Archive for July, 2016

Rais wa Zanzibar Dk Shein, Akutana na Ujumbe wa Kampuni ya Huawei Ikulu Zanzibar

H 1Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, amefanya uteuzi wa viongozi katika taasisi mbali mbali za serikali.

Wateule hao ni Dk. Juma Yakout Juma kuwa naibu Katibu Msaidizi wa Baraza la Mapinduzi na Mwadini Makame Haji kuwa Mkurugenzi Mipango, Sera na Utafiti katika Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.
Katika Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala bora, walioteuliwa ni Abdulla Issa Mgongo kuwa Mkurugenzi Mipango, Sera na Utafiti na Shaibu Ally Mwazema kuwa Mkurugenzi wa Miundombinu ya Taasisi, Utumishi na Maslahi ya watumishi.
Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara maalum za SMZ, Khalid Omar Abdulla anakuwa Mkurugenzi Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa wakati Mashaka Hassan Mwita ameteuliwa kuwa Katibu Tawala Wilaya ya Magharibi A.

Katika Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais,  Issa mlingoti Ally anakuwa Mratibu Mkuu wa Ofisi ya Uratibu wa Shughuli za SMZ Dar es salaam, Ameir Makame Ussi, Mkurugenzi Idara ya Mipango, Sera na Utafiti na Khalid Bakari Amran, Mkurugenzi Idara ya Uratibu wa Shughuli za Serikali.

Wengine ni Riziki Daniel Yussuf aliyeteuliwa kuwa Mkurugenzi Idara ya Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa huku Ali Salim Matta akipewa nafasi ya Ofisa Mdhamini Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Pemba.

Wizara ya Afya walioteuliwa ni Ramadhan Khamis Juma kuwa Mkurugenzi Mipango, Sera na Utafiti na Ofisa Mdhamini Pemba ni Ali Bakari Ali.
Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi, Haji Hamid Saleh anakuwa Mkurugenzi Umwagiliaji Maji.

Wizara ya Habari, Utalii, Utamaduni na Michezo, ni Dk. Omar Abdulla Adam anakuwa Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa, Sensa ya Filamu na Utamaduni.

Katika  Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji, walioteuliwa ni Abdulla Mwinyigogo kuwa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba na Ramadhan Mussa Bakari kuwa Mkurugenzi wa Wakala wa Majengo, ambapo  Omar Ali Omar Bhai anakuwa  Mkurugenzi Uendeshaji na Utumishi katika
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali.

Wizara ya Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira, walioteuliwa ni Tahir M. K. Abdulla kuwa Naibu Katibu Mkuu, na Hemed Salim Hemed anakuwa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Kudhibiti Huduma za Maji na Nishati (ZURA).

Nana Mwanjisi ameteuliwa kuwa Mkurugenzi Mipango, Sera na Utafiti katika Wizara ya Biashara, Viwanda na Masoko.

Imetolewa na idara ya habari maelezo-zanzibar
Julai 20,  2016

Kinana atoa Masharti Endapo Rais Magufuli Atamhitaji Aendelee Kuwa Katibu Mkuu wa CCM

kinanaKATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana ametoa neno endapo Rais John Magufuli atamhitaji kuendelea na wadhifa huo, huku akibainisha kuwa amekutana na changamoto nyingi katika nafasi hiyo kiasi kwamba wakati mwingine alikata tamaa.

Mwanasiasa huyo maarufu ndani ya CCM na nchini, anatarajiwa kuhitimisha uongozi wake wiki hii wakati Mwenyekiti mpya wa CCM Taifa, Rais John Magufuli atakapokabidhiwa uenyekiti huo na kuunda Sekretarieti yake mpya ambayo haijulikani kama itaongozwa tena na Kanali huyo wa zamani wa Jesh

Akizungumza jana na waandishi wa habari baada ya kukagua Ukumbi wa Mkutano Maalumu wa CCM utakaofanyika keshokutwa Jumamosi, Kinana ambaye amekuwa katika nafasi hiyo kwa miaka mitatu na nusu, alisema aliombwa katika nafasi hiyo baada ya kuwa aliamua kustaafu, lakini akakumbana na changamoto mbalimbali.
CCM kuwa mbali na wananchi 
Alisema kuna wakati aliona kama vile chama kiliacha kwenda kwa wananchi na kwamba hakikuwa karibu sana nao.
“Ninyi ni mashahidi, ikabidi kubuni utaratibu mzuri wa kwenda kwa wananchi ili chama kiwe karibu na wananchi, kiwasikilize na kuwa sauti ya wananchi kifuatilie matatizo yao kisimamie utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi,” alisema Kinana na kuongeza kuwa katika kufanya hivyo amekuwa akiwasiliana na Rais na Waziri Mkuu kwa ajili ya matatizo kutatuliwa.
 
“Changamoto ya pili ya kuimarisha umoja na mshikamano ndani ya chama, hapo nyuma kulikuwa na misukosuko kidogo ya umoja na mshikamano, kushutumiana na kulaumiana,” alisema na kuongeza kuwa kazi nyingine aliyofanya ni kuimarisha umoja ndani ya chama, kushirikiana na viongozi wenzake kuhakikisha chama kinajitahidi kwa kadri ya uwezo wake kurejea katika misingi yake ya awali katika maeneo ya uadilifu, uwajibikaji na utendaji kazi kwa ufanisi.
Azuiwa ziarani
Kinana alisema amekwenda wilaya zote, majimbo, mikoa na nusu ya kata za nchi na amesafiri zaidi ya kilometa 192,000, kufanya mikutano zaidi ya 3,700 ya aina mbalimbali ya ndani na nje na haikuwa kazi rahisi
 “Changamoto nilizokutana nazo ambazo lazima nikiri ni pale nilipotaka wakati mwingine kufanya ziara kwenye maeneo fulani fulani niliambiwa ni hatarishi siwezi kwenda kwa hiyo ilibidi nibishane na viongozi na watendaji wakuu wa serikali…nikasema hapana nimeamua kwenda lazima niende,” alisema Kinana.
Katibu huyo akitoa mfano alisema kuna wakati aliamua kutoka kwa boti kutoka Nyamisati wilayani Rufiji kwenda Mafia, viongozi wa Mkoa wa Pwani walifikiri si njia salama ya kusafiri na kumpelekea ujumbe asisafiri kwa boti, bali asafiri kwa ndege, lakini alisema hapana ataondoka kwa boti.
“Walichofanya wakakaa kikao cha Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa na wakaniandikia barua rasmi kwamba tunakushauri usisafiri kwa boti safiri kwa ndege kwa maana nyingine walikuwa wanajivua lawama kwa yatakayotokea, lakini vile vile kunitisha kidogo kwamba si salama zaidi nikawasisitiza hapana,” alieleza Kinana.
Ashitakiwa kwa JK
“Baadaye Rais mstaafu Kikwete alikuwa Msoga, viongozi wa Mkoa wa Pwani wakaenda kumwambia tumezungumza na Katibu Mkuu wako naona hasikii tumemuandikia barua ya kumuomba asisafiri na boti hasikii, Rais akaandika meseji ndefu sana…nikamjibu rais nakuheshimu mamlaka yako ni makubwa si vizuri nikakukatalia, lakini niruhusu nikukatalie kwa sababu hata wananchi wanaosafiri kwenye boti hii wanahatarisha maisha yao, ni vizuri na mimi nikahatarisha maisha yangu hata kidogo… akaniambia nimekuelewa endelea,” alibainisha.
Alisema zipo changamoto nyingi sana nyingine, kwa mfano Mbambabay kwenda Kyela, mkuu wa mkoa akamuambia boti haifai kusafiri akasema mara haiwezi kusafiri imeharibika.
“Nikazungumza na Mwakyembe akapeleka mafundi wakatengeneza, safari haikuwa rahisi, lakini changamoto zilikuwa nyingi sana, kwingine Lupingu kule ni gari moja tu ndio inayoshuka chini hakuna kupishana magari nikaambiwa nisiende nikasema nina kwenda,” alisema na kuongeza kuwa kulikuwa na ubishi mwingi wakati mwingine alionekana mtu mmoja kidogo ambaye hasikilizi ushauri sana.
Pia nyingine zinazotokana na changamoto za wananchi kutolipwa mazao yao kwa wakati, mbolea kutofika kwa wakati, halmashauri kutopata fedha za maendeleo kwa wakati, watumishi wa umma wanaohamishwa kwenda vijijini hawaendi vijijini kwenda kuwahudumia wananchi, tatizo kubwa la migogoro kati ya wakulima na wafugaji kati ya wananchi na hifadhi za taifa.
“Ndio maana mnaniona siku hizi nimenyamaza kwa sababu yale yote niliyokuwa nikiyaombea yanafanyika, umangimeza haupo watu wachape kazi wawahudumie wananchi, uadilifu unapigwa vita, rushwa inapigwa vita, uwajibikaji na uadilifu unahimizwa, utendaji kazi unatakiwa na hayo yasipofanyika mtu anaondolewa mara moja,” alifafanua Kinana ambaye kuanzia mwaka 2014 hadi mwanzoni mwa mwaka jana alitembea kote nchini akikisafisha chama chake na kuibana serikali.
Kurejea kwake CCM
“Yalitokea mazingira ambayo niliombwa na viongozi wastaafu na viongozi wa chama kuniomba niwe mtendaji mkuu wa chama chetu. Si nafasi ambayo niliipenda, bali niliitwa na nikakalishwa wakanisihi na mimi nikakubali sababu ni wito na kwa kuwa ni watu ninaowaheshimu na wana dhamana kubwa kwenye nchi yetu, nikakubali kufanya kazi hiyo,” alisema Kinana akizungumzia jinsi alivyoteuliwa kushika nafasi hiyo.
Alisema amekuwepo katika uongozi ndani ya chama kwa muda mrefu (miaka 25) ndani ya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa, na alihisi ni wakati muafaka wa kung’atuka.
“Mwanasiasa mzuri ni yule anayejua wakati wa kuingia na wakati wa kutoka. Ni wakati mzuri wa kung’atuka kuachia waingie wenye umri wa kati na umri wa vijana kuachia waongoze chama na kuwaamini,” alieleza.
Alisema moja ya mambo ambayo walikubaliana wakati ule akajitahidi kukiimarisha chama, kusimamia na kumsaidia mwenyekiti kusimamia mchakato wa kuwapata wagombea kwenye nafasi zote za Urais, Ubunge na Udiwani. Pia alijitahidi kuendesha shughuli za kampeni na uchaguzi na utakamalizika.
 
“Uchaguzi umekwisha niruhusiwe kupumzika, na wote waliafiki na kukubali sasa muda umefika kwa hiyo nimewakumbusha yale tuliyokubaliana muda wake umefika sasa wengine wakaniuliza hivi ndivyo tulivyokubaliana nikawaambia wazee hamjawa wazee kiasi cha kusahau ndio haya tuliyokubaliana,” alieleza.
Akiombwa na JPM
Alipoulizwa kama akiombwa na Rais Magufuli aendelee kwa Katibu Mkuu, Kinana alisema, “Niseme hajasema, hatujazungumza hilo, likitokea tutaangalia, tutakaa naye kikao kama akiniomba, tutakuwa na kikao na mazungumzo muda utakapofika kama nilivyokuwa na mazungumzo na kikao kama kwa wale walioniomba mwaka 2012.”
Waliokisaliti chama
Akizungumzia walioisaliti CCM katika Uchaguzi Mkuu mwaka jana, mtendaji huyo wa CCM alisema msaliti yeyote adhabu yake ni mbaya sana, hata kwenye chama cha siasa.
“Kwenye CCM wapo watu walioyumba, kulikuwa na wimbi kubwa mwaka jana, watu waliyumba hivi kidogo wakakaa mguu upande huku hawapo na kule hawapo, wako ambao sio tu waliyumba, bali walikiuka maadili na hawakushiriki kwenye shughuli za kampeni,” alisema.
Pia alisema wapo ambao hawakushiriki, hawakusaidia na wakasaidia upinzani na kila mtu atakuwa na adhabu yake kulingana na makosa yake.

“Kama mmekuwa mkifuatilia kuna waliochukuliwa hatua ngazi za wilaya na mikoa. Kwa mfano, Shinyanga 123 walichukuliwa hatua. Wapo wanaotakiwa kuchukuliwa hatua kwenye ngazi za juu, sasa jambo moja mtu yeyote kabla ya kuchukuliwa hatua lazima aelezwe mashtaka yake, apewe fursa ya kusikilizwa, kwa hiyo hawa wote watasomewa mashtaka, watasikiliza na kupewa adhabu kwa kadri itakavyostahili, lakini hatua zitachukuliwa mara baada ya Mkutano Mkuu kumalizika,” alieleza

Rais Dk.Shein akutana na Muigizaji Filamu za Kihindi

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akisalimiana na Mkongwe wa Filamu za Kihindi Bw.Kunal Kapoor aliyefuatana na Msimamizi wa Ofisi ya Utalii ya Zanzibar Mumbai,Nchini  India Bw.Jilesh Babla walipofika Ikulu Mjini Zanzibar leo kwa Mazungumzo

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akisalimiana na Mkongwe wa Filamu za Kihindi Bw.Kunal Kapoor aliyefuatana na Msimamizi wa Ofisi ya Utalii ya Zanzibar Mumbai,Nchini India Bw.Jilesh Babla walipofika Ikulu Mjini Zanzibar leo kwa Mazungumzo

Mfanyabiashara Anayedaiwa Kujipatia Milioni 7 Kwa Dakika Afikishwa Mahakamani Na Kusomewa Mashitaka 199

1Mfanyabiashara Mohamed Mustapha (anayeongea na simu) na wenzake, wakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam jana kukabiliana na tuhuma za kuibia Serikali kodi ya Sh milioni 7 kwa kila dakika kwa kipindi kirefu.
**
Hatimaye mfanyabiashara aliyetajwa na Rais John Magufuli kuwa amekuwa akiibia Serikali takriban Sh7 milioni kwa dakika, amepandishwa kizimbani na wenzake wanne na kusomewa mashtaka 199, wote kwa pamoja.

Mfanyabiashara huyo, Mohamed Mustafa Yusufali na wenzake Alloyscious Gonzaga Mandago, Isaac Wilfred Kasanga, Taherali Sujjauddin Taherali na Mohamed Seif Kabla, walipandishwa kizimbani na kusomewa mashtaka hayo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
 Washtakiwa wote kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka ya kughushi, kuwasilisha nyaraka za uongo kwa mamlaka za Serikali, utakatishaji fedha na kuisababishia Serikali hasara ya zaidi ya Sh15 bilioni.
Katika ya mashtaka hayo, Yusufali maarufu kwa majina ya Mohamedali, Choma au Jamalii anakabiliwa na mashtaka 198 yeye peke yake huku wenzake wakikabiliwa shtaka moja la utakatishaji fedha.
Kutokana na wingi wa mashtaka hayo, waendesha mashtaka wawili; Wakili wa Serikali Mwandamizi, Shadrack Kimaro na Wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Leonard Swai walilazimika kubadilishana ili kuwapa muda wa kupumua.
Kutokana na kukabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi na shtaka la kutakatisha fedha, washtakiwa hao hawakutakiwa kujibu lolote kwa sababu mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi hiyo isipokuwa Mahakama Kuu na kulingana na mashtaka yanayowakabili, hayana dhamana.
Baada ya kumaliza kuwasomewa mashtaka hayo, upande wa mashtaka uliieleza Mahakama kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika.
Hivyo, Hakimu Mkazi, Huruma Shahidi anayesikiliza kesi hiyo aliamuru washtakiwa wapelekwe mahabusu hadi Julai 25, kesi hiyo itakapotajwa tena.
Kabla ya kupandishwa kizimbani, Yusufali alitajwa na Rais Magufuli kuwa ana mashine inayotoa risiti za kielektroniki (EFD) nje ya mfumo wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kuzisambaza kwa wafanyabiashara wengine, hivyo kujiingizia Sh7 milioni kwa dakika.
Rais Magufuli alieleza kuwa mtandao wake unawashirikisha watumishi wa TRA na Wakala wa Usajili wa Kampuni (Brela), hivyo kuisababishia Serikali hasara ya mabilioni ya shilingi.
 Katika mashtaka hayo, Yusufali anakabiliwa na mashtaka 181 ya kughushi, mashtaka 15 ya kuwasilisha nyaraka za uongo, udanganyifu katika kulipa kodi moja, shtaka moja la kuisababishia Serikali hasara ya Sh15,645,944,361, huku shtaka moja tu la utakatishaji fedha ndilo likimhusisha na wenzake.
Waendesha mashtaka hao walidai kuwa mfanyabiashara huyo alikuwa akighushi nyaraka za kampuni mbalimbali, kuonyesha kuwa zimesajiliwa na zinaendesha  shughuli zake nchini kihalali wakati akijua siyo kweli.
Pia, walidai kuwa mfanyabiashara huyo alikuwa akiwasilisha nyaraka za uongo TRA.
Kuhusu shtaka la kutakatisha fedha, upande wa mashtaka ulidai kuwa washtakiwa hao kwa pamoja kati ya Machi 2011 na Januari 2016, walitakatisha Sh1,895,88500 kwa kujifanya kuwa ni malipo ya  mikopo waliyoipokea kwa watu mbalimbali.

Upande wa mashtaka ulidai kuwa kati ya Januari 2008 na Januari 2016, mfanyabiashara huyo alifanya udanganyifu katika kuwasilisha kwa Kamishna Mkuu wa TRA taarifa ya uongo ya marejesho ya mapato, hivyo kuikosesha Serikali mapato ya kodi ya VAT zaidi ya Sh15.6 bilioni