imagesPemba. Watu 19 wakazi wa Kijiji cha Sizini Wilaya ya Micheweni wamelazwa hospitali ya wilaya hiyo baada ya kula samaki aina ya puju ambaye anadhaniwa kuwa na sumu.

Akizungumza kwa simu jana, Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo, Rashid Daud Mkasha alisema wagonjwa hao walifikishwa jana na kwamba wanaendelea vizuri na baadhi yao wameruhusiwa kurudi majumbani.

Alisema watu hao ambao hufuturu kwa pamoja, walipata samaki huyo mkubwa na kukatiana vipande na kupika lakini baadaye usiku walianza kuharisha na kulazimika kwenda hospitalini.

Aliwataka wananchi kuwa waangalifu wanapopata vitoweo vya kuokota kwa kuwa vinaweza vikawasababishia maradhi na hata kifo.

Alisema kati ya watu hao, sita ni wa familia moja ambao ni Salama Ali Said (50) na watoto wake Zainab Hamad Abdallah (25), Amin Hamad Abdallah (16), wajukuu zake Ashura Abdallah Hamad (25), Amour Abdallah Hamad (7) na Fatma Abdallah Hamad (12).

Wengine ni Hakika Nassor Ali (45), Biumbe Athman Makame (45), Ali Omar Abdallah (18), Zainab Ali (30), Hidaya Khamis Ali (20), Hadija Khamis Ali (22), Salama Abdallah Hamad (35), Asha Kombo Bakar (50), Ali Hamad Yusouf (60), Bizume Mbarouk Juma (38), Ali Hamad (18) na Hamad Muhsin Hamad (15)

Alisema wagonjwa wanne kati yao ndio wameathirika zaidi na sumu hiyo ambao hadi sasa wako katika uangalizi wa hali ya juu wa madaktari.

Matukio kama hayo katika kisiwa cha Pemba yamekuwa yakitokea mara kwa mara wakiwamo waliopoteza maisha kwa kula kasa aliyekuwa na sumu.

Advertisements