Balozi wa Vietnam Nchini Tanzania Bwana Nguyen Thanh Nam akisalimiana na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi pamoja na kumpa Taarifa ya ujio wa wataalamu wa Kilimo na Uvuvi wa Vietnam Zanzibar Mwezi Januri mwaka 2014.

Balozi wa Vietnam Nchini Tanzania Bwana Nguyen Thanh Nam akisalimiana na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi pamoja na kumpa Taarifa ya ujio wa wataalamu wa Kilimo na Uvuvi wa Vietnam Zanzibar Mwezi Januri mwaka 2014.

Timu ya Wataalamu mabingwa katika Sekta ya Kilimo na Uvuvi kutoka Nchini Vietnam inatarajiwa kutembelea Visiwa vya Zanzibar kuanzia Tarehe 4 Mwezi Januari mwaka 2013 kuangalia maeneo ambayo Nchi hiyo inaweza kusaidia Taaluma ili kunyanyua uchumi wa Zanzibar.

Ujio wa Timu hiyo ya wataalamu wa Vietnam unafuatia ziara ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohammed Sheni aliyoifanya Nchini humo miezi michache iliyopita.

Balozi wa Vietnam Nchini Tanzania Bwana Nguyen Thanh Nam Alitoa taarifa hiyo wakati alipofika nyumbani kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Mtaa wa Haile Selassie Jijini Dar es salaam.

Balozi Nguyen alisema ziara ya Rais wa Zanzibar imefungua ukurasa mpya wa uhusiano na ushirikiano wa muda mrefu ulipo kati ya Vietnam na Tanzania na Zanzibar kwa ujumla.

Alisema Zanzibar na Vietnam zina wajibu wa kuendelea kushirikiana kwa vile zinafanana katika harakati zao za maendeleo hasa kwenye sekta ya Kilimo na akatolea mfano kile kilimo cha mpunga.

Naye makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameipongeza Nchi hiyo kwa uwamuzi wake wa kukubali kuisaidia Zanzibar kitaaluma katika sekta muhimu za Kilimo na Uvuvi ambazo ndio zenye kubeba idadi kubwa ya wananchi katika kujiendeleza kimaisha.

Balozi Seif alisema Vietnam imekuwa Nchi maarufu Duniani katika uzalishaji wa zao la mpunga ambalo pia wataalamu wake wanaweza kusaidia wakulima wa Zanzibar kuendeleza zao hilo kwa vile ndio chakula kikuu cha wakaazi wa Visiwa vya Zanzibar.

Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alikutana kwa mazungumzo na Balozi wa Jamuhuri ya Watu wa China aliyepo Nchini Tanzania Bw. Lu Youqing nyumbani kwake Mtaa wa Haile Selassie Jijini Dar es salaam.

Katika mazungumzo yao Viongozi hao wawili wamekubaliana kuendeleza uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliopo kati ya pande hizo mbili rafiki mara tu baada ya  Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alisisitiza kuwa uhusiano huo umezidi kupanuka kufuatia pande hizo mbili kusaini mkataba wa ushirikiano katika masuala ya Utamaduni na Michezo.

Balozi Seif alisema mkataba huo hivi sasa umetoa fursa kwa vijana wa pande hizo mbili kuendelea kujifunza tamaduni za kila upande ambazo zimeshaonyesha mafanikio makubwa ya uhusiano huo wa kidugu.

“ Wapo vijana wetu waliopata fursa ya kujifunza tamaduni za ndugu zetu wa China hasa katika mambo ya sarakasi. Lakini kwa upande wao wamepata kujifunza ngoma zetu za utamaduni “. Alisisitiza Balozi Seif.

Naye Balozi wa Jamuhuri ya Watu wa China Nchini Tanzania Bwana Lu Youqing alifahamisha kwamba katika kudumisha uhusiano wa pande hizo mbili Serikali ya Nchi hiyo inakusudia kutuma ujumbe mzito wa Kiserikali kushiriki katika maadhimisho ya Sherehe za miaka 50 sawa na Nusu Karne ya Mapinduzi ya Zanzibar mwezi Januri mwaka ujao.

Bwana Lu alisema Wananchi wa Zanzibar wana haki ya kujivunia  Mapinduzi hayo matukufu yaliyoondoa madhila na uonevu na yamekuwa kigezo kizuri kilichopatikana  katika kudumisha maendeleo miongoni mwa Wananchi wa Visiwa vya Unguja na Pemba.

Aidha Balozi Lu Youqing alieleza kwamba ujumbe wa Viongozi 80 wa Serikali ya Jamuhuri ya Watu wa China ujatarajiwa kuja Nchini Tanzania hivi karibuni kushiriki kongamano la Kimataifa litakalojumuisha Wakuu wa Mikoa wa Tanzania.

Kongamano hilo kubwa limelenga kuwajengea uwezo wa kiutendaji Wakuu hao wa Mikoa ya Tanzania katika masuala mbali mbali ya utawala, Utumishi pamoja na uwajibikaji kwa wananchi.

 

Othman Khamis Ame

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

Advertisements