Kamati ya kitaifa ya maridhiano Zanzibar

Kamati ya kitaifa ya maridhiano Zanzibar

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, amesema Wazanzibari wanapodai mamlaka kamili na  maslahi ya nchi yao hakuna sababu ya kubezwa na kupuuzwa.

Amesema madai hayo hayana maana Zanzibar haitaki muungano, lakini kuwepo Tanzanyika na Zanzibar zenye mamlaka kamili na muungano wa mkataba, ili kila nchi iendeshe mambo yake kwa uhuru.

Akifungua kongamano la pili la kitaifa la Maridhiano ya Wazanzibari huko hoteli ya Bwanai amesema dhamira ya ukombozi wa Zanzibar kupitia Mapinduzi ni kujitawala yenyewe na kuwa na mamlaka kamili.

Amesema dhamira hiyo ya Mapinduzi ilianza kukiukwa baada ya kutiwa saini kwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambao uliipunguzia Zanzibar mamlaka yake.

Malim Seif amesema Zanzibar inataka kurejesha heshima yake kwa kuwa na sera na wizara yake ya ya mambo ya nje, kujiunga na Umoja wa mataifa na jumuiya nyingine za kimataifa ikiwemo jumuiya ya Madola, Umoja wa Afrika na Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Hata hivyo Malim Seif amewataka vijana kuendelea kutunza amani ya nchi kwa kutojihusisha na vitendo vya vurugu katika kudai mamlaka kamili ya Zanzibar.

Nae Mwenyekiti wa Kamati ya Maridhiano Hassan Nassor Moyo amesema maridhiano yaliyoasisiwa na rais Mstaafu wa Zanzibar dkt. Amani Abeid Karume na Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad, yameondoa fitna na chuki zilizodumu kwa muda mrefu.

Akiwasilisha mapendekezo na mjumbe wa kamati hiyo Ismail Jussa Ladhu kwa niaba ya Mzee Moyo amesema kila nchi katika Muungano inapaswa kuwa na uraia wake na sera yake ya mambo ya nje

Kongamano hilo pia limehudhuriwa na Jumuiya za Kiraia, wawakilishi wa vyama vya siasa na mabalozi.

Advertisements