Archive for August, 2013

WANAOISHI UGHAIBUNI WATAKA URAIA WA NCHI MBILI

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed
Shein amesema Serikali haina nia ya kuwanyima wazanzibari wanaoishi
ughaibuni kitambulisho cha mzanzibari mkaazi isipokuwa suala hilo ni la
kisheria hivyo kupewa kwake ni lazima mhusika atimize matakwa ya kisheria.

Kauli hiyo ameitoa hivi karibuni nchini Uholanzi alipokuwa akizungumza na
watanzania wanaoishi nchini humo wakati wa ziara yake ya siku tano kwa
mwaliko wa Waziri Mkuu wa nchi hiyo bwana Mark Rutte.
“Kitambulisho cha mzanzibari ni suala la kisheria hivyo mlengwa ni lazima
atimize matakwa ya kisheria mojawapo ni la mwanachi kukaa katika eneo lake
si chini ya miezi 36” alibainisha Dk. Shein na kuongeza kuwa mzanzibari
mwenye sifa za kupata kitambulisho hicho ikitokea akanyimwa anayo haki ya
kukata rufaa kwa mamlaka husika.
Alieleza kuwa nia ya kuanzisha idara ya Diaspora katika Wizara ya Mambo ya
Nje na kitengo kama hicho katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kunaonesha
sio tu kuwatambua watanzania hao wanaoishi nje ya nchi lakini
kunathibitisha dhamira ya kweli ya serikali ya kuwashirikisha watanzania
popote waliko katika kuleta maendeleo ya nchi.
Dk. Shein aliwapongeza watanzania hao kwa kufuatilia kwa karibu taarifa
kutoka nyumbani na kuonesha kuguswa na baadhi ya matukio yanayotokea
nchini ambayo baadhi yake yanaathiri taswira nzuri ya Tanzania mbele ya
jumuiya ya kimataifa.
“nimefurahi kuona kuwa mnafuatilia kwa karibu matukio yanayotokea nchini
kwetu. Risala yenu imethibitisha maelezo yangu”alieleza Dk. Shein na
kuwaomba watanzania kuwa karibu na Ofisi za Ubalozi za nchi yao ili kupata
taarifa sahihi kuhusu hali ilivyo nchini.
Alisema si kila chombo cha habari au mitandao ya habari inatoa taarifa
sahihi kuhusu Tanzania hivyo suala la kuwasiliana na Ofisi za kibalozi
hawana budi kulizingatia.
Aliwaeleza watanzania hao kuwa ni jambo la kujivunia kuona Serikali
imeufungua tena ubalozi wake nchini Uholanzi baada ya kufugwa kwa miaka
mingi kutokana na sababu za kiuchumi.
“Tuliufunga ubalozi wetu hapa kutokana hali mbaya ya kiuchumi lakini
tumejipanga na tunaufungua upya. Balozi ameshateuliwa na harakati za
kuundaa ubalozi zinaendelea”alieleza Dk. Shein na kumpogeza balozi
Willison Masilingi kwa kuteuliwa kuwa balozi wa Tanzania nchini humo.
Alieleza hatua hiyo ni muhimu katika kuendeleza uhusiano wa Tanzania na
Uholanzi kwa kuwa nchi mbili hizo zimekuwa katika mahusiano mazuri kwa
miaka arobaini sasa.
Akijibu swali kuhusu namna serikali inavyochukua hatua za kusafisha
taswira ya nchi kutokana na matukio ya hivi karibuni ya kumwagiwa
tindikali vijana wawili toka Uingereza huko Zanzibar Dk. Shein alieleza
kuwa hatua zimechukuliwa na bado suala hilo limo mikononi mwa vyombo vya
dola kwa uchunguzi.
“Ni vitendo vilivyoanza muda mrefu tangu mtu wa kwanza kumwagiwa tindikali
mwaka 1996. Hatujui lengo la watu wanaofanya vitendo hivi… ni matukio
yanayotutia aibu, kuharibu sifa ya nchi yetu pamoja na kuhatarisha uchumi
wetu. Hivyo Serikali inalichunguza suala hili (la tindikali) kwa makini
sana” Dk. Shein aliwaeleza watanzania hao.
Alibainisha kuwa matukio kama hayo yanapotokea Serikali huchukua hatua za
haraka ikiwemo kuieleza jumuiya ya kimataifa kwa kutumia njia mbalimbali
za mawasiliano zikiwemo za kidiplomasia na mawasiliano ya wazi kupitia
vyombo vya habari.
Wakati huo huo watanzania wanaoishi nchini Uholanzi wameishukuru Serikali
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuufungua tena Ubalozi wake nchini
Uholanzi.
Shukrani hizo hizo zimetolewa wa Jumuiya ya watanania wanaoishi Uholanzi
katika risala yao kwa Rais wa Zanzibar.
Akisoma risala hiyo Mwenyekiti wa Jumuiya ya watanzania hao Bwana Bulemo
Francis Kweba alisema kufunguliwa kwa ubalozi huo kutawapunguzia gharama
za kufuata huduma za kibalozi mjini Bruxelles Ubelgiji ambako kwa sasa
ndiko zinakopatikana.
Katika risala hiyo watanzania hao waliiomba serikali kuweka utaratibu
mzuri utakaosaidia wao kupata fursa mbalimbali nchini kama vile viwanja
vya kujenga nyumba za kuishi na biashara pamoja na ardhi ya kilimo.
Walishauri serikali kulishughulikia suala la uraia wa nchi mbili kwa
kueleza kuwa lina manufaa makubwa kwa taifa kwani litachochea uwekezaji
nchini kwa kuwa watanzania wengi wamelazimika kuchukua uraia wa nchi
nyingine ili kupata mahitaji ya msingi kama elimu, afya na ajira nzuri.
Katika ziara hiyo Dk. Shein amefuatana na Waziri wa Ardhi, Makazi, Maji na
Nishati wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Ramadhani Abdalla Shaaban,
Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano Rashid Seif Suleiman, Naibu Waziri wa
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mahadhi Juma Maalim na Mshauri wa
Rais Ushirikiano wa Kimataifa, Uwekezaji na Uchumi, Balozi Mohamed Ramia.
Rais wa Zanzibar alimaliza ziara yake nchini Uholanzi jana na anatarajiwa
kurejea nchini kesho (Jumapili)

Advertisements

HERI KWANGU KUFUKUZWA CCM-MANSOUR

Mansour akisalimia na katibu mkuu wa CUF Seif Sharif Hamad

Mansour akisalimia na katibu mkuu wa CUF Seif Sharif Hamad

Aliekuwa mwakilishi wa jimbo la Kiembesamaki kupitia CCM Mansour Yussuf Himid amesema hajutii kuvuliwa uwanachama wa chama hicho kwa kufichua hadharani ukandamizaji dhidi ya maslahi ya Zanzibar.

Akizungumza katika mdahalo wa wazi hoteli ya Bwawani amesema kama suala la mafuta na gesi asili ndio lilisababisha kuvuliwa uwanachama yuko tayari kuacha uongozi wa jimbo hilo akidai hatokwenda mahakamani.

Amedai kufukuzwa kwake kwa kile alichosema suala la mafuta na gesi  asilia kuingizwa kwenye mambo ya muungano ni wizi wa mchana, lakini kauli hiyo ilisaidia kupatikana ufumbuzi wa raslimali hizo.

Himid amesema miongoni mwa mafanikio hayo ni pamoja na baraza la wawakilishi na baraza la mapinduzi kutoa tamko la kutaka kuondolewa raslimali hizo kwenye orodha ya mambo ya muungano….

Aidha Mansour amewataka wananchi kukataa siasa za chuki na ubaguzi ambazo haziwezi kuleta maendeleo ya Zanzibar na usalama wake.

Amesema miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar bado kuna wanasiasa wanaohubiri siasa hizo ni kitendao cha aibu….

Katika mdahalo huo Himid amweapongeza wananchi wa jimbo la Kiembesamaki kwa kukaa nao kwa wema katika kipindi chote alichokuwa madarakani, lakini atafikiria vingine katika uchaguzi mkuu mwaka 2015

ZANZIBAR YAANZA HARAKATI ZA KUCHIMBA MAFUTA NA GESI

BENDEARAHOLANDSerikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Kampuni ya Mafuta ya Shell ya Uholanzi zimetia saini Makubaliano ya Ushirikiano katika kuendeleza sekta ya mafuta na gesi.

Makubaliano hayo yametiwa saini juzi tarehe 28 Agosti, 2013 mjini The Hague ambapo Waziri wa Ardhi, Makazi, Maji na Nishati Ramadhani Abdalla Shaaban alitia saini makubaliano hayo kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Mwakilishi wa Kampuni Shell Tanzania Axel Knospe alitia saini kwa niaba ya  Kampuni hiyo.

Makubaliano hayo yamefikiwa mjini The Hague wakati wa ziara ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed inayoendelea nchini humo.

Kabla ya kusainiwa kwa makubaliano hayo Dk. Shein alifanya mazungumzo na Uongozi wa juu wa kampuni ya Shell  yaliyojielekeza katika kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali ya Zanzibar na Kampuni hiyo.

Kwa mujibu wa makubaliano hayo Kampuni ya Shell itaisaidia Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kujenga uwezo wa kitaalamu, katika hatua za awali za uendelezaji wa sekta hiyo.

Sambamba na hatua hiyo Kampuni ya Shell itasaidia pia shughuli za maendeleo ya vijana katika kuwajengea uwezo kwa kuwapatia elimu na mafunzo mbalimbali yakiwemo ya stadi za ujasiriamali.

Akizungumza mara baada ya kutia saini makubaliano hayo Waziri wa Ardhi, Makazi, Maji na Nishati Ramadhani Abdalla Shaaban alisema “kutiwa saini kwa makubaliano hayo ni hatua moja kubwa na mwelekeo sahihi katika jitihada za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuendeleza sekta ya nishati Zanzibar”

Kwa upande wake Mwakilishi wa Kampuni ya Shell Tanzania Bwana Axel Knospe alieleza kuwa wakati mashauriano yakiendelea kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na ile ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania juu ya kuliondoa suala la mafuta na gesi katika mambo ya muungano, Kampuni hiyo itaendelea na dhamira yake ya ushirikiano na Zanzibar hadi hapo muda utakapokuwa tayari kuanza kazi ya shughuli za uchimbaji mafuta na gesi ambapo itaifanya kazi hiyo kwa kuzingatia uwajibikaji kiuchumi, kijamii, kimazingira na  kuifanya sekta hiyo kuwa endelevu

“wakati Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zikishughulikia kwa pamoja suala la kisheria na kisera kuipatia Zanzibar haki pekee ya kuendeleza sekta ya mafuta na gesi Zanzibar, Kampuni ya Shell itaendelea na dhamira yake ya kushirikiana na Zanzibar hadi hapo muda muafaka utakapofika kuanza shughuli za uchimbaji wa mafuta na gesi” alieleza bwana Axel Knospe.

Wakati akizungumza na Rais wa Zanzibar mjini hapa juzi Waziri wa Biashara ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Uholanzi Bibi Lilianne Ploumen alimueleza Rais kuwa Serikali ya nchi hiyo iko tayari kutumia utaalamu na uzoefu wake katika sekta ya mafuta na gesi kuisaidia Zanzibar kuendeleza sekta hiyo.

Bibi Ploumen alieleza kuwa Serikali ya nchi hiyo iko tayari kutoa fursa za mafunzo kwa watumishi wa Serikali ya Zanzibar katika sekta ya nishati ili kuhakikisha kuwa wanakuwa na uzoefu katika kusimamia rasilimali hizo, utunzaji wa mazingira na ushiriki wa wananchi katika matumizi ya rasilimali hiyo kuepusha migogoro.

“Mambo ya msingi ya kupewa kipaumbele ni pamoja na namna ya uendeshaji, usimamizi na matumizi bora ya rasilimali hizo, ushirikishwaji wananchi na utunzaji mazingira”alieleza bibi Ploumen na kusisitiza haja ya Zanzibar kujifunza kutoka nchi nyingine kuepuka makosa yaliyofanywa na baadhi ya nchi ikiwemo Uholanzi yenyewe.

Dr. Shein anamaliza  ziara yake ya siku tano nchini Uholanzi leo  na anatajiwa kurejea nyumbani Jumapili ijayo.

Katika ziara hiyo Dk Shein amefuatana na Waziri wa Ardhi, Makazi, Maji na Nishati wa

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Ramadhani Abdalla Shaaban, Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano Rashid Seif Suleiman, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mahadhi Juma Maalim na Mshauri wa Rais Ushirikiano wa Kimataifa, Uwekezaji na Uchumi, Balozi Mohamed Ramia.

 

CCM YAITOLEA NJE KAMATI YA MARIDHIANO Z’BAR

JABU

Katib wa kamati maalum ya NEC itikadi na uenezi Waride Bakar Jabu

MOYO

Mwenyekiti wa kamati ya Maridhiano Zanzibar Hassan Nassor Moyo

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinapenda kuuelezea  na kuwajulisha wananchi na Jumuiya ya Kimataifa kuwa hakiitambui  na hakina mnasaba na Kamati ya Maridhiano inayodai kuwa ina uwakilishi wa wajumbe toka vyama vya CCM na CUF  hapa  Zanzibar.

Katibu  wa Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Zanzibar Idara ya Itikadi na Uenezi Waride Bakari Jabu (MB) amesema CCM ina utaratibu na kanuni zake za kuunda kamati na si  kuundiwa au kusemewa na kundi lolote.

Inapotokea haja ya kuunda kamati kama yeyote , wajumbe wake hutokana na maazimio ya vikao halali vya kikatiba na si kukurupuka kama ifanyavyo Kamati inayojiita ya Maridhiano chini ya Mwenyekiti wake Hassan Nassor Moyo.

Chama Cha Mapinduzi kinaitambua Kamati ya Moyo kuwa ni Kamati ya mvurugano yenye malengo na madhumuni binafsi kwa tamaa na kukamilisha haja  na matakwa yao.

Kamati ya Maridhiano ya inayoongozwa na Moyo haitambuliwi na Kamati Malum ya NEC Zanzibar , Kamati Kuu ya CCM na wala Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM  (NEC).

Kitendo chochote cha Kamati hiyo kulihusisha jina la Chama Cha Mapinduzi kihesabiwe na wananchi kuwa ni utapitapi, chokochoko na ukorofi wa kisiasa.

Ni vyema toka sasa wajumbe wanaojiita ni wawakilishi wa CCM katika kamati hiyo wakaeleza wamepata wapi ruhusa au wametumwa na kiongozi gani wa juu wa CCM ili kushiriki kwenye kamati hiyo.

CCM haijamtuma mjumbe yeyote kushiriki kwenye kamati hiyo na kwamba wajumbe hao wamejipeleka wenyewe ili kuwapotosha na kuwaisha wananchi kwa manufaa yao.

Mwisho CCM inawajuulisha Wazanzibari na Watanzania kwa jumla kuwa haihusiki kabisa na Kamati ya maridhiano inayovishirikisha vyama vya  CCM na CUF hapa Zanzibar.

 

 

“KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI”

Waride Bakari Jabu (MB)

Katibu wa Kamati Maalum ya NEC,

Chama Cha Mapinduzi,

ZANZIBAR.

30/08/2013.

MMOJA AFARIKI DUNIA NA 19 WAJERUHIWA PEMBA

PEMBAMTU mmoja amefariki dunia na wengine 19 wamejeruhiwa baada ya gari yaliyokuwa wakisafiria kupinduka  katika eneo la Kichanjaani Ndagoni Mkoa wa kusini Pemba.

Akizungumza na zenji fm radio juu ya tukio hilo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Pemba Saleh Mohamed Saleh alimtaja marehemu huyo kuwa ni Ibrahim Mbarouk Seif  miaka 18, mkaazi wa Kichanjaani Ndagoni .

Ajali hiyo ilitokea majira ya saa 12 asubuhi, wakati gari hiyo ya abiria ikitokea Wesha kwenda mjini Chake Chake ilipokuwa ikipanda mlima eneo la Kichanjaani na kuanguka upande wapili.

Aidha aliitaja gari hiyo iliyopata ajali kuwa ni Z.124 BT yenye ruti Namba 305 Wesha-Chake iliyokuwa ikiendeshwa na Salim Kassim Usi miaka 30 na utingo  Juma Khamis Kombo miaka 20 wakaazi wa Buyuni Wesha.

Kwa upande wake daktari dhamana wa hospitali ya chake chake, Yussuf Hamad amesema kifo cha Marehemeu katika ajali hiyo kilisababishwa na kuvunjika kwa mbavu tatu za mkono wa kulia hali iliyopelekea mapafu yake kutokufanya kazi na kuumia sehemu ya kichwa

MWANAJESHI WA TANZANIA AUWAWA DRC

DRCMwanajeshi  mmoja wa  Tanzania  ameuwawa  baada  ya  Helikopta  za  kikosi  cha  jeshi  la  Umoja  wa  Mataifa ya kuingilia  kati  na  makombora  kushambulia  maeneo  ya  waasi  wa  M23  katika  Jamhuri  ya kidemokrasi  ya  Congo  jana.

Kwa mujibu wa taarifa ya jeshi la wananchi wa Tanzania iliyotumwa kwa vyombo vya habari imemtaja Marehemu huyo kuwa ni Meja Khatibu Mshindo aliyepatwa na mauti wakati akipelekwa hospitali baada ya kupata majaraha yaliyosababishwa na kuangukiwa na bomu.

Majeruhi wengine wanaendelea na matibabu, na hali zao zinaendelea vizuri.

Kwa mujibu wa taarifa ya JWTZ iliyotolea na Kurugenzi ya Habari na Uhusiano Makao Makuu ya Jeshi imesema MONUSCO inaandaa utaratibu wa kuleta mwili wa Marehemu kwa ajili ya mazishi hapa nchini.

Mjumbe  maalumu wa  Umoja  wa  Mataifa  nchini  Congo, Martin Kobler, ambaye  anaongoza  ujumbe  huo  wa  kulinda  amani, amesema  amekasirishwa  na kuuwawa  kwa mwanajeshi huyo  kutoka  Tanzania  na  kwamba  amejitolea  maisha yake  kwa  kuwalinda  raia  mjini  Goma.

Wakati  huo  huo, Rwanda  imezuwia pendekezo lililotolewa  na  Marekani  na  Ufaransa  kuweka  vikwazo dhidi  ya  makamanda  wawili waandamizi katika  kundi  la waasi  la  M23, ikidai  kuwa ushahidi  dhidi  ya  watu  hao ni dhaifu

MWAKILISHI JIMBO LA KIEMBE SAMAKI MANSOUR YUSSUF HIMID AFUKUZWA CCM

Mansour Yussuf Himid akiapishwa na rais wa Zanzibar Dr. Ali Mohammed Shein kuwa waziri asiekuwa na wizara maalum Zanzibar mwaka 2010

Mansour Yussuf Himid akiapishwa na rais wa Zanzibar Dr. Ali Mohammed Shein kuwa waziri asiekuwa na wizara maalum Zanzibar mwaka 2010

Mwakilishi wa jimbo la Kiembesamaki kupitia CCM Mansour Yussuf Himid amefukuzwa uanachama wa chama hicho akidaiwa kuisaliti chama hicho kwa kuunga mkono muungano wa mkataba.

Taarifa kutoka mjini Dodoma zinasema kikao cha halmashauri kuu CCM taifa kilichokutana kwa siku ya tatu leo chini ya mwenyekiti wake rais Jakaya Kikwete kilitoa uamuzi wa kufukuzwa kwa mwanachama huyo.

Kufuatia hatua hiyo chama cha Mapinduzi kitatoa taarifa kwa spika wa baraza la wawakilishi kuondoa udhmini wake kwa mwanachama huyo kama mjumbe wa baraza la wawakilishi jimbo Kiembesamaki.

Hatua hiyo itamfanya spika wa baraza hilo kutangaza kiti cha jimbo hilo kuwa wazi na kuitishwa uchaguzi mdogo wa kugombea nafasi hiyo.

Mjumbe wa kamati kuu ya halmashauri kuu ya CCM taifa Daud Ismail akizungumza na Zenji fm radio amesema kikao hicho kimefikia uwamuzi huo baada ya kupokea madai ya mkoa wa magharib kutaka mwanachama huyo afukuzwe kwa madai ya kupinga sera sera ya serikali mbili ya muungano inayoungwa  mkono na chama

Hata hivyo Himid ambae pia ni mjume wakamati ya maridhiano Zanzibar endapo hajaridhishwa na uamuzi wa kufukuzwa kwake anaweza kukata rufaa mahakama kuu kupinga uwamuzi huo.

Himid aliwahi kuwa waziri asiekuwa na wizara ya maalum katika awamu ya saba inayongozwa na Dr. Ali Mohammed Shein pia aliwahi kuwa naibu waziri wa wizara ya kilimo kabla ya kuwa waziri wa maji ujenzi, nishati na ardhi katika utawala wa rais Amani Abeid Karume.

Himid alionekana kichecheo kutaka kuliondoa suala na mafuta na gesi asilia kwenye orodha ya mambo ya muungano pamoja na kuchukizwa na matatizo ya muungano yanayoikandamiza Zanzibar.

Hivi karibuni mwenyekiti wa kamati ya maridhiano Mzee Hassan Moyo amesema kufukuzwa kwa Himid hakutathiri shughuli za kamati hiyo kutetea muungano wa mkataba.