HHHHKorea ya Kusini imesema inakusudia kukifanya kijiji cha Kibokwa kuwa cha mfano wa maendeleo kwa Tanzania.

Balozi wa nchi hiyo nchini Tanzania  balozi Jeong Il ameeleza hayo katika sherehe za ufunguzi wa jengo la kijiji cha Kibokwa, litakalotumika kwa shughuli mbali mbali zikiwemo za mikutano, ufundi, kilimo na mifugo.

Balozi Jeong Il amesema inawezekana kwa kijiji hicho kupiga hatua kubwa ya maendeleo na kuwa mfano wa kuigwa na vijiji vyengine vya Tanzania.

Amefahamisha kuwa Korea ya Kusini ilikuwa nchi maskini kama ilivyo Tanzania, lakini imeinuka kiuchumi baada ya kuamua kuanzisha vijiji vipya na kuviendeleza kama ilivyo kwa kijiji cha Kibokwa.

Amesema maendeleo ya kijiji hicho yatachochea maendeleo ya vijiji vyengine vya Zanzibar, na kuahidi kuanzisha mradi kama huo Kisiwani Pemba iwapo mradi huo wa Kibokwa utaonyesha mafanikio.

Nae Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad ambaye alikuwa mgeni rsmi katika sherehe hizo, amesema Korea ya Kusini ni marafiki wa kweli, na kwamba Serikali inathamini sana mchango unaotolewa na Korea kupitia miradi mbali ya maendeleo.

Amewataka wananchi wa Kibokwa kuuenzi na kuundeleza mradi huo, sambamba na kuendelea kuwapa mashirikiano wataalamu wa Korea walioko nchini, ili waweze kufanya shughuli zao kwa ufanisi.

Amesema kijiji hicho kimepata bahati ya kuanzishiwa mradi huo ambao ni muhimu kwa maendeleo yao na taifa kwa jumla, na kutaka uhifadhiwe vizuri ili uwe endelevu.

Amesema mradi huo ambao pia unahusisha kilimo cha umwagiliaji katika bonde la Kibokwa, utasaidia utekelezaji wa kauli mbiu ya serikali  katika Mapinduzi ya Kilimo, na hatimaye kupunguza utegemezi wa chakula.

Katika risala yao wananchi wa Kibokwa wameishukuru serikali kwa kuwapelekea mradi huo ambao tayari matunda yake yameanza kuonekana.

Risala hiyo   imetaja baadhi ya mafanikio yalioanza kupatikana kuwa ni pamoja na kupatikana fursa za ajira kwa vijana wa kijiji hicho hasa katika masuala ya ufugaji.

Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na Spika wa Bunge la Jimbo la Kyongsang la Korea ya Kusini Mhe. Song Pil Kak.

Advertisements