Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi CUF Maalim Seif Sharif Hamad, ameipongeza safu mpya ya uongozi ya Chama Cha Mapinduzi CCM, na kuishauri kufanya kazi kwa kuzingatia misingi ya haki na sheria.
Amesema ni wajibu wa viongozi wapya wa Chama hicho kuheshimu sheria za nchi wakati wanapotekeleza majukumu yao, na kuepuka kutumia nafasi hizo kubariki mambo yaliyo nje ya utaratibu wa kisheria.
Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar ameeleza hayo wakati akihutubia mkutano wa hadhara wa CUF uliofanyika viwanja vya Magirisi Melinne katika Jimbo la Mwanakwerekwe, Wilaya ya Magharibi Unguja.
Ameelezea matumaini yake kuwa uongozi mpya wa CCM chini ya Makamu Mwenyekiti wake Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohd Shein kwa upande wa Zanzibar, hautoruhusu kuwepo kwa vikundi visivyokubalika kisheria ambavo vimekuwa vikilalamikiwa kuhusika na vurugu na kuwanyanyasa wananchi.
“Vikosi vya ulinzi kama vile jeshi la polisi, vipo kwa mujibu wa sheria lakini vikundi vyengine hivi ambavyo havitambuliwi kisheria havina sababu ya kuwepo. Ni matumaini yangu kuwa chini ya safu hii mpya ya uongozi ya CCM ikiongozwa na Rais Dkt. Ali Mohd Shein kwa upande wa Zanzibar hautovibariki vikundi hivi kabisa”, alisisitiza Maalim Seif.
Aidha amesema ni vyema kwa viongozi hao kujipanga kisiasa, ili hatimaye nchi iweze kuendeleza siasa za kistaarabu ambazo zitakuwa zinazingatia zaidi ushindani wa hoja na sera.
Katibu Mkuu huyo wa CUF amefahamisha kuwa kazi ya vyama vya upinzani katika nchi ni kuikosoa serikali kwa lengo la kuirekebisha, na havipaswi kukaa kimya wakati vinapoona kasoro hasa za ukiukwaji wa haki za raia.
“Chama chetu kinaendeshwa na dira ya kuitakia mema Zanzibar, hivyo hatutokaa kimya tunapoona haki za raia zinaingiliwa”, alibainisha Maalim Seif na kurejea wito wake kwa Wazanzibari kuungana ili kuwa na sauti moja wakati wanapotetea maslahi ya nchi yao.
Akizungumzia kuhusu mchakato wa ukusanyaji wa maoni kwa ajili ya katiba mpya ya Tanzania Makamu wa Kwanza wa Rais amewata wananchi wa Mkoa wa Mjini Magharibi kujiandaa kwa ajili ya kutoa maoni yao yanayotarajiwa kukusanywa kuanzia tarehe 19 mwezi huu.
Ameiomba tume inayokusanya maoni hayo chini ya Mwenyekiti wake Jaji mstaafu Joseph Warioba   kuweka utaratibu mzuri utakaowawezesha wananchi kutoa maoni yao kwa uhuru bila ya kuingiliwa.
Kwa upande wake Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar Mhe. Hamad Massoud Hamad amesema chama hicho kina mpango wa kufanya uhakiki mpya wa wanachama wake, ili kuimarisha uhai wa chama katika maeneo yote nchini.
Katika mkutano huo Katibu Mkuu wa CUF amewakabidhi kadi wanachama wapya 92 walioamua kujiunga na chama hicho.
Hassan Hamad (OMKR).

Advertisements