Archive for April, 2016

WATU WANNE WAFARIKI PAPO HAPO NA WENGINE 29 WAMEJERUHIWA KATIKA AJALI YA GARI ILIYOTOKEA MKOANI MBEYA

Watu wanne wamekufa papo  hapo na wengine 29 kujeruhiwa baada ya basi la HBS linalodaiwa kuwa ni mali ya kampuni ya Sabena walilokuwa wakisafiria kutoka jijini Mbeya kwenda Tabora kuacha njia na kupinduka katika eneo la maji mazuri, barabara kuu ya Mbeya – Chunya wilayani Mbeya.

Basi hilo likiwa limebeba abiria wengi kuliko uwezo wake, lilianza safari yake ya kuelekea Tabora likitokea jijini Mbeya, lakini inadaiwa kuwa likiwa kwenye mtelemko na kona kali za mlima Mbeya likafeli breki na ndipo dereva wake akaamua kuruka na kuliacha likijiendesha lenyewe hali ambayo ilisababisha lipoteze mwelekeo na kuanguka mtaroni.
Muuguzi wa zamu katika hospitali ya rufaa ya kanda ya nyanda za juu kusini, Jesca Kahangwa amethibitisha kupokea miili ya watu wanne na majeruhi 29 wa ajali hiyo, huku akidai kuwa hali za majeruhi wengi bado ni mbaya.
Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa wa Mbeya, Amos Makalla amewahi katika eneo la ajali na baada ya kupata maelezo ya chanzo cha ajali hiyo, akaliagiza jeshi la polisi kuwatafuta na kuwakamata haraka dereva, kondakta na mmiliki wa gari hilo kwa kosa la kuendesha gari bovu barabarani.

MAGUFULI AIVUNJA BODI YA TCRA

BODIRais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ameivunja Bodi ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na kumsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo Dkt. Ally Yahaya Simba kutokana na kutosimamia ipasavyo Mkataba wa utekelezaji wa mfumo wa usimamizi wa mawasiliano ya simu (TTMS), na kusababisha nchi kupoteza mapato ya takriban shilingi bilioni 400 kwa mwaka.

Rais Magufuli amechukua hatua hiyo leo tarehe 26 Aprili, 2016 Ikulu Jijini Dar es salaam baada ya kufanya kikao cha kazi kati yake na viongozi na wataalamu kutoka Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Wizara ya fedha na Mipango na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).

Tarehe 22 Machi, 2013 Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA) iliingia mkataba na kampuni ya SGS juu ya uwekaji, uendeshaji na uhamishaji wa mapato ya simu ambapo kampuni hiyo ilipaswa kutekeleza vipengele vitano lakini mpaka sasa kampuni ya SGS haijaanza kutekeleza kipengele kidogo kinachohusiana na uthibiti wa mapato ya simu za ndani (Offnet), hali ambayo imesababisha serikali kukosa mapato yanayokadiriwa kuwa shilingi bilioni 400 kwa mwaka.

Pamoja na kuivunja bodi ya TCRA inayoongozwa na Profesa Haji Semboja na Kumsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa TCRA Dkt. Ally Yahaya Simba, Rais Magufuli pia amemuagiza Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa Mnyaa kumteua Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo mara moja.

Aidha, Rais Magufuli amewataka Waziri Prof. Mbarawa, Katibu Mkuu na Naibu Katibu katika wizara hiyo kuchukua hatua mara moja ili mfumo wa ukusanyaji wa mapato ya simu kwa simu za ndani (Offnet) uanze kufanya kazi, na nchi ipate mapato yanayostahili kukusanywa.

“Waziri hakikisha unachukua hatua mara moja, nataka tukusanye mapato yote ya serikali yanayostahili na sitasita kuchukua hatua  dhidi ya yoyote atakayekwamisha jambo hili” Amesisitiza Rais Magufuli.

Gerson Msigwa

Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
26 Aprili, 2016

LUCY KIBAKI AFARIKI

Image captionLucy kibaki na mkewe wakati wa kampeni za uchaguzi mwaka 2007

Mke wa kwanza wa rais Lucy Kibaki amefariki katika hospitali mmoja mjini London kwa ugonjwa usiojulikana.

Lucy alipata umaarufu kwa kumchapa kofi mpiga picha mmoja mwaka 2005 wakati alipovamia afisi za kituo kimoja cha habari mwaka 2005 akikasirishwa na vile habari moja ilivyoandikwa.

Katika kumbukumbu ya kumuhenzi bi Kibaki rais wa Kewnya Uhuru Kenyatta alimsifu kwa jukumu lake kukabiliana na ugonjwa wa ukimwi nchini Kenya.

Image captionLucy Kibaki pamoja na aliyekuwa mke wa aliyekuwa rais wa Marekani George Bush ,Laura Bush.Picha kwa niaba ya Getty Images

Bwana Kenyatta alimrithi mumewe bwana Kibaki ambaye alitawala kutoka mwaka 2002 hadi 2013.

Bi Kibaki aliyezaliwa mwaka 1940,alijiondoa katika maisha ya hadharani wakati wa mwisho wa utawala wa mumewe.

Image captionLucy Kibaki na mumewe Mwai KIbaki wakiwapungia mkono wafuasi wao mda mchache baada ya kibaki kuwasilisha stakhabadhi zake za uchaguzi katika tume ya uchaguzi mwaka 2007.Picha ni kwa niaba ya Getty images

Mara ya mwisho kuonekana hadharani ni mwezi Agosti mwaka 2010,wakati alipofurahishwa na kupatikana kwa katiba mpya.

Image captionLucy Kibaki na mumewe aliyekuwa rais wa Kenya Mwai Kibaki pamoja na mkewe marehemu Kijana Wamalwa wakati wa misa ya kifo cha Wamalwa.Picha kwa niaba ya Getty Images

Bwana Kenyatta alisema kuwa alikuwa mgonjwa kwa kipindi cha mwezi mmoja uliopita ambapo amekuwa akipata matibabu nchini Kenya na Uingereza.Bi Kibaki ni mwalimu ambaye aliwacha kazi yake kabla ya ndoa yake na kibaki mwaka 1962 ili kuwalea wanawe

WANAFUNZI WA OPEN UNIVERSITY KITUO CHA ZANZIBAR WAPEWA DOZI

Kulia ni mmiliki wa Zanziar Islamic News Blog akiwa na wanafunzi wenzake wa chuo kikuu huria wakijadili ana na mhadhiri wa chuo hicho Dr. Hamza Kondo wakiwa zanzibar

Kulia ni mmiliki wa Zanziar Islamic News Blog akiwa na wanafunzi wenzake wa chuo kikuu huria wakijadili ana na mhadhiri wa chuo hicho Dr. Hamza Kondo wakiwa zanzibar

MMILIKI WA ZANZIBAR ISLAMIC NEWS BLOG

Kushoto ni mmiliki wa Blog ya Zanziar Islamic News akikaguliwa na Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria Dr. Hamza Kondo wakati akiwa katika mafunzo ya vitendo Zenji Fm radio Zanzibar

Kushoto ni mmiliki wa Blog ya Zanziar Islamic News akikaguliwa na Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria Dr. Hamza Kondo wakati akiwa katika mafunzo ya vitendo Zenji Fm radio Zanzibar

Marais kuamua kuhusu bomba la mafuta Kampala

MagufuliImage copyrightStatehouse Tanzania
Image captionRais Magufuli na Rais Museveni waliafikiana kuhusu ujenzi wa bomba kutoka Uganda hadi Tanga

Viongozi wa Kenya, Uganda na Tanzania mwishoni mwa wiki wanatarajiwa kutoa uamuzi wa mwisho kuhusu ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Uganda na Kenya hadi pwani.

Mwaka jana, Kenya na Uganda zilikuwa zinashauriana kuhusu mpango wa kujenga bomba la kusafirisha mafuta kutoka Hoima, magharibi mwa Uganda, hadi bandari ya Lamu katika Pwani ya Kenya.

Bomba hilo la mafuta lilikusudiwa kutumiwa kusafirisha mafuta ghafi kutoka eneo la Ziwa Albert nchini Uganda na kutoka eneo lenye mafuta Kenya la Lokichar.

Rais Uhuru Kenyatta na Rais Yoweri Museveni walikutana nchini Uganda Agosti mwaka jana na kuafikiana kwamba ujenzi wa bomba hilo ulifaa kuharakishwa.

Lakini Rais wa Tanzania Dkt John Magufuli alikutana na Rais Museveni Machi mwaka huu na wawili hao wakakubaliana kuhusu mpango wa kujengwa kwa bomba la kusafirisha mafuta kutoka Uganda hadi bandari ya Tanga katika pwani ya Tanzania.

Baadaye, Rais Magufuli alikutana na makamu wa rais wa kampuni ya Total Afrika Mashariki Bw Javier Rielo na wakaafikiana kwamba ujenzi wa bomba hilo linalokadiriwa kuwa la urefu wa kilomita 1,410 uanze haraka iwezekanavyo.

Kampuni ya mafuta ya Total ndiyo inayofadhili ujenzi huo.

Bw Javier alisema kampuni yake inatarajia kutumia dola za kimarekani karibu bilioni 4 ambazo tayari zimeshaandaliwa.

Hatua ya Tanzania kuafikiana na Uganda ilionekana kwenda kinyume na mpango wa Kenya na Uganda kujenga bomba la pamoja na siku chache baadaye Rais Kenyatta alimwalika Rais Museveni kwa mazungumzo jijini Nairobi.

Lakini wawili hao hawakuafikiana kwenye mkutano huo uliofanyika 21 Machi na badala yake iliafikiwa kwamba kuundwe kundi la wataalamu kutoka Kenya, Tanzania na Uganda kufanya utathmini wa njia mbalimbali ambazo zinaweza kutumiwa kufanikisha ujenzi wa bomba hilo na kuamua ni gani ifaayo zaidi kwa kuzingatia gharama, changamoto katika ujenzi, miundo mbinu iliyopo na inayojengwa, hazina ya mafuta iliyogunduliwa na uwezo wa bandari za Lamu, Mombasa na Tanga.

MuseveniImage copyrightUhuru Kenyatta Facebook
Image captionRais Museveni alikutana na Rais Kenyatta baadaye Nairobi

Mkutano mwingine wa viongozi hao wawili ulipangiwa kufanyika mjini Kampala baada ya wiki mbili lakini hilo halikufanyika.

Mkutano wa sasa unafanyika kama sehemu ya muungano wa maendeleo wa kaskazini kuhusu miundo mbinu ambao unashirikisha Rwanda, Kenya, Sudan Kusini na Uganda. Nchi za Burundi na Tanzania pia zimealikwa.

Mawaziri wa kawi wa nchi zote tatu wamekuwa wakikutana Kampala wiki hii na ripoti katika vyombo vya habari zinaonesha huenda Uganda na Tanzania zimeafikiana kuendelea na bomba la kutoka Hoima hadi Tanga.

Makadirio ya urefu wa bomba

  • Kenya upande wa Kaskazini: Hoima, Lokichar, Lamu (1,476 km)
  • Kenya upande wa Kusini: Hoima, Nakuru, Mombasa (1,256 km). Bomba jingine likitoka Lokichar hadi Nakuru (288km)
  • Tanga kwa Pamoja: Lokichar, Hoima, Tanga (2,028 km)
  • Tanga (Uganda na Tanzania pekee): Hoima, Tanga (1,443 km)
  • Kenya Pekee: Lokichar, Lamu (891 km)

Waziri wa kawi wa Tanzania Prof Sospeter Muhongo amenukuliwa na gazeti la serikali la Tanzania la Daily News akisema kwamba Uganda imeamua bandari ya Tanga ndiyo ifaayo.

“Sisi (mawaziri) tumeidhinisha mapendekezo ya kamati za kiufundi yanayopendelea bandari ya Tanga. Hatua inayofuata sasa ni kuwafahamisha Viongozi wa Nchi kwa hatua zaidi,” Prof Muhongo amenukuliwa na gazeti hilo.

Gazeti la Daily Nation la Kenya, likinukuu duru kutoka mkutano unaoendelea Kampala, limesema huenda Kenya ikaamua kujenga bomba lake kivyake baada ya kushindwa kushawishi Tanzania na Uganda zikubali bomba la pamoja lipitie Kenya.

Chanzo BBC

BARABARA YA KWANZA YA JUU KUJENGWA DAR-ES-SALAAM

Image captionMradi wa ujenzi ukizinduliwa

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ameweka jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa barabara ya juu (Flyover) katika makutano ya barabara ya Nyerere na Mandela, eneo la Tazara Jijini Dar es salaam ambayo inatarajiwa kukamilika ifikapo Oktoba 2018.

Sherehe ya uzinduzi wa mradi huo imefanyika kando ya eneo la makutano ya barabara ya Nyerere na Mandela Jijini Dar es salaam, ambapo pamoja na Rais Magufuli aliyeongozana na Mkewe Mama Janeth Magufuli, imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Mawaziri, Wabunge, Mameya wa Jiji la Dar es salaam na Balozi wa Japan hapa nchini Mheshimiwa Masaharu Yoshida.

Barabara hiyo ya juu itakuwa ya kwanza kujengwa hapa nchini na ujenzi wake umepangwa kugharimu takribani shilingi Bilioni 100 ambapo kati ya fedha hizo shilingi Bilioni 93.44 zitatolewa na Japan kupitia Shirika lake la Ushirikiano wa Kimataifa (JICA), na Serikali ya Tanzania itatoa shilingi Bilioni 8.3.

Barabara ya juu itakayojengwa itakuwa na njia nne na urefu wa mita 300 kutokea maeneo ya katikati ya Jiji la Dar es salaam kuelekea uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, na inatarajiwa kupunguza kero ya msongamano wa magari yaendayo na yatokayo Uwanja wa ndege na Bandari ya Dar es salaam.

Akizungumza kabla ya kuweka jiwe la msingi la mradi huo, Rais Dkt. John Pombe Magufuli amesema barabara hiyo inajengwa ikiwa ni utekelezaji wa ahadi ya serikali yake ya kumaliza tatizo la msongamano wa magari Jijini Dar es salaam, ambao kwa mwaka 2013 pekee utafiti umeonesha ulisababisha upotevu wa shilingi Bilioni 411.55

Rais Magufuli amebainisha juhudi nyingine za kukabiliana na msongamano wa magari Jijini Dar es salaam kuwa ni pamoja na kujenga barabara ya njia sita ya Dar es salaam hadi Chalinze ambayo itakuwa na Flyover tano, ujenzi wa barabara nyingine za juu katika makutano ya barabara za Nelson Mandela, Morogoro na Sam Nojuma eneo la Ubungo na ujenzi wa daraja jipya la Salander lenye urefu wa kilometa 6.23 kuanzia Coco Beach hadi hospitali ya Agha Khan.

Juhudi nyingine ni ujenzi wa awamu ya pili wa miundombinu ya mabasi yaendayo haraka katika barabara za Kilwa, Chang’ombe na Kawawa, na ujenzi wa awamu ya tatu wa miundombinu ya mabasi yaendayo haraka katika barabara za Nyerere – Gongo la Mboto na Uhuru – Azikiwe.

Aidha, Rais Magufuli amezungumzia awamu ya kwanza ya mradi wa mabasi yaendayo haraka, kuwa serikali yake imelazimika kusimamisha kuanza kwa huduma hiyo baada ya kubaini dosari katika mkataba wa mradi ambazo zingesababisha serikali kupoteza fedha nyingi na wananchi kutwishwa mzigo mzito wa viwango vikubwa vya nauli, na amewahakikishia wananchi wa Dar es salaam kuwa mabasi hayo yataanza kutoa huduma hivi karibuni baada ya kurekebisha kasoro zilizobainika.

Dkt. Magufuli pia amezungumzia usafi wa Jiji la Dar es salaam kwa kuwataka viongozi wa Manispaa zote za Jiji, kuhakikisha wanatafuta namna ya kudhibiti utupaji hovyo wa takataka ikiwemo kutoza faini kubwa kwa watakaokamatwa wakitupa takataka hovyo.