Muwakilishi wa Kampuni ya Kimataifa ya Ujenzi wa Bandari ya China Bwana Xu Xinpei akibadilishana mawazo na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif.

Muwakilishi wa Kampuni ya Kimataifa ya Ujenzi wa Bandari ya China Bwana Xu Xinpei akibadilishana mawazo na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif.

Kampuni ya Ujenzi wa Bandari ya Jamuhuri ya Watu wa China { CHEC } imeonyesha shauku ya kutaka kujenga Bandari kubwa hapa Zanzibar kwa lengo la kuifanya Zanzibar kuwa katika ramani ya Dunia kwa utoaji wa huduma za Kimataifa za usafiri wa Baharini.

Kauli hiyo imetolewa na Muwakilishi wa Kampuni hiyo yenye Tawi la Ofisi yake Nchini Tanzania Bwana Xu Xinpei wakati akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.

Bwana Xu Xinpei alisema Zanzibar imebarikiwa kuwa na eneo zuri la uwekezaji katika masuala ya usafiri wa Bandari Sambamba na Utalii jambo ambalo Kampuni hiyo imevutiwa kutaka kuwekeza katika Sekta hizo.

Alisema mradi huo ambao kitaalamu umekisiwa kugharimu zaidi ya Dola za Kimarekani  Milion  40 unaweza kutoa fursa kwa meli kubwa za Makontena pamoja na Watalii kutoka Bara la Asia kuitumia Bandari hiyo.

Alisema hatua hiyo mbali ya kuimarisha uhusiano wa muda mrefu uliopo kati ya Jamuhuri ya Watu wa China na Zanzibar na Tanzania kwa ujumla lakini pia utaongeza kasi ya Kibiashara  katika mwambao wa Afrika Mashariki.

“ Tumekuwa tukishuhudia  ongezeko kubwa la uwekezaji ndani ya Visiwa vya Zanzibar ambalo linaonekana kutawaliza zaidi na wawekezaji wa Bara la Ulaya wakati uwezo kama huo unawezekana pia kufanywa na wawekezaji wa Bara la Asia hasa China “. Alisema Mwakilishi wa Kampuni hiyo ya ujenzi wa Bandari ya China Bwana Xu Xinpei.

Akizungumzia suala la uwekezaji katika Sekta ya Utalii Bwana Xu Xinpei aliiomba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuipatia  Kampuni yake eneo maalum kwa ajili ya ujenzi wa Hoteli kubwa ya Kitalii hapa Nchini.

Alisema ujenzi wa Hoteli hiyo unaweza kuamsha ari kwa wageni na watalii kutoka Kisiwa cha Hainan Nchini China kutembelea Zanzibar kitendo ambacho kitaongeza kasi ya ushirikiano wa pande hizo mbili.

Alieleza kwamba Jamuhuri ya Watu  wa China imekuwa ikivunja rekodi ya idadi kubwa ya watalii wanaotembea na kuzunguuka maeneo mbali mbali ya Kihistoria Ulimwenguni.

Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi  aliuomba Uongozi wa Kampuni hiyo kufanya mawasiliano na Mamlaka ya Uwekezaji Vitega Uchumi Zanzibar  {ZIPA } na ile ya Ardhi ili kuona malengo waliyoyapanga  yanafanikiwa na kuleta ustawi wa pande zote mbili.

Balozi Seif alisema Zanzibar na China na hasa Kisiwa cha Hainan zimekuwa na uhusiano wa kipindi kirefu kutokana  na  watu wake pamoja na mimea inayofanana kimazingira.

Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alikutana kwa mazungumzo na Balozi wa Malawi Nchini Tanzania Balozi Flossie Gomile Tijaonga ofisini kwake Vuga.

Katika mazungumzo yao viongozi hao waligusia uhusiano na ushirikiano uliopo wa muda mrefu kati ya Tanzania na Malawi ambao umeasisiwa na Viongozi wa mwanzo  wa Mataifa hayo.

Alisema bado upo umuhimu wa kuendelezwa kwa uhusiano huo  kutokana na Historia ya kudai uhuru kutoka kwa wakoloni iliyosimamiwa na  Rais wa Kwanza wa Tanzania Marehemu Mwalimu Julius K. Nyerere na mwenzake wa Malawi Marehema Kamuzu Banda.

Naye kwa upande wake Balozi wa Malawi Nchini Tanzania Balozi Flossie Gomile Tijaonga alisema Mataifa hayo mawili yamekuwa yakishirikiana kiuchumi kwa kipindi kirefu.

Balozi Flossie Gomile alisema Malawi imekuwa ikiitumia Bandari ya Dar es salaam kwa miaka mingi kupitishia bidhaa na mizigo yake kitendo ambacho kinastahiki kiendelezaw kwa faina ya pande hizo mbili.

Mwanadiplomasia huyo wa Malawi Nchini Tanzania ameipongeza Zanzibar na Watu wake kutokana na mazingira mazuri pamoja na ukarimu wa watu wake unaotoa fursa ya watu wa mataifa mbali mbali duniani kupendelea kutembelea Zanzibar.

Alisema hiyo inatokana na Historia kubwa ya Zanzibar katika Nyanja za Kimataifa hasa katika masuala ya Biashara na Utalii.

 

Othman Khamis Ame

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

5/4/2014.

 

 

Advertisements