Shirika la Human Rights linasema watu 24 wameuwawa nchini Kenya

Wakenya wakipiga foleni kupiga kura mwaka 2017
Image captionWakenya wakipiga foleni kupiga kura mwaka 2017

Muungano mkuu wa upinzani nchini Kenya, ambao ulishindwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, umeapa kuendelea na maandamano wenye nia ya kubatilisha kile ambacho unasema kuwa, matokeo “feki” ya uchaguzi mkuu.

Seneta James Orengo ameiambia BBC kuwa chama chake, kinachoongozwa na Bwana Raila Odinga, hakitapinga matokeo ya uchaguzi mkuu mahakamani, huku akisema kuwa Uhuru Kenyatta tayari ametoa vitisho kwa majaji..

Tume ya uchaguzi Kenya yatoa fomu za matokeo

Ndovu mkubwa auawa Kenya

Kufikia sasa watu 11 wameuwawa katika ghasia za baada ya uchaguzi mkuu, ambazo zilianza mara tu baada ya Uhuru Kenyatta kushinda kutangazwa mshindi kwa muhula wa pili mnamo usiku wa kuamkia Jumamosi.

Mpinzani wake mkuu Bwana Raila Odinga, amedai kuwa uchaguzi huo ulikubwa na wizi mkubwa wa kura.

Uhuru Kenyatta kushoto) na Mpinzani wake Raila Odinga (kulia)
Image captionUhuru Kenyatta kushoto) na Mpinzani wake Raila Odinga (kulia)

Kaimu Waziri wa usalama wa ndani, Fred Matiangi, amewataja waandamanaji kama “wahalifu”.

Kiongozi mmoja mkuu wa chama cha uipinzani, Bwana Johnson Muthama, amesema kuwa, polisi wanajaribu kuwalazimisha watu “wakubali matokeo hayo.”

Tume ya kutetea haki za kibinadamnu nchini Kenya, imetoa orodha ya juu ya wahasiriwa wa ghasia hizo huku ikisema kuwa ni watu 24 ndio ambao wameuwawa katika visa vinavyohusiwa na uchaguzi huo, huku ikiongeza kuwa polisi wanatumia nguvu kupita kiasi.

SOURCE BBC/SWAHILI

Advertisements

Bunge la Afrika Kusini limeshindwa tena kumuondoa Rais Zuma

Rais wa Afrika Kusini amenusurika kwa mara nyingine katika kura ya kutokuwa na imani naye iliyopigwa na bunge la nchi hiyo ambapo awamu hii ilikuwa ni ya tofauti kwani ilikuwa ni kura ya siri.

Rais Zuma kwa vipindi  mfululizo ameshuhudia maandamano na kura za kutokuwa na imani zikipigwa kwa lengo la kumtaka ajiuzulu kutokana na tuhuma mbalimbali za rushwa na upendeleo zinazomkabili.
Kutokana na kura zilizopigwa jana na bunge la nchi hiyo, jumla ya kura hizo ni 384 huku waliosema hawana imani naye wakiwa 177, wenye imani wakiwa ni 198 na kura zilizoharibika ni 9.
Kwa mujibu wa matokeo hayo, Wabunge 40 wa chama tawala, ANC wamepiga kura ya kutokuwa na imani na Rais Jacob Zuma hivyo kutaka ang’atuke.
Viongozi mbalimbali wa ANC pamoja na wabunge wengine wa chama hicho, wametaka wabunge hao (40) wachukuliwe hatua za kinidhamu kwa kile kilichodaiwa kuwa ni kukisaliti chama.
Muda mfupi baada ya bunge kutangaza matokeo hayo yaliyokuwa yakisubiriwa kwa hamu, wafuasi wa Rais Zuma walionekana wakicheza na kuimba kwa furaha nje ya jengo la bunge wakisherehea ushindi huo.
Aidha, kwa upande mwingine imeripotiwa kuwa, fedha ya Afrika Kusini (Rand) imeporomoka kwa zaidi ya asilimia 1 baada ya kutangazwa kuwa Rais Zuma ameshinda kwenye kura hiyo.
ANC imempongeza Rais Zuma kufuatia ushindi huo huku kikisema kwamba, mara zote kimekuwa kikitoa makada wenye kuaminika katika nafasi za serikali.
Rais Zuma amepigiwa kura ya kutokuwa na imani naye kwa zaidi ya mara 5 ambapo mara zote amefanikiwa kuruka kiunzi na kuendelea kusalia madarakani

Kenyatta anaongoza katika matokeo ya uchaguzi Kenya

Matokeo ya mwanzo ya uchaguzi mkuu wa Kenya yanaendelea yanayonesha kuwa Rais Uhuru Kenyatta anaongoza na pengo kubwa dhidi ya mpinzani wake mkuu Raila Odinga.

Kenia Wahlen Präsident Uhuru Kenyatta bei Stimmabgabe (picture-alliance/abaca/A. Wasike)

Mgombea wa uchaguzi wa rais kwa tikiti ya muungano wa upinzani – NASA Raila Odinga ameyakataa matokeo yaliyotolewa mpaka sasa akisema tume ya uchaguzi inahitajika kisheria kuonyesha fomu zilizotiwa saini na waangalizi wa vyama kutoka kila kituo cha kupigia kura zikiidhinisha matokeo kitu ambacho hakijafanyika. “Fomu namba 34 hazipoaswi kuja baada ya matokeo. Zinapaswa kuandamana na matokeo. Hivyo tunakataa matokeo yote yaliyotangazwa mpaka sasa, na tunataka IEBC itoe fomu namba 34  kutoka vituo vyote kabla matokeo mengine yote hayajatangazwa” amesema Raila

Badala yake, tume hiyo ya uchaguzi inamwonyesha kwenye tovuti yake, Rais Uhuru Kenyatta akiwa kifua mbele na asilimia 55 ya kura dhidi ya Odinga ambaye ana asilimia 44 baada ya karibu robo tatu ya vituo vya kupigia kura kuwasilisha matokeo yao.

Kenia Raila Odinga PK in Nairobi (Reuters/B. Ratner)Odinga anasema matokeo yanayotolewa sio ya kweli

Hata hivyo, tume hiyo haijatoa habari kuhusu ni majimbo gani yaliyohesabiwa, hivyo haikuwa wazi kujua kama ngome za wafuasi wa Kenyatta au za upinzani, au kutoka pande zote mbili zimehesabiwa au la. Odinga anapinga tarakimu hizo akisema uongozi wa Kenyatta umezusha shaka kwa kuwa umebaki pale pale tangu zoezi la kujumlisha kura lilianza na haziendani na kile ambacho anaambiwa na mawakala wa chama chake ambazo zinaonyesha kuwa wako kifua mbele. Lakini upande wa chama cha Jubilee umepinga kauli ya NASA ukisema muungano huo unakwenda kinyume na uamuzi uliotolewa na mahakama baada ya wao wenyewe kuwasilisha kesi mahakamani wakitaka matokeo yanayotangazwa katika kituo cha kupigia kura yawe ndiyo ya mwisho. Raphael Tuju ni Katibu Mkuu wa chama cha Jubilee “Tunaona wao sio wakweli. Kwa wao sasa kubadilisha msimamo wao. Sidhani kama unaweza kubadilisha sharia wakati mchakato ukiendelea. Sheria ni sheria na lazima sote tuziheshimu”

Kamishna wa IEBC Rosyln Akombe amesema kuna chama ambacho hakukitaja, kilichopinga kutolewa kwa matokeo hayo, lakini kama tume wameamua kuendelea kuyatangaza “Tumeamua kama tume kuwa tutaendelea kutoa matokeo, ili vyombo vya habari, na wakenya wawe na fursa ya kuendelea kupata matokeo, na pia tunaamini hio ni kuheshimu sheria tulizo nazo na pia uamuzi uliofanywa na mahakama” Amesema Akombe

Kenia Ezra Chiloba Leiter der Wahlkommission (Getty Images/AFP/T. Karumba)Tume ya uchaguzi inaendelea kutoa matokeo ya awali

Chini ya katiba ya kenya, matokeo ya kila kituo cha kupigia kura yanapaswa kujazwa kwenye fomu ambayo inatiwa saini na waangalizi kutoka kila chama katika kituo hicho, kisha kuchapishwa na tume ya uchaguzi kwenye tovuti ya umma. Hatua hiyo inapaswa kusaidia kuhakikisha kuwa uchaguzi haufanyiwi mizengwe na vyama vinaweza kuthibitisha matokeo.

Odinga aligombea katika chaguzi mbili zilizopita na akashindwa zote, ambapo alitoa madai ya wizi w akura kufuatia dosari zilizojitokeza katika chaguzi hizo. Katika mwaka wa 2007, wito wake wa kufanyika maandamano ulizusha machafuko ya kikabila ambayo yalisababisha vifo vya watu 1,200. Katika mwaka wa 2013, alituliza ghasia kwa kuwasilisha malalamiko yake mahakamani.

Mshindi wa kinyang’anyiro cha urais lazima apate Zaidi ya asilimia 50 ya kura pamoja na robo moja au kura Zaidi katika karibu kaunti 24 kati ya 47 za Kenya, kwa mujibu wa maafisa. Kama mgombea anayeongoza hatoweza kutimiza kiasi hicho, wagombea wawili wakuu wataingia katika duru ya pili ya uchaguzi.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/reuters
Mhariri: Zainab Aziz

Odinga apinga matokeo ya urais yanayotangazwa na tume Kenya

Raila Odinga

Mgombea urais wa muungano wa upinzani nchini Kenya National Super Alliance (Nasa) Raila Odinga amepinga matokeo ambayo yanaendelea kutangazwa na tume ya uchaguzi nchini humo, IEBC.

Bw Odinga amewaambia wanahabari kwamba tume hiyo imekuwa ikitangaza matokeo kwenye tovuti yake na kufuata utaratibu ufaao.

Waziri mkuu huyo wa zamani amesema kabla ya matokeo yoyote kutangazwa, IEBC inafaa kuwapa maajenti wa vyama Fomu 34A kutoka vituoni.

Amesema kwa sasa, bila kuwepo kwa fomu hizo, ni vigumu kubaini matokeo yanayopeperushwa yanatoka wapi.

“Mfumo umeacha kufanya kazi. Sasa ni mitambo inayopiga kura. IEBC wamesema kwamba hakuna chama chochote kilichopinga matokeo. Lakini vyama vitapingaje matokeo bila kujua asili yake? Ni fomu 34A pekee zinazoonesha chanzo cha matokeo,” amesema.

“Kwa hivyo, tunakataa matokeo yote yaliyotangazwa kwa sasa na kuitaka tume ya IEBC itoe fomu 34A za kila kituo kabla ya matokeo zaidi kutangazwa.”

IEBC imekuwa ikitangaza matokeo ya urais mtandaoni, na kufikia saa tisa na robo alfajiri, matokeo hayo yalikuwa yanamuonyesha Rais Uhuru Kenyatta wa chama cha Jubilee akiwa mbele na kura 6331140 (55.27%) naye Bw Odinga akiwa na kura 5031737 (43.92%).

Matokeo hayo ni ya kutoka vituo 295319 kati ya vituo 40883 nchini humo.

“Hii ni kompyuta inayopiga kura,” alisema Bw Odinga akikataa matokeo hayo.

Hali ya wasiwasi imekuwa ikitanda katika kituo cha taifa cha kujumlishia na kutangaza matokeo katika ukumbi wa Bomas jijini Nairobi.

Matokeo yalianza kutiririka baadaye Jumanne jioni baada ya shughuli ya kuhesabiwa kura kuanza. Matokeo hayo yamekuwa yakionesha Bw Kenyatta akiongoza.

Wakala mkuu wa muungano huo wa upinzani, naibu waziri mkuu wa zamani Musalia Mudavadi alikuwa awali amehutubia wanahabari na kutaja matokeo yanayotangazwa na tume hiyo kama utapeli.

Alitoa wito kwa wafuasi wa muungano huo kupuuzilia mbali matokeo yanayotangazwa.

 

SOURCE BBC/SWAHILI

Kenya yajiandaa kwa uchaguzi

Wakenya milioni 19 wanatarajia kushiriki kwenye uchaguzi wa kihistoria hapo kesho, huku matayarisho yote yakikamilika

Bildkombo Kandidaten Wahlen Kenia 2017

Wakenya milioni 19 wanatarajia kushiriki kwenye uchaguzi wa kihistoria hapo kesho, huku matayarisho yote yakikamilika. Kiongozi wa chama tawala cha Jubilee, Rais Uhuru Kenyatta, anakutana tena na hasimu wake wa kisiasa, Raila Odinga, wa muungano mkuu wa upinzani, NASA, kwenye kinyang’anyiro kinachotazamiwa kuwa cha vuta-nikuvute baina ya wawili hao, licha kuwepo wagombea wengine saba wa urais.

Siku ya mwisho kabla ya uchaguzi

Afisa wa uchaguzi Kenya akikagua vijisanduku na vifaa vingine vya kupia kuraAfisa wa uchaguzi Kenya akikagua vijisanduku na vifaa vingine vya kupia kura

Zikiwa zimesalia saa za kuhesabu, Wakenya wanasubiri kuchagua viongozi watakaowaongoza kwa kipindi kingine cha miaka mitano siku ya Jumanne. Uchaguzi huu unaowagharimu walipakodi wa Kenya shilingi bilioni 49 unaonekana kuwa ghali zaidi ukilinganishwa na chaguzi katika mataifa jirani.

Zaidi ya wagombea 1,000 watachaguliwa na Wakenya milioni 19 kwenye nafasi za urais, ugavana, useneta, ubunge, uwakilishi wa kinamama na wa kaunti. Kuna vituo elfu 40,883 vya kupigia kura vitakavyolindwa na maafisa 150,000 wa idara za usalama. Zaidi ya waangalizi 9,000 wa kitaifa na wa kigeni wameidhinishwa kuangalia uchaguzi huu.

Wito wa amani

Jijini Nairobi hali ni tulivu huku shughuli za kawaida zikipungua. Hakuna misongamano ya magari na kelele ambazo huhanikiza jiji hili na baadhi ya maduka yamefungwa.

Rais Uhuru Kenyatta alipokuwa kwenye kampeni Nairobi Julai 21Rais Uhuru Kenyatta alipokuwa kwenye kampeni Nairobi Julai 21

Rais Uhuru Kenyatta, ambaye alikamilisha kampeni zake katika mji wa Nakuru juzi Jumamosi, aliwaomba Wakenya wapige kura kwa amani, huku kinara wa upinzani Raila Odinga aliyekamilisha kampeni zake katika Bustani ya Uhuru jijini Nairobi, akiwataka wafuasi wake wajitokeze kwa wingi kupiga kura. Huku Rais Kenyatta akiomba ridhaa ya kuongoza ya kipindi kingine cha miaka mitano, Odinga anaona wakati huu ataibuka mshindi, kwani ameziba mianya mingi ambayo ilikuwa inavuja kwenye chaguzi zilizopita.

Ushindani mkali kati ya Uhuru na Raila

Kura ya maoni iliyofanywa mwezi Januari ilimuweka Rais Kenyatta mbele kwa asilimia 47 dhidi ya Odinga aliyekuwa na asilimia 30. Hata hivyo, juma lililopita kwenye utafiti mwingine, Odinga alikuwa anaongoza kwa asilimia 47 dhidi Kenyatta aliyekuwa na asilimia 46. Wachambuzi wa masuala ya siasa wakisema kuwa uamuzi wa upinzani kutosambaratika hadi sasa umechangia kuchupa kwa Odinga kwenye utafiti huo.

Mgombea urais wa muungano wa upinzani NASA Raila Odinga alipokuwa kwenye kampeni Nairobi Agosti 5Mgombea urais wa muungano wa upinzani NASA Raila Odinga alipokuwa kwenye kampeni Nairobi Agosti 5

Taasisi ambazo zinahusika kwenye uchaguzi huu, zimetoa hakikisho kuwa ziko tayari kuendesha uchaguzi huru wa haki na wa kuaminika. Macho yote yatakuwa yakielekezwa kwenye tume inayosimamia uchaguzi huu, IEBC, idara ya usalama na idara ya mahakama.

Tangazo la IEBC hapo jana kuwa matokeo kwenye vituo 11,000 vya kupigia kura hayatapeperushwa kwa njia ya elektroniki yanatamausha, kwani maeneo mengi yaliyotajwa yamo kwenye miji.

Hata hivyo, matumaini ya Wakenya ni kuwa uchaguzi huu utaendeshwa kwa njia huru na wa haki. Baada ya uchaguzi huu kukamilika, wachambuzi wanashikilia kuwa, tume ya kusimamia uchaguzi italazimika kurekebisha vile ambavyo imekuwa ikiwasiliana na umma, kwani yalekea kuwa huo umekuwa upungufu wake mkubwa.

 

Mwandishi: Shisia Wassilwa/DW Nairobi

Mhariri: Mohammed Khelef

Maamuzi ya Mahakama kuu kuhusu dhamana ya Manji

Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam Leo imeyatupilia mbali maombi ya dhamana yaliyowasilishwa na   Mfanyabiashara maarufu Tanzania Yusuf Manji baada ya kukubaliana na mapingamizi yaliyowasilishwa na DPP.
Maombi hayo yametupiliwa mbali na Jaji Isaya Arufani.
Kabla ya kutupiliwa mbali, maombi hayo, Manji alisimama na kuieleza mahakama kukataa kuwakilishwa na Wakili Peter Kibatala kwa sababu za kisiasa.
Amedai, alipopeleka maombi ya dhamana alimpa maelekezo wakili Joseph Tedayo lakini alishangaa kesi ilipofika mahakamani hapo kwa ajili ya kisikilizwa maombi yake ya dhamana wakili Kibatala ndiyo alifika kumuwakilisha.
Kutokana na hayo, Manji ameiomba Mahakama mawakili, Alex Mgongolwa, Hudson Ndusyepo na Seni Malimi ndio wawe wanamuwakilisha katika maombi hayo.
 Hivyo DPP akiwakilishwa na mawikili Paul Kadushi na Simon Wankyo walidai kuwa, wamesilisha kiapo kinzani kupinga maombi hayo ya dhamana wakiwa na hoja tatu.
Hoja hizo ni kuwa, Mahakama Kuu haina mamlaka ya kusikiliza maombi hayo ya dhamana na kwamba yanapaswa kusikilizwa na mahakama ya kifisadi kwa kuwa mshtakiwa anakabiliwa na makosa ya uhujumu uchumi.
Ameongeza kiqa vifungu vya kisheria vilivyotumika kuleta maombi hayo siyo sahihi na pia hati ya kiapo iliyoambatanishwa  kuunga mkono maombi hayo ina dosari kisheria ambazo haziwezi kurekebishika.
Kadushi aliiomba mahakama kusikiloza kwanza mapingamizi ya DPP kabla ya kuanza kusikiliza maombi ya dhamana.
Hata hivyo Wakili Mgongolwa akiwakilisha jopo la mawakili wa Manji walikubaliana na mapingamizi ya DPP kuwa ni kweli yana msingi na maombi ya dhamana yanadosari.
Kufuatia kukiri huko, Kadushi aliiomba mahakama kutupilIa mbali maombi hayo ya dhamana.
Akitoa uamuzi, Jaji Arufani amekubaliana na mleta Maombi (Manji) kuwa hawakilishwi na Kibatala. Pia amesema mahakama kuu haina mamlaka ya kusikiliza maombi hayo hivyo ameyatupilia mbali.
Katika maombi hayo ya dhamana, Yusuf Manji anaiomba Mahakama Kuu itengue hati ya kunyimwa dhamana iliyowasilishwa na Mkurgenzi wa Mashtaka (DPP) kwa kuwa ana matatizo ya kiafya akisumbuliwa na matatizo ya moyo.
Kwa mujibu wa hati ya maombi hayo, Manji anadai kuwa anasumbuliwa na maradhi ya moyo  na kwamba ameambatanisha vyeti vya daktari katika maombi yake.
Katika kesi ya msingi,  Manji na wenzake wanatuhumiwa kukutwa na mihuri ya mbalimbali ya JWTZ isilivyo halali vyote vikiwa na thamani ya Sh. milioni 236.5.
Mbali na Manji, washtakiwa wengine ni,  Ofisa Rasilimaliwatu Deogratias Kisinda (28), Mtunza Stoo, Abdallah Sangey (46) na Mtunza Stoo msaidizi, Thobias Fwele (43)

Uhuru, Raila wasema wana imani watapata ushindi mkubwa Jumanne


Wafuasi wa chama cha Jubilee (kushoto) na wale wa muungano wa NASA wanahuduria mikutano ya mwisho ya kampeni zao katika uwanja wa Afraha, Nakuru, na Uhuru Park, Nairobi siku ya Jumamosi.

Wafuasi wa chama cha Jubilee (kushoto) na wale wa muungano wa NASA wanahuduria mikutano ya mwisho ya kampeni zao katika uwanja wa Afraha, Nakuru, na Uhuru Park, Nairobi siku ya Jumamosi.

Wagombea wa urais nchini Kenya walikuwa na shughuli mbali mbali Jumapili zikiwa zimesalia siku mbili kabla ya uchaguzi mkuu wa Jumanne. Kulingana na kanuni za tume ya uchaguzi na mipaka, IEBC, ni kinyume cha sheria kufanya shughuli zozote za kampeni saa 48 kabla ya zoezi la uchaguzi kuanza.

Rais Uhuru Kenyatta alijiunga na waumini kwenye makanisa mawili mjini Nairobi na kuwaomba Wakenya wa tabaka mbali mbali kudumisha amani wakati wa uchaguzi huo.

Kulingana na msemaji wa kampeni ya Kenyatta, baadaye mwanasiasa huyo alifanya mikutano kadhaa na viongozi wa chama chake na kuthibisha mawakala watakaowakilisha chama hicho katika vituo mbali mbali vya kupigia kura nchini kote.

Mapema Jumapili, Kenyatta aliwatakia Wakenya zoezi la upigaji kura lenye amani. “Uwe wa Imani ya kikriso, Kiislamu au yoyote nyingine, naomba tufanye uchaguzi kwa amani,” alisema.

Raila na Uhuru wakati wa mikutano yao ya kampeni za mwisho.

Raila na Uhuru wakati wa mikutano yao ya kampeni za mwisho.

Naye mgombea kwa tikiti ya NASA, Raila Odinga, alikutana na baadhi ya wafuasi wake katika eneo la Karen na baadaye kufanya mikutano na viongozi wa mrengo wake na kutoa orodha ya maafisa wa kushughulikia kipindi cha mpito iwapo atashinda kwenye kinyang’anyiro hicho.

Viongozi hao wawili walifanya mikutano miwili ya mwisho siku ya Jumamosi ambayo ilihudhuriwa na maelfu ya watu. Odinga alikuwa kwenye bustani za Uhuru Park, mjini Nairobi, huku Kenyatta akiongoza mkutano wake katika uwanja wa Afraha Stadium, Nakuru, takriban kilomita 160 kutoka Nairobi.

Rais Uhuru Kenyatta ambaye anagombea urais kwa muhula wa pili alifanya mkutano wa mwisho wa kampeni siku ya Jumamosi kwenye uwanja wa Afraha Stadium, kaunti ya Nakuru. Aliongoza maombi na kuwataka Wakenya kupiga kura kwa amani.

Rais Uhuru Kenyatta ambaye anagombea urais kwa muhula wa pili alifanya mkutano wa mwisho wa kampeni siku ya Jumamosi kwenye uwanja wa Afraha Stadium, kaunti ya Nakuru. Aliongoza maombi na kuwataka Wakenya kupiga kura kwa amani.

Kenyatta aliongoza maombi ya amani na kuwataka Wakenya kujitokeza kwa wingi, huku Odinga pia akiwataka wafuasi wa NASA kupiga kura kwa amani.

“Naomba mtupe nafasi nyingine ili kuendelea na miradi tuliyoanzisha wakati wa muhula wetu wa kwanza,” alisema Kenyatta.

“Nawasihi pia muwachague wawaniaji wa nyadhifa zingine kwa tikiti ya Jubilee ili tuendeleze ajenda yetu katika bunge, kaunti na kwingineko,” aliongeza.

Mgombea mwenza wa Kenyatta, William Samoei Arap Ruto alisema waliamua kufanya mkutano wa mwisho mjini Nakuru kwa sababu “ndiko chama chetu cha Jubilee kilizaliwa.”

Naye Raila odinga, ambaye anawania urais kwa mara ya nne, aliambia halaiki ya wafuasi wake kwamba ako tayari kuchukua usukani. “Nimeona dalili kubwa za ushindi kwenye uchaguzi wa Jumanne,” alisema.

“Nawaalika nyote kwa karamu ya ushindi kwenye Ikulu siku ya Jumamosi,” aliongeza huku waliohudhuria wakishangilia.

Mgombea urais wa muungano wa National Super Alliance, Raila Odinga, ahutubia wafuasi wake katika bustani za Uhuru Park mjini Nairobi mnamo siku ya Jumamosi. Alisema yuko tayari kuhika usukani wa Kenya na kwamba ameona dalili kubwa za ushindi.

Mgombea urais wa muungano wa National Super Alliance, Raila Odinga, ahutubia wafuasi wake katika bustani za Uhuru Park mjini Nairobi mnamo siku ya Jumamosi. Alisema yuko tayari kuhika usukani wa Kenya na kwamba ameona dalili kubwa za ushindi.

Raila alisema iwapo NASA itaunda serikali, ufisadi utatokomezwa. “Nitaenda nchini Tanzania na kutafuta suluhisho la kimagufuli,” alisema, huku akiashiria kutumia mfano wa uongozi wa rais wa Tanzania, John Pombe Maufuli – ambaye ni rafiki yake wa siku nyingi – kama kigezo cha kupambana na ulaji rushwa.

Mgombea mwenza, Stephen Kalonzo Musyoka, alisema polisi hawasemai ukweli kuhus kifo cha aliyekuwa naibu mkurugenzi wa idara ya mawasiliano na teknolojia kwenye tume ya IEBC, Chis Msando, ambaye mwili wake ulipatikana katika chumba cha kuhifadhi miti cha City, wiki moja iliyopita, baada ya afisa huyo kuripotiwa kupotea siku mbili kabla ya hapo.

“Polisi wanawadanganya Wakenya kwamba wanafanya uchunguzi,’ alisema Musyoka.

Rais Kenyatta anawania urais kwa mara ya tatu baada ya kushindwa na Mwai Kibaki mnamo mwaka wa 2002 na kumshinda Raila Odinga manamo mwaka wa 2013 kwenye uchaguzi uliozua utata na msindi wake kuamriwa na mahakama kuu.

Tayari vifaa vya kupigia kura vimefika katika vingi vya vituo na serikali imetangaza kwamba itatumia maafisa 150,000 kulinda amani wakati wa zoezi hilo.

Wawaniaji wengine wa urais pamoja na wagombea wa nyadhifa mbali mbali pia walifanya mikutano katika maeneo tofauti tofauti na kuwarai wapiga kura kuwachagua. Jumamosi ilikuwa siku ya mwisho ya kufanya kampeni.

Licha ya hali ya wasiwasi kwamba uchaguzi huenda ukagubikwa na ghasia, wachambuzi wametaja kipindi cha kampeni za mwaka huu kama ambacho hakikuwa na visa vingi vya vurugu.