WATU wasiojulikana wamelishambuliya kwa kulichoma moto kanisa la waumini wa Siloam liliopo Kiyanga kilomitar 7 nje kidogo ya mji wa Unguja na kusababisha uharibifu mkubwa.

Hili ni tukio la pili kwa kanisa hilo lenye wafuasi 100 kushambuliwa ambapo mwaka jana watu wasiojulikana walivunja ukuta wa kanisa hilo ambapo ujenzi wake ulikuwa tayari umekamilika.

Mkurugenzi wa upelelezi wa jeshi la Polisi (DCI) Yussuf Ilembo alithibitisha kushambuliwa kwa kanisa hilo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika eneo la tukio la kanisa huko Kiyanga.

Ilembo akifuatana na timu ya makachero alisema katika hatua za mwanzo za uchunguzi huo inaonesha kuwepo kwa hujuma kwa watu kushambuliya kanisa kwa kulichoma moto,ambapo baadhi ya sehemu za ndani ya kanisa hilo zimeharibika.

‘Tunafanya uchunguzi ndio unaona kikosi cha makachero wakiwa na vifaa vyao wakipima eneo lililoharibiwa kwa moto’alisema Ilembo na kukiri kwamba ni mara ya pili kwa kanisa hilo kushambuliwa.

Alisema wataanza kufuatia kumbukumbu za nyuma kuhusu taarifa za kukamatwa kwa baadhi ya watu waliohusikana na tukio la kwanza la kuvunjwa kwa kanisa hilo.

Mchungaji msaidizi wa kanisa hilo, Bi Penuel Wisdom Elisha alisema wafuasi wake hivi sasa wapo katika sherehe za sikukuu ya pasaka, alisema alipokea simu kutoka kwa mlinzi wa kanisa hilo majira ya saa 11 za usiku ambapo alipewa taarifa ya kushambuliwa kwa kanisa hilo kwa watu kurusha mawe na baadaye kushoma moto.

Hata hivyo mchungaji msaidizi Elisha alikiri kuwepo kwa msunguano wa mgogoro wa muda mrefu na uongozi wa msikiti wa Kiyanga ambao umekuwa ukihoji sababu za kujengwa kwa kanisa hilo na nani aliyewapa kiwanja.

‘Hapa tunakabiliwa na mgogoro wa muda mrefu na uongozi wa msikiti wa Kiyanga ambapo mwaka jana walituita na kutuuliza nani aliyetupa kiwanja na kama tunayo hati ya kujenga kanisa’alisema.

Anasema katika kikao hicho walionesha hati ya kumiliki kiwanja pamoja na shunguli za ujenzi wa kanisa hilo kihalali.

‘Ndiyo maana mimi sitaki kuuita huu ni mgogoro…..sisi tunamiliki kiwanja hichi kihalali sasa tatizo wapo watu hawataki tuwepo hapa kwa ajili ya kujenga kanisa tu’alisema.

Alisema katika tukio la kuvunjwa kwa kanisa hilo mwaka jana watu kadhaa walishikiliwa na polisi lakini katika kipindi kifupi waliachiwa na ndiyo maana wamekuwa wakitoa vitisho mara kwa mara.

Mlinzi mmoja wa kanisa hilo aliyejitambulisha kwa jina la Mussa Jackson alisema kwa muda wa wiki mbili sasa wamekuwa wakipokea taarifa za vitisho vya aina mbali mbali ambapo wameviripoti polisi.
‘Hapa matukio ya taarifa za vitisho ni za kawaida tangu tulipoanza kujenga kanisa hili ambapo baadhi ya majirani huku hawataki kuendelea na ujenzi wa kanisa letu’ alisema Jackson
Advertisements