Archive for December, 2012

MALIM SEIF AMJULIA HALI SHEIKH SORAGA

soragaMakamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad leo amefanya ziara ya kumtembelea Katibu wa Mufti wa Zanzibar Sheikh Fadhil Soraga, na kumuombea apone haraka.

Amesema mtihani uliompata Sheikh Soraga mwezi uliopita wa kumwagiwa maji yanayosadikiwa tindikali haukutarajiwa, na kumtaka kuendelea kuwa na subra wakati akiendelea kupatiwa matibabu.

Sheikh Soroga anaendelea kupatiwa matibabu nyumbani kwake Mwanakwerekwe baada ya kurejea nchini India alikokuwa akipatiwa matibabu ya awali.

Nae Sheikh Soraga amesema hali yake sasa anaendelea vizuri licha ya kupata majeraha mabaya katika sehemu za usoni na kifuani.

Amewashukuru madaktari wa hospitali ya Miotnchini India kutokana na huduma bora walizokuwa wakimpatia katika kipindi chote alichukuwa hospitalini.

Sheikh Soraga ambaye anaweza kuzungumza vizuri, alirejea nchini tarehe 16 mwezi huu akitokea India, alikokuwa akipatiwa matibabu ya awali baada ya kumwagiwa tindikali n mtu asiejulikana

MATAIFA YA MAGHARIBI KUUNGA MKONO MAMLAKA HURU YA ZANZIBART

Malim Seif Sharif Hamad

Malim Seif Sharif Hamad

Katibu mkuu wa chama cha wananchi CUF, Malim Seif Sharif Hamad amesema jumuiya ya kimataifa itaunga mkono maamuzi ya wazanzibari watakayoamua juu ya mabadiliko ya katiba mpya ya Tanzania.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara wa chama hicho huko Kibandamaiti amesema chama hicho kimekutana na mabalozi mbali mbali wa nchi za magharibi kuelezea msimamo wao juu ya maamuzi ya Zanzibar.

Malim Seif amesema haki ya kujiamulia hatma ya mamlaka ya Zanzibar iko mikoni mwa wananchi hivyo maamuzi yao yataheshimiwa.

Aidha Malim Seif ametaka kuweko baraza la katiba la Zanzibar kutoa maoni yao juu ya rasimu ya mabadiliko ya katiba mpya itakayoandaliwa kabla ya kutiwa saini na rais wa Tanzania

Malim Seif pia amewataka vijana kutokubali kushawishiwa kwa kujiingiza kuingia kwenye vitendo vya vurugu zinazohatarisha amani ya nchi.

CHUO KIKUU ZANZIBAR SUZA KUANZISHA VITIVO VYA SAYANSI ZA MAZINGIRA, BAHARINI, CHEMIA NA TIBA

 

Dr. Shein akihutubia wanafunzi waliomaliza chuo kikuu cha taifa Zanzibar SUZA huko Tunguu

Dr. Shein akihutubia wanafunzi waliomaliza chuo kikuu cha taifa Zanzibar SUZA huko Tunguu

RAIS wa Zanzibar na Mwenekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ametoa wito kwa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), kuendelea kutoa mafunzo mbali mbali kwa kuzingatia mahitaji katika sekta kadhaa na hali ya mwenendo wa soko la ajira hivi sasa hapa nchini.

 

Dk. Shein ambaye pia, ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), aliyasema hayo katika Mahafali ya nane Chuo Kikuu hicho yaliofanyika katika viwanja vya majengo mapya ya chuo hicho huko Tunguu, nje kidogo ya mji wa Zanzibar.

 

Katika hotuba yake Dk.Shein alieleza kuwa katika kufanikisha jambo hilo, ni lazima Chuo hicho kiwe karibu na Tume ya Mipango ili kuona maeneo ambayo inapaswa kuyazingatia katika fani zinazotolewa Chuoni hapo.

 

Alisema kuwa umefika wakati Chuo kijielekeze kwenye mahitaji ya nchi yanayohitajika hivi sasa kwani tayari baadhi ya fani ikiwemo Sheria mahitaji yake si makubwa hasa ikizingatiwa na wingi wa wahitimu wanaohitimu katika vyuo vikuu kila mwaka hapa nchini.

 

Dk. Shein alisema kuwa akiwa Mkuu wa Chuo atatimiza wajibu wake ipasavyo na ataendelea kuwa karibu na Chuo sambamba na kufuatilia kwa karibu shughuli za Chuo hasa kutokana na dhama hiyo aliyopewa kwa mujibu wa sheria.

 

“Pamoja na majukumu mengine niliyonayo lakini na hili ni langu na nitaendelea kulitekeleza kwa moyo wangu wote kwa kushirikiana na wale wote wanaohusika”,alisema Dk. Shein.

 

Aidha, alisema kuwa Serikali inatambua umuhimu wa kugharamia masomo ya elimu ya juu na kila mwaka inajitahidi kuongeza idadi ya wanafunzi wanaodhaminiwa na serikali kwa kadri hali inavyoruhusu.

 

Dk. Shein alisisitiza kuwa hadi mwisho wa mwaka huu wa 2012 Serikali imeongeza idadi ya wanafunzi wa taasisi za elimu ya juu inaowadhamini kutoka wanafunzi 209 wapya hadi 800 na kuongeza bajeti ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu ya Zanzibar kutoka Tshs. Bilioni 4 hadi Bilioni 8.

 

Kwa kutilia mkazo hatua hiyo, Dk. Shein aliitaka Bodi iendelee kuwa makini na kuhakikisha inafanya uadilifu katika uteuzi wa wanafunzi wanaostahiki kupewa mikopo”Bodi isipendee mtu kwa sura na haipendezi katika kuwasaidia wananchi wa nchi moja ukapitisha upendeleo.. tufuate utaratibu uliopo”,alisisitiza Dk. Shein.

 

Aidha, Dk. Shein aliwataka na wale wanaopewa mikopo kuhakikisha kwamba fedha hizo walizokopeshwa wanazirudisha baada ya kumaliza masomo yao ili na wengine wanufaike nazo.

 

Dk. Shein alieleza kuwa Serikali inaendelea na jitihada za kuwajengea uwezo watu wake ili waweze kujiajiri wenyewe kupitia vikundi vya ushirika vya vijana na wanwake na kusisitiza kuwa hivi karibuni Serikali itazindua mfuko kwa ajili ya kuvisaidia vikundi mbali mbali.

 

Alieleza kuwa uamuzi wa Chuo hicho kuhamia Tunguu umesaidia sana kukiwezesha kukua na kuwa na mazingira mazuri zaidi ya kufanyia kazi huku akieleza kufarajika kwake na Chuo hicho katika kufuatilia masuala ya Utafiti wa Elimu ya Sayansi.

 

Pia, Dk. Shein alieleza kufarajika kwake na taarifa ya kuwepo kwa hatua za kuimarisha utendaji wa Chuo kwa kupitia upya Dira na Dhamira ya Chuo pamoja na kujiwekea kauli mbiu ya kukifanya Chuo kuwa Chuo bora katika ukanda wa Afrika Mashariki.

 

Pamoja na hayo alieleza kuvutiwa kwake na hatua ya Chuo ya kuanzisha masomo ya Shahada ya Uzamivu (PhD) ya Lugha ya Kiswahili kwa kushirikiana na mabigwa wanaoishi nchi za nje (Diaspora). Dk. Shein pia, katika Mahafali hayo alitoa zawadi mbali mbali kwa wahitimu waliofanya vizuri katika masomo yao.

 

Jumla ya wanachuo 273 wamemaliza masomo ya Digrii ya Sanaa na Ualimu,Sayansi na Ualimu na Sayansi na Compyuta. Wanachuo 167 wamemaliza Diploma ya Lugha na Ualimu, Sayansi na Ualimu na Kompyuta ambapo pia, wanachuo 57 wamehitimu mafunzo ya Cheti cha Sayansi na Kompyuta,Ukutubi na Teknolojia ya Habari.

 

Mapema Makamu Mkuu wa Chuo cha SUZA, Profesa Idrisa Rai alieleza dhamira ya Chuo hicho kuwa ni kujenga jamii yenye maarifa na elimu itakayoweza kutatua changamoto za Karne ya ishirini na moja na zitakazokuja baadae, kwa kupitia Elimu na Tafiti muafaka na zenye Ubora. Pia alitoa pongezi wka Dk. Shein kwa kukipa kipaumbele chuo hicho.

 

Profesa Rai alieleza mipango ya baadae ya Chuo hicho kuwa ni pamoja na kuanzisha Skuli ya Tiba, Tkonohama na Teknolojia ya Habari, Uongozi wa Hoteli na Utalii, Biashara, Kilimo na Uhandisi.

 

Pia, kwenye mwaka ujao Chuo hicho kimepanga kuanzisha masomo pamya ya Shahada ya Pili ya Sayansi na Mazingira ya Baharini, Sayansi ya Chemia, Kiswahili na Shahada ya Kwanza ya Mazingira na Tiba, Jiografia na Sayansi ya Mazingira, Elimu Mjumuisho na Ualimu, Ualimu wa Michezo na Diploma ya Lugha ya Kichina.

 

Katika Mahafali hayo viongozi mbali mbali walihudhuria akiwemo Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad, Mawaziri, Mabalozi wadogo wanaofanya kazi zao hapa Zanzibar, wawakilishi , Wabunge na wengineo

AL QOSWA INVESTMENT KUWEKEZA ZANZIBAR

 

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamd akizungumza na Makamu wa Rais wa Kampuni ya Al Aqswa ya Abu Dhabi, Sheikh Hemed Al- Kaff huko hoteli ya Serena Dar es Salaam jana. 9Picha na Salmin Said, OMKR

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamd akizungumza na Makamu wa Rais wa Kampuni ya Al Aqswa ya Abu Dhabi, Sheikh Hemed Al- Kaff huko hoteli ya Serena Dar es Salaam jana. 9Picha na Salmin Said, OMKR

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad ameihakikishia kampuni ya AL QOSWA Investment ya Abu Dhabi kuwa Zanzibar kuna fursa na maeneo mengi ya uwekezaji vitega uchumi ambayo inaweza kufungua miradi yake kwa ajili ya kujiimarisha zaidi pamoja na kuwasaidia wananchi wa Zanzibar.

 

Maalim Seif amesema hayo leo alipokuwa na mazungumzo na ujumbe kutoka kampuni hiyo ambao uliongozwa na Makamu wa Rais wa kampuni hiyo, Sheikh Hemed Al- Kaff, yaliyofanyika katika hoteli ya Serena mjini Dar es Salaam.

 

Makamu wa Kwanza wa Rais ameueleza ujumbe huo kuwa,  miongoni mwa maeneo ambayo Zanzibar inavutia sana wawekezaji ni katika sekta ya miundo mbinu, sekta ya ujenzi na biashara.

 

Amesema Zanzibar hivi sasa inahitaji kushirikiana na wawekezaji kwa ajili ya ujenzi wa bandari mpya ya kisasa, upanuzi wa uwanja wa ndege pamoja na ujenzi na upanuzi wa bandari huko Pemba, ikiwemo ya Wete.

 

Naye, Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko, Nassor Ahmed Mazrui katika mazungumzo hayo, alisema mkazo mwengine mkubwa umewekwa katika uwekezaji wa ujenzi wa kituo cha maonesho ya kibiashara kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati, ambapo eneo kwa ajili ya kazi hiyo limeshatengwa.

 

Waziri Mazrui alisema eneo jengine ni uanzishwaji wa viwanda vya kusarifu zao la karafuu na mwani, ili kuyaongezea thamani zaidi na yaweze kuwapa maslahi makubwa zaidi wazalishaji.

 

Alisema iwapo Zanzibar kwa kushirikiana na wawekezaji mbali mbali itaweza kuongeza ubora wa zao la mwani, na litaweza kuuzwa kwa bei kubwa kama ilivyio nchini Filipines, ambayo imechukua juhudi kubwa kulisarifu zao hilo kabla ya kuliuza.  

 

Naye Makamu wa Rais wa kampuni hiyo ya Abu Dhabi, Sheikh Hemed Al – Kaff amesema amefarajika sana kupata taarifa hizo na kuahidi kampuni yake itazifanyia kazi, ili iwee kuona maeneo itakayoweza kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika uwekezaji.

 

Alisema itazidi kuwasiliana na Serikali katika hatua za kutafuta maeneo ya uwekezaji na ana matumaini makubwa, kampuni yake itaweza kuitumia fursa iliyopo.

KOREA KUIUNGA MKONO ZANZIBAR KILIMO CHA MPUNGA

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein  amefanya mazungumzo na Balozi wa Jamhuri ya Korea, Mhe.Chung IL, na kumueleza kuwa hatua ya nchi hiyo kuinga mkono Zanzibar katika kuimarisha kilimo cha mpunga wa kumwagilia maji ni ya busara na ya kupongezwa.
 
Dk. Shein alimueleza Balozi huyo kuwa Zanzibar inathamini uhusiano na ushirikiano kati yake na nchi hiyo na uamuzi wa Korea wa kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta yake ya kilimo hasa cha kumwagiliaji maji ni uthibitisho wa wazi wa mashirikiano.
 
Katika mazungumzo hayo yaliofanyika Ikulu mjini Zanzibar, Dk. Shein alitoa pongezi kwa Korea kwa hatua yake hiyo na kueleza kuwa juhudi hizo ndio chachu kwa Zanzibar katika kuzidisha azma yake ya kutekeleza Mapinduzi ya Kilimo.
 
Dk. Shein pia, alimpongeza Balozi huyo kwa kuendelea kuiunga mkono Tanzania ikiwemo Zanzibar katika kuimarisha sekta zake za maendeleo ikiwemo kilimo.
 
Dk. Shein alimueleza Balozi huyo kuwa kilimo cha umwagiliaji maji kimetiliwa mkazo mkubwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na katika kufanikisha azma hiyo mikakati kabambe imewekwa na serikali ikiwa ni pamoja na kuanisha mabonde 57 yenye hekta 8,521 ambazo zinaweza kutumika katika kilimo hicho.
 
Tayari zaidi ya hekta 700 zilizomo katika eneo hilo zimeshawekewa miundombinu ya umwagiliaji na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inaendelea na mradi mkubwa wa kilimo cha umwagiliaji kwa msaada wa Serikali ya Jamhuri ya Korea ambapo jumla ya hekta 2000 tayari zimeshafanyiwa tathimini yakinifu.
 
Aidha, Dk. Shein aliunga mkono wazo la Korea la kutaka kuanzisha mashiruikiano katika usafiri wa anga kwa kuleta ndege zitakazofanya safari moja kwa moja kati ya Korea na Zanzibar kupitia Mashirika ya nchi hiyo.
 
Alieleza kuwa hatua hiyo itasaidia katika kuzidisha ushirikiano sambamba na kuimarisha sekta ya utalii hapa nchini kwa kuweza kupata watalii wengi kutoka nchini humo.
 
Nae, Balozi wa Jamhuri ya Korea nchini Tanzania alimueleza Dk. Shein kuwa mradi huo wa kilimo cha mpunga wa umwagiliaji maji mchakato wake unakwenda vizuri na unatarajiwa kuanza wakati wowote.
 
Balozi huyo ambaye amekuja kujitambulisha kwa Rais, alimueleza Dk. Shein kuwa Korea itaendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta zake za maendeleo ikiwemo kilimo, na kusisitiza kuwa nchi yake kupitia ubalozi wa nchi hiyo utachukua juhudi katika kuhakikisha hilo linafanikiwa.
 
Katika mazungumzo hayo pia, Balozi Chung alimueleza Dk. Shein kuwa nchi yake itaangalia uwezekano wa kuanzisha safari za ndege za moja kwa moja hadi Zanzibar kupitia mashirika yake ya ndege kwani tayari hivi karibuni imeshaanzisha nchini Kenya.
 
Aidha, Balozi huyo alipongeza mikakati iliyowekwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kuimarisha sekta zake za maendeleo huku akipongeza amani na utulivu iliyopo nchini na kupongeza juhudi za Dk. Shein katika kuhakikisha amani na utulivu huo unadumishwa na kuendelezwa.
 
Wakati huo huo, Dk. Shein alifanya mazungumzo na Balozi Mdogo wa Msumbiji anayefanya kazi zake hapa Zanzibar  Mhe.  Bernado Contantino Lidimba ambaye alifika Ikulu kwa ajili ya kumuaga Rais.
 
Mazungumzo ya viongozi hao yalijikita zaidi katika kuimarisha uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliopo kati ya Msumbiji na Zanzibar.
 
Dk. Shein alimueleza Balozi huyo kuwa Zanzibar na Msumbiji zina historia kubwa iliyowaunganisha watu wa  pande mbili hizo na kuwapelekea kuishi kama ndugu wa damu kwa muda mrefu hadi hivi leo.
 
Kutokana na hali hiyo Dk. Shein alimueleza Balozi huyo kuwa ipo haja kuzidishwa mashirikiano kwa pande mbili hizo ili uhusiano na ushirikiano huo uimarike hasa katika sekta za maendeleo na uchumi.
 
Nae Balozi   Lidimba alimueleza Dk. Shein kuwa amefarajika kwa kiasi kikubwa kufanya kazi Zanzibar na ameona jinsi Wazanzibari wanavyothamini uhusiano uliopo kati yao na Msumbiji.
 
Alieleza kuwa udugu wa Msumbiji na Zanzibar kwa sasa umeimarika zaidi katika sekta ya uchumi. Aliongeza kuwa hivi sasa wafanyabiashara wengi wamekuwa wakifanya biashara zao kati ya Msumbinji na Zanzibar hasa biashara ya mbao na kueleza kuwa hatua hiyo imepelekea kuzidi kuimarika kwa uhusiano baina ya pande mbili hizo.
 
Sambamba na hayo, Balozi huyo alitoa ombi lake kwa Rais kuwa iwapo Serikali ya Mapinduzi Zanzibar itafanikiwa katika azma yake ya kununua meli yake kubwa basi ni vyema ikafanya safari zake hadi nchini humo kwa kuzingatia kuwa sekta ya biashara imezidi kuimarika kati ya Zanzibar na Msumbiji. Pia alieleza kuwa hatua hiyo itaimarisha uchumi kwa pande zote mbili.

SORAGA AWASILI NCHINI BAADA YA MATIBABU INDIA

SORAGAKatibu wa Mufty Zanzibar, Sheikh Fadhil Suleiman Soraga amewasili
Zanzibar jana kutoka nchini India alikokwenda kwa matibabu
baada ya kumwagiwa Tindi kali.

Kwenye Uwanja wa Ndege wakimataifa wa Abeid Amani Karume Zanzibar Sheikh Soraga alipokewa na Mufti wa Zanzibar pamoja na Mawaziri, Viongozi wa na wauminmi wa Dini ya Kiislamu.

Akizungumza kwenye Uwanja wa Ndege wa Zanzibar baada yakuwasili kwake Sheikh Soraga amesema hali ya afya yake
inaendelea vizuri.

Aidha Sheikh Soraga ameishukuru Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa msaada mkubwa wa matatibabu yake nchini India.

Sheikh Soraga alimwagiwa Tindi Kali na mtu asijulikana
wakati alipokuwa akifanya mazoezi Alfajiri miezi miwili iliopita na
kusababisha sehemu za uso wake na kifua kuumiwa

A.F.P NAO WAPO

 WAKULIMA

13/12/2012

 

 

CHAMA CHA WAKULIMA TANZANIA

UKIUKWAJI WA UHURU WA VYOMBO VYA HABARI NA WANA HABARI NCHINI.

 

Ukiukwaji wa uhuru wa vyombo vya habari na wana habari nchini bado unaendelea kila uchao na hii unatokana na ukosefu wa kuheshimu sheria katiba na haki za binaadamu sambamba na uhuru wa habari kwa mujibu wa sheria.

Ukiukwaji huu unafanywa na baadhi ya wana siasa na vyombo ya dola na unatishia amani kwa tathnia hii ya habari.

Wakati ukizingatia watu wote wako chini ya sheria na hakuna alojuu ya sheria na kwa mujibu wa sheria. Wanahabari wako ndani ya katiba zote mbili ya SMT na SMZ kifungu namba kumi na nane 18 (2) na vyama vya siasa wamo ndani ya katiba namba 5 ya 1992 sambamba na vyombo vya dola wanaotambuliwa kuwa usalama wa raia na mali zao lakini la kushangaza inakuwaje watu wamo ndani ya katiba ya nchi lakini chombo kimoja kinamvunjia haki mwenziwe na kumletea hatarishi kwa kutumia ubabe wa kisiasa na uvunjaji wa sheria na katiba na haki za binaadamu kwa mijibu wa sheria.

Lakini la kuzinagatia kuwa Taifa hili litapata maendeleo zaidi litapo kuwa na mashirikiano na kuhisimiana mkubwa kumuhishimu mdogo na mdogo kumuhishimu mkubwa kwa mujibu wa sheria na mashirikiano hayo kati ya vyama vya siasa, vyombo vya ulinzi na usalama, wana habari na jamii kwa ujumla, na Watanzania wote kwa ujumla ndipo tutapata mafanikio makubwa ya habari.

Kwasababu habari ndio chachu ya maendeleo na mafanikio baina ya Taifa kwa Taifa, Jamii kwa Jamii na kiunganisho kikubwa cha Serikali na Wananchi wake. Kwa hivyo kutafuta habari katika jamii na serikali haki ya mwandishi wa habari kwa mujibu wa sheria. Sambamba na unapofichua habari au kuibua habari ni kuitendea haki jamii na Taifa kwa ujumla habari ziwe za ukweli zilizo fanyiwa utafiti na hiyo ndio habari inayotakiwa na wananchi na Taifa kwa ujumla.

Habari ni usawa kutoka pande zote mbili, habari inatakiwa iwe ya kweli isiwe sawa na hadithi na tutofautishe habari na hadithi, kutoa habari zisizo za uhakika ni ukiukwaji wa habari kwa mujibu wa sheria.

Bado ulimwengu unahitaji habari kwa kuhabarisha na kuelimisha kama vile kuondoa ukiukwaji wa haki za binaadamu na hivisasa unyanyasaji wa kijinsia, Unyanyapaa haki za walemavu na wanawake na watoto.

Mwisho tunawaomba wanahabari na jamii kwa ujumla tuzikatae sheria tunazoziona zinakandamiza haki za habari na kudumaza habari kwa nia ya kukuza habari kwa mujibu wa sheria.

MKURUGENZI WA MIPANGO YA UENDESHAJI SERA AFP

 

RASHID MCHENGA.

 

TEL: 0773-560243, 0715-560243