Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar balozi Seif Ali Iddi akiuongoza Ujumbe wa Zanzibar wakati wa mazungumzo yake na Uongozi wa Shirika la Kimataifa la Ushafirishaji kwa njia ya anga la Transworld kwenye makao makuu ya Shirika hilo Jabel Ali Industrial Estate economy Free Zone { UAE }.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar balozi Seif Ali Iddi akiuongoza Ujumbe wa Zanzibar wakati wa mazungumzo yake na Uongozi wa Shirika la Kimataifa la Ushafirishaji kwa njia ya anga la Transworld kwenye makao makuu ya Shirika hilo Jabel Ali Industrial Estate economy Free Zone { UAE }.

Wakati  Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ikiendelea na juhudi zake za  kuimarisha Miundo mbinu katika Sekta mbali mbali za Kiuchumi na Ustawi wa Jamii baadhi ya Kampuni, Mashirika na hata wawekezaji binafsi wa ndani na nje ya nchi wanaonekana kuzidi  kushawishika na kasi ya kutaka kuwekeza Zanzibar.

Shirika la Kimataifa linaloshughulikia masuala ya usafirishaji wa anga la Transworld lenye makamo makuu yake Dubai limefikia uamuzi wa kutaka kuwekeza kwenye Sekta ya mawasiliano ya anga kwa kujenga Kituo kikubwa cha uuzaji wa  vifaa vya  ndege zinazopata hitilafu ya kiufundi ndani ya ukanda wa jangwa la Sahara Barani Afrika.
Mwenyekiti wa Shirika hilo Bwana Abdullah Al – Sulaimani alitoa kauli hiyo wakati Uongozi wa Shirika lake ulipofanya mazungumzo na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi  Seif Ali Iddi anayemaliza ziara yake Dubai katika Muungano wa Mataifa ya Falme za Kiarabu { UAE }.
Bwana Abdullah alimueleza Balozi Seif na Ujumbe wake kwamba Kituo hicho kitakachokuwa na hadhi ya  Kimataifa kinatarajiwa kutoa huduma kwa ndege za aina ya boeing, Airbus, ATR pamoja na ndege zote zinazotumia  viwanja vya ndege vilivyomo ndani ya Bara la Afrika.
Alieleza kwamba awamu ya kwanza na huduma zitazotolewa  na kituo hicho zitalenga katika uuzwaji wa vifaa mbali mbali vya ndege ambapo awamu ya pili itajikita zaidi katika kutoa fursa kwa ndege zenye kupata hitilafu kupatiwa huduma za kiufundi kwenye kituo hicho.
Mwenyekiti huyo wa Trasworld alifahamisha kwamba Mpango huo utakwenda sambamba na utolewaji wa mafunzo kwa wananchi wazawa watakaopata nafasi ya kufanya kazi kwenye Kituo hicho.
“ Kwa vile sisi ni wazawa wa Visiwa vya Zanzibar hamu yetu ni kuona Elimu na fursa tulizonazo huku tuliko pia tunazitumia kwa kuneemesha na nyumbani. Ahadi yetu ya kutaka kuwekeza vitega uchumi nyumbani iko pale pale “. Alifafanua Bwana Abdullah Al – Sulaimani.
Mwenyekiti huyo wa Transworld  alieleza kuwa Taasisi yake pia iko tayari kutoa huduma bora na za kitaalamu kwa kutumia vifaa vya kisasa katika upakuzi na upakizi wa mizigo kwenye uwanja wa ndege wa Zanzibar endapo watapatiwa fursa hiyo na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Alisema kutokana na mabadiliko ya dunia yaliyopo hivi sasa ya sayansi na Teknolojia tabia ya kuendelea kuchukuwa mizigo kwa kutumia mikono kwenye viwanja vya ndege imepitwa na wakati.
“ Mambo ya kuchukuwa mizigo kwa mikono haitakuwepo tena. Tunachotaka kuona Uwanja wa Ndege wa Zanzibar unatoa huduma za usafiri wa anga katika kiwango kinachokubalika  Kimataifa kabisa “. Alieleza Bwana Abdullah.
Akizungumzia miradi mengine ya uwekezaji Mwenyekiti huyo wa Shirika la Kimataifa linaloshughulikia masuala ya usafirishaji wa anga la Transworld alisema leseni kwa ajili ya ufunguzi wa Benki ya Shirika hilo Zanzibar uko katika hatua za mwisho.
Alisema Benki hiyo itakuwa na uwezo wa kutoa huduma zaidi kwa Wananchi na hata wale wawekezaji wanaoamuwa kutaka kuweka miradi yao ya kiuchumi na maendeleo Nchini Tanzania.
“ Malengo yetu ni kuhakikisha huduma zinazotolewa na benki hiyo hazilalamikiwi na wateja kiasi ambacho mfumo wetu utaifanya iwe na hadhi ya pili katika kutoka huduma ikitanguliwa na Benki ya Watu wa Zanzibar Limited {PBZ } “. Alifahamisha Bwana Abdullah.
Aidha Mwenyekiti huyo wa Transworld alifafanua kwamba Taasisi yake iko katika hatua za mwisho za kukamilisha taratibu zilizopo ili ijenge Hoteli kubwa nay a kisasa Zanzibar itakayotowa huduma na kusaidia sekta ya Utalii Nchini.
Naye Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif ameuahidi Uongozi wa Shirika hilo la Transworld kwamba Serikali ya Mapindujzi ya Zanzibar  itahakikisha kwamba inatoa ushirikiano wa karibu kwa shirika hilo ili kuona malengo yaliyokusidiwa kwa pande hizo mbili yanatekelezwa kwa wakati.
Balozi Seif alifahamisha kwamba masuala yote yatakayohitajika kutekelezwa kisheria likiwemo suala la ardhi yanakamilishwa na Serikali kupitia taasisi zake katika kipindi kifupi kijacho.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliviagiza vyombo na taasisi zinazohusika na masuala hayo kuharakisha taratibu zinazohitajika ili kutoa fursa kwa wawekezaji hao kuanza matayarisho kwa ajili ya miradi waliyoikusudia kuwekeza Zanzibar.
“ Nakuahidini kwamba yale masuala yote tuliyokubaliana na yanahitaji kufanyia kazi kisheria likiwemo suala la ardhi wahusika nawaagiza kuyafanyia kazi na utekelezaji wake ukamilike ndani ya wiki moja “. Alifafanua Balozi Seif.
Mazungumzo hayo pia yalijumuisha Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mohamed Aboud Mohamed, Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko Mh. Nassor Ahmed Mazrui pamoja na  Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mh. Othman Masoud Othman.
Wengine ni Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Nd. Khamis Mussa, Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, makazi, Maji, Nishati na Madini Nd. Ali Khalil Mirza, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Nd. Abdulla Mzee Abdulla na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uwekezaji Vitega Uchumi Zanzibar { ZIPA } {Salum Khamis.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi na ujumbe wake anatarajiwa kurejea nyumbani Zanzibar kesho Jumanne Tarere 19 Novemba 2013 mnamo majira ya saa 10.00 za jioni baada ya kumaliza ziara yake Nchini Marekani na Dubai.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
18/11/2013.