watoto wa shuleNa Juma Abdalla-Zanzibar Islamic News

Hakuna kitu kinachotia aibu, fedheha  kashfa au kutia uchungu kusikia Zanzibar bado kuna watu madhalim, mafisad, mahusda wanaofanya vitendo vya ubakaji watoto wadogo wasiokuwa na hatia wanaotegemewa kuwa nguvu kazi ya taifa la baadae.

Vitendo hivyo vya ukatili vinavyoendelea kila kona za wilaya za Unguja na Pemba dhidi ya watoto  ni ukiukwaji wa haki za binadamu na vinapaswa kulaniwa sio tu kwa wanaharakiti, lakini pia kwa wananchi wote.

Hivyo watu wanaofanya vitendo hivyo wanajisikia vipia kumbaka mtoto wake  mwenye umri mdogo wengine hata chini ya mwezi mmoja wa kuzaliwa, lakini la kushangaza zaidi kusikia baba mzazi ndie anaehusika na matukio hayo.

Chama cha wandishi wa habari Tanzania TAMWA kwa kushirikiana na shirika la Umoja wa Mataifa UNFPA, katika kukabiliana na vitendo hivyo kimefanya utafiti wa kihabari kufahamu kwa undani matukio ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto yanayondelea kufanwa kila siku.

Utafifi huu ni mwendelezo wa tafiti mbalimbali zilizotangulia zilizolenga kubainisha vitendo vya udhalilishaji wanaofanyiwa wanawake na watoto.

Utafiti wa kitaifa (DHS) uliofanywa mwaka 2010 unaonesha zaidi ya asilimia 39 ya wanawake nchini wanafanyiwa vitendo vya ukatili tangu wakiwa na umri wa miaka 15 na wengi wanaofanyia ukatili ni waume au baba zao wenye jukumu la kulinda usalama wa maisha yao.

Mwezi April mwaka 2012 na mwanzoni mwa mwaka 2013, TAMWA ilifanya utafiti kwenye skuli za sekondari za mikoa 20 ikiwemo mika 16 ya Tanzania bara na mikoa mine ya Zanzibar na kubaini mambo yanayokwamisha wanafunzi wa kike kukatisha masomo yao na wengine kufeli mitihani ya taifa.

Utekelezaji wa tafifi zote hizi ni sehemu ya kuweka umuhimu wa TAMWA katika mpango wake wa miaka mitano (2010-2014) kujikita na utetezi na kusimamia haki za wanawake na watoto.

Katika makala hii inangalia zaidi juu ya utafiti wa kihabari ulifanywa na wandishi wa habari Zanzibar katika wilaya ya Kaskazini ‘A’ na ‘B’, dhidi ya vitendo vya ubakaji wanaofanyiwa watoto wadogo.

Utafiti uliofanywa katika kipindi cha Januari 2012 hadi November 2013 umethibitisha tatizo la ubakaji kwa wilaya ya Kaskazini ‘B’ ni kubwa, jumla ya kesi 242 za kubakwa zimeripotiwa katika maeneo tofauti ya wilaya hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Wizara ya Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Vijana, Wanawake na watoto vitendo vya ubakaji vimechukua asilimia 80 ya udhalilishaji wote unaofanywa Zanzibar.

Takwimu kutoka kituo cha mkono kwa mkono ( one stop centre) Kivunge zimeonyesha kwa kipindi cha Januari hadi September mwaka 2013 wamepokea kesi 134 za udhalilishaji kati ya hizo kesi za ubakaji 81 sawa na asilimia 60 ya matukio yote ya udhalilishaji yanaytokea mkoa wa Kaskazini Unguja.

Dawati la jinsia mkoa wa Kaskazini Unguja limeripoti kesi 66 za kubakwa, kituo cha polisi Mahonda kimeripoti kesi 63 na mahakama ya Mfenesini imeripoti kesi 30 kwakipindi cha mwaka 2012/2013. Kati ya kesi 63 zilizoripotiwa kituo cha polisi Mahonda kesi 31   mwaka 2012 na kesi 32  mwaka 2013.

Akitoa taarifa za ubakaji afisa Ustawi wa Jamii Zanzibar Biubwa A. Mohammed amesema katika kesi za udhalilishaji kesi za ubakaji zinashika nafasi ya pili.

Utafiti huo umegundua vikwazo vinavyokwamisha kesi kupelekwa mahakamani ni pamoja na rushwa, muhali wa kifamilia, polisi kutoa uwamuzi kinyume na sheria na wazazi au walezi kutojua sheria ikiwemo kutunza ushahidi.

Kati ya kesi za kubaka 242 zilizoripotiwa Mkoa wa Kaskazini Unguja utafiti umeonyesha kituo cha polisi Mahonda mwaka 2012 kilipokea kesi 30 za kubakakati ya hizo nane ndio zilizofikishwa mahakamani na kesi moja ilipatiwa uwamuzi. Aidha kesi 30 za kubaka zilifikishwa mahakama ya Mfenesini na kesi saba ndio zilizopatikana na hatia.

Afisa wanawake na watoto Wilaya ya Kaskazini ‘B’ Zuwena Hamad Omar amesema watendaji wakuu wa kubaka ni walimu wa skuli, madrassa na ndugu wa karibu wa familia.

Amesema vikwazo vinavyochangia kesi za ubakaji kutofikishwa mahakamani ni ruswa iliyoshamiri zaidi katika jeshi la polisi na Mahakama.

Bi Zuwena ametoa mfano wa kesi moja ya Kibeni wilayani humo mtoto wa miaka miwili aliebakwa na mbakaji alikutwa na wazazi na baba wa mtoto, taratibu zote zilifuatwa na ushahidi ulipatikana, lakini hadi sasa mwaka wa pili hakuna hukumu iliyotolewa.

‘’Jamii imekuwa ikitupia lawama jeshi la polisi kujihusisha na rushwa kwa kuwaelekeza au kuwatisha wazazi wa watoto waliobakwa kuzimaliza kesi hizo kienyeji’’. Alisema Bi Zuwena wakati alipohojiwa.

Mkuu wa dawati la jinsia kituo cha polisi Mahonda Insp. Fadhila Mustafa Ali amebainisha sababu zinazosababisha kesi zisifike mahakamani ni wazazi wanakwenda polisi iwapo hawatakubaliana na wakosaji au mhusika hajajulikana,lakini anapojuikana husulihishana wenyewe na polisi wanabaki na jalada wanasubiri mhusika,lakini matokei yake hatokei.

Utafiti umebaini pia viongozi wa vijiji (masheha) baadhi yao wanachangia kuongezeka kwa ubakaji dhidi ya watoto wa kike na kulawiti watoto wa kiume kutokana na kuficha taarifa wanazopelekewa au kuzisikia kwenye maeneo yao.

Hali hii imejitokeza katika shehia ya Kidazini ambapo sheha aliripoti katika kijiji chake kwa muda wa miaka mitatu hakuna tukio la ubakaji lililoripotiwa kutokana na kupatiwa mafunzo, lakini mwandishi wa wilaya ya Kaskazini ‘B’ Kashmir Haji amesema miezi miwili iliyopita ameripoti matukio mawili ya ubakaji kwa watoto wa miaka tisa na mine ndani ya shehia hiyo, taarifa hizo pia zimethibitishwa na jeshi la polisi mkoa wa Kaskazini Unguja.

Hali hii inathibitisha bado mtindo wa kuficha taaria za vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia upo hasa ikiwa tukio limemgusa sheha au viongozi wengine.

Jamii pia imetajwa chanzo cha kuongezeka matukio ya ubakaji na kulawiti kwani baadhi yao hawaripoti matukio hayo katika vyombo vya sheria.

Akitoa mfano katika shehia ya Mtetema Bw. Makame Hamad mtoto wake wa kike miaka 16 alitoroshwa, lakini hakutoa taarifa katika vyombo vya sheria alikubaliana na wazazi wa kijana aliemtorosha binti yake amuwowe lakini alipokataliwa mwanawe kuolewa alipeleka shauri hilo mahakamani.

Akizungumza kuhusu kadhia hii Afisa wanawake Wilaya ya Kaskazini ‘B’ Bi Zuwena Hamad amesema inapotokea mtu hajui taratibu za kupita kesi huishia hivyo hivyo na kutoa mfano wa mtoto aliebakwa Bumbwini, baba wa mtoto aliripoti kesi polisi, lakini aliambiwa wazi shtaka lake halifiki popote na kuelekezwa kuyamaliza kifamilia.

Baba wa mtoto huyo hakuridhika na kauli hiyo na kupeleka shauri hilo kwa afisa wanawake wa wilaya na hatimae alimsaidia kuifikisha kesi mahakamani.

‘’ mara nyingi kesi huwa hazifiki mahakamani na huwa zinaishia polisi kwa kutakiwa wakubaliane, iwapo zitafika basi ushahidi unachukua muda mrefu’’. Alibainisa afisa huyo.

Bi Zuwena amefafanua kuna kesi ziko chini ya upelelezi zaidi ya miezi mine, wakati sheria No. 7 ya mwaka 2004 ya mwenendo ya makosa ya Jinai ya Zanzibar ( Criminal Procedure Act.) inataka kesi ikifikia miezi minne kama haina ushahidi ifutwe.

Baadhi ya wananchi waliochangia tukio hili wengi wao wanawalaumu polisi kwa kutotimiza wajibu wao hasa kwa matukio ya udhalilishaji. Walitolea mfano kesi hiyo ya Bumbwini ya mtoto aliebakwa ingawa wahusika walipeleka dai lao kituoni, lakini polisi walijibu wazi mtendaji hawezi kuchukuliwa hatua zozote kwa sababu ni mtoto wa kigogo, hali inayonesha udhaifu uliopo katika jeshi la polisi.

Utafiti huu wa wanahabari pia umebaini bado suala la utowaji wa hukumu kwa kesi za ubakaji na kulawiti ni mgumu kutokana na kesi nyingi kurundikana mahakamani bila ya kuwa na maamuzi yoyote au kuishia njiani.

Taarifa kutoka kituo cha polisi Mahonda  kuanzia Januari hadi Septemba 2012 kati ya kesi 32 za kubaka zilizoripotiwa katika mkoa wa Kaskazini Unguja, kesi mbili zimepatikana na hatia. Aidha kwa mwaka 2013 kati ya kesi 30 za kubaka kesi moja imepatikana na hatia.

Kukosekana kwa elimu ya kuhifadhi ushahidi imetajwa ni miongoni mwa vikwazo vinavyo  kipindi hicho .changia vinavyochagia upatikanaji wa hukumu.

Utafiti huu umebaini ni watu wachache wanaowapeleka watoto wao wao waliobakwa katika vituo vya polisi au hospitali bila ya kuwasafisha kutoana na sababu za kimila kuwa mtoto akitoka bila ya tohara anaweza kudhuruka na kuchangia kwa nafasi kubwa kukosekana ushahidi.

Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar DPP, imesema bado baadhi ya watu hawana uelewa kuwa mtoto anapobakwa hatakiwi aoshwe mpaka apelekwe hospitali, hata hivyo bado wazee wengi watoto wao wanapobakwa huwaosha kwa kuona uchafu kumuwekea mtoto wake, katika hali hiyo kunasababisha ushahidi kukosekana.

Mwanasheria kutoka afisi ya DPP Bw. Walid Mohammed Adam amesema hospitali pia kuna upungufu kwani watu wanapokwenda kutoa taarifa za kubakwa mara nyingi daktari huwa hayupo au huelekezwa aondoke na kurudi kesho na kumlazimu mzee kumkosha mtoto wake kwa vile ni vigumu kumuweka na chafu.

Amevitaja vikwazo vingine vinavyokwaza kupatikana kwa hukumu, zinatokana na taasisi husika likiwemo jeshi la polisi, mahakama na hospitali kwa kubadilisha PF au kupoteza kabisa, kuchelewesha mashahidi kulipwa pesa zao na kuahirishwa kwa kesi mara kwa mara.

‘’ shahidi anaweza kuitwa zaidi ya mara tatu kwenda kutoa ushahidi, lakini kesi huwa haiendeshwi na akawa kapoteza muda wake pia kupoteza nauli hivyo husababsha kuvunjika moyo na kuiacha kesi njiani’’. Alisema afisa wa DDP.

Bw. Nadhif kutoka chuo cha Mafunzo alisema alikuwa na kesi ya mtoto wa kaka yake kesi hiyo imetolewa SAMOS mara 12, lakini iliendeshwa mara tatu mara zote tisa kesi imekuwa ikiahirishwa na hatimae mama wa mtoto ambae ni shahidi wa kesi hiyo alichoka na kuamua kuiacha.

Vikwazo vingine ni kukimbia kwa mtuhumiwa baada ya kupewa dhamana, mashahidi kukaataa kufika mahakamani kutoa ushahidi kwa kuhofia kutengwa na jamii, mashahidi kukosa nauli ya kwenda kutoa ushahidi mahakamani pia baadhi ya wazazi kuona aibu kutoa ushahidi mahakamani kwa kuhofia taarifa za mtoto wao kuenea mtaani.

Tume ya kurekebisha sheria Zanzibar imetaja sababu za kukosekana hukumu ni pamoja na upungufu uliomondani ya sheria, Bw. Khamis Mwita kutoka tume hiyo amesema sheria zinahitaji kufanyiwa marekebisho ili zindae na mazingira sio na sio kuangalia zaidi katika mikataba ya kimataifa.

Akitoa mfano wa CEDAW unazungumza ubakaji ndani ya ndoa wakati sheria za Zanzibar hakuna ubakaji ndani yandoa, amezitaja sheria nyingine zinazohitaji kufanyiwa marekabisho katika sheria ni suala la kupiga mke, kupiga bodi, waganga wa jadi wanaowafanyia dawa wateja wao ndani yake huwa na ubakaji.

Daktari dhamana wa hospitali ya Kivunge Bw. Yussuf amesema kituo cha mkono kwa mkono Mahonda hakuna vitendea kazi, wafanyakazi hawatoshi, kituo kinatakiwa kiwe na daktari maalum kusimamia matukio ya ubakaji tofauti na hali ya sasa daktari wa zamu ndie hutoa huduma katika kituo hicho.

Vile vile matokeo ya utafiti yamebaini baadhi ya wazee wamekata tama na matendo ya ukiukwaji wa maadili ya watoto wao na kuamua kuwacha matukio hayo yaendelee bila ya hatua yoyote.

Akitoa mfano Bi Aziza wa ofisi ya DPP amesema mama wa mtoto aliebakwa aliitwa mara tatu kwenda mahakamani kutoa ushahidi hakufika na kulazimika kutumwa askari kumkamatwa alipoulizwa kwanini wa mahakama alisema atawafunga watu mara ngapi na mtoto wake hana adabu. Kwa sababu wakati kesi yake inaendelea mahakamani ametafuta bwana mwengine kwa hiyo haoni sababu ya kupoteza muda wake.

Vitendo vya ubakaji Zanzibar bado ni tatizo kubwa na vilipofikia sasa tuseme basi, lakini jamii inahitaji kuelimishwa umuhimu wa kuripoti kesi hizi vituo vya sheria na  kuacha tabia kuyatatua matukio haya kienyeji.

Tume ya kurekebisha tabia itowe elimu kwa jamii ili ifahamu ifahamu wakati gani sheria zinahitaji kurekebishwa kudai haki yao hiyo.

Sheria zirekebishwe ili ushahidi wa mtoto ukubalike, kwa vile kesi za kubaka hukosa ushahidi kutokana na watendaji wa matukio kufanya kwa siri hivyo ushahidi wa mwanzo ni muathirika na akiwa mtoto mdogo ushahidi wake haukubaliki.we

Katika utafiti huu jamii imeshauri itungwe sheria ya kulazimisha mashahidi kwenda mahakamani kutoa ushahidi na kupewa adhabu kwa atakaepinga ili kuzifanya kesi za kubaka kupata hokum.

Kundwe mtandao utakaojumuisha polisi, mahakama, ustawi wa jamii, wanasheria ili kushughulikia matukio ya udhalilishaji kwa pamoja na kuwa na takwimu za aina moja. Adhabu za makosa ya ubakaji ziongezwe zaidi ili kudhibiti matukio hayo.

Je? Katika hilo tunahitaji usaidizi kutoka nje ya nchi.

Advertisements