imagesRAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa Serikali itaendelea kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha inafikia hatua nzuri katika kutoa huduma kwa jamii  hasa watoto mayatima huku akisisitiza haja ya kuwalea katika maisha bora na yenye furaha.

 

Dk. Shein aliyasema hayo leo katika sherehe ya siku ya motto yatima, zilizofanyika katika ukumbi wa Salama Bwawani mjini Zanzibar na kuhudhuriwa na viongozi mbali mbali akiwemo Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad, Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabih, Balozi wa Uturuki Mhe. Ali Daud Gul,wazee, wazazi pamoja na watoto yatima kutoka ndani na nje ya Zanzibar.

 

Dk. Shein alisema kuwa azma ya Serikali ni kujenga misingi imara kwa jamii ya watoto na watu wazima ili kuwajengea wananchi maisha bora zaidi.

 

Alisema kuwa  hatua za kusaidia watoto yatima zinakwenda sambamba na juhudi za serikali ya Mapinduzi Zanzibar tokea kuasisiwa na Marehemu Mzee Abeid Amani Karume alipofungua nyumba ya watoto yatima Forodhani mara tu baada ya Mapinduzi ya Januari 12, 1964.

 

Aliongeza kuwa katika kuendeleza huduma hiyo, Serikali ikishirikiana na Taasisi ya ZAYEDESA imewahamisha watoto yatima kwenda nyumba ya kisasa Mazizini na inatoa ushiriki mkubwa na Taasisi ya SOS katika kuendeleza kijiji cha watoto yatima Mombasa Unguja ambapo ipo skuli ya msingi na Sekondari pamoja na kupitisha Sheria Namba 6 ya mwaka 2011 yenye lengo la kuhakikisha haki za watoto, ulizni na ustawi wao.

 

Katika hotuba yake hiyo Dk. Shein alisema kuwa misaada na shughuli zao ni kuipunguzia mzigo Serikali ambayo hutumia kiasi kikubwa cha fedha katika uimarishaji wa sekta hizo hapa Zanzibar.

 

Dk. Shein aliwanasihi wazazi kuunga mkono juhudi  za Jumuiya ya Muzdalifa kwa kuwekeza katika kuwalea vyema watoto yatima ambao mara nyingi wanakuwa nyuma.

 

Alieleza kuwa wazazi na walezi wanawajibu mkubwa kwa watoto yatima kwa kuwapa elimu, chakula kizuri, kuwapenda na kuwakinga na unyanyasaji, hasa wa kijinsia jambo ambalo litapelekea kuwa na vijana madhubuti walio na afya njema, elimu na uzalendo

 

“Suala la malezi mema kwa watoto yatima ni la lazima kwani wasemavyo wahenga’usipoziba ufa utajenga ukuta”,alisema Dk. Shein.

 

Aidha, Dk. Shein alieleza kuwa kuvunjika kwa amani ni miongoni mwa mazingira yanayosababishwa na binaadamu na kupelekea kuwepo kwa watoto yatima wengi.

 

Alisema kuwa  dunia imekuwa ikishuhudia hali ilibvyokuwa mbaya katika baadhi ya nchi, Mashariki ya Kati, Asia na hata eneo la Afrika ambapo maelfu ya watoto wamebakia yatima kutokana na kukosa amani.

 

Alisisitiza kuwa hali hiyo inabainisha umhyimu wa kutunza amani na usalama kwani bila ya amani ni mtafaruku wa jamii na kuhatarisha maisha ya watoto.

 

Pamoja na hayo, Dk. Shein alitoa nasaha kwa jamii kujali na kudumisha amani miongoni mwa jamii pamoja na kujikinga na maradhi thakili na hatari ya ukimwi kwani ni maradhi yanayosababisha vifo vya wazazi na hatimae kuwaacha watoto yatima.

 

Dk. Shein alieleza haja ya kuzingatia hali iliyojitokeza nchini hivi sasa ya kuwepo watoto wanaoishi katika mazingira magumu ambapo wengine hukosa mahala pa kula, kulala, hawapati elimu na kwa jumla wanakuwa hawana mwelekeo mwema wa maisha yao.

 

“Ni wajibu wetu tushirikiane ili tuweze kuwaondoshea hali hii watoto wetu…naipongeza Wizara ya Ustawi wa Jamii, Maendeleo ya Vijana, Wanawake na Watoto kwa jitihada zao ni vyema taasisi nyengine zikashiriki katika kuliondoa tatizo hili  ambalo lipo mijini”,aliongeza Dk. Shein.

 

Sambamba na hayo, Dk. Shein aliitaka Wizara ya Katiba na Sheria kuendelea kuwa karibu na Jumuiya ya Muzdalifah na kutoa shukurani kwa Jumuiya zote za ndani na nje ya Zanzibar zikiwemo I.H.H ya Uturuki, WEFA ya Ujerumani na Al-ANSAR FOUNDATION ya Uiengereza kwa kutoa michango yao mikubwa ya kuiunga mkono Jumuiya ya Muzdalifah ili iweze kufaya kazi zake vizuri.

 

Nae Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Abubakar Khamis, alieleza kuwa Serikali imekuwa ikishirikiana na taasisi mbali mbali katika kuhakikisha watoto yatima wanapata huduma zinazostahiki ili waweze kuishi vizuri.

 

Nae Mbunge Mstaafu wa Bunge la Uturuki Mhe. Husnu Tuna akitoa salamu zake kutoka kwa Jumuiya ya I.H.H alisema kuwa  tatsisi hiyo imekuwa ikitoa misaada ya kibinadamu ambayo lengo lake ni kuondoa matatizo ya watoto mayatima ambapo imekuwa ikiiunga mkono Tanzania kwa mwaka wan ne hivi sasa na inalea mayatima 29,000 katika nchi 41.

 

Aidha, katika risala yao Jumuiya ya Muzdalifah ilieleza kuwa imekuwa ikitoa huduma mbali mbali zikiwemo huduma za kuwasaidia watoto yatima, huduma afya, maskulini, madrasat, zakka, sadaka, maafa, kuchimba visima na huduma nyenginezo.

 

Nao watoto yatima walieleza furaha zao kwa mgeni rasmi kwa kuungana nao katika siku yao hiyo adhimu na kutoa ombi lao la kuitaka siku hii iwe ya Kitaifa

 

Advertisements