Rais Mstaafu wa Tanzania Ali Hassan Mwinyi

Rais Mstaafu wa Tanzania Ali Hassan Mwinyi

Rais mstaafu wa Awamu ya Pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi amevunja ukimya kuhusu namna mchakato wa kumpata mgombea urais wa CCM, ulivyokuwa mkoani Dodoma mpaka akapatikana Dk John Magufuli.

Mwinyi ambaye ni mwanachama wa Baraza la Wazee la CCM, lenye mamlaka na ushawishi katika vikao vyote vya juu vya chama hicho, alizungumzia mchakato huo jana alipokuwa akitoa salamu za Sikukuu ya Idd, baada ya kumaliza swala katika viwanja vya Mnazi Mmoja, jijini Dar es Salaam.

“Mambo yalikuwa magumu kidogo kule Dodoma, lakini tunashukuru Mwenyezi Mungu jahazi lilifika salama, kwa pamoja tuendelee kuwa watulivu hadi Uchaguzi Mkuu utakapofika na tuilinde amani,” alisema Mzee Mwinyi.

Mzee Mwinyi alimshukuru Mungu akisema japo mambo yalikuwa magumu wakati wa mchakato wa kumtafuta mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi, suala hilo lilimalizika salama bila kuwepo kwa tatizo lolote. Alisema uchaguzi mkuu utakapofika mwezi Oktoba, Watanzania wanapaswa kuchagua viongozi wazuri watakaoleta amani, mapatano na maendeleo.

Alitaka Watanzania waachane na fikra za kibaguzi kwani hakuna aliye bora kuliko binadamu mwingine hapa duniani, huku akishauri waumini wa dini zote kuombea Taifa lipite salama katika uchaguzi huo

Advertisements