Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein,akisalimiana na Waziri wa Afya na  Ustawi wa Jamii wa India Shri Ghulam Nabi Azad, alipowasili katika hoteli ya Oberoi Mjini New Delhi alipofikia Rais na Ujumbe wake wakiwa katika ziara ya kiserikali Nchini India

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein,akisalimiana na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii wa India Shri Ghulam Nabi Azad, alipowasili katika hoteli ya Oberoi Mjini New Delhi alipofikia Rais na Ujumbe wake wakiwa katika ziara ya kiserikali Nchini India

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imewataka wadau katika sekta ya madawa nchini India kuchangamkia fursa zilizoko Zanzibar za kuwekeza kwa kuanzisha viwanda na hata kuweka vituo vya kusambazia bidhaa zao katika masoko mengine ya nchi za ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

 

Wito huo umetolewa jana na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein wakati alipokuwa akizungumza na wanachama wa Baraza la Kuhamasisha Biashara ya Madawa Nchi za Nje la India (PHARMEXCIL) katika mkutano uliofanyia mjini Hyderabad, India.

 

Aliwaeleza wanachama wa Baraza hilo kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inatilia mkazo upatikanaji wa madawa katika hospitali nchini hivyo ingependa kuona viwanda vya kutengeneza madawa vinajengwa kuondosha tatizo la uhaba wa madawa mara kwa mara.

 

Alibainisha kuwa tangu kiwanda cha Serikali cha kutengeneza madawa kilipokufa miaka ya themenini Serikali imekuwa ikipata shida katika kuzipatia hospitali zake madawa ya kutosha na kwa muda unaotakiwa kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo gharama kubwa za kununulia madawa pamoja na utaratibu wenyewe kuwa na urasimu mkubwa.

 

Kwa hiyo aliwaeleza washiriki wa mkutano huo kuwa suala la uanzishwaji wa viwanda vya madawa na mahitaji mengine ya hospitali ni jambo linalopewa kipaumbele na Serikali.

 

Aliwaeleza washiriki wa mkutano huo kuwa kuna fursa pia ya kushirikiana na Zanzibar katika kufanya utafiti wa madawa ya asili ambayo India ina utaalamu na uzoefu wa miaka nyingi katika enea hilo.

 

Kwa minajili hiyo Dk. Shein alihimiza ushirikiano wa karibu kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Afya ya Zanzibar na PHARMEXCIL huku akieleza matumaini yake kuwa katika muda si mrefu kutakuwa na mawasiliano rasmi yatakayo wezesha pande hizo kutia saini makubaliano ya ushirikiano.

 

Halikadhalika alibainisha kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itatuma ujumbe wa wataalamu katika kipindi fupi kijacho kuja kuzungumza Baraza hilo kufuatilia matokeo ya mkutano huo.

 

Akizungumza katika mkutano huyo Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dk. Mohamed Saleh Jidawi alieleza kuwa Wizara yake iko tayari kuwapa ushirikiano unaohitajika wale wote ambao wataamua kuwekeza Zanzibar kwa kuwa Serikali na wananchi inawahitaji.

 

Akizidi kufafanua alisema kuwa Zanzibar kijiografia ipo katika nafasi nzuri ya kuwa mlango wa bidhaa za makampuni zinazozalishwa Zanzibar kuingia katika masoko ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na Jumuiya ya Uchumi ya Nchi za Kusini mwa Afrika-SADC.

 

Wakati huo huo wanachama wa Baraza la PHARMEXCIL wameonesha nia ya kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na wanangalia namna wanavyoweza kutumia fursa iliyopo kufanyabiashara na kuwekeza Zanzibar.

 

Meneja Mkuu wa PHARMEXCIL Dk. Padmanabhuni Appaji amesema kuwa mkutano huo umekuwa wa manufaa kwa kuwa wanachama wake wamepata fursa ya kufahamu fursa zilizoko Zanzibar katika sekta yao.

 

Kwa hiyo Baraza lake linasubiri kwa hamu ujumbe wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar utakapofika Hyderabad kuzungumza namna ya ushirikiano.

 

Dk. Appaji alieleza kufurahishwa kwake na wananchama wa Baraza lake kupata wasaa kubadilishana mawazo na Mheshimiwa Rais na Ujumbe wake na kwamba mazungumzo ya mkiutano huo yamekuwa ya manufaa kwa wananachama wake.

 

Wakati wa maswali na majibu baadhi ya wajumbe waliofuatanana Mheshimiwa Rais walijibu maswali na kutolea ufafanuzi masuala mbalimbali yaliyoulizwa na washirkia wa mkutano huo.

 

Katika ziara hiyo Dk Shein amefuatana na Mke wake Mama Mwanamwema Shein, Waziri wa Fedha Omar Yusuf Mzee, Waziri wa Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Vijana, Wanawake na Watoto Bibi Zainab Omar Mohamed, Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko Nassor Ahmed Mazrui, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Dk. Mahadhi Juma Maalim na Balozi wa Tanzania nchini India Injinia John Kijazi.

 

Wengine ni Katibu Mkuu Wizara ya Afya Mohamed Saleh Jidawi, Katibu Mkuu Kilimo na Maliasili Affan Othman Maalim na Mshauri wa Rais Ushirikiano wa Kimataifa, Uwekezaji na Uchumi Balozi Mohamed Ramia.

 

Kabla ya kuondoka Hyderabad kwenda Bengaluru zamani Bangalore Dk. Shein alitembelea kiwanda cha kutengeneza madawa cha NATCO Pharma Limited.  Ataendelea na ziara yake leo hapa Bengaluru kwa kutembelea hospitali ya Manipal iliyopo mjini hapa na ataondoka baadae jioni kwenda jiji la Mumbai kuendelea na ziara yake

Advertisements