Kuku wa Peduu kutoka Brazil

Kuku wa Peduu kutoka Brazil

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inatarajia kuongeza kodi ya uingizaji wa kuku kutoka nje ya nchi kwa asilimia 100 ili kulinda soko la wafugaji wa ndani.
Hatua hiyo ya serikali imekuja baada ya wajumbe wa baraza la wawakilishi kuitaka serikali kupiga marufuku kuingizwa kuku wa Peduu kutoka nchini Brazil wanaodaiwa kushusha soko la wafugaji wa ndani.
Waziri wa nchi ofisi ya makamu wa pili wa rais Mohammed Aboud Mohammed amesema kuwekewa kodi kubwa kuku hao kutasaidia kulinda soko hilo kutokana na wanachi wengi  kujiajiri katika sekta hiyo.
Hata hivyo amesema serikali itaandaa mkutano wa kitaifa wa kujadili athari za kupiga marufuku kuku hao kuingizwa nchini baada ya kuonekana soko la ndani halitoshelizi mahitaji na kuathiri sekta ya utalii.
Nae waziri wa mifugo na uvuvi Abdilahi Jihad Hassan amesema serikali inatarajia kujenga soko kubwa litakalofanana na soko la Fery mjini Dar es Salaam katika eneo la Malindi kwa ufadhili wa serikali ya Japan.
Akijibu hoja za wajumbe wa baraza la wawakilishi waliochangia hotuba ya  bajeti ya wizara hiyo amesema ujenzi wa soko hilo  unatarajiwa kuanza Julai mwakani baada ya serikali ya Japan kupitisha mradi huo.
Hata hivyo hotuba ya bajeti ya wizara hiyo imeshindikana kupitishwa kufuatia kuzuka hoja ya kuitaka serikali kupiga marufu uingizaji wa kuku kutoka Brazil, madai yanayopingwa na serikali.

Advertisements