Siku moja baada ya mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Edward Lowassa kusema atagombea tena urais katika uchaguzi ujao, CCM imesema inamsubiri na ina uhakika itamshinda tena kwa kuwa tayari ameshachuja na wala sio tishio.

Lowassa aliweka rekodi ya kuwa mgombea wa upinzani aliyepata kura nyingi baada ya kugombea kwa tiketi ya Chadema na kuungwa mkono na vyama vingine vitatu vya upinzani katika Uchaguzi Mkuu uliopita.
Alipata kura milioni 6.07, takriban mara tatu ya kura ambazo wapinzani wamekuwa wakipata katika chaguzinne za awali. Mshindi alikuwa John Magufuli wa CCM aliyepata kura milioni 8.8.
Waziri huyo mkuu wa zamani ametangaza nia ya kusimama tena kugombea urais wakati alipofanya mahojiano na waandishi wa Nation Media Group jijini Nairobi, Kenya ambako alikwenda kuhudhuria mazishi ya aliyekuwa waziri wa mambo ya ndani, lakini CCM imesema asitarajie ushindi.
Alipoulizwa kuhusu tamko la Lowassa, katibu wa itikadi na uenezi wa CCM, Humphrey Polepole alisema mbunge huyo wa zamani wa Monduli si tishio na hayuko katika fikra za chama hicho.
“Katika orodha ya vitu muhimu, Lowassa hatumfikirii kabisa na si tishio hata kidogo,” alisema Polepole ambaye katika uchaguzi uliopita aliapa kuzunguka nchi nzima kumpinga Lowassa.
Polepole alisema kwa sasa chama hicho kimejikita kutekeleza Ilani yake inayotokana na ahadi za wananchi, kama kushughulikia changamoto za uadilifu kwa viongozi ndani ya CCM na Serikali.
“Tunatimiza wajibu wetu vizuri tuliotumwa na Watanzania na kazi inaonekana. Nje ya hapo tunasubiri Watanzania watupatie haki yetu katika uchaguzi ujao, na tumeshajipangia kupata ushindi wa zaidi ya asilimia 70, kwa hiyo hatumfikirii kabisa,” alisema Polepole.
Hata hivyo, jina la Lowassa limekuwa gumzo katika vikao vya chama hicho tawala na alisababisha wajumbe watatu wa Kamati Kuu ya CCM kuchukuliwa hatua, wenyeviti wanne wa mikoa kuvuliwa uongozi na uanachama na wengine kadhaa kuadhibiwa kwa njia tofauti.
Hiyo ilitokana na baadhi kuendelea kumuunga mkono baada ya kujivua uanachama wa CCM na kujiunga upinzani, akiwa Waziri Mkuu wa kwanza kufanya hivyo tangu siasa za ushindani zirejeshwe mwaka 1992.
SOURCE: MPEKUZI
Advertisements