MagufuliImage copyrightStatehouse Tanzania
Image captionRais Magufuli na Rais Museveni waliafikiana kuhusu ujenzi wa bomba kutoka Uganda hadi Tanga

Viongozi wa Kenya, Uganda na Tanzania mwishoni mwa wiki wanatarajiwa kutoa uamuzi wa mwisho kuhusu ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Uganda na Kenya hadi pwani.

Mwaka jana, Kenya na Uganda zilikuwa zinashauriana kuhusu mpango wa kujenga bomba la kusafirisha mafuta kutoka Hoima, magharibi mwa Uganda, hadi bandari ya Lamu katika Pwani ya Kenya.

Bomba hilo la mafuta lilikusudiwa kutumiwa kusafirisha mafuta ghafi kutoka eneo la Ziwa Albert nchini Uganda na kutoka eneo lenye mafuta Kenya la Lokichar.

Rais Uhuru Kenyatta na Rais Yoweri Museveni walikutana nchini Uganda Agosti mwaka jana na kuafikiana kwamba ujenzi wa bomba hilo ulifaa kuharakishwa.

Lakini Rais wa Tanzania Dkt John Magufuli alikutana na Rais Museveni Machi mwaka huu na wawili hao wakakubaliana kuhusu mpango wa kujengwa kwa bomba la kusafirisha mafuta kutoka Uganda hadi bandari ya Tanga katika pwani ya Tanzania.

Baadaye, Rais Magufuli alikutana na makamu wa rais wa kampuni ya Total Afrika Mashariki Bw Javier Rielo na wakaafikiana kwamba ujenzi wa bomba hilo linalokadiriwa kuwa la urefu wa kilomita 1,410 uanze haraka iwezekanavyo.

Kampuni ya mafuta ya Total ndiyo inayofadhili ujenzi huo.

Bw Javier alisema kampuni yake inatarajia kutumia dola za kimarekani karibu bilioni 4 ambazo tayari zimeshaandaliwa.

Hatua ya Tanzania kuafikiana na Uganda ilionekana kwenda kinyume na mpango wa Kenya na Uganda kujenga bomba la pamoja na siku chache baadaye Rais Kenyatta alimwalika Rais Museveni kwa mazungumzo jijini Nairobi.

Lakini wawili hao hawakuafikiana kwenye mkutano huo uliofanyika 21 Machi na badala yake iliafikiwa kwamba kuundwe kundi la wataalamu kutoka Kenya, Tanzania na Uganda kufanya utathmini wa njia mbalimbali ambazo zinaweza kutumiwa kufanikisha ujenzi wa bomba hilo na kuamua ni gani ifaayo zaidi kwa kuzingatia gharama, changamoto katika ujenzi, miundo mbinu iliyopo na inayojengwa, hazina ya mafuta iliyogunduliwa na uwezo wa bandari za Lamu, Mombasa na Tanga.

MuseveniImage copyrightUhuru Kenyatta Facebook
Image captionRais Museveni alikutana na Rais Kenyatta baadaye Nairobi

Mkutano mwingine wa viongozi hao wawili ulipangiwa kufanyika mjini Kampala baada ya wiki mbili lakini hilo halikufanyika.

Mkutano wa sasa unafanyika kama sehemu ya muungano wa maendeleo wa kaskazini kuhusu miundo mbinu ambao unashirikisha Rwanda, Kenya, Sudan Kusini na Uganda. Nchi za Burundi na Tanzania pia zimealikwa.

Mawaziri wa kawi wa nchi zote tatu wamekuwa wakikutana Kampala wiki hii na ripoti katika vyombo vya habari zinaonesha huenda Uganda na Tanzania zimeafikiana kuendelea na bomba la kutoka Hoima hadi Tanga.

Makadirio ya urefu wa bomba

  • Kenya upande wa Kaskazini: Hoima, Lokichar, Lamu (1,476 km)
  • Kenya upande wa Kusini: Hoima, Nakuru, Mombasa (1,256 km). Bomba jingine likitoka Lokichar hadi Nakuru (288km)
  • Tanga kwa Pamoja: Lokichar, Hoima, Tanga (2,028 km)
  • Tanga (Uganda na Tanzania pekee): Hoima, Tanga (1,443 km)
  • Kenya Pekee: Lokichar, Lamu (891 km)

Waziri wa kawi wa Tanzania Prof Sospeter Muhongo amenukuliwa na gazeti la serikali la Tanzania la Daily News akisema kwamba Uganda imeamua bandari ya Tanga ndiyo ifaayo.

“Sisi (mawaziri) tumeidhinisha mapendekezo ya kamati za kiufundi yanayopendelea bandari ya Tanga. Hatua inayofuata sasa ni kuwafahamisha Viongozi wa Nchi kwa hatua zaidi,” Prof Muhongo amenukuliwa na gazeti hilo.

Gazeti la Daily Nation la Kenya, likinukuu duru kutoka mkutano unaoendelea Kampala, limesema huenda Kenya ikaamua kujenga bomba lake kivyake baada ya kushindwa kushawishi Tanzania na Uganda zikubali bomba la pamoja lipitie Kenya.

Chanzo BBC

Advertisements