RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein  amefanya mazungumzo na Balozi wa Jamhuri ya Korea, Mhe.Chung IL, na kumueleza kuwa hatua ya nchi hiyo kuinga mkono Zanzibar katika kuimarisha kilimo cha mpunga wa kumwagilia maji ni ya busara na ya kupongezwa.
 
Dk. Shein alimueleza Balozi huyo kuwa Zanzibar inathamini uhusiano na ushirikiano kati yake na nchi hiyo na uamuzi wa Korea wa kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta yake ya kilimo hasa cha kumwagiliaji maji ni uthibitisho wa wazi wa mashirikiano.
 
Katika mazungumzo hayo yaliofanyika Ikulu mjini Zanzibar, Dk. Shein alitoa pongezi kwa Korea kwa hatua yake hiyo na kueleza kuwa juhudi hizo ndio chachu kwa Zanzibar katika kuzidisha azma yake ya kutekeleza Mapinduzi ya Kilimo.
 
Dk. Shein pia, alimpongeza Balozi huyo kwa kuendelea kuiunga mkono Tanzania ikiwemo Zanzibar katika kuimarisha sekta zake za maendeleo ikiwemo kilimo.
 
Dk. Shein alimueleza Balozi huyo kuwa kilimo cha umwagiliaji maji kimetiliwa mkazo mkubwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na katika kufanikisha azma hiyo mikakati kabambe imewekwa na serikali ikiwa ni pamoja na kuanisha mabonde 57 yenye hekta 8,521 ambazo zinaweza kutumika katika kilimo hicho.
 
Tayari zaidi ya hekta 700 zilizomo katika eneo hilo zimeshawekewa miundombinu ya umwagiliaji na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inaendelea na mradi mkubwa wa kilimo cha umwagiliaji kwa msaada wa Serikali ya Jamhuri ya Korea ambapo jumla ya hekta 2000 tayari zimeshafanyiwa tathimini yakinifu.
 
Aidha, Dk. Shein aliunga mkono wazo la Korea la kutaka kuanzisha mashiruikiano katika usafiri wa anga kwa kuleta ndege zitakazofanya safari moja kwa moja kati ya Korea na Zanzibar kupitia Mashirika ya nchi hiyo.
 
Alieleza kuwa hatua hiyo itasaidia katika kuzidisha ushirikiano sambamba na kuimarisha sekta ya utalii hapa nchini kwa kuweza kupata watalii wengi kutoka nchini humo.
 
Nae, Balozi wa Jamhuri ya Korea nchini Tanzania alimueleza Dk. Shein kuwa mradi huo wa kilimo cha mpunga wa umwagiliaji maji mchakato wake unakwenda vizuri na unatarajiwa kuanza wakati wowote.
 
Balozi huyo ambaye amekuja kujitambulisha kwa Rais, alimueleza Dk. Shein kuwa Korea itaendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta zake za maendeleo ikiwemo kilimo, na kusisitiza kuwa nchi yake kupitia ubalozi wa nchi hiyo utachukua juhudi katika kuhakikisha hilo linafanikiwa.
 
Katika mazungumzo hayo pia, Balozi Chung alimueleza Dk. Shein kuwa nchi yake itaangalia uwezekano wa kuanzisha safari za ndege za moja kwa moja hadi Zanzibar kupitia mashirika yake ya ndege kwani tayari hivi karibuni imeshaanzisha nchini Kenya.
 
Aidha, Balozi huyo alipongeza mikakati iliyowekwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kuimarisha sekta zake za maendeleo huku akipongeza amani na utulivu iliyopo nchini na kupongeza juhudi za Dk. Shein katika kuhakikisha amani na utulivu huo unadumishwa na kuendelezwa.
 
Wakati huo huo, Dk. Shein alifanya mazungumzo na Balozi Mdogo wa Msumbiji anayefanya kazi zake hapa Zanzibar  Mhe.  Bernado Contantino Lidimba ambaye alifika Ikulu kwa ajili ya kumuaga Rais.
 
Mazungumzo ya viongozi hao yalijikita zaidi katika kuimarisha uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliopo kati ya Msumbiji na Zanzibar.
 
Dk. Shein alimueleza Balozi huyo kuwa Zanzibar na Msumbiji zina historia kubwa iliyowaunganisha watu wa  pande mbili hizo na kuwapelekea kuishi kama ndugu wa damu kwa muda mrefu hadi hivi leo.
 
Kutokana na hali hiyo Dk. Shein alimueleza Balozi huyo kuwa ipo haja kuzidishwa mashirikiano kwa pande mbili hizo ili uhusiano na ushirikiano huo uimarike hasa katika sekta za maendeleo na uchumi.
 
Nae Balozi   Lidimba alimueleza Dk. Shein kuwa amefarajika kwa kiasi kikubwa kufanya kazi Zanzibar na ameona jinsi Wazanzibari wanavyothamini uhusiano uliopo kati yao na Msumbiji.
 
Alieleza kuwa udugu wa Msumbiji na Zanzibar kwa sasa umeimarika zaidi katika sekta ya uchumi. Aliongeza kuwa hivi sasa wafanyabiashara wengi wamekuwa wakifanya biashara zao kati ya Msumbinji na Zanzibar hasa biashara ya mbao na kueleza kuwa hatua hiyo imepelekea kuzidi kuimarika kwa uhusiano baina ya pande mbili hizo.
 
Sambamba na hayo, Balozi huyo alitoa ombi lake kwa Rais kuwa iwapo Serikali ya Mapinduzi Zanzibar itafanikiwa katika azma yake ya kununua meli yake kubwa basi ni vyema ikafanya safari zake hadi nchini humo kwa kuzingatia kuwa sekta ya biashara imezidi kuimarika kati ya Zanzibar na Msumbiji. Pia alieleza kuwa hatua hiyo itaimarisha uchumi kwa pande zote mbili.

Advertisements