fb8d02567119aefc7251055a5ad40298_LBunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limeazimia kuwajibishwa kwa mawaziri Profesa Sospeter Muhongo, Profesa Anna Tibaijuka na Mwanasheria Mkuu wa Serikali Jaji Frederick Werema, kutokana na sakata la uchotaji wa fedha katika akaunti ya Tegeta Escrow, iliyokuwa Benki Kuu (BoT) kwa kutaka mamlaka ya uteuzi kutengua uteuzi wao. Mbali na hao, yumo Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi na Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco). Aidha, Waziri Mkuu wa nchi hiyo Mizengo Pinda ameahidi kuwa Serikali itatekeleza maazimio yote manane yaliyopitishwa jana jioni na Bunge baada ya mjadala mkali wa siku tatu na mvutano wa siku moja juzi, katika kupitisha maamuzi hayo ambayo yalifikiwa kwa maridhiano. Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe alisoma maazimio hayo manane jana bungeni baada ya kufikiwa kwa maridhiano kati ya Kamati yake, Kambi ya Upinzani, Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Serikali. Maazimio katika azimio la pili, Zitto alisema viongozi hao wa umma na maofisa wa ngazi za juu serikali wanapaswa kuwajibika kwa sababu wamehusishwa na vitendo vya kijinai katika sakata hilo, linalohusisha kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania (IPTL).

Advertisements