CCMMAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Zanzibar Mh: dk Ali Mohamed Shein amesema CCM, haijaungana na wala haina nia ya kuunga na chama cha wananchi CUF kisiasa kama baadhi ya watu wanavyodhani.

 

Alisema kilichofanyika ni kuwepo kwa Serikali ya umoja wa kitaifa ‘SUK’ katika utendaji wa kazi ngazi ya serikalini, na sio kuungana na chama hicho kisiasa.

 

Makamu Mwenyekiti huyo alitoa tamko hilo jana, wakati alipokua akizungumza na wanaccm, wapenda amani na wananchi wa Jimbo la Tumbe wilaya ya Micheweni Pemba, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku sita kisiwani humo.

 

Alisema sio kweli kuwa CCM hivi karibuni, kimeungana na Chama cha wananchi CUF kisiasa, bali kilichojitokeza na kushirikiana katika kuanzisha serikali ya umoja wa kitaifa, ambapo hilo liliendana na marekebisho ya katiba ya Zanzibar.

 

Alieleza kuwa katika uwepo wa Serikali hiyo ya Umoja wa kitaifa bado sera na mipango inayotekelezwa ya chama cha Mapinduzi ambacho ndio chama tawala kwa muda mrefu sasa.

 

Aliongeza kuwa katika hilo, CCM kinawanachama wake, sera zake na mipango yake ya kila siku, kama kilivyo chama hicho cha CUF na kubainisha kuwa hakuna pahala waliposaini kuungana kisiasa.

 

‘’Tanzania vipo vyama vya siasa 19 na vinaweza kuzidi, lakini CCM hakuna hata chama kimoja nchini kilichounga na mwalimu wa demokrasia CCM, bali sisi tupo kimpango wetu’’,alifafanua.

 

Katika hatua nyengine Makamu Mwenyekiti huyo wa CCM Zanzibar, alisema pia kuanzishwa kwa mfumo huo wa vyama vingi nchini, haukuja kwa ajili ya kufanyiana vitishio, kudharauliana wala kubaguana kama baadhi ya wengine wanavyofanya.

 

Alieleza kuwa katika siku za hivi karibuni, kumeibuka viongozi wengine kutoka serikalini, wamekuwa wakiwafanyia vitisho masheha, kwa kuwalazimisha kimaneneo kutoa barua za kupata kitambulisho vya uzanzibari ukaazi.

 

Alifafanua kua wanachokifanya masheha ni kufuata sheria, baada ya kuelekezwa na taaisis husika, hivyo sio busara kwa viongozi hao kuwaona masheha kama wanakiuka sheria.

 

‘’Suala hili la vitambulisho vya uzanzibari ukaazi, tafadhalini msilihusishe na na vyama vya siasa, hili ni la serikali na linatambulika kikatiba na sio la upande mmoja’’,alisema.

 

Aidha Makamu Mwenyekiti huyo wa CCM Zanzibar ambae pia ni rais wa Zanzibar dk Ali Mohamed Shein, amewataka wananchi kuendelea kuyathamini na kuyaenzi mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964.

 

Alisema mapinduzi hyo, ndio yaliomkumboa mwanachi wa taifa hili na leo hii, kua ameweza kujitea maendeleo yake mwenyewe na kupata furasa kadhaa zikiwemo za kiuchumi.

 

Alitolea mfano kwa serikali hii ya awamu ya saba inayoongozwa na yeye, kuwa imeamua kulipandisha hadhi zao la karafuu ambalo kwa muda mrefu wakulima walikuwa wamelisahau na kutoona faida yeyote.

 

Hata hivyo amewataka wanaccm hao na wananchi wa Jimbo la Tumbe, wilaya ya Micheweni  kuendelea kuwapuuza wale wanaobeza na kudharau Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

 

Alifafanua zipo fursa kadhaa zilizopatika kwa Zanzibar kupitia Muungano huo, ikiwa ni pamoja na kujenga umoja na udugu kwa muda mrefu.

 

Mapema Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa kaskazini Pemba Mberwa Hamad Mberwa, amempongeza makamu mwenyekiti huyo wa CCM Zanzibar, kutokana na kuendelea na utekelezaji wa ahadi zake.

 

Alisema katika Jimbo hilo la Tumbe wananchi kadhaa wamekuwa wakifikiwa na huduma muhimu za kijamii ikiwa ni pamoja na huduma ya maji safi na salama, umeme, elimu ingawa baadhi ya huduma hizo zinahitilafu ndogo ndogo.

Advertisements