kip

HALI YA KUPINDUPINDU ZANZIBAR

UTANGULIZI

Tangu mwezi wa Septemba mwaka jana, Mripuko wa Kipindupindu bado unaendelea kuvikumba visiwa vya Unguja na Pemba. Hadi kufikia sasa jumla ya wagonjwa 2391 wameshalazwa katika vituo 17 vya matibabu vilivyokwisha funguliwa Unguja na Pemba. Wagonjwa 1363 kati ya hao wamelazwa katika vituo 7 vya Unguja na wagonjwa 1028 wamelazwa katika vituo 10 vya Pemba. Jumla ya vifo 23 vimeripotiwa katika kipindi hicho, 19 vilitokea Unguja na 10 vilitokea Pemba.

Vituo vya matibabu vilivyofunguliwa kwa Unguja ni Chumbuni, Uzi, Muungoni, Uroa, Ukongoroni, Fujoni na Gamba; na kwa upande wa Pemba ni Wete, Kojani, Mjinikiuyu, Micheweni, Makangale, Maziwang’ombe, Kiuyumbuyuni, Chakechake, Mkoani, na Vitongoji. Kambi mbili za Chumbuni na Gamba ndizo zinazoendelea kupokea wagonjwa kwa sasa na 15 zilizobaki zimeshafungwa baada ya kutokua na wagonjwa, zikiwemo kambi zote 10 za Pemba na 5 za Unguja

IDADI YA WAGONJWA KWA WIKI

Wastani wa wagonjwa 10 hadi 25 walikua wakipokelewa kwa siku na 80 hadi 120 kwa wiki katika wiki mbili (2) zilizopita. Hata hivyo idadi hii imeonekana kupungua kidogo katika wiki hii iliyoishia Jumatatu ya tarehe 4/4/2016 ambapo wastani wagonjwa sita (6) hadi 12 wamekua wakipokewa kwa siku na 73 walipokelwa kwa wiki. Kitakwimu, upungufu huu bado hautoi dalili ya kupungua kwa mripuko kwani kuna kila dalili za kuendelea kwa kasi kwa maambukizo katika maeneo mbalimbali.

Kati ya wagonjwa 73 waliolazwa wiki hii wagonjwa 62 walilazwa chumbuni, wanene (8) kituo cha Gamba na watatu (3) Kituo cha Fujoni, ambapo 42 kati yao walikua wanaume na 31 wanawake. Asilimia 15 kati ya wagonjwa wote walikua watoto chini ya miaka mitano (5)

Wilaya za Maghribi A na B Unguja ndizo zilizoongoza kwa kutoa wagonjwa wengi zaidi katika wiki 2 za hivi karibuni. Asilimia 62 ya wagonjwa wote walitokea wilaya za Maghribi A na B hasa maeneo ya Mtoni, Mtoni kidatu, Mtopepo, Fuoni na Mwera; ikifuatiwa na wilaya ya Mjini asilimia 29 hasa maeneo ya Malindi, Jangombe, Makadara Amani na Kidongechekundu; Wilaya ya Kaskazini A asilimia 12 kutoka maeneo ya Mkokotoni, Pwanimchangani, Kandwi, Matemwe na Kidoti Mvuleni; wilaya ya Kaskazini B asilimia 4 kutoka maeneo ya Bumbwini misufini, Mahonda na Fujoni; na wilaya ya Kati asilimia 2 kutoka maeneo ya Mwera, Kidimni na Koani. Wilaya ya Kusini haikutoa wagonjwa katika kipindi hicho mbali na wagonjwa watatu (3) wa kuharisha kutoka uzi na Kitogani ambao hawakuthibitishwa kuwa na Kipindupindu.

Mbali na mvua ndogondogo zinazoendelea katika kipindi hiki, sababu kuu zilizopelekea ongezeko hili la wagonjwa ni wananchi kutokufata maelekezo yanayotolewa na wataalam wa Afya juu ya kujikinga na Maradhi ya Kipindupindu. Wananchi wengi bado wanaendelea na tabia hatarishi zinazopelekea maradhi ya kuharisha ikiwemo kutokuchemsha maji ya kunywa, kutonawa mikono kwa maji na sabuni wakati wa kula na kutoka chooni, kutokutumia vyoo ipasavyo, kutupa ovyo kinyesi na penpa pamoja na kuongezeka uchafu katika mazingira tunayoishi na wafanyabiashara wa chakula kutokufuata masharti ya usafi na usalama wa chakula katika biashara zao.

WITO KWA WANANCHI

Kipindupindu ni ugonjwa unaoweza kuepukwa kirahisi iwapo kila mtu atazingatia masharti ya kiafya yanayotolewa kila siku na wataalam wetu wa Afya. Kila mmoja kati yetu ana jukumu katika kupambana na maradhi haya yanayoendelea kuathiri afya na maisha yetu kila siku. Taasisi zote za kiserikali za kiraia zikiwemo kamati za shehia, vikundi vya kijamii na mashirika mbalimbali zinatakiwa kutoa mchaongo wao wa hali na mali katika jitihada za kupambana na maradhi haya.

Kipindupindu kinaweza kuepukwa iwapo tu kila mmoja wetu atazingatia masharti ya kiafya katika kuhifadhi mazingira na usalama wa chakula na maji kwa kufanya yafuatayo:

  1. Kunywa maji safi na salama kwa kuyachemsha au kutia dawa.
  2. Kuwa waangalifu na vyakula unavyokula: Ni vyema kula vyakula vyenye uvuguvugu, matunda na mboga za majani zioshwe vizuri kwa maji ya mtiririko.
  3. Kutumia choo wakati wa kujisaidia muda wote
  4. Kuhifadhi kinyesi kwa usalama ikiwemo kinyesi cha watoto, penpas na kadhalika na kuweka choo na msalani safi muda wote.
  5. Kuosha mikono kwa maji yenye kutiririka na sabuni baada ya kutoka msalani, baada ya kumsafisha mtoto aliyejisaidia, kabla ya kumlisha na kumnyonyesha mtoto, kabla ya kutayarisha, kabla ya kupika na wakati wa kula.
  6. Kwa mgonjwa anaeharisha na kutapika anatakiwa kupelekwa haraka kituoni huku akipewa maji kwa wingi ili kurejesha maji yaliyopotea.
  7. Kuweka mazingira yetu safi kila wakati ikiwemo kusafisha majaa, kutochafua mito na mitari ya maji,

 

KUMBUKA: KIPINDUPINDU KINAZUILIKA, CHUKUA TAHADHARI ILI KUJIKINGA WEWE, FAMILIA NA JAMII INAYOKUZUNGUKA, KWANI KINGA NI BORA NA RAHISI KULIKO TIBA.

Advertisements