Archive for February, 2013

AL-YOUSUF KUINUFAISHA ZANZIBAR

LLLRAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesifu azma ya Jumuiya ya Al-Youseif ya kuja kuekeza  hapa Zanzibar.

Dk. Shein aliyasema hayo wakati alipokuwa na mazungumzo na Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Sheikh Al-Yousef huko Ikulu mjini Zanzibar na kutumia fursa hiyo kwa kumpongeza kiongozi huyo kwa azma yake hiyo.

Katika mazungumzo hayo, Dk. Shein alisema kuwa hatua hiyo itasaidia katika kuimarisha sekta ya uekezaji hapa nchini sambamba na kukuza uchumi na kuimarisha sekta za maendeleo ikiwemo ufugaji, kilimo na hata kukuza sekta ya ajira.

Aidha, Dk. Shein alitoa pongezi kwa Jumuiya ya  Al- Youseif kwa azma yake ya kuunga mkono juhudi za Serikali anayoiongoza katika kuwasaidia wanawake kwa kuanzisha benki itakayotoa mikopo kwa ajili ya wanawake pekee.

Alisema kua hatua hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa katika kuwasaidia wanawake katika juhudi za kupambana na umasikini na kuweza kuinua kipato chao cha maisha.

Dk. Shein alieleza kuwa miongoni mwa azma na malengo yake ilikuwa ni kuhakikisha kuwa wanawake wanasaidiwa na kuungwa mkono katika juhudi zao za kupambana na umasikini kwa kuanzishwa benki ambayo itakuwa maalum kwa kuwapa wanawake huduma hizo za mikopo ya fedha.

Pamoja na hayo, Dk. Shein alimueleza Sheikh Al-Yousef kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar itahakikisha inaweka mazingira mazuri katika sekta ya uwekezaji ikiwa ni pamoja na kuhakikisha mradi anaotaka kuanzisha unaenda vizuri.

Nae Sheikh Al-Yousef alimueleza Dk. Shein kuwa lengo na madhumini ya Jumuiya yake ni kuekeza kwa kuanzisha mradi wa kuzalisha mayai ya kuku, ngombe na wanyama wengine, mradi ambao unatarajiwa kuzalisha mayai milioni moja ya kuku kwa siku.

Alisema kuwa tayari hatua za awali zimeshaanza kuchukuliwa ikiwa ni pamoja na kuleta mashine kadhaa sambamba na kutafuta soko zaidi nje ya Zanzibar. Pia, alitumia fursa hiyo kwa kuishuruku Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kumtengea eneo la ardhi kwa ajili ya kuendesha mradi huo.

Aidha, Sheikh Al-Youseif alimueleza Dk. Shein kuwa amekusudia kuanzisha mradi wa kuchimba visima 80 Unguja na Pemba na kuahidi kuleta mashine mpya, kubwa na za kisasa kwa ajili ya kuchimbia visima.

Alieleza kuwa mashine hizo za kuchibia visima zitakuwa maalum pamoja na pampu za kisasa za kusukumia maji kutoka visimani ambazo zitakuwa na nguvu kubwa ya kusukumia maji.

Kwa upande wa Benki ya Wanawake, Sheikh Al-Youseif alisema kuwa mtaji maalum utawekwa na Jumuiya yake kwa ajili ya kuwasaidia wanawake watakaowekwa katika  makundi maalum ambapo utawahusisha wanawake wakiwemo wajane, vizuka, vijana, wajasiriamali na wanawake wengineo.

Pia, Mwenyekiti huyo wa Jumuiya ya Al-Youseif, alieleza azma yake ya kuendelea na mradi mkubwa wa maji huko kisiwani Pemba katika kijiji cha Kiuyu na maeneo mengineyo.

Sheikh Al-Youseif alimueleza Dk. Shein azma yake ya kujenga nyumba 400 za mkopo nafuu huko kisiwani Pemba kwa ajili ya wananchi ambapo kwa hivi sasa tayari taratibu za awali zimeanza kuchukuliwa.

Sambamba na hayo, Sheikh Al-Youseif alipongeza juhudi za Dk. Shein katika kuimarisha amani, utulivu na maendeleo hapa nchini na kusisitiza kuwa sifa hizo zimekuwa zikizungumzwa duniani kote na ndio miongoni mwa sababu zilizompelekea kuja kuekeza Zanzibar

KOREA YA KUSINI KUJENGA KIJIJI CHA MFANO ZANZIBAR

HHHHKorea ya Kusini imesema inakusudia kukifanya kijiji cha Kibokwa kuwa cha mfano wa maendeleo kwa Tanzania.

Balozi wa nchi hiyo nchini Tanzania  balozi Jeong Il ameeleza hayo katika sherehe za ufunguzi wa jengo la kijiji cha Kibokwa, litakalotumika kwa shughuli mbali mbali zikiwemo za mikutano, ufundi, kilimo na mifugo.

Balozi Jeong Il amesema inawezekana kwa kijiji hicho kupiga hatua kubwa ya maendeleo na kuwa mfano wa kuigwa na vijiji vyengine vya Tanzania.

Amefahamisha kuwa Korea ya Kusini ilikuwa nchi maskini kama ilivyo Tanzania, lakini imeinuka kiuchumi baada ya kuamua kuanzisha vijiji vipya na kuviendeleza kama ilivyo kwa kijiji cha Kibokwa.

Amesema maendeleo ya kijiji hicho yatachochea maendeleo ya vijiji vyengine vya Zanzibar, na kuahidi kuanzisha mradi kama huo Kisiwani Pemba iwapo mradi huo wa Kibokwa utaonyesha mafanikio.

Nae Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad ambaye alikuwa mgeni rsmi katika sherehe hizo, amesema Korea ya Kusini ni marafiki wa kweli, na kwamba Serikali inathamini sana mchango unaotolewa na Korea kupitia miradi mbali ya maendeleo.

Amewataka wananchi wa Kibokwa kuuenzi na kuundeleza mradi huo, sambamba na kuendelea kuwapa mashirikiano wataalamu wa Korea walioko nchini, ili waweze kufanya shughuli zao kwa ufanisi.

Amesema kijiji hicho kimepata bahati ya kuanzishiwa mradi huo ambao ni muhimu kwa maendeleo yao na taifa kwa jumla, na kutaka uhifadhiwe vizuri ili uwe endelevu.

Amesema mradi huo ambao pia unahusisha kilimo cha umwagiliaji katika bonde la Kibokwa, utasaidia utekelezaji wa kauli mbiu ya serikali  katika Mapinduzi ya Kilimo, na hatimaye kupunguza utegemezi wa chakula.

Katika risala yao wananchi wa Kibokwa wameishukuru serikali kwa kuwapelekea mradi huo ambao tayari matunda yake yameanza kuonekana.

Risala hiyo   imetaja baadhi ya mafanikio yalioanza kupatikana kuwa ni pamoja na kupatikana fursa za ajira kwa vijana wa kijiji hicho hasa katika masuala ya ufugaji.

Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na Spika wa Bunge la Jimbo la Kyongsang la Korea ya Kusini Mhe. Song Pil Kak.

Jumuiya za Kiislamu Z’bar zalaani mauaji ya Padri

Baraza la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Zanzibar limelaani vikali matukio ya kushambuliwa na kuuliwa viongozi wa Dini likiwemo tukio la hivi karibuni la kupigwa risasi na kuuwawa Padri Mushi kulikofanywa na watu wasiojulikana huko Zanzibar. Baraza hilo pia limefafanua kuwa, uhai ni tunu kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu hivyo hakuna mwenye mamlaka ya kuiondoa haki hiyo isipokuwa yeye Mweyewe Mwenyezi Mungu. Limesema kuwa, kutokana na ukweli huu ndio maana Sheria za Kiislamu zimeweka wazi kuwa mtu mwenye kumuuwa mwenziwe naye auliwe kama inavyoelezwa katika Kitabu cha Quran Tukufu. Aidha limevitaja vitendo vya kiharamia vya kushambuliwa viongozi wa dini kuanzia kumwagiwa tindi kali Sheikh Soraga, kuuawa Padri Mushi hadi kushambuliwa kwa mapanga na kuuliwa Sheikh Ali Khamis Bin Ali Khatibu wa Mwakaje kuwa ni vitendo visivyokubaliki na Uislamu.

Baraza la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Zanzibar limesema wahusika wa vitendo hivyo watahesabika kuwa wahalifu bila ya kujali dini zao kwani vitendo vya kihalifu na kiharamia kamwe haviwezi kunasibishwa na dini fulani. Limeviomba vyombo husika kufanya upelelezi wa kina kuhusu matukio hayo kwa kuzingatia uadilifu na misingi ya kazi zao ili kuwabaini wahalifu na kufikishwa katika vyombo vya kisheria

MATOKEO YA KIDATO CHA NNE 2012

 

KWANINI UISLAMU UNYONGWE KWA KITANZI KWA KISINGIZIO CHA MAUWAJI YA PADRI ?

 

Kumb: 06/1434 AH                      10 Rabi-ul Thani 1434 AH          20/02/2013 CE

            

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

 

 

KWANINI UISLAMU UNYONGWE KWA KITANZI KWA KISINGIZIO CHA MAUWAJI YA PADRI ?

Kufuatia mauwaji ya kupigwa risasi kwa Padri wa Kanisa Katoliki  Evaristus Mushi, padri dhamana wa kanisa la St. Joseph Zanzibar yaliyotokea siku ya jumapili asubuhi, sisi Hizb ut-Tahrir Afrika Mashariki tunapenda kufafanua  yafuatayo:

Kwa bahati mbaya sana tukio hili limekuwa kana kwamba lilikuwa likisubiriwa na wanasiasa pamoja na viongozi wa kikiristo kwa lengo la kutoa msukumo zaidi wa ajenda ya kilimwengu ya chuki na uadui dhidi ya Uislamu na Waislamu. Kwa upande wa wanasiasa, kwa hakika ni fedheha kubwa isiyomithilika kwamba, badala ya kulikabili suala la kushindwa kulinda  maisha ya raia na mali zao tahamaki baadhi yao wamerukia  kuhitimisha kwamba tukio hili ni ‘tukio la ugaidi’.  Kauli hii ni jaribio la kutengeza ufahamu jumla (public opinion) wa kuuhusisha Uislamu na Waislamu moja kwa moja na tukio hilo. Ilhali wanasisa wanaepuka na kujisahaulisha kwa makusudi ukweli kwamba tukio hili lilitokea asubuhi kweupee! na karibu mno na Kituo kidogo cha Polisi. Pia wanaepuka ukweli wa kushindwa kwao kukabiliana na mfumo wa kiuchumi wa kibepari ambao unakuza pengo la kipato baina ya maskini na matajiri.Kitu kinachopelekea raia kuwa katika hali

ya kukata tamaa, kutoaminiana  na  kuzusha uadui baina yao.

Amma kuhusiana na viongozi wa kanisa, badala ya kuukabili Uislamu kwa mjadala wa kimfumo wanaficha udhaifu wao kwa kudandia tukio hili nao pia kuchochea zaidi chuki na uadui wa kilimwengu unaosukumwa na mataifa ya Magharibi dhidi ya Uislamu na Waislamu, vile vile wanafanya mbinu ya kuushawishi uchunguzi  wa tukio hili uwe na maslahi upande wao na mabwana wao wa kisiasa. Aidha, tukio hili linathibitisha tena kuwepo saratani iliyokita mizizi ndani ya Tanzania ya kuwapendelea Wakiristo, kwa kuwa tukio hili moja tu limeinua juu hisia ya serikali kiasi cha kuleta wachunguzi kutoka nje. Ilhali upande wa pili wanaharakati wa Kiislamu bado wanaendelea kusota korokoroni bila ya dhamana, na serikali inaonekana haijali wala kusikia kilio  chao.

 Pia, Hizb ut -Tahrir tunapenda kuweka bayana kwamba kuuwa wachungaji na viongozi wa kidini, kuchoma moto majumba ya ibada na makanisa ni jambo lisiloruhusiwa ndani ya Uislamu. Na ni ukweli unaojuulikana na kila mtu namna dola ya Kiislamu ya Khilafah huko nyuma ilivyowatizama kwa uadilifu wasiokuwa waislamu, kiasi kwamba mpaka leo wanaendelea kuwepo katika nchi kubwa za kiislamu ambazo  idadi ya Waislamu ni kubwa zaidi.

Mwisho, tunatoa mwito kwa walio makini na waadilifu katika wakiristo kuingia ndani ya Uislamu. Na ikiwa hawajawa tayari, basi wajitenge mbali na mitego ya makafiri wa madola ya Magharibi hususan Marekani ambao wana kampeni ya uadui isiyomalizika dhidi ya Waislamu na Uislamu. Tunawaeleza wakiristo kwamba: Marekani ni dola ambayo daima hukandamiza nchi ndogo, kupora rasilmali zake na kuleta mtafaruku na migongano baina ya raia. Aidha, tunawakumbusha wakiristo na wasiokuwa Waislamu kwa jumla kwamba, hapana shaka yoyote  Uislamu utatawala tena dunia na utawatunza wote katika hali ya uadilifu na insafu kama ulivyowahi huko nyuma. Katika mwaka wa 638 AD wakati Padri Sophrinius wa Palestina alipolisalimisha eneo  la ardhi hiyo chini ya dola ya Kiislamu  ya Khilafah, khalifah Umar ra. aliandika waraka maalum kwa watu wa Aelia unaosomeka:

KWA JINA LA ALLAH, ARRAHMAN, ARRAHIYM

“Huu ni Waraka wa mkataba kutoka kwa Umar  Mtumwa wa Allah, Amiri wa Waislamu, kwa watu wa Aelia. Anachukuwa dhamana ya usalama wa maisha yao, mali zao, makanisa yao na misalaba yao…Makanisa yao yasivunjwe wala yasiondoshwe, na kisiondoshwe
chochote katika vitu vyao. Wasilazimishwe katika mambo ya dini, na wala asidhuriwe
yoyote”.

Ikiwa huo ndio uadilifu wa Uislamu kwa wasiokuwa Waislamu, basi hali itakuwaje lau watu hao wataingia ndani ya  Uislamu ? Muda umeshafika kwa wao kuchukuwa fursa hii adhimu ya kuingia ndani ya Uislamu  mara moja.

………………….

 

Masoud Msellem

Naibu Mwakilishi kwa Vyombo vya Habari

Hizb-ut Tahrir Afrika Mashariki

Tel +255 778 870609

Pepe:  jukwalakhilafah@gmail.com

Tovuti  Rasmi ya Hizb ut- Tahrir

www.hizb-ut-tahrir.org

Tovuti ya Afisi ya Habari

   www.hizb-ut-tahrir.info

WATATU WAKAMATWA KENYA KUFUATIA MAUWAJI YA PADRI ZANZIBAR

2013-02-17 10.58.55-1649158318MAKACHERO wa Jeshi la Polisi nchini wamewatia mbaroni vijana watatu wanaotuhumiwa kuhusika katika mauaji ya Padri Everist Mushi (55) wa Kanisa Katoliki mjini Zanzibar.


Watuhumiwa hao wamekamatwa mjini Nairobi, Kenya kutokana na ushirikiano wa Jeshi la Polisi la Tanzania na Polisi wa Kenya kwa mwamvuli wa Shirikisho la Polisi wa Kimataifa (Interpol).

Habari za kuaminika kutoka Nairobi, Kenya zimesema kuwa watuhumiwa hao ambao majina yao yamehifadhiwa, walitiwa nguvuni juzi mjini humo walipowasili wakitokea Mombasa, mashariki mwa nchi hiyo.

Watuhumiwa hao ambao walikuwa wakiingia katika maficho kukwepa mkono wa dola, wanadaiwa kutumia jahazi kusafiria kutoka Zanzibar hadi Mombasa, Kenya kabla ya kusafiri kwa magari hadi Nairobi ambako walitiwa nguvuni.

Habari na Jamii Forums.

KANISA LACHOMWA MOTO

WATU wasiojulikana wamelishambuliya kwa kulichoma moto kanisa la waumini wa Siloam liliopo Kiyanga kilomitar 7 nje kidogo ya mji wa Unguja na kusababisha uharibifu mkubwa.

Hili ni tukio la pili kwa kanisa hilo lenye wafuasi 100 kushambuliwa ambapo mwaka jana watu wasiojulikana walivunja ukuta wa kanisa hilo ambapo ujenzi wake ulikuwa tayari umekamilika.

Mkurugenzi wa upelelezi wa jeshi la Polisi (DCI) Yussuf Ilembo alithibitisha kushambuliwa kwa kanisa hilo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika eneo la tukio la kanisa huko Kiyanga.

Ilembo akifuatana na timu ya makachero alisema katika hatua za mwanzo za uchunguzi huo inaonesha kuwepo kwa hujuma kwa watu kushambuliya kanisa kwa kulichoma moto,ambapo baadhi ya sehemu za ndani ya kanisa hilo zimeharibika.

‘Tunafanya uchunguzi ndio unaona kikosi cha makachero wakiwa na vifaa vyao wakipima eneo lililoharibiwa kwa moto’alisema Ilembo na kukiri kwamba ni mara ya pili kwa kanisa hilo kushambuliwa.

Alisema wataanza kufuatia kumbukumbu za nyuma kuhusu taarifa za kukamatwa kwa baadhi ya watu waliohusikana na tukio la kwanza la kuvunjwa kwa kanisa hilo.

Mchungaji msaidizi wa kanisa hilo, Bi Penuel Wisdom Elisha alisema wafuasi wake hivi sasa wapo katika sherehe za sikukuu ya pasaka, alisema alipokea simu kutoka kwa mlinzi wa kanisa hilo majira ya saa 11 za usiku ambapo alipewa taarifa ya kushambuliwa kwa kanisa hilo kwa watu kurusha mawe na baadaye kushoma moto.

Hata hivyo mchungaji msaidizi Elisha alikiri kuwepo kwa msunguano wa mgogoro wa muda mrefu na uongozi wa msikiti wa Kiyanga ambao umekuwa ukihoji sababu za kujengwa kwa kanisa hilo na nani aliyewapa kiwanja.

‘Hapa tunakabiliwa na mgogoro wa muda mrefu na uongozi wa msikiti wa Kiyanga ambapo mwaka jana walituita na kutuuliza nani aliyetupa kiwanja na kama tunayo hati ya kujenga kanisa’alisema.

Anasema katika kikao hicho walionesha hati ya kumiliki kiwanja pamoja na shunguli za ujenzi wa kanisa hilo kihalali.

‘Ndiyo maana mimi sitaki kuuita huu ni mgogoro…..sisi tunamiliki kiwanja hichi kihalali sasa tatizo wapo watu hawataki tuwepo hapa kwa ajili ya kujenga kanisa tu’alisema.

Alisema katika tukio la kuvunjwa kwa kanisa hilo mwaka jana watu kadhaa walishikiliwa na polisi lakini katika kipindi kifupi waliachiwa na ndiyo maana wamekuwa wakitoa vitisho mara kwa mara.

Mlinzi mmoja wa kanisa hilo aliyejitambulisha kwa jina la Mussa Jackson alisema kwa muda wa wiki mbili sasa wamekuwa wakipokea taarifa za vitisho vya aina mbali mbali ambapo wameviripoti polisi.
‘Hapa matukio ya taarifa za vitisho ni za kawaida tangu tulipoanza kujenga kanisa hili ambapo baadhi ya majirani huku hawataki kuendelea na ujenzi wa kanisa letu’ alisema Jackson