IMETOLEWA LEO TAREHE 10/12/2012

 BILA shaka Mchakato wa Marekebisho ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, umekuwa ukiendelea Nchini kote, kwa mujibu wa Sheria na pia kuitekeleza Haki ya Msingi, ya Wananchi kushiriki na kuwasilisha maoni yao, ambayo ni sehemu muhimu ya mamuzi yatakayoamua hatma ya Nchi kwa kufuata taratibu zilizowekwa.

Kwa upande wa Zanzibar, na kama ilivyo Nchini kote, zoezi la wananchi kutoa maoni juu ya Katiba waitakayo, linaelekea ukingoni, likiwajumuisha Wananchi wa Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, walioonekana kujitokeza kwa wingi, mbele ya Tume ya Kuratibu Maoni, nao wakitekeleza haki yao ya kidemokrasia.

Kwa Wilaya ya Mjini Unguja, zoezi hilo limekuja wakati muafaka ambapo Ulimwengu unaadhimisha miaka 64 ya Siku ya Kimataifa ya Haki za Binaadamu, iliyotokana na Azimio la Umoja wa Mataifa, la Disemba 1948, ambalo Tanzania, Zanzibar, ikiwa sehemu yake, ni  Mwanachama wake; na kwamba matarajio ya Umma na Serikali kwa ujumla, yalikuwa ni kushuhudia “Sauti” ya Wananchi ikisikika kama ilivyo kauli ya Mwaka huu ya Umoja wa Mataifa kwamba “SAUTI YANGU NI MUHIMU” yaani ‘MY VOICE COUNTS’.

La kusikitisha mno, ambalo ni kinyume na Sheria, na pia linalokiuka maagizo hata ya Viongozi Wakuu wa Nchi hii, akiwamo Raisi wa Jamhuiri ya Muungano wa Tanzania Mhe Jakaya Kikwete, na pia Raisi wa Zanzibar, Mhe Dokta Ali Mohamed Shein, ya kuwataka wananchi wapewe uhuru wa kutoa maoni yao, ni kuona kwa makusudi wananchi wa Zanzibar wakinyimwa HAKI YAO YA KUTOA MAONI, mbele ya Tume ya Kuratibu na Kukusanya Maoni juu ya Marekebisho ya Katiba.

Hilo limetendeka Mchana wa Jumatatu hii, tarehe 10 Disemba, 2012, katika Kiwanja cha Mzalendo, Jimbo la Magomeni, Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja, kutokana na kile kilichothibitika kuwa ni hila na ushawishi wa Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM ambaye ni Muwakilishi wa Jimbo hilo, Bw. Salmin Awadh Salmin, pamoja na Waziri Mstaafu wa   Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Bi Fatma Said Ali, ambaye pia ni Kamishna wa Tume hiyo, waliolivuruga zoezi hilo na hatimaye Wananchi kushindwa kabisa kutoa maoni yao.

Chama cha Wananchi, CUF, kimeshtushwa sana na hali hiyo ambayo wazi wazi imelenga kuchafua zoezi halali, na pia kuinyima Mamlaka halali (Tume ya Kuratibu Maoni ya Katiba) nafasi yake ya kuendesha harakati zake, usoni kwa umma, kutokana na jeuri ya kisiasa na utashi binafsi..

Masikitiko makubwa ni kwamba, tokea Zoezi hilo lilipoanza katika Mkoa wa Kusini Unguja, mnamo tarehe 2 Julai, 2012, na hadi tarehe 5 Disemba, 2012 lilipomaliza katika Wilaya ya Magharibi Unguja, haijawahi kutokea hali hiyo wala kile kinachochukuliwa na Umma wa Wananchi wa Zanzibar, kuwa ni kitendo cha jeuri na ufedhuli, usioweza kuvumilika.

Pamoja na busara nyingi zilizotumika kuepusha maafa, na kuitaka Tume ya Kuratibu Maoni ya Katiba pia kuwaomba radhi wananchi ambao walikwishahudhuria Kituoni hapo,  kwa ajili ya kuwasilisha maoni yao,  Chama cha CUF kinatoa wito kwa mamlaka husika kuwachukulia hatua za kinidhamu Viongozi sasa ni wakati wa Tume kuchukua hatua zinazofaa kwa mujibu wa sheria ili kuondoa jeuri na kiburi vya viongozi madhalimu hao ambao watapeleka kuvuruga zoezi hilo muhimu katika nchi yetu.

Chama cha Wananchi, CUF, pia kinaiarifu na kuitanabahisha Tume ya Kuratibu Maoni ya Katiba, kuwa Umma wa Wananchi wa Zanzibar sasa umekosa imani na baadhi ya Makimishna wa Tume hiyo, akiwamo Bi Fatma Said Ali, kwa kushindwa kuficha hisia na ukereketwa wa kisiasa.

Chama cha CUF, kinauarifu umma na pia kuikumbusha Tume ya Kuratibu Maoni ya Wananchi kwamba walichotenda Viongozi hao ni uvunjifu wa amani, kinyume na Sheria na pia kukiuka Kifungu cha 21 (a) (i)(ii)  na kama ambavyo adhabu yake imetajwa katika Kifungu C cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Sura ya 83 ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania.

 

SALUM BIMAN

MKRUGENZI HAKI ZA BINAADAM,HABARI, UENEZI, MAHUSIANO NA UMMA

HAKI SAWA KWA WOTE

 

 

Advertisements