Kamishna wa jeshi la polisi Zanzibar Mussa Ali Mussa

Kamishna wa jeshi la polisi Zanzibar Mussa Ali Mussa

Jeshi la polisi Zanzibar limefanikiwa kumkamata mtu anaedaiwa kuhusika na mauwaji ya Padri wa kanisa Katoliki Evarest Mushi yaliotokea mapema mwaka huu.

Akizungumza na wandishi wa habari kamishna wa jeshi la polisi Zanzibar Mussa Ali Mussa amesema mtuhumiwa huyo Omar Mussa Makame mkaazi wa Mwanakwerekwe ametambuliwa na watu walioshudia tukio hilo lilitokea katika maeneo ya Bububu.

Amesema baada ya kuchora michoro ya sura ya mtu aliehusika na tukio hilo kwa kutumia watu walioshuhudia na kuitoa kwenye vyombo vya ulinzi, wananchi na mitandao ya kijamii mhalifu huyo ametambuliwa.

Kamishna Mussa amesema mwananchi aliesaidia kutambuliwa kwa mtu huyo atazawadiwa shilingi milioni 10 kufuatia jeshi la polisi kuahidi kutowa zawadi ya kiwango hicho cha fedha.

Hata hivyo amesema kwa usalama wa mtu aliesaidia kukamatwa kwa mhalifu huyo na sababu za kiupelelezi tukio la kuimkabidhi fedha hizo litafanyika kwa njia za siri

        Aidha Kamishna Mussa amewataka wananchi kuendelea kutoa ushirikiano wa hali ya juu ili kufanikisha upelelezi wa matukio mengine yaliopita ikiwemo kujeruhiwa kwa viongozi wa kidini.

Amesema jeshi la polisi litaendelea kutunza siri zap watu watakaotoa taarifa hizo.

Advertisements