Spika wa baraza la wawakilishi Pandu Amei Kificho

Spika wa baraza la wawakilishi Pandu Amei Kificho

Salmin Awadh SalminWARAKA wa Baraza la Wawakilishi juu ya maoni ya Katiba, umezua jambo baada ya Wajumbe wa Baraza hilo wa CCM, kuukataa na kudai Spika wa Baraza hilo, Pandu Ameir Kificho, aliwasaliti kwani alishindwa kuishirikisha Kamati ya Uongozi ya Baraza hilo katika uandaaji wake.

 

Waraka huo ambao uliibuka juzi wakati Wajumbe wa Baraza la Katiba wakiwa wameanza kufanya mjadala wa Bunge la Katiba, Mjini Dodoma, kwa kupitia kanuni za Bunge, ambapo leo wajumbe wa Bunge hilo wanatarajiwa kupiga kura ya maamuzi kama Bunge litumie  mfumo wa kupiga kura ya siri ama dhahiri.

 

Mwishoni mwa wiki iliyopita baadhi ya Wajumbe wa CCM Zanzibar,  waliibuka na kukataa waraka uliokuwa umesambazwa, unaodai Wajumbe wa Baraza hilo, kuwa wanaunga mkono mfumo wa Serikali tatu.

 

Waraka huo, tangu uzuke tayari kumekuwa na vikao kadhaa vya Chama hicho, kilichomuhoji Spika Kificho kamaanautambua ambapo hapo awali ilidaiwa kuukataa lakini ulikuwa na saini yake.

 

Akizungumza na Waandishi wa Habari Mnadhimu wa CCM wa Baraza la Wawakilishi ambaye pia ni Katibu wa Kamati ya Uongozi ya Baraza la Wawakilishi, Salmin Awadh Salmin, alisema Kamati yao na Wajumbe wa Baraza hilo kutoka Chama hicho, hawautambui.

 

Alisema wanaukataa waraka huo, kwa vile uliandaliwa kwa kuwashirikisha viongozi wachache

wa Baraza hilo, ambao walijibebea jukumu hilo zito na kuwasingizia Wajumbe wa baraza hilo.

 

“Sisi Wawakilishi wa CCM, naomba ieleweke hatukuwa sehemu ya maoni yaliowasilishwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba  kwa vile jambo hilo lilifanywa kwa siri bila ya kutolewa taarifa kwa viongozi wakiwamo viongozi wa Kamati ya uongozi” Alisema Salmin.   

 

 Alisema ni jambo la ajabu na kushangaza kuona taasisi kubwa kama hiyo, kuweza kutekeleza waraka huo kwa kificho kwani ilitakiwa baada ya kuandaliwa wangelipewa Wajumbe wa Kamati ya Uongozi ya CCM kuupitia.

 

Alisema jambo halikufanyika kiasi ambacho inaonesha mambo hayo yaliandaliwa kwa makusudi ili wasiweze kutambua kiliomo ndani ya waraka huo.

 

“Taarifa na maoni hayo yaliotolewa kwa niaba ya Baraza la Wawakilishi hayakuwa na baraka wala kuvihusisha vikao husika na hivyo kubeba zaidi maoni binafsi ya viongozi waliohusika”Alisema

 

Mnadhimu huyo, alisema inawezekana viongozi hao, walikuwa na dhamira njema na pana zaidi hadi hadi kufikia kuwasahau wajumbe wenzao.

 

Akiendelea alisema ingawa tatizo hilo limetokea, lakini bado wataendelea kiona wanasimamia kuitekeleza ilani, kanuni na miongozo ya Chama hicho.

 

Alisema ni vyema kwa Wajumbe wa Bunge hilo, kuona wanatumia Bunge hilo kujenga taifa imara kwa kuandaa Katiba yenye maslahi mapana na yenye maisha marefu kwa kuimarisha Muungano huo.

 

Salmin alitoa wito, kwa wanachama na Wapenzi wa Chama hicho, kufahamu kwamba Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi hawawajawasaliti juu ya msimamo wa Chama hicho hasi sasa.

“Tutasimamia maelekezo hatutokisaliti Chama chetu na Wanachama wake tutasimamia maelekezo na miongozo ya CCM kwa gharama yoyote huku tukiamini kwamba Muungano imara na endelevu nni Muungano wa serikali mbili” Alisema Salmini.

 

Alisema ni vyema kwa wanachama wa chama hicho na wananchi kuona wanakuwa makini katika kuufuatilia  mchakato wa Katiba ili kuweza kubaini dhamira za wapotoshaji wa malengo mema ya waasisi wa taifa hilo.

 

Alisema wao binafsi wanaamini muongozo wa Chama hicho una dira pana yenye muono wa mbali zaidi katika sualahilo.

 

Alisema inawezekana kuchelewa kulitambua suala hilo linaweza likawa ni kumzo kwao kwa vile waraka huo uliandaliwa tangu Febuari 5, 2013, lakini hali hiyo ilitokana na kuwapo kwa usiri mkubwa uliokuwa umegubika suala hilo, kwani ulipewa jina la ujanja ujanja bila ya kuwekwa wazi na wajumbe kuuelewa baada ya kuitwa Waraka wa maoni ya Baraza la Wawakilishi.

 

Kutokana na hali hiyo, Mwenyekiti huyo, alisema Kamati yao inasisitiza kuwa hauitambui, kwa vile hakuna alieshirikishwa na vyema kwa wajumbe waliouandaa kujitokeza hadharani kuelezea dhamira na malengo yao kwanini walifanya hivyo.

 

Akiendelea alisema anatambua huenda mazingira ya maoni binafsi yalichukua jukumu la kuisemea taasisi hiyo ili kutimiza jambo hilo ovu kwa taasisi hiyo bila ya kuwashirikisha waliowengi.

 

Kutokana na hali hiyo, Katibu huyo, alisema kwa vile jambo hilo halikubaliki kutokana  na msimamo wa chama hicho unaeleweka wazi na kila Mwanachama wa CCM kuunga mkono mfumo awa serikali mbili, bado suala hilo litapitia katika ngazi mbali mbali za Chama hicho kikiwemo kikao cha Wabunge na Wawakilishi cha Bunge linaloendelea.

 

Alisema Chama cha CCM kina utaratibu mkubwa wa kushughiulikia watu wanaokisaliti chama na hawana uhakika wa hivi sasa kama watachukua hatua za kumuwajibisha Spika huyo na watasubiri mchakato wa Chama.

 

Alisema wameamua kuchukua hatua hiyo, kwa vile hapo awali wakati wa mahojiano waliyoyafanya na Spika huyo aliukataa waraka huo kwa kueleza kuwa hakuhusika kuuindaa lakini juzi jioni alikubali kwamba ulitokana  na yeye na saini iliyowekwa ilikuwa ni ya kwake.

 

Kutokana na hali hiyo alisema kinachoonekana kuwapo kwa mkanganyiko ambao unataka kujitokeza wa kuukataa waraka huo, ambapo tayari hivi sasa Spika huyo ameukubali kutolewa naye.

 

Alisema inafurahisha kuona Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohammed Shein, kueleza bayana juzi katika uzinduzi wa miaka 50 ya Muungano ameeleza wazi kuunga mkono msimamo wa serikali mbili, jambo ambalo wanakubaliana naye na inakuwa vigumu kuona baadhi ya wanachama hao kuanza kwenda kinyume na maamuzi hayo ya Chama chao

Advertisements