Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Balozi wa Jamuhuri ya Watu wa Kenya Nchini Tanzania Balozi Mutinda Mutiso hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Balozi wa Jamuhuri ya Watu wa Kenya Nchini Tanzania Balozi Mutinda Mutiso hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetoa pole kwa Wananchi wa Jamuhuri ya Watu wa Kenya kutokana na maafa ya moto mkubwa uliokikumba Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Jomo Kenyata Kiliopo Mjini Nairobi Nchini humo na kusababisha hasara kubwa ambayo bado haijajuilikana.

Moto huo umesabisha safari zote za ndege zilizopangwa kuingia na kutoka kwenye uwanja huo kusitishwa na kupelekea ndege hizo kutua katika viwanja vyengine vya ndege vya Eldoret, Mombasa na Nchi jirani za Afrika Mashariki.
Pole hiyo imetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati alipofanya mazungumao na Balozi wa Kenya Nchini Tanzania Balozi Mutinda Mutiso aliyefika kumuaga hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar baada ya kumaliza muda wa utumishi wake wa miaka minne hapa Nchini.
Balozi Seif alisema Wananchi wa kenya wamekumbwa na maafa hayo yaliyosababisha kutishia kutetereka kwa uchumi wake unaotegemea kwa kiasi kikubwa huduma zinazotolewa na Uwanja huo katika ukanda mzima wa Bara la Afrika ukiunganisha ndegembali mbali  za Kimataifa.
Alisema gharama za kuufanyia matengenezo uwanja huo ni kubwa kufuatia moto huo uliotokea mapema  alfajiri ya Jumatano katika eneo la kuwasili abiria kabla ya kusambaa hadi maeneo mengine likiwemo lile la Idara ya Uhamiaji.
Alifahamisha kwamba umefika wakati kwa Waafrika kuwa makini na vitendo vya kuwatia hofu wananchi { Ugaidi } ambavyo vinaweza kusababisha ukosefu wa utulivu na amani miongoni mwa Jamii.
Alimueleza Balozi Huyo wa Jamuhuri ya Watu wa Kenya Nchini Tanzania kwamba Vitendo vya Kigaidi vinavyoonekana kujitokeza katika Nchi mbali mbali Duniani vikilikumba pia Bara la Afrika humfanya Mtu aishi katika maisha ya hofu na wasi wasi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimpongeza Balozi huyo wa Kenya Nchini Tanzania kwa juhudi zake za utumishi zilizochangia kuimarika  zaidi kwa uhusiano wa kudugu uliopo kati ya Kenya na Tanzania na Zanzibar kwa ujumla.
Balozi Seif alisema Wananchi wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania hasa wale wanaoishi katika ukanda wa Pwani ya Mwambao wa Afrika Mashariki wamekuwa na uhusiano wa karibu na kidugu na wenzao wa Taifa la Kenya.
Alishauri uhusiano huo ukazidi kuimarishwa kwa faida ya wananachi wa pande hizo mbili hasa kwa kuzingatia zaidi muingiliano uliopo kupitia Jumuia ya Afrika Mashariki iliyounganisha harakati za kiuchumi za mataifa wanachama.
Mapema Balozi wa Jamuhuri ya Watu wa Kenya Nchini Tanzania Balozi Mutinda Mutiso alisema upo umuhimu wa wana Jumuiya ya Afrika Mashariki kuendelea kuikuza na kuithamini Lugha ya Kiswahili kwa lengo la kuipa heshima yake Kimataifa.
Balozi Mutiso alisema inasikitisha kuona wenye Lugha ya Kiswahili wanaendelea kusua sua wakati lugha yenyewe kimataifa inazungumzwa takriban na watu zaidi ya Milioni mia mbili na arubaini duniani kote ikiwa lugha ya nne kwa ukubwa duniani hivi sasa.
“ Takwimu za watu wanaozungumza Kiswahili Duniani ndizo zilizonishawishi mimi kufikia uwamuzi wa kutunga Kamusi la Kingereza kwa Kiswahili kupitia mfumo wa Kidiplomasia ili kutoa mchango wangu katika kukuza lugha yetu ya Afrika Mashariki. Mchango wangu huu pia nimekusudia uwasaidie wanadiplomasia wenzangu “. Alifafanua Balozi Mutinda.
Akizungumzia mchakato wa Katiba Mpya ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ambao hivi sasa unapita katika hatua ya Rasimu ya Katiba hiyo Balozi Mutinda Mutiso ameipongeza Tanzania kwa hatua yake hiyo yenye muelekeo wa kutandika Demokrasia zaidi.
Balozi Mutinda alisema Waafrika walio wengi wanatarajia kukiona kipindi cha mpito  cha kuelekea kwenye Katiba Mpya Nchini Tanzania kinakuwa kigezo na mfano bora wa kuigwa na kuungwa mkono na Mataifa mbali mbali ya Bara la Afrika.
Aliipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliyoamua kufuata mfumo wa Umoja wa Kitaifa ambao umeleta utulivu, amani na umoja miongoni mwa Wazanzibari walio wengi baada ya mgongano wa mrefu wa kisiasa uliovikumba vyama vikuu viwili vya kisiasa.
Balozi Mutinda alisema inapendeza kuona Zanzibar hivi sasa imetulia kisiasa kwa kuwa na mfumo huo wa Serikali ya pamoja unaofaa kupongezwa na kuigwa na Mataifa mengine yanayotaka kuelekea kwenye demokrasia zaidi ndani na nje ya Bara la Afrika.
 
Advertisements