Waziri wa fedha Tanzania Saada Mkuya

Waziri wa fedha Tanzania Saada Mkuya

MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, amelishushia tuhuma nzito Baraza la Mawaziri, baada ya kudai baadhi ya mawaziri walioteuliwa hawana elimu ya kutosha
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Profesa Lipumba alisema mmoja wa mawaziri hao ni Waziri wa Fedha, Saada Mkuya.

Alisema chama chake, kina wasiwasi na elimu ya Waziri Mkuya, kutokana na wasifu wake kutoonyesha vyuo alivyosoma wakati wa kupata shahada ya kwanza na ya pili katika masuala ya biashara.


Alisema katika tovuti ya Bunge, wasifu wa waziri huyo umeonyesha sehemu aliyosoma elimu ya sekondari na kuhitimu kidato cha sita.


Alisema katika tovuti hiyo, haionyeshi chuo alichosoma shahada ya kwanza ya biashara, ingawa inaonyesha masomo aliyochukua jambo ambalo linatia mashaka uhalali wake kuongoza wizara hiyo nyeti.


“Ukiingia kwenye tovuti ya Bunge, utaona wasifu wake kuanzia elimu ya msingi hadi kidato cha sita na shule alizosoma, lakini kuanzia elimu ya shahada imeonyesha masomo aliyochukua na kupata shahada ya kwanza ya biashara, haionyeshi vyuo, jambo ambalo linatia mashaka,” alisema Lipumba.

Alisema nafasi aliyopewa inahitaji kiongozi mwenye upeo wa hali ya juu, kuweza kupambanua mambo yanayohusu uchumi wa nchi kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali za kifedha za ndani na nje ya nchi.

“Napata wasiwasi kama Rais Jakaya Kikwete, aliangalia wasifu wa waziri wake kwa sababu asingeweza kumchagua kushika nafasi kubwa kama hii, wakati vyeti vyake vina mashaka,” aliongeza.


Alisema kitendo cha kumuweka mtu mwenye vyeti vya mashaka, kunaweza kusababisha nchi kuyumba kiuchumi, kuongezeka kwa deni la taifa, kwa sababu uamuzi wake unatokana na ufahamu wake.

WAZIRI AJIBU

Akizungumza na MTANZANIA Jumatatu kuhusu madai hayo, Waziri Mkuya alisema elimu yake wala haina mashaka, kwani alisoma kidato cha tano na sita katika Shule ya Sekondari Lumumba mjini Zanzibar.


Baada ya hapo, alijiunga na masomo ya diploma ya Biashara katika Chuo cha Stamford cha Malaysia, ambapo pia alichukua diploma nyingine ya biashara nchini Uingereza.


Alisema mbali na masomo hayo, pia amesoma shahada ya pili ya biashara katika Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) na kuhitimu mwaka 2009.

“Nimehitimu Shahada ya Uzamili ya Utawala na Biashara (MBA) ya Chuo Kikuu cha WATT kilichopo Edinburgh, Scotland.

“Kwa sasa nachukua Shahada ya Uzamivu (PhD) ya Utawala wa Biashara Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, tawi la Dar es Salaam,” alisema Mkuya

Advertisements