JABU

Katib wa kamati maalum ya NEC itikadi na uenezi Waride Bakar Jabu

MOYO

Mwenyekiti wa kamati ya Maridhiano Zanzibar Hassan Nassor Moyo

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinapenda kuuelezea  na kuwajulisha wananchi na Jumuiya ya Kimataifa kuwa hakiitambui  na hakina mnasaba na Kamati ya Maridhiano inayodai kuwa ina uwakilishi wa wajumbe toka vyama vya CCM na CUF  hapa  Zanzibar.

Katibu  wa Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Zanzibar Idara ya Itikadi na Uenezi Waride Bakari Jabu (MB) amesema CCM ina utaratibu na kanuni zake za kuunda kamati na si  kuundiwa au kusemewa na kundi lolote.

Inapotokea haja ya kuunda kamati kama yeyote , wajumbe wake hutokana na maazimio ya vikao halali vya kikatiba na si kukurupuka kama ifanyavyo Kamati inayojiita ya Maridhiano chini ya Mwenyekiti wake Hassan Nassor Moyo.

Chama Cha Mapinduzi kinaitambua Kamati ya Moyo kuwa ni Kamati ya mvurugano yenye malengo na madhumuni binafsi kwa tamaa na kukamilisha haja  na matakwa yao.

Kamati ya Maridhiano ya inayoongozwa na Moyo haitambuliwi na Kamati Malum ya NEC Zanzibar , Kamati Kuu ya CCM na wala Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM  (NEC).

Kitendo chochote cha Kamati hiyo kulihusisha jina la Chama Cha Mapinduzi kihesabiwe na wananchi kuwa ni utapitapi, chokochoko na ukorofi wa kisiasa.

Ni vyema toka sasa wajumbe wanaojiita ni wawakilishi wa CCM katika kamati hiyo wakaeleza wamepata wapi ruhusa au wametumwa na kiongozi gani wa juu wa CCM ili kushiriki kwenye kamati hiyo.

CCM haijamtuma mjumbe yeyote kushiriki kwenye kamati hiyo na kwamba wajumbe hao wamejipeleka wenyewe ili kuwapotosha na kuwaisha wananchi kwa manufaa yao.

Mwisho CCM inawajuulisha Wazanzibari na Watanzania kwa jumla kuwa haihusiki kabisa na Kamati ya maridhiano inayovishirikisha vyama vya  CCM na CUF hapa Zanzibar.

 

 

“KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI”

Waride Bakari Jabu (MB)

Katibu wa Kamati Maalum ya NEC,

Chama Cha Mapinduzi,

ZANZIBAR.

30/08/2013.

Advertisements