Dr. Shein akihutubia wanafunzi waliomaliza chuo kikuu cha taifa Zanzibar SUZA huko Tunguu

Dr. Shein akihutubia wanafunzi waliomaliza chuo kikuu cha taifa Zanzibar SUZA huko Tunguu

RAIS wa Zanzibar na Mwenekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ametoa wito kwa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), kuendelea kutoa mafunzo mbali mbali kwa kuzingatia mahitaji katika sekta kadhaa na hali ya mwenendo wa soko la ajira hivi sasa hapa nchini.

 

Dk. Shein ambaye pia, ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), aliyasema hayo katika Mahafali ya nane Chuo Kikuu hicho yaliofanyika katika viwanja vya majengo mapya ya chuo hicho huko Tunguu, nje kidogo ya mji wa Zanzibar.

 

Katika hotuba yake Dk.Shein alieleza kuwa katika kufanikisha jambo hilo, ni lazima Chuo hicho kiwe karibu na Tume ya Mipango ili kuona maeneo ambayo inapaswa kuyazingatia katika fani zinazotolewa Chuoni hapo.

 

Alisema kuwa umefika wakati Chuo kijielekeze kwenye mahitaji ya nchi yanayohitajika hivi sasa kwani tayari baadhi ya fani ikiwemo Sheria mahitaji yake si makubwa hasa ikizingatiwa na wingi wa wahitimu wanaohitimu katika vyuo vikuu kila mwaka hapa nchini.

 

Dk. Shein alisema kuwa akiwa Mkuu wa Chuo atatimiza wajibu wake ipasavyo na ataendelea kuwa karibu na Chuo sambamba na kufuatilia kwa karibu shughuli za Chuo hasa kutokana na dhama hiyo aliyopewa kwa mujibu wa sheria.

 

“Pamoja na majukumu mengine niliyonayo lakini na hili ni langu na nitaendelea kulitekeleza kwa moyo wangu wote kwa kushirikiana na wale wote wanaohusika”,alisema Dk. Shein.

 

Aidha, alisema kuwa Serikali inatambua umuhimu wa kugharamia masomo ya elimu ya juu na kila mwaka inajitahidi kuongeza idadi ya wanafunzi wanaodhaminiwa na serikali kwa kadri hali inavyoruhusu.

 

Dk. Shein alisisitiza kuwa hadi mwisho wa mwaka huu wa 2012 Serikali imeongeza idadi ya wanafunzi wa taasisi za elimu ya juu inaowadhamini kutoka wanafunzi 209 wapya hadi 800 na kuongeza bajeti ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu ya Zanzibar kutoka Tshs. Bilioni 4 hadi Bilioni 8.

 

Kwa kutilia mkazo hatua hiyo, Dk. Shein aliitaka Bodi iendelee kuwa makini na kuhakikisha inafanya uadilifu katika uteuzi wa wanafunzi wanaostahiki kupewa mikopo”Bodi isipendee mtu kwa sura na haipendezi katika kuwasaidia wananchi wa nchi moja ukapitisha upendeleo.. tufuate utaratibu uliopo”,alisisitiza Dk. Shein.

 

Aidha, Dk. Shein aliwataka na wale wanaopewa mikopo kuhakikisha kwamba fedha hizo walizokopeshwa wanazirudisha baada ya kumaliza masomo yao ili na wengine wanufaike nazo.

 

Dk. Shein alieleza kuwa Serikali inaendelea na jitihada za kuwajengea uwezo watu wake ili waweze kujiajiri wenyewe kupitia vikundi vya ushirika vya vijana na wanwake na kusisitiza kuwa hivi karibuni Serikali itazindua mfuko kwa ajili ya kuvisaidia vikundi mbali mbali.

 

Alieleza kuwa uamuzi wa Chuo hicho kuhamia Tunguu umesaidia sana kukiwezesha kukua na kuwa na mazingira mazuri zaidi ya kufanyia kazi huku akieleza kufarajika kwake na Chuo hicho katika kufuatilia masuala ya Utafiti wa Elimu ya Sayansi.

 

Pia, Dk. Shein alieleza kufarajika kwake na taarifa ya kuwepo kwa hatua za kuimarisha utendaji wa Chuo kwa kupitia upya Dira na Dhamira ya Chuo pamoja na kujiwekea kauli mbiu ya kukifanya Chuo kuwa Chuo bora katika ukanda wa Afrika Mashariki.

 

Pamoja na hayo alieleza kuvutiwa kwake na hatua ya Chuo ya kuanzisha masomo ya Shahada ya Uzamivu (PhD) ya Lugha ya Kiswahili kwa kushirikiana na mabigwa wanaoishi nchi za nje (Diaspora). Dk. Shein pia, katika Mahafali hayo alitoa zawadi mbali mbali kwa wahitimu waliofanya vizuri katika masomo yao.

 

Jumla ya wanachuo 273 wamemaliza masomo ya Digrii ya Sanaa na Ualimu,Sayansi na Ualimu na Sayansi na Compyuta. Wanachuo 167 wamemaliza Diploma ya Lugha na Ualimu, Sayansi na Ualimu na Kompyuta ambapo pia, wanachuo 57 wamehitimu mafunzo ya Cheti cha Sayansi na Kompyuta,Ukutubi na Teknolojia ya Habari.

 

Mapema Makamu Mkuu wa Chuo cha SUZA, Profesa Idrisa Rai alieleza dhamira ya Chuo hicho kuwa ni kujenga jamii yenye maarifa na elimu itakayoweza kutatua changamoto za Karne ya ishirini na moja na zitakazokuja baadae, kwa kupitia Elimu na Tafiti muafaka na zenye Ubora. Pia alitoa pongezi wka Dk. Shein kwa kukipa kipaumbele chuo hicho.

 

Profesa Rai alieleza mipango ya baadae ya Chuo hicho kuwa ni pamoja na kuanzisha Skuli ya Tiba, Tkonohama na Teknolojia ya Habari, Uongozi wa Hoteli na Utalii, Biashara, Kilimo na Uhandisi.

 

Pia, kwenye mwaka ujao Chuo hicho kimepanga kuanzisha masomo pamya ya Shahada ya Pili ya Sayansi na Mazingira ya Baharini, Sayansi ya Chemia, Kiswahili na Shahada ya Kwanza ya Mazingira na Tiba, Jiografia na Sayansi ya Mazingira, Elimu Mjumuisho na Ualimu, Ualimu wa Michezo na Diploma ya Lugha ya Kichina.

 

Katika Mahafali hayo viongozi mbali mbali walihudhuria akiwemo Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad, Mawaziri, Mabalozi wadogo wanaofanya kazi zao hapa Zanzibar, wawakilishi , Wabunge na wengineo

Advertisements