Na Juma Abdallah Ali

Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa hifadhi ya jamii ZSSF Abdulwakili Haji Hafidh

Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa hifadhi ya jamii ZSSF Abdulwakili Haji Hafidh

Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar ZSSF unatarajia kupunguza mafao ya kinua mgongo kwa wanachama wake wenye mishahara mikubwa baada ya kubainika michango yao hailingani na mafao wanayolipwa.

Mpango huo utawathiri zaidi viongozi walioteuliwa na rais wakiwemo mawaziri wanaoendeleza michago yao ya utumishi kabla ya uteuzi wao wa ngazi ya siasa.

Akizungumza katika uzinduzi wa bodi mpya ya sita ya ZSSF, Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko huo Abdulwakili Haji Hafidh amesema wanachama wa mfuko wanaostaafu wanalipwa mafao makubwa yasiolingana na michango yao hasa wenye mishahara mikubwa.

Amesema mfuko umeandaa mapendekezo ya kuifanyia marekebisho sheria ya mfuko yatakayotoa uwamuzi mgumu wa kupunguza mafao ya wanachama wenye mishahara mikubwa ili kuufanya mfuko huo kuwa endelevu.

‘’Haya tunasema ni maamuzi magumu ya kuyapunguza mafao yale tunayona kwamba mafao yake ni makubwa kuliko hali halisi ya michango yao….hali itakayohatarisha ‘sustainability’ ya mfuko wetu’’.

‘’Wenzetu wenye mishahara ya juu wanapata utakuta michango yao inakuwa midogo kuliko kinua mgongo wanachokipata mfano hai mwenzetu mmoja hapa kati yetu viongozi amechangia kama 60,000,000 lakini ukingalia mafao atakayopta milioni 243’’. Alisisitiza mkurugenzi huyo.

Haji amesema ulipaji wa mafao ya mfuko unaongezeka kila mwaka na hadi kufikia May mwaka huu zaidi ya shilingi Bilioni saba zimelipwa katika mafao mbali mbali na July mwaka huu zitatumika zaidi ya shilingi bilioni Nane yanayopita lengo lililowekwa na mfuko.

Amefahamisha tafiti zilizofanywa mwaka 2002, 2005, 2010, 2012 hadi 2013 wataalamu wametoa mapendekezo ya kufanyiwa marekebisho sheria ya mfuko huo hasa vipengele vya michango.

‘’Kutokana na ‘study’ hizi iko haja ya kufanya marekebisho tumepeleka ‘proposal’ yetu wizarani (Wizaa ya Fedha Zanzibar) na tunafikiria karibuni hivi itajadiliwa katika vikao vya Makatibu wakuu’. Alisema Hafidh.

Kwa mujibu wa Katibu mkuu wizara ya fedha Zanziba Mussa Khamis mapendekezo hayo yatawasilishwa katika kikao cha Baraza la Wawakilishi kinachofuata Octoba mwaka huu.

Aidha Hafidh amesema mfuko huo unaondelea na ujenzi wa mnara wa kumbukumbu ya miaka 50 ya Mapinduzi Zanzibar eneo la Michenzani ikiwa sehemu ya uwekezaji pia unatarajia kujenga hoteli ya kibiashara na maduka makubwa ‘shooping more’ katika eneo hilo.

Amesema mfuko huo pia unatarajia kuwekeza ujenzi wa Dahalia na nyumba za gharama nafuu kwa ushirikiano na kampuni moja ya Afrika Kusini eneo la Tunguu wilaya ya Kati.

Pia mfuko huo unatarajia kuanza ujenzi wa nyumba za kisasa eneo la Mbweni nje kidogo ya mji wa Zanzibar zitakazouzwa kwa wanachama wa mfuko na kuwekeza hisa katika baadhi ya benki ziliopo Zanzibar zenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 148.

Akizindia bodi hiyo waziri wa Fedha Zanzibar Omar Yussuf Mzee amesema michango inayotolewa na mafao wanaliolipwa wanachama wa mfuko huo kwa hivi sasa hauwezi kuendelea kwa miaka ijayo.

Amesema wizara imeandaa rasimu ya sheria ya kubadilisha baadhi ya vifungu na kupemdekeza vingine ili mfuko huo uwe endelevu.

Waziri Mzee amevitaja baadhi ya vifungu hivyo ni mfumo wa uchangiaji na ulipaji wa mafao, kuweka muda wa kuchangia na kunufaika na mafao badala ya miaka mitano ya sasa pamoja na kuongezwa kima cha michango kutoka asilimia tano ya mwanachama na asilimia 10 ya mwajiri.

Amesema ili mfuko huo uwe endelevu amewaomba wajumbe wa baraza la wawakilishi kuunga mkono mapendekezo ya marekebisho ya sheria ya mfuko wa ZSSF iliyotungwa mwaka 1998 yatakapowasilshwa kwa wajumbe hao kujadiiwa.

‘’Leo unachangia kidogo unachukua mafao makubwa tena makubwa mara tano zaidi lakini kwa sababu sheria ndio iliyopo hatuwalaumu wao….sheria inatakiwa irekebishwe itaibadilsha ‘formula’ hii’’. Alisisitiza Mzee.

Aidha Mzee ameitaka bodi hiyo mpya chini ya mwenyekiti wake Dr. Suleiman Rashid Mohammed kuwekeza katika miradi yenye tija ikiwemo ujenzi wa maduka makubwa eneo la Darajani na Michenzani.

Amesema mfuko huo hauna fedha na zilizokuwepo ni za wanachama hivyo uwekezaji wa mairadi hiyo utausaidia mfuko  kuwalipa fedha zao kwa wakati.

‘’ Si vizuri leo mtu anastaafu, utumishi wanampabarua kwamba leo umemaliza muda, ZSSF anakaa miezi sita hajapata ‘Cheque’ mimi ningelifurahi zaidi barua ya kustaafu unapewa mkonowa kulia ‘Cheque’ yako unapewa mkono wa kushoto kwa wakati mmoja’’. Alisema Mzee.

Waziri Mzee pia ameutaka mfuko huo kutekeleza sheria ya ulipaji wa mafao ya uzazi hata kwa kiwango kidogo kutokana na kuwepo idadi kubwa ya wanachama  wanaojifungua, lakini hawapati msaada wowote wa ZSSF pamoja na kuwapatiadhamana ya mikopo wafanyakazi.

Mwenyekiti wa bodi ya mfuko wa ZSSF Dr. Suleiman Rashid Mohammed ameahidi kuyapatia ufumbuzi matatizo yanayoukabili mfuko huo na kuahidi atatumia uzowefu wake wa uwekezaji kusaidia mfuko huo kuwekeza miradi yenye faida.

Amesema chini ya uongozi wake mfuko huo hautaichia serikali kubeba mzigo mkubwa wa mfuko na utajitahidi kulipa mafao ya wanachama kwa wakati.

Mfuko wa ZSSF ulioanzishwa mwaka 1998 hadi sasa una zaidi ya wanachama 70,000 na mali ya kiasi ya shilingi bilioni 150 na kulipa mafao yanayokadiriwa kufikia shilingi bilioni saba hadi kufikia May mwaka huu.

Advertisements