WANANCHI wa kijiji cha Makangale na vijiji vya jirani katika wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba ambao wanakabiliwa na tatizo la barabara wametakiwa kufanya subira kwa sababu Serikali imeanza kulitatufutia ufumbuzi tatizo hilo.  
Wito huo umetolewa  na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein wakati alipokuwa akizungumza na wananchi hao katika siku yake ya kwanza ya ziara yake ya siku sita kisiwani Pemba.
 
Aliwaeleza wananchi hao kuwa katika hatua ya kwanza tatizo hilo linashughulikiwa kwa kuijenga barabara inayopitia msitu wa Ngezi kwa kuitia kifusi eneo lililo nje ya msitu wakati sehemu iliyopita katika msitu huo itajengwa kwa kutumia saruji, mchanga na kifusi kuepuka uchafuzi wa mazingira katika eneo la msitu.
 
“Hatuwezi kujenga barabara ya lami ndani ya msitu wala barabara ya kifusi kwa kuhofia kuharibu mazingira lakini tutaijenga barabara hiyo kama watalaalamu walivyoshauri kwa kutumia mchanga, saruji na kifusi kwa sehemu zilizo ndani ya msitu na sehemu ya nje ya msitu kwa kifusi”alisema.
 
Wakati jitihada za kuijenga barabara zinafanyika serikali kwa upande mwingine ina mpango wa kujenga barabara ya lami yenye urefu wa kilomita 13.3 kutoka Kiuyu hadi Makangale  ambayo itapita nje ya msitu huo.
 
“Mbali ya kuijenga hii ya sasa lakini tuna mpango wa kujenga barabara ya lami ya kilomita 13.3 kutoka Kiuyu hadi Makangale ambayo itaondosha kabisa tatizo lenu la barabara ambapo mtakuwa na uchaguzi kutumia barabara hiyo mpya ya lami au hii inayopita katika msitu”aliwaeleza.
 
Hatua hizo za kujenga barabara alieleza Dk. Shein kuwa zinatokana na maagizo yake aliyoyatoa katika ziara yake aliyoifanya mwaka jana kwa wizara tatu ambazo alizitaka kulitafutia ufumbuzi tatizo lao.
 
“Wakati wa ziara yangu mwaka jana niliziagiza Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Wizara ya Ardhi na wizara ya Miundombinu kukaa pamoja na Wizara ya Kilimo na Maliasili kuangalia namna ya kujenga barabara bila ya kuathiri msitu” Dk Shein aliwakumbusha wananchi hao.
 
Katika ziara yake hiyo Rais alikagua ujenzi wa barabara za Wete- Konde inayojengwa kwa fedha kutoka Serikali ya Mpinduzi Zanzibar na Benki ya Afrika. Barabara nyingine aliyotembelea ni ya Mapofu hadi Mzambarauni iyojengwa kupitia msaada wa fedha kutoka Mfuko wa Changamoto za Milenia.
 
Wakati huo huo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amewapongeza wananchi wa Shumba Mjini, Wilaya ya Micheweni, kwa uamuzi wao wa kuchagia elimu ya watoto wao.
 
Pongezi hizo amezitoa leo wakati alipokuwa akizungumza na wananchi hao mara baada ya kuweka jiwe la msingi la madarasa mane ya skuli ya Karume.
 
“nawapongeza kwa uamuzi wenu wa kuongeza madarasa mane; ni uamuzi wa busara, hekima na kimaendeleo…mmejinyima mengi kwa uamuzi wenu huu” aliwaeleza.
 
Dk Shein alisema serikali inaendelea na sera yake ya kutoa elimu bila malipo ingawa hivi sasa kutokana na mzigo mkubwa wa kugharimia elimu nchini imeweka utaratibu wa wazazi kuchagia kama ambavyo wananchi wa Shumba walivyofanya.
 
Rais anatarajiwa kuendelea na ziara yake kesho (Jumatatu) katika mkoa huo wa Kaskazini

Advertisements