Archive for March, 2013

Mahakama Kuu Kenya yasema Uhuru alichaguliwa kihalali

8A411BBD-10FA-4F25-8F17-7714BDF92195_w443_r1Mahakama kuu ya Kenya imetangaza muda mfupi uliopita kuwa Uhuru Kenyatta alichaguliwa kihalali katika uchaguzi mkuu uliopita Kenya. Uamuzi huo unakuja wiki kadhaa baada ya uchaguzi kufuatia hatua ya mpinzani wake Raila Odinga kupinga matokeo hayo na kufungua madai mahakama kuu. Leo mahakama kuu inasema uchaguzi ulikuwa huru na halali.

Wakenya wamekuwa wakisubiri uamuzi wa mahakama kwa shauku kubwa. Polisi Ijumaa ilitoa ilani kwa wafuasi wa pande zote mbili kujiepusha na kushereheka au kulalamika kufuatia uamuzi wa mahakama.

Kulingana na ratiba Uhuru Kenyatta ataapishwa rasmi kuchukua uongozi wa Kenya Aprili 9, 2013

Advertisements

UCHAGUZI WA MABARAZA KATIBA WAVURUGIKA ZANZIBAR

BIMANI..Chama cha wananchi CUF kimeitaka tume ya mabadiliko ya katiba kufuta matokeo ya kuwapata wajumbe wa mabaraza ya katiba ya wilaya katika baadhi ya shehia za mkoa wa mjini maghari ikidai uchaguzi huo umevurugwa.

Akizungumza na Zenji fm radio juu ya uchaguzi huo mkurugenzi wa haki za binadamu, habari na mawasiliano ya Umma Salim Bimani amesema uchaguzi huo umejaa utashi wa kisiasa.

Amesema baadhi ya masheha katika mkoa huo wametoa karatasi zap kupigia kura zisizotambulika, kutumiwa vitambulisho vya ukaazi, kuahirisha uchaguzi kabla ya wakati, kutumika majina ya wasiokuwa wakaazi na kupiga kura kwa askari wa vikosi

Bimani amesema tume hiyo lazima iratibu upya uchaguzi huo ili kuhakikisha taratibu za kuwapata wajumbe watatu kila shehia watakaoshiriki katika mabaraza ya katiba ya wilaya zinafuatwa.

Uchaguzi wa mabaraza ya katiba umepangwa kufanyika kuanzia ele hadi tarehe mosi mwezi ujao.

SMZ KUTOA HUDUMA KWA WATOTO YATIMA

imagesRAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa Serikali itaendelea kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha inafikia hatua nzuri katika kutoa huduma kwa jamii  hasa watoto mayatima huku akisisitiza haja ya kuwalea katika maisha bora na yenye furaha.

 

Dk. Shein aliyasema hayo leo katika sherehe ya siku ya motto yatima, zilizofanyika katika ukumbi wa Salama Bwawani mjini Zanzibar na kuhudhuriwa na viongozi mbali mbali akiwemo Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad, Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabih, Balozi wa Uturuki Mhe. Ali Daud Gul,wazee, wazazi pamoja na watoto yatima kutoka ndani na nje ya Zanzibar.

 

Dk. Shein alisema kuwa azma ya Serikali ni kujenga misingi imara kwa jamii ya watoto na watu wazima ili kuwajengea wananchi maisha bora zaidi.

 

Alisema kuwa  hatua za kusaidia watoto yatima zinakwenda sambamba na juhudi za serikali ya Mapinduzi Zanzibar tokea kuasisiwa na Marehemu Mzee Abeid Amani Karume alipofungua nyumba ya watoto yatima Forodhani mara tu baada ya Mapinduzi ya Januari 12, 1964.

 

Aliongeza kuwa katika kuendeleza huduma hiyo, Serikali ikishirikiana na Taasisi ya ZAYEDESA imewahamisha watoto yatima kwenda nyumba ya kisasa Mazizini na inatoa ushiriki mkubwa na Taasisi ya SOS katika kuendeleza kijiji cha watoto yatima Mombasa Unguja ambapo ipo skuli ya msingi na Sekondari pamoja na kupitisha Sheria Namba 6 ya mwaka 2011 yenye lengo la kuhakikisha haki za watoto, ulizni na ustawi wao.

 

Katika hotuba yake hiyo Dk. Shein alisema kuwa misaada na shughuli zao ni kuipunguzia mzigo Serikali ambayo hutumia kiasi kikubwa cha fedha katika uimarishaji wa sekta hizo hapa Zanzibar.

 

Dk. Shein aliwanasihi wazazi kuunga mkono juhudi  za Jumuiya ya Muzdalifa kwa kuwekeza katika kuwalea vyema watoto yatima ambao mara nyingi wanakuwa nyuma.

 

Alieleza kuwa wazazi na walezi wanawajibu mkubwa kwa watoto yatima kwa kuwapa elimu, chakula kizuri, kuwapenda na kuwakinga na unyanyasaji, hasa wa kijinsia jambo ambalo litapelekea kuwa na vijana madhubuti walio na afya njema, elimu na uzalendo

 

“Suala la malezi mema kwa watoto yatima ni la lazima kwani wasemavyo wahenga’usipoziba ufa utajenga ukuta”,alisema Dk. Shein.

 

Aidha, Dk. Shein alieleza kuwa kuvunjika kwa amani ni miongoni mwa mazingira yanayosababishwa na binaadamu na kupelekea kuwepo kwa watoto yatima wengi.

 

Alisema kuwa  dunia imekuwa ikishuhudia hali ilibvyokuwa mbaya katika baadhi ya nchi, Mashariki ya Kati, Asia na hata eneo la Afrika ambapo maelfu ya watoto wamebakia yatima kutokana na kukosa amani.

 

Alisisitiza kuwa hali hiyo inabainisha umhyimu wa kutunza amani na usalama kwani bila ya amani ni mtafaruku wa jamii na kuhatarisha maisha ya watoto.

 

Pamoja na hayo, Dk. Shein alitoa nasaha kwa jamii kujali na kudumisha amani miongoni mwa jamii pamoja na kujikinga na maradhi thakili na hatari ya ukimwi kwani ni maradhi yanayosababisha vifo vya wazazi na hatimae kuwaacha watoto yatima.

 

Dk. Shein alieleza haja ya kuzingatia hali iliyojitokeza nchini hivi sasa ya kuwepo watoto wanaoishi katika mazingira magumu ambapo wengine hukosa mahala pa kula, kulala, hawapati elimu na kwa jumla wanakuwa hawana mwelekeo mwema wa maisha yao.

 

“Ni wajibu wetu tushirikiane ili tuweze kuwaondoshea hali hii watoto wetu…naipongeza Wizara ya Ustawi wa Jamii, Maendeleo ya Vijana, Wanawake na Watoto kwa jitihada zao ni vyema taasisi nyengine zikashiriki katika kuliondoa tatizo hili  ambalo lipo mijini”,aliongeza Dk. Shein.

 

Sambamba na hayo, Dk. Shein aliitaka Wizara ya Katiba na Sheria kuendelea kuwa karibu na Jumuiya ya Muzdalifah na kutoa shukurani kwa Jumuiya zote za ndani na nje ya Zanzibar zikiwemo I.H.H ya Uturuki, WEFA ya Ujerumani na Al-ANSAR FOUNDATION ya Uiengereza kwa kutoa michango yao mikubwa ya kuiunga mkono Jumuiya ya Muzdalifah ili iweze kufaya kazi zake vizuri.

 

Nae Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Abubakar Khamis, alieleza kuwa Serikali imekuwa ikishirikiana na taasisi mbali mbali katika kuhakikisha watoto yatima wanapata huduma zinazostahiki ili waweze kuishi vizuri.

 

Nae Mbunge Mstaafu wa Bunge la Uturuki Mhe. Husnu Tuna akitoa salamu zake kutoka kwa Jumuiya ya I.H.H alisema kuwa  tatsisi hiyo imekuwa ikitoa misaada ya kibinadamu ambayo lengo lake ni kuondoa matatizo ya watoto mayatima ambapo imekuwa ikiiunga mkono Tanzania kwa mwaka wan ne hivi sasa na inalea mayatima 29,000 katika nchi 41.

 

Aidha, katika risala yao Jumuiya ya Muzdalifah ilieleza kuwa imekuwa ikitoa huduma mbali mbali zikiwemo huduma za kuwasaidia watoto yatima, huduma afya, maskulini, madrasat, zakka, sadaka, maafa, kuchimba visima na huduma nyenginezo.

 

Nao watoto yatima walieleza furaha zao kwa mgeni rasmi kwa kuungana nao katika siku yao hiyo adhimu na kutoa ombi lao la kuitaka siku hii iwe ya Kitaifa

 

MBUNGE WA CHAMBANI CUF SALIM HEME KHAMIS AFARIKI DUNIA

Mbunge wa Chambani (CUF), Salim Hemed Khamis (60) amefariki dunia jana katika hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) alikokuwa amelazwa baada ya kuanguka ghafla juzi kwenye Ofisi za Bunge, Dar es Salaam.

Kifo cha mbunge huyo kimewagusa wengi akiwamo Rais Jakaya Kikwete ambaye ametoa ndege yake ili kusafirisha mwili wa marehemu kwenda Pemba. Ofisi ya Bunge imethibitisha kutokea kwa kifo hicho cha mbunge huyo na kueleza kuwa, alipatwa na ugonjwa wa kiharusi uliosababishwa na ugonjwa wa moyo (Hypertension).

Khamis anatarajiwa kusafirishwa kisha kuzikwa leo kijijini kwao Chambani, Pemba baada ya jitihada za kumsafirisha jana kushindikana na wabunge wengi kuomba kushiriki kumuaga.
Mbunge huyo atasafirishwa leo saa tatu asubuhi baada ya shughuli ya kuaga itakayofanyika kwenye Viwanja vya Ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam. Spika wa Bunge, Anne Makinda ametangaza kusitishwa kwa shughuli zote za Kamati za Bunge hadi Jumanne Aprili 2, kutokana na msiba huo.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, Makinda alisema: “Ninatoa pole kwa familia ya marehemu, wananchi wa Chambani, Wajumbe wa Kamati ya Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa, wabunge wote na Watanzania wote kwa jumla”.

Khamis alianguka juzi saa 10.50 asubuhi wakati akishiriki kwenye kikao cha Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kilichofanyika katika ofisi za Bunge jijini Dar es Salaam.

Kaimu Katibu wa Bunge, John Joel alisema wamepokea taarifa za kifo hicho kwa masikitiko ambacho kilisababishwa na kupasuka kwa mshipa wa damu kichwani.

“Tumeelezwa na daktari kuwa Mbunge Salim amefariki kutokana na kupasuka kwa mishipa ya damu ambayo ilimiminikia kwenye ubongo wake na kuenea kichwani,” alisema Joel. Alisema kutokana na hali hiyo shughuli zote za uchambuzi wa bajeti zilizokuwa zikifanywa na kamati za Bunge, zimeahirishwa kwa mujibu wa taratibu zilizopo hadi tutakapomaliza shughuli za mazishi.

Joel alisema kwa upande wa Bunge, shughuli za msiba zitaongozwa na Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa ambaye ni Mwenyekiti wa kamati ambayo marehemu alikuwa mjumbe.

Alisema Bunge linamshukuru Rais Kikwete kwa kutoa ndege yake kwa ajili ya kupeleka mwili huo Pemba na kwamba hatua hiyo itatoa fursa kwa wabunge wengi kushiriki mazishi.
Alisema kutokana na hali hiyo wabunge 12 wakiongozwa na Lowassa watakwenda kushiriki kwenye msiba.

Wabunge, CUF waomboleza
Baadhi ya wabunge jana walionekana kuchanganyikiwa baada ya kupata taarifa za msiba huo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti walisema kuwa kifo hicho ni cha ghafla kwa sababu Salim alikuwa kwenye vikao vya Bunge tangu walipoanza vikao vya kamati.

“Tangu tuanze vikao vya kamati tulikuwa naye na alionekana kuwa mwenye afya, kwangu mimi ni pigo nimepata kwa sababu alikuwa mwalimu kisiasa katika Chama cha CUF,” alisema Rajab Mohamed Khamis, ambaye ni Mbunge wa Ole (CUF).

Kwa upande wake, Mbunge wa Peramiho CCM, Jenister Mhagama alishtuka na kuonekana kutoamini taarifa hizo, jambo ambalo lilimfanya ashindwe kuzungumza chochote.
Wabunge wengi walionekana wakihaha kutafuta usafiri ili wawezekwenda Muhimbili huku baadhi yao wakienda kujiandaa na safari ya kwenda Pemba

KKKT-MWANAKWEREKWE LATOA MSAMAHA WA MAUWAJI YA PADRI MUSHI

Kanisa la KKKT la Mwanakwerekwe limesema liko tayari kuwasamehe watu waliohusika na mauwaji ya padri wa kanisa katoliki Everest Mush iwapo watajitokeza hadharani na kutubu dhambi hiyo.

Akizungumza na Zanzibar islamic news Blog kuhusiana na siku ya Pasaka Mchungaji kiongozi wa kanisa hilo Shukur Maloda amesema ingawa kesi ya tukio hilo iko mahakamani, lakini kanisa linayonafasi ya kusemehe.

Amesema msamaha katika imani ya Kikiristo inatanguliwa na toba, ikiwemo kukiri kosa hilo na hatimae kufikia maridhiano….

Kauli hiyo ya kanisa la KKKT imekuja kufuatia kukamatwa kwa mtu anaetuhumiwa kuhusika na mauwaji hayo.

Aidha Mchungaji Maloda amewataka wananchi wa madhehebu ya dini mbali kushirikiana katika kudumisha amani na utulivu ili kuzuwia  vitendo vya uhalifu vikiwemo mauwaji ya viongozi wa kidini.

Kanisa la KKKT la Mwanakwerekwe pia limetoa wito kwa serikali kuvipatia vifaa vya ulinzi vya kupambana na magenge ya wahalifu kwa vikundi vya ulinzi vinavyoanzishwa na wananchi.

MTU ALIEMUUWA PADRI MUSHI AKAMATWA ZANZIBAR

Kamishna wa jeshi la polisi Zanzibar Mussa Ali Mussa

Kamishna wa jeshi la polisi Zanzibar Mussa Ali Mussa

Jeshi la polisi Zanzibar limefanikiwa kumkamata mtu anaedaiwa kuhusika na mauwaji ya Padri wa kanisa Katoliki Evarest Mushi yaliotokea mapema mwaka huu.

Akizungumza na wandishi wa habari kamishna wa jeshi la polisi Zanzibar Mussa Ali Mussa amesema mtuhumiwa huyo Omar Mussa Makame mkaazi wa Mwanakwerekwe ametambuliwa na watu walioshudia tukio hilo lilitokea katika maeneo ya Bububu.

Amesema baada ya kuchora michoro ya sura ya mtu aliehusika na tukio hilo kwa kutumia watu walioshuhudia na kuitoa kwenye vyombo vya ulinzi, wananchi na mitandao ya kijamii mhalifu huyo ametambuliwa.

Kamishna Mussa amesema mwananchi aliesaidia kutambuliwa kwa mtu huyo atazawadiwa shilingi milioni 10 kufuatia jeshi la polisi kuahidi kutowa zawadi ya kiwango hicho cha fedha.

Hata hivyo amesema kwa usalama wa mtu aliesaidia kukamatwa kwa mhalifu huyo na sababu za kiupelelezi tukio la kuimkabidhi fedha hizo litafanyika kwa njia za siri

        Aidha Kamishna Mussa amewataka wananchi kuendelea kutoa ushirikiano wa hali ya juu ili kufanikisha upelelezi wa matukio mengine yaliopita ikiwemo kujeruhiwa kwa viongozi wa kidini.

Amesema jeshi la polisi litaendelea kutunza siri zap watu watakaotoa taarifa hizo.

JENGO LA GHOROFA 15 LAPOROMOKA MJINI DAR ES SALAAM

Inaarifiwa takriban watu zaidi ya kumi wamefarriki na wengine bado wamenaswa kwa vifusi

Inaarifiwa takriban watu zaidi ya kumi wamefarriki na wengine bado wamenaswa kwa vifusi

Watu wasiopungua 40 wanahofiwa wamekwama wakati jumba moja linalojengwa la ghorofa lilipo poromoka leo asubuhi mjini Dar-es-Salaam mji mkuu wa kiuchumi wa Tanzania.Hayo ni kwa mujibu wa mkuu wa mkoa wa Daresalam Saidi Mecky Sadiky.Amesema amearifiwa kulikuwa na watu sitini katika  eneo hilo la ujenzi,wengi wao ni wafanyakazi,lakini pia wachuuzi na watoto waliokuwa wakicheza karibu na eneo hilo. Hakuna ripoti kuhusu idadi ya watu waliofariki-lakini watatu  kati ya 19 waliookolewa wanasemekana ni mahatuti na hawana fahamu.Jumba hilo linalojengwa la ghorofa 15 linakutikana katika mtaa wa biashara na ofisi za serikali jijini Dar-es-Salaam.Waokozi na wakaazi wanasaidiana kuwaokoa wahanga wa ajali hiyo.Watu wasiopungua wanne walipoteza maisha yao na wengine kadhaa kujeruhiwa wakati jengo moja lililokuwa likijengwa lilipoporomoka katika mji huo wa Dar-es-Salaam mnamo mwaka 2008