Archive for May, 2014

RAIS ZUMA APISHWA KWA MUHULA WA PILI

Rais wa AFrika ya Kusini Jacob Zuma

Rais wa AFrika ya Kusini Jacob Zuma

Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini ameapishwa kwa muhula wa pili wa uongozi.

Maelfu ya wafuasi, wakipepea bendera za taifa, walishangilia ndege za jeshi za Afrika Kusini zilipopita juu ya uwanja wa sherehe

Viongozi wa nchi 20 walikuwako katika sherehe hiyo.

Katika hotuba yake ya kutawazwa Rais Zuma aliahidi kuwa serikali yake itakuza uchumi na nafasi za ajira.

Chama chake cha ANC kilishinda uchaguzi awali mwezi huu ambapo kilipata kura zaidi ya asili-mia-60.

Hii ni mara ya tano kwa chama cha ANC kushinda katika uchaguzi na kimeongoza nchi tangu utawala wa ubaguzi wa rangi kumalizika

 

Chanzo BBC

 

 

SERIKALI YA UMOJA WA KITAIFA MASHAKANI-BALOZI IDD

balozi seif ali iddi makamu wa pili wa rais zanzibar

balozi seif ali iddi makamu wa pili wa rais zanzibar

Makamu wa pili wa rais Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amesema serikali ya umoja wa kitaifa inaendelea kupata misukosuko kutokana na kebehi na kejeli dhidi ya viongozi kupitia majukwaa ya kisiasa.

Amesema hali hiyo imesababisha baadhi ya wajumbe wa baraza la wawakilishi kutaka kuwasilisha hoja binafsi ya kuulizwa wananchi kama wanahitaji kuendelea na serikali ya umoja wa kitaifa au la.

Akijibu hoja za wajumbe wa baraza hilo waliochangia hotuba ya bajeti ya ofisi ya makamu wa pili wa rais balozi Iddi amewataka wanasiasa kuacha kutoa maneno ya kuwachonganisha wananchi na viongozi wa juu wa serikali..

Hata hivyo balozi Iddi amesema hali ya amani na utulivu bado ni nzuri kutokana na kuwepo serikali ya umoja wa kitaifa kwa viongozi wa vyama vya siasa walioko serikali kuendelea kushirikiana.

Nae waziri wa nchi ofisi ya makamu wa pili wa rais Mohammed Aboud amesema ugawaji wa majimbo unaotaka kufanywa na tume ya uchaguzi Zanzibar unatokana utekelezaji wa katiba.

Hata hivyo amesema ugawaji wa majimbo, mipaka na majina haufanyiki bila ya kuwashirikisha wahusika wakuu wakiwemo wajumbe wa baraza la wawakilishi na vyama vya siasa..

Wajumbe wa baraza hilo wamepitisha hotuba ya bajeti ya kadirio ya mapato na matumizi ofisi ya makamu wa pili wa rais kwa mwaka wa fedha 2014/2015 yatatkayogharimu zaidi ya shilingi Bilioni 19.98.

JUMUIYA YA MAIMAM ZANZIBAR YAONYA WANAOTAKA KUINDOA SERIKALI YA UMOJA WA KITAIFA

MAIMAMUJumuiya ya Maimam Zanzibar JUMAZA imesema inashangazwa na baadhi ya wanasiasa wanaopiga vita serikali ya umoja wa kitaifa kwa kutoa kauli za wazi ikiwemo kutakapeleka hoja binafsi baraza la wawakilishi ya kuondoa serikali hiyo.

Kwa mujibu wa barua ya wazi iliyotumwa kwa rais wa Zanzibar Dr. Ali Mohamed Shein imesema wanasiasa hao wanajali zaidi maslahi yao na lengo lao ni kuirejesha Zanzibar katika siasa za chuku na uhasama zilizosababisha wananchi kususiana shughuli zao za kijamii.

Jumuiya hiyo ya Maimamu imewakumbusha viongozi wa siasa ahadi waliochukua mbele ya Mwenyezi Mungu ya kulinda maelewano ya wazanzibari, utulivu na amani ya nchi.

Aidha JUMAZA imeonya juu ya lugha za kebehi na ubaguzi zinazotolewa hadharani na baadhi ya wanasiasa zinaweza kutishia mustakabali wa amani, utulivu na mshiakano.

Barua ya Jumuiya hiyo iliyotiwa saini na katibu mtendaji wake Muhidin Zubeir imetaja kauli hizo za matusi na ubaguzi zinazotolewa hadharani zinaweza kutishia amani ya nchi.

Barua hiyo ya wazi ya JUMAZA iliyotumwa kwa rais na kusambazwa kwenye vyombo vya habari imekuja huku spika wa baraza la wawakilishi akiwaonya wajumbe wa baraza hilo kujiepusha na kauli zinazoashiria ugazi

ZANZIBAR KUZALISHA MADAKTARI 38 IFIKAPO SEPTEMBER MWAKA HUU

Mkurugenzi Mauzo  Kimataifa wa Maonyesho ya biashara kutoka Nchini Uturuki { Meridyen International Fair Organisation Limited } Bwana Nuvit Becan akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi  Seif azma ya Taasisi yake kutaka kufanya maonyesho ya Kibiashara Zanzibar.

Mkurugenzi Mauzo Kimataifa wa Maonyesho ya biashara kutoka Nchini Uturuki { Meridyen International Fair Organisation Limited } Bwana Nuvit Becan akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif azma ya Taasisi yake kutaka kufanya maonyesho ya Kibiashara Zanzibar.

Zanzibar inatarajia kujenga Historia mpya katika kuzalisha Madaktari  38 kwa mkupuo mmoja ifikapo mwezi Septemba mwaka huu baada ya Vijana wazalendo wa fani ya Udaktari { Medical Doctor – M.D } kukamilisha mafunzo yao ya miaka sita.

Mkuu wa Mafunzo wa Madaktari Mabingwa kutoka Jamuhuri ya Watu wa Cuba wanaoendesha Mafunzo hayo katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja Dr. Irene Nodarse Torres alieleza hayo wakati akitoa shukrani kwa niaba ya wenzake  mara baada ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kukagua makazi yao.

Balozi Seif alifanya ziara hiyo kuangalia matengenezo makubwa yaliyofanywa ndani ya Nyumba ya Madaktari hao Mabingwa Kutoka Cuba hapo mkabala na Bustani na Victoria iliyopo Mnazi Mmoja Mjini Zanzibar.

Dr. Irene alisema Wanafunzi  Madaktari hao 38 ni miongoni mwa 50 wanaopata Taaluma kutoka mabingwa  wa Taaluma ya Afya kutoka Cuba ambapo wengine 21  wa awamu ya pili wanaendelea na mafunzo kama hayo Kisiwani Pemba.

Alisema ni fahari kwao kuona Wanafunzi hao wanamaliza mafunzo yao kwa mafanikio makubwa katika kiwango kinachokubalika  cha utowaji wa mafunzo ya fani ya Udaktari kimataifa.

Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliipongeza Jamuhuri ya Watu wa Cuba kwa juhudi zake ilizozichukuwa katika kusaidia wataalamu wa  kuendesha mafunzo hayo.

Balozi Seif alisema kukamilika kwa mafunzo hayo kutaziwezesha  Hospitali na Vituo vingi vya afya hapa Nchini kupata wataalamu watakaosaidia wananchi kupata huduma za Afya  kitaalamu zaidi.

Mapema Katibu Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar Dr. Saleh Mohamed Jidawi alisema jengo hilo hivi sasa liko katika kiwango cha kuridhisha kufuatia matengenezo makubwa yaliyofanywa katika nyumba hiyo.

Dr. Jiadawi alisema hivi sasa umebaki usumbufu wa upatikanaji wa wakati wa huduma za Maji safi tatizo ambalo Wizara imelazimika kuweka tangi kubwa la kuhifadhia huduma hiyo kwa kutumia mashine maalum ili kuwaondoshea kabisa tatizo hilo.

“ Wizara tulilazimika kuwajengea tangi kubwa la kuhifadhia maji kwa vile baadhi ya wakati hasa kipindi cha mwezi wa Disemba na Januari huduma hii inakuwa adimu kupatikana katika eneo hili kutokana na kukumbwa kwa kiangazi “. Alisema Dr. Jidawi.

Akigusia maradhi ya Dengue yaliyoibuka hapa Zanzibar hivi karibu Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Afya alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba juhudi zinaendelea kuchukuliwa na wataalamu wa afya katika kudhibiti maradhi hayo yanayosababishwa na Mbu.

Dr. Jidawi alisema hadi sasa wagonjwa sita wameripotiwa kukumbwa na maradhi hayo ambao wanaendelea kupatiwa huduma na uangalizi chini ya Madaktari katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja.

Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Afya aliwaomba wananchi kuendelea kutunza mazingira yao kwa kuondosha vidimbwi vya maji machafu, kutumia vyandarua pamoja na kufika Hospitali wakati wanapopatwa na dalili za maradhi.

Balozi  Seif Ali Iddi mwaka jana alifanya ziara fupi kwenye Makazi ya Madaktari Mabingwa hao wa Cuba kuangalia mazingira halisi ya nyumba hiyo na kuagiza  kufanywa matengenezo makubwa jengo hilo.

Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alikutana na Ujumbe wa Watu watatu wa Taasisi ya Kimataifa ya Maonyesho ya Kibiashara kutoka Nchini Uturuki { Meridyen International Fair Organisation Limited }.

Katika mazungumzo yao yaliyofanyika Ofisini kwa Balozi Seif ndani ya Jengo la Baraza la Wawakilishi Mbweni Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar Mkurugenzi Mauzo  Kimataifa wa Taasisi hiyo Bwana Nuvit Becan alisema lengo la Taasisi yake ni kufanya maonyesho ya Kibiashara hapa Zanzibar.

Bwana Nuvit alisema juhudi zinaendelea kuchukuliwa katika kuwasiliana na taasisi husika hapa Zanzibar ili kuona maeonyesho hayo yanafanyika hapa Zanzibar ili kutoa fursa kadhaa kwa wajasiri amali wa Visiwa vya Zanzibar kujitangaza Kimataifa.

Naye Mwakilishi wa Maonyesho ya Atlantic kutoka Nchini Nigeria Bwana Ayodejo Olugbade wanaoshirikiana pamoja na Taasisi hiyo ya Uturuki alisema uwamuzi wa maonyesho hayo ni kuzitangaza kwa pamoja bidhaa zinazozalishwa Bara la Afrika na Uturuki.

Bwana Ayodejo alisema bidhaa za Kilimo, Biashara Viwanda pamoja na vitu vya sanaa vimepewa nafasi zaidi katika kuvitangaza ndani ya maonyesho yanayoandaliwa na kufanya kwa pamoja na Taasisi hizo.

Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekuwa ikitanua shughuli zake za uchumi  kwa kuitumia sekta ya Utalii na Biashara.

Alisema Sekta hizo zinaweza kufanikiwa kwa kupiga hatua kubwa ya maendeleo endapo zitafikia maamuzi ya kutumia fursa za kujitangaza kupitia maonyesho mbali mbali ya Kimataifa.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliuhakikishia ujumbe huo wa Kimataifa wa Maonyesho ya Biashara kutoka Uturuki kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iko tayari kutoa msukumo ili kuona maonyesho hayo yanafanikiwa kufanyika hapa Zanzibar.

Taasisi ya Kimataifa ya Maonyesho ya Biashara Kutoka Nchini Uturuki tayari imeshafanya maonyesho ya Kibiashara katika mataifa mbali mbali Barani Afrika ikiwemo Tanzania Bara tokea mwaka 1985

 

 

SMZ HAINA MKATABA WA KUUNGANISHA PEMBA NA UNGUJA

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imesema hakuna mkataba wowote uliofikiwa wa kuviunganisha visiwa vya Unguja na Pemba na kupatikana jina la Zanzibar.

Spika wa Baraza la Wawakilishi Pandu Ameir Kificho

Spika wa Baraza la Wawakilishi Pandu Ameir Kificho

Akijibu suala katika kikao cha baraza la wawakilishi waziri wa nchi ofisi ya makamu wa pili wa rais Mohammed Aboud amesema visiwa hivyo vipo tangu enzi za dahari vya nchi moja. Amesema  wananchi wa visiwa vya Unguja na Pemba wanahaki ya kuishi sehemu yoyote na haina maana kuzungumzia masuala ya kujigawa kwa pande mbili na kutaka kuondoshwa hisia hizo…. Nae Spika wa Baraza la Wawakilishi Pandu Ameir Kificho amepiga marufuku masuali ya kibaguzi yenye kuulizia mkataba wa Pemba na Unguja na kauli za kuwahamasishawatu wa upande mmoja kuhama. Aidha Kificho amewataka wananchi kuishi kwa umoja, amani na utulivu na kuwanya wajumbe wachache wenye tabia ya kuhoji mkataba wa Unguja na Pemba kauli hizo hazipaswi kuzungumzwa…. Kauli hizozilizopigwa marufuku na spika Kificho zilijitokeza wakati wa kujadili rasimu ya katiba kwenye bunge maalum la katiba mjini Dodoma.

MAOFISA WIAZARA YA FEDHA ZANZIBAR WALALAMIKIWA

Mwakilishi wa jimbo la Kwamtipura Hamza Hassan Juma

Mwakilishi wa jimbo la Kwamtipura Hamza Hassan Juma

Mwakilishi wa jimbo la Kwamtipura Hamza Hassan Juma amewalalamikia watendaji wa serikali kushindwa kuhudhuria kwa wakati vikao vya baraza la wawakilishi vinavyojadili bajeti ya serikali.

Akizungumza kabla ya kuwasilisha maoni ya kamati za wenyeviti kuhusu bajeti ya serikali kwa mwakawa fedha 2014/2015 ametaka kuahirishwa baraza hilo kwa muda wa dakika 10 ili kupigiwa simu watendaji hao wahudhurie kikao hicho.

Amesema watendaji hao wakiwemo makatibu wakuu, wakurugenzi na manaibu wao pamoja na maafisa wao kutoka wizara na taasisi za serikali ndio wasimamizi wakuu katika utekelezaji wa bajeti hiyo.

Hivyo amesema kutohudhuria kwao kutaifanya michango inayotolewa ndani ya baraza hilo kutozingatiwa..

Kufuatia hali hiyo spika wa baraza hilo Pandu Ameir Kificho amepinga hoja hiyo na kusema uendeshaji wa vikao unazingatia idadi ya wajumbe waliokuwemo ndani

WANAFUNZI JIFUNZENI MFUMO WA TEKNOLOJIA YA MAWASILIANO

413Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema wakati umefika kwa Wanafunzi Nchini kuendelea kujifunza Taaluma mbali mbali kupitia mfumo wa kisasa wa Teknoloji ya Habari na mawasiliano { Teknohama } ili kwenda sambamba na mabadiliko ya Sayansi Ulimwenguni.

Balozi Seif alisema hayo katika hafla fupi ya kukabidhi msaada wa Kompyuta 230 kwa ajili ya Skuli mbali mbali Unguja na Pemba iliyofanyika Makao Makuu ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya amali Mazizini Nje kidogo ya Maji wa Zanzibar.

Msaada huo wa Kompyuta 230 zilizofikishwa hapa Zanzibar ni miongoni mwa Kompyuta  2,500 zilizoahidiwa kutolewa msaada na Rotary Klabu ya Kimataifa inayojishughulisha na Kituo cha uungaji na matengenezo ya Kompyuta katika Mji wa Seattle Nchini Marekani.

Rotary Klabu hiyo ilifikia uamuzi huo wa kutoa msaada kufuatia ziara yake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar  Balozi Seif aliyoifanya Seattle  Marekani mwishoni mwa mwaka 2013 kuhudhuria Mkutano wa 15 wa Chama cha Wafanyabiashara wenye asili ya Bara la Afrika wa Kaskazini Mashariki ya Pacific.

Balozi Seif alisema suala la ajira hivi sasa limekuwa likizingatia zaidi muajiriwa  katika Taasisi yoyote ile mbali ya ujuzi wake wa kitaalamu lakini pia unahusishwa na ufahamu wa suala la mtandao wa mawasiliano ya kompyuta.

Alieleza kwamba jamii inapozungumzia suala la sayansi na Teknolojia kwa sasa sio Physics na Chemistry lakini hata fani ya mitandao wa mawasiliano na Kompyuta  imepewa nafasi kubwa zaidi ambayo pia inatoa fursa ya kurahisisha masomo hayo.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliwataka walimu na wanafunzi watakaobahatika kupatiwa Kompyuta na vifaa hivyo katika awamu ya kwanza kuhakikisha kwamba  wanavitunza katika mazingira yatakayoviwezesha kudumu kwa muda mrefu zaidi.

Alisema hatua hiyo kwa kiasi kikubwa itaendelea kuwapa moyo watu, Mashirika na hata Taasisi zinazoamuwa kujitolea kusaidia vifaa na miradi mbali mbali katika sekta ya elimu.

Balozi Seif aliushauri Uongozi wa skuli mbali mbali nchini kufikiria kujenga vyumba maalum vitakavyokuwa na sifa ya kuwekwa kwa vifaa vya Kompyuta pale wakati utakaporuhusu kufanywa hivyo.

Mapema Naibu katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Nd. Abdulla Mzee Abdulla alisema awamu ya mwanzo ya msaada huo wa Kompyuta, Vifaa vyake pamoja na baadhi ya vitabu itaelekezwa kwa skuli 15 za Msingi ,Sekondari na baadhi ya vituo vya elimu Unguja na Pemba.

Nd. Mzee alizitaja skuli na vituo hivyo kuwa ni pamoja na Mtende, Chuo cha Sayansi ya Afya,Chuo cha Hoteli na Utalii, Kampuni ya Zitec itakayojishughulisha na matengenezo ya vifaa hivyo pamoja na Skuli ya Makunduchi.

Nyengine ni Kituo cha PSI, Skuli ya Alraudha, Utaani, Vitongoji, Kengeja, Vikokotoni, Kitope Lumumba, Mchanga Mdogo pamoja na skuli ya Sekondari ya Tumekuja.

Naye Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mh. Ali Juma Shamhuna ameishukuru Klabu ya Rotari ya Seattle Nchini Marekani pamoja na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kwa juhudi wanazochukuwa katika kuimarisha sekta ya elimu hapa Zanzibar.

Balozi Seif katika ziara yake ya mwezi Novemba mwaka jana Mjini Seattle Nchini Marekani alipata fursa ya kukitembelea kituo cha uungaji na matengenezo ya Kompyuta { Inter Connection } cha Rotary Clabu katika mji  huo .

Mkurugenzi wa Kituo hicho Bwana Charles Brennik kupitia Klabu hiyo alitoa tamko na ahadi ya kuisaidia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Kompyuta 2,500 kwa ajili ya maskuli mbali mbali hapa Zanzibar.

Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alitembelea Mradi wa Ujenzi wa Skuli ya msingi, Vyoo pamoja na Tangi la Maji katika Kijiji cha Kiwengwa unaofadhiliwa na Mradi wa Kimataifa wa Give kutoka Nchini Marekani.

Wanafunzi 46 wa vyuo na skuli mbali mbali  za Sekondari kutoka Nchini Marekani wamepiga kambi  kwa zaidi ya wiki moja sasa katika Kijiji cha Kiwengwa wakiendelea na kazi mbali mbali za kujitolea katika ujenzi wa Skuli hiyo.

Kiongozi wa Wanafunzi hao Bwana Criss Backam alimueleza Balozi Seif kwamba wanafunzi hao ni mkupuo wa kwanza katika kuendeleza mradi huo katika awamu ya kwanza ya ujenzi huo iliyoanza mwezi Mei, Juni na kumalizia mwezi wa Septemba.

Bwana Criss alisema awamu ya pili ya wanafunzi hao itaingia mwezi Disemba na kuendelea na ujenzi huo hadi Mwezi Febuari mwakani ambapo alisema taaluma ya matumizi ya chupa za maji iliyobuniwa Nchini Nicaragua Amerika ya Kusini katika ujenzi huo inatumika ili kutunza mazingira ya kijiji hicho.

Akitoa shukrani zake Balozi Seif Ali Iddi ambae pia ni Mbunge wa Jimbo la Kitope aliwapongeza wanafunzi hao kutoka Marekani kwa uamuzi wao waliochukuwa wa kusaidia maendeleo ya Elimu katika Visiwa vya Zanzibar.

Balozi Seif alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inathamini juhudi hizo zenye nia ya kuwakomboa wananchi hasa watoto wa vijijini ambao kwa muda mrefu walikuwa wakikosa fursa muhimu za kielimu kutokana na mazingira yao ya kimaisha.

Wanafunzi hao wa Skuli mbali mbali za Sekondari Nchini Marekani wanatarajiwa kuondoka Zanzibar  kwa kupitia Dar es salaam na Arusha ili kuona sehemu za kihistoria pamoja na  mbuga za Taifa kabla ya kurejea nchini kwao siku ya Ijumaa.

 

Othman Khamis Ame