Archive for November, 2012

WALIOSABABISHA AJALI YA MV. SKYGIT MAHAKAMANI

Baadhi ya maiti wa ajali ya meli ya Mv. Skygit waliohifadhiwa katika kituo cha kupokelaa maiti Maisara, mjini Zanzibar

Tume ya kuchunguza ajali ya meli ya Mv Sagit iliyozama August mwaka huu imependekeza mmiliki na nahodha wa chombo hicho washitakiwe kwa kosa la kusababisha vifo kutokana na uzembe.

Akisoma tarifa ya tume hiyo kwa wandishi wa habari katibu mkuu kiongozi Dr. Abdulhamid Yahaya Mzee amesema mmiiki wa meli hiyo Said Abdurahman Juma, nahodha Makame Mussa Makame na meneja wa Seagul Dar es Salaaam Omar Mkonje wafikishwe mahakamani kwa kusababisha vifo vya zaidi ya watu 81 na wengine 112 kupotea

Aidha Dr. Mzee amewataja wafanyakazi wengine watakaochukuliwa hatua za kinidhamu ni mkaguzi na kaimu mrajisi wa meli wa zamani Zanzibar Juma Seif Juma, mkaguzi wa kujitegemea Capteni Saad Shafi Adam kwa kufutwa uteuzi wake pamoja na maafisa wawili wa usalama bandarini kwa kuruhusu abiria wengi kusafiri kwa meli hiyo.

Dr. Mzee amesema meli hiyo ilipakia abiria 431 ambao ni zaidi ya abiria 250 walioruhusiwa kisheria kusafiri kwa wakti mmoja na meli hiyo.

Akizungumzia ulipaji wa fidia amesema tume imependekeza mmiliki wa meli kuwalipa fidia familia za abiria waliokufa na kupotea kima cha mshahara wa chini wa miezi 80 na asilimia 75 kwa waliopata ulemavu na asilimia 50 waliokolewa salama.

Tume hiyo ya kuchunguza ajali ya meli ya Mv Skagit iliyoundwa na August mwaka huu na rais wa Zanzbiar Dr. Ali Mohammed Shein pia imependekeza kuimarishwa sheria za usafiri wa baharini na uokozi.

Advertisements

DR. SHEIN AWAONYA UAMSHO KWA MARA YA MWISHO

Dr. Shein

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti CCM Zanzibar Dkt Ali Mohammed Shein ameendelea kukemea vikali vikundi vya watu vilivyojificha chini ya mwamvuli wa kidini kufanya vurugu na kutishia amani kwamba havitavumiliwa.

 

Amesema haiwezekani kuwaruhusu watu wachache kuwafanyia vurugu wengi wakati kila mtu ana haki ya kuheshimiwa na kuishi kwa salama katika jamii.

 

Akizungumza kwenye Mkutano wa hadhara Kibanda maiti mjini Zanzibar, Dk Shein amesema wananchi wa Tanzania wana uhuru wa kuamini dini waitakayo bila ya kubughudhiwa wala kuingiliwa katika ibada zao lakini panapoingia fujo na vurugu Serikali haiwezi kukaa kimya.

 

Amesema hakuna mtu anayekatazwa kuabudu lakini kufanyafujo na kuharibu mali za watu hakustahamiliki na kuongeza kuwa vikosi vya ulinzi vitaendelea na kazi yao kwa mujibu wa sheria kuona vurugu na fujo hazitokei tena.

 

Dkt. Shein ameongeza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuilinda Serikali ya Umoja wa Kitaifa na kuheshimu maridhianao ya kisiasa yaliyopo ili kuleta maendeleo kwa Wananchi wote.

 

Amesema Serikali ambayo anaiongoza itaendelea kuwalinda na kuwaletea maendeleo wananchi wote bila kujali tofauti zao kama ambavyo sheria za nchi zinavyoelekeza.

 

Ameongeza kuwa yeye ni Kiongozi Jasiri ambaye haongozi kwa kubahatisha bali hutumia Katiba ya nchi sambamba na kanuni nyingine zinazosaidia kuendesha nchi na kuwaletea wananchi maendeleo.

 

Kuhusu kuimarisha chama cha CCM Makamu Mwenekiti huyo amewataka wanaCCM kushikamana katika kuimarisha chama chao ikiwa ni pamoja na kuziimarisha Maskani za Chama hicho ambazo ndio nguzo imara za ushindi wa Chama.

 

Aidha amewataka WanaCCM kutembea kifua mbele kutokana na mafanikio yaliyopatikana chini ya uongozi wake na kwamba uwezekano wa CCM kuendelea kuongoza dola mwaka 2015 ni mkubwa.

 

Akizungumzia kuhusu Muungano Dkt. Shein amesema ulitokana na Mapinduzi matukufu ya Zanzibar mwaka 1964 hivyo akiwa Rais ataendelea kuulinda chini ya Mfumo uliopo wa Serikali mbili.

 

Aidha amewataka wanaCCM katika mchakato uliopo wa Katiba mpya kutoogopa kutoa maoni yao kwa Tume ya Katiba ambapo pia aliwakumbusha WanaCCM kuwa Sera ya Chama katika muungano ni Serikali mbili.

 

Awali Akitoa salamu zake Katibu Mkuu wa CCM Abrahman Omar Kinana amemuhakikishia Dkt Shein ushirikinao wa kutosha wa kukiimarisha Chama hicho nakwamba chini ya uongozi wake CCM Bara na Zanzibar itakuwa inafanya kazi kwa mashirikiano makubwa.

 

Mapema WanaCCM wa mikoa minne kichama ya Unguja walitoa salamu zao za pongezi na kumuomba Makamu Mwenyekiti huyo wa CCM Zanzibar kutowafumbia macho watu ambao wanahatarisha amani na utulivu uliopo nchini.

 

Mkutano huo wa CCM wa kuwashukuru wanachama umekuja kufuatia ushindi wa asilimia 100 ambao Rais Shein aliupata kwa kuchaguliwa kuwa Makamu Mweyekiti wa Chama hicho kwa upande wa Zanzibar

MAALIM SEIF APONGEZA SAFU YA UONGOZI CCM

Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi CUF Maalim Seif Sharif Hamad, ameipongeza safu mpya ya uongozi ya Chama Cha Mapinduzi CCM, na kuishauri kufanya kazi kwa kuzingatia misingi ya haki na sheria.
Amesema ni wajibu wa viongozi wapya wa Chama hicho kuheshimu sheria za nchi wakati wanapotekeleza majukumu yao, na kuepuka kutumia nafasi hizo kubariki mambo yaliyo nje ya utaratibu wa kisheria.
Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar ameeleza hayo wakati akihutubia mkutano wa hadhara wa CUF uliofanyika viwanja vya Magirisi Melinne katika Jimbo la Mwanakwerekwe, Wilaya ya Magharibi Unguja.
Ameelezea matumaini yake kuwa uongozi mpya wa CCM chini ya Makamu Mwenyekiti wake Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohd Shein kwa upande wa Zanzibar, hautoruhusu kuwepo kwa vikundi visivyokubalika kisheria ambavo vimekuwa vikilalamikiwa kuhusika na vurugu na kuwanyanyasa wananchi.
“Vikosi vya ulinzi kama vile jeshi la polisi, vipo kwa mujibu wa sheria lakini vikundi vyengine hivi ambavyo havitambuliwi kisheria havina sababu ya kuwepo. Ni matumaini yangu kuwa chini ya safu hii mpya ya uongozi ya CCM ikiongozwa na Rais Dkt. Ali Mohd Shein kwa upande wa Zanzibar hautovibariki vikundi hivi kabisa”, alisisitiza Maalim Seif.
Aidha amesema ni vyema kwa viongozi hao kujipanga kisiasa, ili hatimaye nchi iweze kuendeleza siasa za kistaarabu ambazo zitakuwa zinazingatia zaidi ushindani wa hoja na sera.
Katibu Mkuu huyo wa CUF amefahamisha kuwa kazi ya vyama vya upinzani katika nchi ni kuikosoa serikali kwa lengo la kuirekebisha, na havipaswi kukaa kimya wakati vinapoona kasoro hasa za ukiukwaji wa haki za raia.
“Chama chetu kinaendeshwa na dira ya kuitakia mema Zanzibar, hivyo hatutokaa kimya tunapoona haki za raia zinaingiliwa”, alibainisha Maalim Seif na kurejea wito wake kwa Wazanzibari kuungana ili kuwa na sauti moja wakati wanapotetea maslahi ya nchi yao.
Akizungumzia kuhusu mchakato wa ukusanyaji wa maoni kwa ajili ya katiba mpya ya Tanzania Makamu wa Kwanza wa Rais amewata wananchi wa Mkoa wa Mjini Magharibi kujiandaa kwa ajili ya kutoa maoni yao yanayotarajiwa kukusanywa kuanzia tarehe 19 mwezi huu.
Ameiomba tume inayokusanya maoni hayo chini ya Mwenyekiti wake Jaji mstaafu Joseph Warioba   kuweka utaratibu mzuri utakaowawezesha wananchi kutoa maoni yao kwa uhuru bila ya kuingiliwa.
Kwa upande wake Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar Mhe. Hamad Massoud Hamad amesema chama hicho kina mpango wa kufanya uhakiki mpya wa wanachama wake, ili kuimarisha uhai wa chama katika maeneo yote nchini.
Katika mkutano huo Katibu Mkuu wa CUF amewakabidhi kadi wanachama wapya 92 walioamua kujiunga na chama hicho.
Hassan Hamad (OMKR).