weteMabaharia 12 wa meli ya mizigo MV Wete wamezuiliwa nchini Madagasca kwa zaidi ya miezi mitatu baada ya kushindwa kulipia gharama kufuatia meli hiyo kuingia nchini humo wakati ikielekea Moritius.

Akizungumza na Zenji Fm radio baadhi ya wazazi wa mabaharia hao amesema watoto wao wameshikiliwa baada ya mmiliki wa meli hiyo kushindwa kulipa shilingi milioni 17 wanazodaiwa mabaharia hao.

Meli hiyo ilingia Madagasca baada ya kupata hitlafu ya kifundi na kupewa huduma ikiwemo kukwamuliwa kwenye mchanga ambapo kila baharia anadaiwa shilingi milioni moja na laki tatu.

Aidha wazazi hao wamevitaka vyombo vya usalama kulifuatilia suala hilo ili kuona watoto wao wanarudi nyumbani……

        Nae mkurugenzi wa Mamlaka ya usafiri baharini Zanzibar Abdi Omar amesema mmiliki wa meli hiyo amewasiliana na wizara ya mambo ya nje kupitia balozi wa Tanzania nchini Msumbiji ili kushughulikia mabaharia hao.

Ameiambia Zenji fm radio mabaharia hao wamekamatwa na walinzi wa pwani baada ya meli yao kuingia nchini humo kwa madai ya kukosa kibali cha kusafirisha mizigo

        Mabaharia wanaoshikiliwa ni Nahodha Amour Ali Juma, Revinda Jeram Harua, Mohamed Amir Mohammed, Khatib Salum Bakar, Omar Hassan Mwalim, Mussa Yussuf Mussa na Ali Amour  Ali.

Wengine ni Eduward Felis Visso, Haji Ali Haji, Yussuf Ayoub Rashid, Mbarouk Bakar Khamis na Salum Khamis Hassan.

Meli hiyo ya Mv. Wete inayofanya shughuli za usafirishaji wa mizigo katika ukanda wa bahari ya Hindi inamililikwa na Said Mbuzi.

 

Advertisements