Dr. Shein

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti CCM Zanzibar Dkt Ali Mohammed Shein ameendelea kukemea vikali vikundi vya watu vilivyojificha chini ya mwamvuli wa kidini kufanya vurugu na kutishia amani kwamba havitavumiliwa.

 

Amesema haiwezekani kuwaruhusu watu wachache kuwafanyia vurugu wengi wakati kila mtu ana haki ya kuheshimiwa na kuishi kwa salama katika jamii.

 

Akizungumza kwenye Mkutano wa hadhara Kibanda maiti mjini Zanzibar, Dk Shein amesema wananchi wa Tanzania wana uhuru wa kuamini dini waitakayo bila ya kubughudhiwa wala kuingiliwa katika ibada zao lakini panapoingia fujo na vurugu Serikali haiwezi kukaa kimya.

 

Amesema hakuna mtu anayekatazwa kuabudu lakini kufanyafujo na kuharibu mali za watu hakustahamiliki na kuongeza kuwa vikosi vya ulinzi vitaendelea na kazi yao kwa mujibu wa sheria kuona vurugu na fujo hazitokei tena.

 

Dkt. Shein ameongeza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuilinda Serikali ya Umoja wa Kitaifa na kuheshimu maridhianao ya kisiasa yaliyopo ili kuleta maendeleo kwa Wananchi wote.

 

Amesema Serikali ambayo anaiongoza itaendelea kuwalinda na kuwaletea maendeleo wananchi wote bila kujali tofauti zao kama ambavyo sheria za nchi zinavyoelekeza.

 

Ameongeza kuwa yeye ni Kiongozi Jasiri ambaye haongozi kwa kubahatisha bali hutumia Katiba ya nchi sambamba na kanuni nyingine zinazosaidia kuendesha nchi na kuwaletea wananchi maendeleo.

 

Kuhusu kuimarisha chama cha CCM Makamu Mwenekiti huyo amewataka wanaCCM kushikamana katika kuimarisha chama chao ikiwa ni pamoja na kuziimarisha Maskani za Chama hicho ambazo ndio nguzo imara za ushindi wa Chama.

 

Aidha amewataka WanaCCM kutembea kifua mbele kutokana na mafanikio yaliyopatikana chini ya uongozi wake na kwamba uwezekano wa CCM kuendelea kuongoza dola mwaka 2015 ni mkubwa.

 

Akizungumzia kuhusu Muungano Dkt. Shein amesema ulitokana na Mapinduzi matukufu ya Zanzibar mwaka 1964 hivyo akiwa Rais ataendelea kuulinda chini ya Mfumo uliopo wa Serikali mbili.

 

Aidha amewataka wanaCCM katika mchakato uliopo wa Katiba mpya kutoogopa kutoa maoni yao kwa Tume ya Katiba ambapo pia aliwakumbusha WanaCCM kuwa Sera ya Chama katika muungano ni Serikali mbili.

 

Awali Akitoa salamu zake Katibu Mkuu wa CCM Abrahman Omar Kinana amemuhakikishia Dkt Shein ushirikinao wa kutosha wa kukiimarisha Chama hicho nakwamba chini ya uongozi wake CCM Bara na Zanzibar itakuwa inafanya kazi kwa mashirikiano makubwa.

 

Mapema WanaCCM wa mikoa minne kichama ya Unguja walitoa salamu zao za pongezi na kumuomba Makamu Mwenyekiti huyo wa CCM Zanzibar kutowafumbia macho watu ambao wanahatarisha amani na utulivu uliopo nchini.

 

Mkutano huo wa CCM wa kuwashukuru wanachama umekuja kufuatia ushindi wa asilimia 100 ambao Rais Shein aliupata kwa kuchaguliwa kuwa Makamu Mweyekiti wa Chama hicho kwa upande wa Zanzibar

Advertisements