uchaguzi huo.

Akizungumza na wandishi wa habari huko afisi ya wilaya CUF Vuga amesema taarifa hizo alizonukuliwa kamishna wa polisi Zanzibar zina lengo la kupotosha ushahidi dhidi ya kadhia ya kupigwa iliyomkuta siku hiyo.

Makame amesema siku ya tukio hilo alipigwa na vijana watatu kati yao wawili walikamatwa na jeshi la polisi kituo cha Bububu, lakina anashangazwa bado hawajafunguliwa mashtaka

MOYO AGOMA KURUDISHA KADI CCM

Mwasiasa mkongwe Zanzibar Hassan Nassor Moyo amesema hawezi kurejesha kadi ya CCM kwa viongozi aliowatangulia kufuatia matamshi yake ya mabadiliko ya mfumo wa muungano yanayokwenda kinyume na sera za chama hicho.
Akizungumza katika mjadala wa wandishi wa habari kuhusu muungano huko hoteli ya Mazson amesema hawezi kurejesha kadi yake kwa viongozi wa sasa wa CCM kwa kile alichodai sio wanzilishi wa chama.
Moyo ambae ni mwanzilishi wa chama cha ASP na CCM amesema iwapo atamua kurejesha kadi ataikabidhi kwa mwanzilishi mwenzake ambae ni makamo mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara Peus Msekwa akidai amepata tabu nae kuunganisha ASP na TANU na kuzaliwa CCM.
Moyo mwenye kadi ya CCM nambari saba amesema haoni sababu ya kurejesha kadi yake kwa kile alichodai kusema ukweli juu ya mabadiliko ya muungano
Kauli hiyo ya Moyo ambae aliwahi kutumikia serikali ya Mapinduzi Zanzibar na muungano katika nafasi za uwaziri imekuja kufuatia makamo wa pili wa rais Balozi Seif Ali Iddi kuwataka wananchama wa CCM wanaokwenda kinyume na sera ya chama hicho ya serikali mbili kurejesha kadi za uanachama kwa hiari yao.
Mzee Moyo ambae ni muumini wa mungano wa Tanganyika na Zanzibar anataka mfumo wa muungano huo ufanyiwe mabadiliko kwa kuwa na serikali tatu au uwe wa mkataba.