Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Ali Mohamed Shein (wa tatu kushoto) akiwakaribisha Mashekhe katika futari aliyoiandaa kwa Wananchi waumini wa Dini ya Kiislamu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba huko Viwanja vya Ikulu ya Wete jana.[Picha na Ramadhan Othman,Pemba.]

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Ali Mohamed Shein (wa tatu kushoto) akiwakaribisha Mashekhe katika futari aliyoiandaa kwa Wananchi waumini wa Dini ya Kiislamu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba huko Viwanja vya Ikulu ya Wete jana.[Picha na Ramadhan Othman,Pemba.]

MAANA YA ‘SAUMU’


Neno ‘Saumu’ ki lugha ya Kiarabu lina maana ya kujizuia. Pia ni neno ambalo lilitumika kabla ya zama za Uislamu. Baadaye Uislamu ulipokuja ukalijaalia neno hili kuwa ni moja kati ya maneno yatumikayo kiibada.Ama maana ya neno hili Kisheria, ni kujizuia kutokana na mambo yanayobatilisha Saumu yaitwayo ‘al-Muftiraat’.Kinyume cha watu wengi wanavyodhani kwamba Saumu hasa ni kujizuia kula na kunywa tu. La Hasha! Bali Saumu ni kukihifadhi kila kiungo chako kutokana na mambo yasiyotakikana.

Amesema Imam Ja’far Assadiq, “Kufunga siko kujilinda na kula na kunywa tu, bali utakapofunga hifadhi (chunga) macho yako, ulimi wako, tumbo lako, masikio yako na uchi wako. Vile vile ilinde mikono yako, pendelea sana kunyamaza ila katika heri (tu kama kusoma Qur’ani n.k.) na umhurumie mtumishi wako.”

Naye Mtume (s.a.w.) amesema: “Mambo matano hutengua Saumu ya mtu: Uongo, kuseng’enya, kufitinisha, kula viapo vya uongo na (mwanamke) ku mkazia macho mwanamume asiye maharimu wake au (mwanamume) kumkazia macho mwanamke asiye maharimu wake kimatamanio.

Kuseng’enya kumekatazwa katika kauli hii ya Mtume (s.a.w.) na badala yake tunahimizwa na hadithi nyingi tujiepushe na lolote la kutuharibia Saumu zetu.

Mtume (s.a.w.) anasema: “Mwenye kufunga huwa ibadani wakati wowote hata kama analala madamu hajaitengua Saumu yake kwa usengenya. Kwa hapa utaona kwamba, kule kutokula na mfano wake kama tulivyo yabaini hapo mbeleni siko kufunga hasa kunakotakikana, bali kufunga ni kujizuia na makatazo yote na mabaya.

NYAMA MDOMONI

Siku moja Mtume (s.a.w.) alimsikia mwanamke mmoja akisengenya na hali amefunga. Mtume (s.a.w.) akamwitishia chakula ili ale, yule mwanamke akasema: “Mimi nimefunga”. Mtume akaendelea kuhimiza chakula iletwe mara moja ili yule bibi ale naye, yule bibi azidi kukariri kuwa angali anafunga. Hapo Mtume akamwambia: “Unafungaje na hali menoni mwako mna kipande cha nyama? Yule mwanamke akazidi kubishana na huku Mtume amwambia “Hebu tia mkono wako kinywani mwako” na kweli alipouingiza mkono wake menoni, alitoa kipande cha nyama. Hapo Mtume (s.a.w.) akamwambia “Waona? Wataka kula nyama ya nduguyo aliyekufa? Yaani kusengenya ni sawa na kula nyama ya mfu tena nduguyo.

Hapo waona ndugu? Kwa hakika kile kipande cha nyama mdomoni mwa yule bibi kilipatikana kwa kule kusengenya, na yeyote asengenyaye huwa Saumu yake si sawa na huwa amekula nyama ya mfu tena nduguye.

PIA KUTUKANANA

Siku moja Mtume (s.a.w.) alimsikia mwanamke mmoja akimtusi msichana wake – mfanya kazi – na yule bibi alikuwa amefunga, Mtume,(s.a.w.) akaitisha maji ampe yule bibi afuturu (na ilikuwa ungali mchana). Yule bibi akasema “Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, hakika mimi nimefunga” Mtume (s.a.w.) akajibu, “Unawezaje kuzitusi mtu au kuteta naye na hali umefunga? Wewe tayari Saumu yako ni batili, yaani si makbuli.

Viungo vyako ni hadiya ya Mwenyezi Mungu kwako, kwa hivyo haifai kuvifaniya hiana.

Katika masiku haya ya Saumu, na mengine pia ambayo ni heshima kuu na utukufu kwa Waislamu, ni lazima kujilinda.

MIGUU: Isielekee kulikokatazwa ambako kunajulikana kama Makadara, kwenda disco, kwenda sinema na kadhalika, na badali yake ni muhimu lau tutakwenda misikitini, kutembeleana kwa heri kama alivyotuhimiza Mola wetu kwa kutuambia: “Saidianeni katika mema na kwa kumcha Mwenyezi Mungu, lakini msisaidiane katika kumwasi Mola na kufanyiana uadui. Na kujilinda huku kuendelee hata baada ya Ramadhani.

MIKONO: Izuie kuwadhuru watu kwa kuwaibia, kuua, kupiga na kadhalika, na badala yake ishikishe Qur’ani, iamkize jamaa na kadhalika.

MACHO: Usiyatizamishe ulichokatazwa. Kuwaangalia watu wasio wa maharimu yako, kutamani kisicho chako na kadhalika bali fungua Msahafu usome.

MASIKIO: Usisikilize upuzi uliokatazwa kama nyimbo, kusengenya, udaku n.k.badala yake nenda ukasikilize mawaidha na kama hayo ambayo ndani yake mna radhi ya Allah.

———————————————————————————————–

NASAHA ZA DINI

 
“Dini ni nasaha, wakauliza kwa nani ? Akasema Mtume : Kwa Allah, Mtume wake, kwa viongozi wa waislamu na watu wa kawaida” Hadith Tukufu

 
MINBARI YA RAMADHANI    
     
Hii ni kutokana na mnasaba wa kuingia mwezi mtukufu wa Ramadhani. Minbari ya Ramadhani itakuwa ikikuletea mawaidha yahusiyanayo na funga ya Ramadhani, ili uweze kuijua funga na hatimaye uweze kufunga kama alivyoamrisha Mwenyezi Mungu Mtukufu na kama alivyofunga Bwana Mtume -Rehema na Amani zimshukie – ambaye ndiye kigezo chetu chema. Sambamba na Minbari ya Ramadhani, website yako itakuwa ikikuletea TUNDA LA RAMADHANI. Kupitia tunda la Ramadhani utajifunza hadithi mbili tatu za Mtume zihusianazo na funga tukufu ya Mwezi mtukufu wa Ramadhani. Hadithi hizi zitakuwa zikifuatiwa na maelezo mafupi ili kuziweka wazi kwa wasomaji.i) MINBARI YA RAMDHANI NA KHUTBA YA MTUME KATIKA KUUKARIBISHA MWEZI MTUKUFU WA RAMADHANI :

Jueni na eleweni enyi ndugu zanguni Waislamu kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu amejaalia mafanikio ya duniani ni ya muda mfupi, yenye kwisha na kuondoka, na mafanikio ya akhera ndiyo yenye kusalia/kubakia milele. Haya mafanikio ya kudumu, hayapatikani ila kwa kupitia barabara ngumu ya “TAQ-WA” kumcha Mwenyezi Mungu na kumtii na kumfuata Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie-. Katika jumla ya nguzo kuu za Taqwa ni kuufunga huu mwezi mtukufu wa Ramadhani ambao Allah ameujaalia kuwa ni REHMA kwa viumbe. Nao kama mjuavyo ndio mwezi ambao imeteremshwa ndani yake Qur-ani Tukufu ikiwa ni muongozo kwa watu wote. Muongozo uliosheheni hoja wazi za uongofu na upambanuzi baina ya haki na batili. Ramadhani pia ni mwezi ambao hufunguliwa ndani yake milango ya pepo na kufungwa milango ya moto. Ni kwa kuuzingatia umuhimu na nafasi ya mwezi wa Ramadhani, ndipo Bwana Mtume akaitoa Khutba yake tukufu, khutba ya kihistoria, khutba kongwe katika kuupokea na kuukaribisha mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Imepokelewa na Salmaan Alfaarisy – Allah amuwie Radhi – amesema : Alitukhutubia Mtume wa Mwenyezi Mungu – Rehema na Amani zimshukie – katika siku ya mwisho ya mwezi wa Shaabani, akasema : “Enyi watu, umekufikieni mwezi mtukufu wenye baraka. Ndani ya mwezi huu umo usiku wa LAYLATIL QADRI usiku ambao ni bora kuliko miezi alfu moja. Mwenyezi Mungu amejaalia funga ya mwezi huu kuwa ni FARADHI na kisimamo (cha ibada) cha usiku wake kuwa ni SUNA. Atakayejikurubisha (kwa Mola wake) ndani ya mwezi huu kwa (kutenda) jambo lolote la kheri, (malipo, jazaa yake) itakuwa ni kama mtu aliyetekeleza fardhi katika miezi mingine. Na atakayetekeleza fardhi katika mwezi huu, atakuwa ni kama mtu aliyetekeleza fardhi sabini katika miezi mingine. Na mwezi huu ni mwezi wa SUBIRA, nao ni mwezi ambao mwanzo wake ni REHEMA na katikati yake ni MAGHFIRA/MSAMAHA WA ALLAH na mwisho wake ni KUACHWA HURU NA ADHABU YA MOTO. Yeyote atakayemfuturisha mfungaji ndani ya mwezi huu, (ujira wa futari hiyo) utakuwa ni maghfira ya madhambi yake (mfuturishaji) na kuachwa huru na adhabu ya moto na atapata ujira kama aupatao mfungaji bila ya kupungua chochote katika ujira/thawabu zake (mfungaji)”. Tukasema : Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, sio sote tunaweza kupata (kitu) cha kumfuturisha huyo mfungaji. (Mtume) akawajibu : “Mwenyezi Mungu humpa thawabu hizi yule atakayemfuturisha mfungaji ndani ya mwezi huu kwa onjo/funda ya maziwa au (kokwa ya) tende au funda ya maji. Na atakayemshibisha ndani ya mwezi huu mfungaji, itakuwa ujira (wa shibe hiyo) ni maghufira ya madhambi yake (mshibishaji) na Mola wake atamnywesha katika hodhi (birika) langu funda moja ambayo hatopata kiu baada yake kabisa. Na atakuwa na ujira kama aupatao mfungaji bila ya kupungua chochote katika ujira wake (mfungaji). Na atakayempunguzia kazi mtumishi/mfanyakazi wake ndani ya mwezi huu, Mwenyezi Mungu atamghufiria madhambi yake na kumuacha huru na adhabu ya moto. Basi kithirisheni sana ndani ya mwezi huu mambo manne. Mtamridhisha Mola wenu kwa kutenda mambo mawili kati ya manne hayo; na mambo mawili hamjikwasii (hamna budi) nayo. Ama hayo mambo mawili mtakayoridhisha nayo Mola wenu ni shahada (kushuhudia kwamba hapana Mola apasaye kuabudiwa kwa haki ila ALLAH) na mumtake maghfira. Na ama yale mambo mawili msiyojikwasia nayo ni mumuombe Mola wenu pepo na mjilinde/mjikinge kwake na (adhabu) ya moto”. Ibn Khuzaymah katika sahihi yake.

MAELEZO : Ikiwa tunafuatana pamoja, tunaweza tukaigawa hadithi hii tukufu ambayo ni khutba kongwe iliyo hai hadi leo na itaendelea kuwa hai mpaka mwisho wa dunia. Khutba hii iliyotolewa na Khatibu mahiri, Bwana Mtume katika kuukaribisha mwezi mtukufu wa Ramadhani, inagawanyika katika sehemu kuu tatu au tuseme ina vipengele vikuu vitatu. Ukiizingatia hadithi utakuta mwanzo wa khutba yake, Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie – anawafahamisha maswahaba na umma mzima juu ya utukufu, ubora, cheo na nafasi ya mwezi wa Ramadhani. Kuna hekima/falsafa gani ndani ya maelezo haya ? Mtume anauelezea mwezi wa Ramadhani ni mwezi wa namna gani ili muislamu aujue, kwani waswahili husema asiyekujua hakuthamini. Akishaujua atauthamini na kuupa hadhi yake unayostahili. Kuuthamini na kuupa heshima mwezi wa Ramdhani ni kuzidisha sana TWAA kwa Mwenyezi Mungu kwa kufanya namna mbali mbali za ibada na mambo mengine ya kheri.

Sehemu ya pili ya hadithi, Bwana Mtume anataja fadhila/faida na ubora wa mwezi wa mtukufu wa Ramadhani na kuwa ibada yeyote inayofanywa ndani ya mwezi huu hailingani kithawabu/kiujira na ile ibada inayofanywa katika miezi mingine. Kwa hiyo basi, Ramadhani ni ndio musimu wako wa ibada. Kadhalika Bwana Mtume anatuelezea malipo na thawabu adhimu anazozipata mja mwenye kumfuturisha nduguye muislamu katika mwezi huu wa Ramadhani. Hapa Bwana Mtume anaashiria moyo wa ukarimu na upendo utakiwao waislamu wajipambe na kuwa nao. Kwani waislamu wakipendana watakuwa ni wamoja na mshikamano, na wakishikamana watautawala ulimwengu na hapatakuwa na nguvu ya kuwashinda, si magharibi wala mashariki.

Kisha ndipo Bwana Mtume akaikhitimisha khutuba yake kwa kutoa wito muhimu kwa waislamu. Akawataka wakithithirishe sana kumpwekesha Mola wao kwa kuleta kalima ya shahada na wamtake sana maghfira. Hali kadhalika akawataka waislamu wakithirishe mno kumuomba Mola wao pepo na wamuombe awakinge na moto wa jahanamu. Ili kuutekeleza wito huu ndipo wanazuoni wetu wema -Allah awarehemu- wakatuwekea uradi uletwao msikitini ndani ya mwezi wa Ramadhani. Chimbuko la uradi huu ni ile sehemu ya mwisho ya hadithi. Uradi wenyewe ni huu :

ASH-HADU AN LAA ILAHA ILLA-LLAHU NASTAGHFIRULLAH, NAS-ALUKAL-JANNATA WANA’UDHU BIKA MINAN-NAAR ALLAHUMMA INNAKA AFUWWUN, TUHIBBUL-AFWA FA’FU ‘ANNAA YAA KARIIM

Tunashuhudia kuwa hapana Mola apasaye kuabudiwa kwa haki ila Allah, Tunakuomba maghfira (msamaha wa madhambi) Ewe Allah, Tunakuomba pepo na tunajikinga kwako na moto, Ewe Allah, wewe mimi ni msamehevu na unapenda msamaha, basi tusamehe Ewe KARIMU.

Haya shime ndugu zanguni waislamu, tukithirishe kuuleta uradi huu ndani ya mwezi wa mavuno; mwezi mtukufu wa Ramadhani. Kwa kufanya hivyo tutakuwa tumeuitikia wito wa Bwana Mtume kwa maslahi na faida yetu wenyewe.

TUNDA LA RAMADHANI :

Karibu ndugu yangu muislamu katika bustani ya Bwana Mtume -Rehema na Amani zimshukie – uchume utakavyo na kula kiasi chako matunda matamu, mazuri yasiyokwisha hamu; matunda ya Ramadhani. Ili ufaidike na kunufaika na matunda haya unatakiwa uingie ndani ya bustani hii tukufu kwa unyenyekevu, utulivu, adabu, heshima na usikivu.

TUNDA LA KWANZA – DUA YA KUFUTURU

Amepokea Ibn Majah kutokana na hadithi ya Abdillah Ibn Amri (amesema Mtume) : YUNA MFUNGAJI WAKATI WA KUFUTURU KWAKE DUA ISIYOREJESHWA (yenye kujibiwa bila ya kipingamizi)”. Ni kwa sababu hiyo ndiyo Mtume alikuwa akisema (wakati wa kufuturu) :

[ALLAHUMMA INNIY LAKA SWUMTU WA’ALAA RIZQIKA AFTWARTU FAGH-FIRLIY MAA QADDAMTU WA MAA AKHARTU DHAHABAD-DHWAMAU WABTALLIT-‘URUQU WATHABATAL AJRU IN-SHAALLAHU TAALA]

Maana yake : “Ewe Mola wa haki ni kwa ajili yako tu nimefunga na nimefuturu kwa riziki yako. Basi (nakuomba) unisamehe dhambi zangu zilizotangulia na zijazo. Kiu kimeondoka na mishipa imelowana na ujira umethibiti pindipo atakapo Mwenyezi Mungu Mtukufu”

Haya shime ndugu zanguni waislamu, tumuige Mtume wetu katika hili na mengineyo ili tutengenekewe duniani na akhera. Usikubali kuipoteza fursa hii adimu ya kukubaliwa duao, omba na Mola Karimu atakupa.

TUNDA LA PILI : FADHILA ZA KUHARAKIA KUFUTURU :

Imepokelewa hadithi kutoka kwa Abuu Hurayrah – Allah amuwie Radhi – amesema, Amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu – Rehema na Amani zimshukie- “AMESEMA MWENYEZI MUNGU : HAKIKA WAJA WANGU WAPENDEZAO SANA KWANGU NI WALE WAHARIKIAO KUFUTURU” Ahmad na Tirmidhi.

MAELEZO : Ni vema mtu akafanya haraka kufuturu, maadam ana uhakika wa kutua/kuzama kwa jua. Ikiwa hana uhakika, basi ni vema akasubiri adhana ili asije akafuturu kabla ya muda. Haya zingatia upendwe na Mola wako

—————————————————————————————————————

ISEMAVYO QUR-ANI TUKUFU KUHUSIANA NA SWAUMU YA RAMADHANI

SWAUMU YA RAMADHANI KATIKA DIRISHA DOGO.

ISEMAVYO QUR-ANI TUKUFU KUHUSIANA NA SWAUMU YA RAMADHANI:

Allah Mtukufu anasema: “ENYI MLIOAMIMNI! MMELAZIMISHWA KUFUNGA (swaumu) KAMA WALIVYOLAZIMISHWA WALIOKUWA KABLA YENU ILI MPATE KUMCHA ALLAH. SIKU CHACHE TU (kufunga huko). NA ATAKAYEKUWA MGONJWA KATIKA NYINYI AU KATIKA SAFARI (akafungua baadhi ya siku), BASI (atimize) HISABU KATIKA SIKU NYINGINE. NA WALE WASIOWEZA, WATOE FIDIA KWA KUMLISHA MASIKINI. NA ATAKAYEFANYA WEMA KWA RADHI YA NAFSI YAKE, BASI NI BORA KWAKE. NA (huku) KUFUNGA NI BORA KWENU IKIWA MNAJUA. (mwezi huo mlioambiwa kufunga) NI MWEZI WA RAMADHANI AMBAO IMETEREMSHWA KATIKA (mwezi) HUO HII QUR-ANI ILI IWE UWONGOZI KWA WATU, NA HOJA ZILIZO WAZI ZA UWONGOFU NA UPAMBANUZI (wa baina ya haki na batili). ATAKAYEKUWA KATIKA MJI KATIKA HUU MWEZI (wa Ramadhani) AFUNGE. NA MWENYE KUWA MGONJWA AU SAFARINI, BASI (atimize) HISABU (ya siku alizoacha kufunga) KATIKA SIKU NYINGINE. ALLAH ANAKUTAKIENI YALIYO MEPESI NA WALA HAKUTAKIENI YALIYO MAZITO, NA PIA (anakutakieni) MTIMIZE HISABU HIYO. NA (anakutakieni) KUMTUKUZA ALLAH KWA KUWA AMEKUONGOZENI, ILI MPATE KUSHUKURU”. [2:183-185]

Aya hii tukufu imeanza kwa kuwaita waislamu kwa jina la imani ili kuiamsha kani ya imani ndani ya nyoyo zao. Na kuwaandaa kiroho kuitika na kupokea amri/maagizo watakayopewa kwa mujibu wa imani yao. Kwa sababu shani na tabia ya muumini wa kweli ni kumtii Mola wake Mtukufu katika kila analomuamrisha kutenda au kutotenda. Aya hii imebainisha ubainifu kamili na timilifu wa fadhila (ubora) ya swaumu ya Ramadhani. Falsafa/hekima yake na rehema ya Allah Mtukufu kwa waja wake kupitia fardhi hii ya swaumu.

Katika jumla ya hukumu nyingi tunazozipata ndani ya aya hii. Ni kwamba aya imewazihisha kwamba muislamu ana hali tatu katika kuilekea fardhi hii ya swaumu ya Ramadhani:-

HALI YA KWANZA:

Muislamu atakapokuwa mgonjwa ndani ya mwezi wa Ramadhani, anaumwa maradhi ambayo ghalibu mtu hutarajiwa kupona. Na kama atafunga maradhi yatazidi au atachelewa kupona. Au yumo safarini, katika hali mbili hizi; hali ya ugonjwa na ile ya safari. Uislamu unampa rukhsa ya kula katika mwezi wa Ramadhani kwa sharti kwamba ukiondoka udhuru uliomuhalalishia kula. Azikidhi (azilipe) siku zote alizokula ndani ya Ramadhani. Na kuondoka kwa udhuru kunapatikana kwa mgonjwa kupona na kurejea katika siha yake ya kawaida. Itakayomuwezesha kumudu makali ya njaa na joto la kiu. Na kwa msafiri ni kwa kurejea katika makazi yake au kuamua kuwa mkazi huko alikokwenda. Na dalili ya rukhsa hii ya kula aliyopewa mgonjwa na msafiri na kisha kukidhi ni kauli yake Allah: “…NA ATAKAYEKUWA MGONJWA KATIKA NYINYI AU KATIKA SAFARI (akafungua baadhi ya siku), BASI (atimize) HISABU KATIKA SIKU NYINGINE…” [2:184]

HALI YA PILI:

Muislamu atakapokuwa mgonjwa katika mwezi wa Ramadhani, anaumwa maradhi ambayo kupona hakutarajiwi. Au akawa ni mzee mkongwe hasiyeweza kufunga. Katika hali na mazingira haya, sheria imewahalalishia kula na kumpa masikini kibaba cha chakula kwa kila siku. Hii ni kwa sababu hawa wana nyudhuru zisizotazamiwa kuondoka kama ilivyo kwa watu wa hali ile ya kwanza. Ni kwa mantiki hii ndio Uislamu ukawawajibishia hawa kutoa fidia bila ya kulipa kwa dalili ya kauli yake Allah Mtukufu: “…NA WALE WASIOWEZA, WATOE FIDIA KWA KUMLISHA MASIKINI…” [2:184]

HALI YA TATU:

Muislamu atakapokuwa ndani ya mwezi wa Ramadhani mzima (sio mgonjwa) na akawa ni mkazi (sio msafiri). Na wala hana udhuru unaomzuia kufunga mithili ya mwanamke kuwemo hedhini. Katika hali na mazingira haya Allah amemuwajibishia na kumfaradhishia swaumu kwa dalili ya kauli tukufu ya Allah: “…ATAKAYEKUWA KATIKA MJI KATIKA HUU MWEZI (wa Ramadhani) AFUNGE…” [2:185]

Kwa hivyo ni haramu kwa muislamu ambaye ni mzima na si msafiri kuacha kufunga kwa makusudi swaumu ya mwezi mtukufu wa Ramadhani. Akiamua kutokufunga bila ya idhini ya sheria atakuwa miongoni mwa waliopata khasara duniani na akhera kwa sababu ya kuivunja amri ya Allah. Imepokewa na Abuu Hurayrah-Allah amuwiye radhi-kwamba Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema: “Ye yote atakayefungua (atakayekula) siku moja katika Ramadhani bila ya rukhsa wala maradhi. Haitoikidhi (siku hiyo) swaumu ya umri mzima ajapofunga”.Tirmidhiy, Abuu Daawoud, Nasaai, Ibn Maajah, Ibn Khuzaymah & Al-Baihaqiy

MAANA YA SWAUMU:

Swaumu ni neno la Kiarabu lililobeba dhana ya ibada ya funga ambayo ni nguzo ya nne miongoni mwa nguzo tano za Uislamu. Neno hili linafasiriwa kwa maana mbili; maana ya kilugha (maana isiyo rasmi) na maana ya kisheria (maana rasmi).

SWAUMU KATIKA LUGHA:

Kilugha isimu (nomino)- “swaumu”-inabeba dhana ya kujizuia kutenda kitu cho chote kiwacho. Maana hii ya swaumu kilugha inachimbuka kupitia kauli tukufu ya Allah: “…HAKIKA MIMI NIMEWEKA NADHIRI KWA (Allah) MWINGI WA REHEMA YA SWAUMU (kufunga), KWA HIVYO LEO SITASEMA NA MTU”. [19:26]

Yaani Bibi Maryamu mama yake Nabii Isa-Amani ya Allah iwashukie-aliwaambia waliomuuliza kuhusiana na suala la mwanawe huyo. Naye akaambiwa na Allah awajibu, mimi nimeweka nadhiri kwa Mwingi wa rehema kutokuzungumzia suala la mwanangu huyu; Isa. Katika kauli yake Bi.Maryamu ndani ya aya hii amelitumia neno SWAUMU kumaanisha KUJIZUIA kuongelea suala la mwanawe. Na hapa ndipo ilipotwaliwa maana ya swaumu kilugha.

SWAUMU KATIKA SHERIA:

Kwa mtazamo wa sheria swaumu ni kujizuia na vyote vyenye kubatilisha swaumu kwa lengo la kuabudu. Katika kipindi kinachoanzia na kuchomoza kwa alfajiri na kumalizikia na kuzama/kutua kwa jua. Kujizuia huku kunaambatana na nia ya swaumu ambayo ni wajibu iletwe kabla ya kuanza kwa kipindi cha swaumu yenyewe.

SWAUMU YA RAMADHANI IMEFARADHISHWA LINI?

Kumbukumbu sahihi za tarekh (history) zinaonyesha kwamba Allah Mtukufu amewafaradhishia waislamu swaumu ya Ramadhani. Katika mwezi wa Shaabani, mwaka wa pili wa Hijrah. Hii inamaanisha kwamba katika kipindi chote cha utume cha Makkah; kipindi cha miaka isiyopungua kumi na tatu, swaumu ilikuwa bado haijafaradhishwa. Ikaja kufaradhishwa mwaka wa pili tangu tangu Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-kuhamia Madinah.

NINI HUKUMU YA SWAUMU YA RAMADHANI NA DALILI YAKE NI IPI?

Swaumu ya Ramadhani ni mojawapo ya nguzo za Uislamu na wala haisihi kwa muislamu kulitilia shaka hilo. Kwani swaumu ya Ramadhani imethibiti kwa “nassi”-nukuu ya Qur-ani Tukufu ambayo muislamu hawi muislamu ila kwa kuiamini. Tena imethibiti kwa Sunnah Tukufu ya Mtume wa Allah na kwa Ijmaa ya wanazuoni wa Kiislamu.

Ama kuthibiti kwake katika Qur-ani kunapatikana kupitia katika kauli tukufu ya Allah: “ENYI MLIOAMINI! MMELAZIMISHWA KUFUNGA (swaumu) KAMA WALIVYOLAZIMISHWA WALIOKUWA KABLA YENU ILI MPATE KUMCHA ALLAH”. [2:183]

Na katika kauli yake: “…ATAKAYEKUWA KATIKA MJI KATIKA HUU MWEZI (wa Ramadhani) AFUNGE…” [2:185]

Na katika Sunnah swaumu ya Ramadhani imethibiti kupitia hadithi nyingi sahihi za Bwana Mtume. Miongoni mwake ni kauli yake Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie: “Uislamu umejengwa juu ya nguzo tano:

 1. Kushuhudia kwamba hapana Mola afaaye kuabudiwa kwa haki ila Allah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allah, na
 2. Kusimamisha swala, na
 3. Kutoa zakkah, na
 4. Kufunga Ramadhani, na
 5. Kuhiji nyumba ya Allah kwa mwenye kumudu gharama za njia ya kuendea huko”.

Na uma umekongamana juu ya uwajibu na ufaradhi wa swaumu ya mwezi wa Ramadhani kwa kila muislamu. Na atakayeupinga uwajibu huo, huwa amejitoa mwenyewe uislamuni. Anakuwa si muislamu tena kwa kuipinga kwake mojawapo ya nguzo za Uislamu. Imepokelewa kutoka kwa Ibn Abbas-Allah awawiye radhi-kwamba Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema: “Kishiko cha Uislamu na nguzo za dini ni tatu, juu yake (nguzo hizo) umejengwa Uislamu. Atakayeiacha moja miongoni mwake, basi yeye kwa (kuiacha nguzo) hiyo ni KAFIRI aliye halali (kumwagwa) damu (yake):

Kushuhudia kwamba hapana Mola afaaye kuabudiwa kwa haki ila Allah,

Swala za fardhi, na

Swaumu ya Ramadhani”.

Abuu Ya’alaa & Dailamiy

NINI HEKIMA/FALSAFA YA KUFARADHISHWA SWAUMU?

Allah Mtukufu amewafaradhishia waja wake ibada ya swaumu ya Ramadhani kwa hekima tukufu. Na malengo mema ambayo manufaa yake huwarejea wenyewe, hekima hizo ni pamoja na:-

Kupandikiza Ikhlaaswi na ucha-Mungu nyoyoni. Kwa sababu mfungaji hakusudii kwa swaumu yake ila radhi ya Muumba wake. Na kutumainia kupata thawabu zake na kuichelea adhabu yake. Hii ndio sababu aya inayoitaja swaumu imekhitimishwa na kauli yake Allah: “…ILI MPATE KUMCHA ALLAH…” Yaani enyi waumini kwa kuitekeleza kwenu fardhi hii ya swaumu mtajihakikishia kupata daraja ya ucha-Mungu. Na kinga ya nafsi zenu dhidi ya kila lisilolingana na kwenda sambamba na imani yenu.

Swaumu inauadilisha na kuuadabisha moyo sambamba na kuisadia nafsi kuwa katika mstari wa wima na usafi. Na inauvika moyo utoharifu na utakaso.

Swaumu inamjengea mwanadamu uwezo wa kujimiliki na kujiendesha. Na hivyo kumuwezesha kuushinda utumwa wa matamanio na matashi mabaya ya nafsi. Na kumuundia mja silaha muhimu kabisa katika maisha yake. Silaha ya subira na ujasiri mbele ya machungu na magumu yote ya maisha ambayo huja bila ya hodi wala taarifa.

Swaumu ina mchango mkubwa sana katika kumfundisha mwanadamu kiamalia (kwa njia ya matendo). Kwani ni sehemu ya maumbile ya mwanadamu kutokuijua thamani ya neema aliyonayo ila baada ya kuikosa neema husika au wakati wa kuihitajia. Mfungaji atakapoyahisi machungu ya njaa na joto la kiu. Hisia hizi zitamfanya kuitambua kiamalia hali ya mafakiri na wahitaji na hivyo kumpelekea kuwaonea huruma. Na hatimaye kuwakunjulia mkono wa msaada. Hili ndilo lililowasukuma baadhi ya wanazuoni kusema: Swaumu ni unyimi uliowekwa na sheria, kuadabishwa kwa njia ya njaa na ni unyenyekevu na kujitupa kwa Allah.

Swaumu ni tiba ya mwili iupao uimara na siha njema na pozo la baadhi ya maradhi. Kwa sababu aktharia ya watu hupatwa na maradhi kwa ajili ya israfu yao katika kula na kunywa. Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-anasema: “Mwanadamu hajapatapo kujaza chombo shari kuliko tumbo lake. Vinamtosha mwanadamu vijitonge vitakavyousimamisha uti wa mgongo wake. Ikiwa hapana budi, basi theluthi moja (ya tumbo) iwe ni ya chakula, theluthi nyingine ya maji na theluthi nyingine ya pumzi yake”. Tirmidhiy

Swaumu ya Ramadhani hulipa tumbo mapumziko ya mwezi mmoja kila mwaka. Mapumziko ambayo hupelekea kutumika kwa ziada ya chakula na mafuta iliyojikusanya mwilini kwa kipindi cha miezi kumi na moja. Ziada ambayo lau itaendelea kusalia mwilini huwa ni sababu na chanzo cha maradhi mengi ambayo yanawataabisha wengi katika wanadamu wa zama hizi.

Hizi ni baadhi ya hekima na sehemu ndogo ya falsafa ambazo kwa ajili yake Allah Mtukufu ameufaradhishia umati huu swaumu kama alivyozifaradhishia nyumati za kabla yetu. Na amesema kweli Allah pale aliposema: “ENYI MLIOAMINI! MMELAZIMISHWA KUFUNGA (swaumu) KAMA WALIVYOLAZIMISHWA WALIOKUWA KABLA YENU ILI MPATE KUMCHA ALLAH”.

MWEZI MWANDAMO WA RAMADHANI HUTHIBITIJE?

Kuingia na kuanza kwa mwezi wa Ramadhani huthibiti kwa mojawapo ya mambo mawili yafuatayo:-

Kukamilika na kumalizika kwa mwezi wa Shaabani. Siku thelethini za mwezi wa Shaabani zikikamilika, basi siku ya thelathini na moja ndio itakayokuwa siku ya kwanza ya Ramadhani kwa kutinda (kukata).

Kuona mwezi mwandamo. Ukionekana mwezi mwandamo wa Ramadhani katika usiku wa mwezi thelathini Shaabani. Ramadhani itakuwa imekwishaingia na kuwajibisha swaumu kwa mujibu wa kauli ya Allah: “…ATAKAYEKUWA KATIKA MJI KATIKA HUU MWEZI (wa Ramadhani) AFUNGE…”

Na kauli ya Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie: “Fungeni mtakapouona mwezi na fungueni mtakapouona. Na mkifunikwa na wingu (mkashindwa kuuona), basi kamilisheni idadi ya siku thelathini (za Shaabani)”. Muslim

Na kunatosha katika kuthibiti kuonekana kwa mwezi kuona kwa mtu mmoja muadilifu au watu wawili waadilifu. Kwa sababu Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alijuzisha uonaji wa mtu mmoja kwa mwezi mwandamo wa Ramadhani. Kama ilivyokuja katika hadithi sahihi iliyopokelewa na Abuu Daawoud na wengineo. Ama kuonekana kwa mwezi wa Shawwal (mfunguo mosi) kwa ajli ya kufungua, hakuthibiti ila kwa kuona mashahidi wawili waadilifu. Kwa sababu Bwana Mtume hakujuzisha kuona kwa mtu mmoja muadilifu katika mwezi wa kufungua. Kama lilivyothibiti hilo mbele za Twabaraaniy na Daaruqutwniy

TANBIHI:

Atakayeuona mwezi mwandamo wa Ramadhani kutamuwajibikia yeye kufunga hata kama ushahidi wake wa kuuona mwezi hautathibiti mbele ya kadhi na ukakataliwa. Na atakayeuona mwezi wa kufungua na ushahidi wake usikubaliwe, hatafungua kwa dalili ya kauli yake Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie: “Huko kufunga ni siku mnayofunga na kufungua ni siku mnayofungua. Na kuchinja ni siku mnayochinja”. Tirmidhiy

Ni fardhi kifaaya kwa waislamu kujishughulisha kuutafuta mwezi wa mwandamo magharibi ya siku ya ishirini na tisa ya miezi ya Shaabani (kwa kufunga). Na Ramadhani (kwa kufungua), ili wawe katika ithibati ya kuanza na kumalizika kwa swaumu na kujitoa katika shaka. Kwani imekuja katika hadithi tukufu iliyopokelewa na Bi.Aysha-Allah amuwiye radhi-kwamba Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alikuwa akijihifadhi (akijichunga) katika Shaabani zaidi kuliko anavyojihifadhi katika miezi mingine. Kisha hufunga kwa kuuona mwezi (mwandamo wa) Ramadhani. Ukimgubikia (yaani huo mwezi mwandamo wa Ramadhani) huhisabu siku thelathini (za Shaabani), kisha ndipo hufunga”.

MIONGONI MWA FADHILA ZA RAMADHANI.

Zimepokelewa hadithi nyingi katika kutaja fadhila za mwezi wa Ramadhani, miongoni mwazo ni kauli yake Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie:-

“Umekujieni mwezi wenye baraka, Allah Mtukufu amekufaradhishieni swaumu yake. Hufunguliwa ndani yake milango ya pepo na kufungwa milango ya moto na mashetani hutiwa pingu. Ndani yake kuna usiku mmoja ambao ni bora kuliko miezi alfu moja”. Ahmad, Nasaai & Al-Baihaqiy

“Hakika Allah Mtukufu amekufaradhishieni swaumu ya Ramadhani, nami nimekusunishieni kisimamo chake. Basi atakayeufunga (mwezi huo) kwa imani na kwa kutaraji malipo kwa Allah. Hutoka madhambi yake kama siku aliyozaliwa na mama yake”.

“Namuapia yule ambaye nafsi ya Muhammad iko mikononi mwake, harufu ya kinywa cha mfungaji mbele ya Allah ni nzuri zaidi kuliko harufu ya miski. Yuna mfungaji furaha mbili anazozifurahikia; anapofuturu hufurahia futari yake na atakapokutana na Mola wake ataifurahia swaumu yake.

Mbeya (aina) tatu za watu dua yao hairejeshwi:-

 1. Mfungaji mpaka afungue, na
 2. Haji mpaka arejee, na
 3. Dua ya mwenye kudhulumiwa”.

Hii ni sehemu ndogo tu ya hadithi za Mtume zilizopokelewa katika kutaja fadhila, utukufu na ubora wa mwezi wa Ramadhani. Na ikiwa hizo ndizo thawabu za wafungaji wa mwezi huu kwa imani, kwa kutarajia malipo ya Allah, kwa kutumai kupata radhi yake na kwa kuichelea adhabu yake. Basi bila ya shaka khasara ya wasiofunga katika mwezi huu bila ya udhuru unaozingatiwa kisheria. Hakuna aijuaye khasara yao hiyo ila Allah pekee ambaye ndiye atakayeilipa kila nafsi kwa yote iliyoyatenda.

NGUZO ZA SWAUMU, SHARTI ZA KUSIHI SWAUMU NA SWAUMU NI WAJIBU KWA NANI?

NGUZO ZA SWAUMU:

Swaumu ya Ramadhani ina nguzo kuu mbili za msingi, ambazo kusihi kwa swaumu kunazitegemea.

Kujizuia na yote yenye kufunguza tokea kuchomoza kwa alfajiri mpaka kuzama kwa jua, kwa ushahidi wa neno lake Allah Mtukufu: “…NA KULENI NA KUYWENI MPAKA UBAINIKE KWENU WEUPE WA ALFAJIRI KATIKA WEUSI WA USIKU. KISHA TIMIZENI SWAUMU MPAKA USIKU…” [2:187]

Nia, kwa maana ya muislamu kunuia kufunga mwezi wa Ramadhani. Na nia mahala pake ni moyoni na sio lazima kama ambavyo si vibaya kuitamka kwa ulimi. Na jopo la mafaqihi linaona ni wajibu kuileta nia katika kila usiku wa Ramadhani kabla ya kuchomoza kwa alfajiri. Huku ni kuifanyia kazi kauli yake Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie: “Asiyeleta nia ya swaumu usiku, hana swaumu”. Tirmidhiy

Na uwajibu huu wa nia ni kwa upande wa swaumu ya fardhi tu. Ama swaumu za suna, nia inatosha hata baada ya kuingia kwa mchana maadamu mtu hajatenda lo lote miongoni mwa yabatilishayo swaumu. Kwani imepokelewa kutoka kwa Bibi Aysha-Allah amuwiye radhi-kwamba Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-aliingia kwake siku moja na kuuliza: “Je, mna cho chote?” Nikamjibu: Hapana, akasema: “Basi hakika mimi nimefunga”. Muslim

SWAUMU NI WAJIBU KWA NANI?

Mafaqihi wamekongamana kwamba swaumu ya Ramadhani ni wajibu kwa kila:-

 • Muislamu,
 • Mwenye akili timamu,
 • Baleghe (mtu mzima),
 • Asiye na udhuru wenye kumuhalalishia kula.

Sharti hizi za kuwajibisha swaumu ya Ramadhani kwa mja, mafaqihi wamezichimbua katika kauli yake Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie: “Kalamu imeondoshwa kwa mbeya (aina) tatu za watu:

 1. Kwa mwendawazimu mpaka arudiwe na akili, na
 2. Kwa mtu aliyelala mpaka aamke, na
 3. Kwa mtoto mdogo mpaka afikiliye baleghe”.

Ahmad & Abuu Daawoud

Na kauli yake Bwana Mtume katika kubainisha upungufu wa dini kwa mwanamke: “Je, hakuwa anapoingia hedhini haswali na hafungi?” Bukhaariy

UFAFANUZI:

Ama sharti ya Uislamu ni kwa sababu Uislamu ndio msingi mkuu wa taklifu (kulazimiwa na hukumu za sheria) kwa mja. Baleghe (ukubwa) kwa sababu ndio wakati/mahala ambapo taklifu huanza kwa mja. Akili timamu ni kwa sababu ndio chombo kinachomuwezesha mja kumaizi na kutambua mambo. Na ama kutokuwa na udhuru ni kwamba katika jumla ya fadhila zake Allah kwa waja wake. Ni kuyaondoshea ufaradhi wa swaumu baadhi ya makundi ya waja wake. Mara nyingine uondoshaji huo unakuwa ni kwa njia ya wajibu wa muda maalumu kama ilivyo kwa mwanamke mwenye hedhi au nifasi. Hawa ni haramu kwao kufunga katika kpindi chote cha hedhi/nifasi mpaka watakapotwaharika. Na wakati mwingine huwa ni kwa ajili ya rukhsa maalumu (msamaha wa Allah) kama ilivyo kwa mgonjwa, msafiri, kikongwe na wengineo kama tutakavyowabainisha baadaye-Inshaallah Taala.

SHARTI ZA KUSIHI SWAUMU:

Na mambo manne haya tuliyoyataja yaani Uislamu, baleghe, akili timamu na kutokuwa na udhuru uhalalishao kula, ndio sharti za kuwajibisha swaumu. Na wakati huo huo yanafaa kuwa sharti za kusihi kwa swaumu. Ila baadhi ya mafaqihi wameongezea sharti nyingine ya tano nayo ni kuwa wakati uwe unaruhusu kufunga. Kwani hakusihi kufunga katika siku za Idi mbili; Idi ya mfunguo mosi na ile ya mfunguo tatu. Wala katika zile siku tatu za kuanika nyama ambazo ni mwezi kumi na moja, kumi na mbili na kumi na tatu katika mfunguo tatu. Kwa sababu ni haramu kufunga katika siku hizi.

HUKUMU YA SWAUMU KWA WATOTO.

Watoto ambao hawajafikilia umri wa baleghe si WAJIBU kwao swaumu ya Ramadhani. Lakini ni jukumu la wazazi kuwazoesha kidogo kidogo kufunga tangu wadogo, ili wainukie na mazoea ya ibada ukubwani. Kwani imepokewa kutoka kwa Rubayyi Bint Muaadh-Allah amuwiye radhi-amesema: Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alipeleka salamu mchana wa siku ya Ashura katika vitongoji vya Answaari akisema: “Aliyepambazukiwa hali ya kuwa kafunga, basi na aitimize swaumu yake. Na aliyepambazukiwa ilhali hakufunga, basi na afunge baki ya siku yake”. Tukawa tukiifunga siku hiyo (ya Ashura) baada ya hapo na tukiwafungisha watoto wetu wadogo. Na tukienda msikitini na kuwafanyia wanasesere wa sufi, mmoja wao akililia chakula tunampa (mwanasesere huyo kuchezea)”. Bukhaariy & Muslim

Hadithi hii sahihi inafahamisha kwamba hakuna kizuizi kuwazoesha watoto wadogo kufunga kabla ya kufikilia umri wa kubaleghe; umri wa taklifu. Lakini iwe ni kwa hatua baada ya hatua.

HUKUMU YA KUFUNGA SIKU YA SHAKA.

Makusudio ya “siku ya shaka” ni mwezi thelathini Shaabani iwapo mwezi haukuandama usiku wa kuamkia siku hiyo. Ikaingia shaka je, siku hiyo ni mwezi thelathini Shaabani au ni mwezi mosi Ramadhani? Basi ni karaha/haramu kufunga siku hii ila itakapowafikiana na ada ya mtu ya kufunga, hapo si karaha wala haramu. Hii ni kama vile mtu kuwa na mazoea ya kufunga suna za Jumatatu na Alkhamisi, na siku ya shaka ikaangukia katika mojawapo ya siku mbili hizi. Na sababu ya ukaraha huu wa kufunga siku ya shaka ni kule kupingana kwake na kauli yake Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie: “Fungeni kwa kuuona (mwezi mwandamo wa Ramadhani) na fungueni kwa kuuona (mwezi mwandamo wa Shawwal). Na mkifunikwa na wingu (mkashindwa kuuona), basi kamilisheni idadi ya siku thelathini za Shaabani”.

Na kwa sababu ya kauli yake: “Msiitangulie swaumu ya Ramadhani kwa (kufunga) siku moja au siku mbili (kabla yake). Ila iwe ni swaumu anayoifunga mtu (kwa ada), basi na afunge siku hiyo”. Tirmidhiy, Ahmad, Bukhaariy, Muslim, Abuu Daawoud, Nasaai & Ibn Maajah.

NYUDHURU ZINAZOMUHALALISHIA MTU KUACHA KUFUNGA.

Allah Mtukufu ameiasisi na kuisimamisha sheria ya kiislamu juu ya misingi ya wepesi, huruma, kuondosha uzito na madhara na kuwakalifisha watu lililomo katika uweza wao. Hili linashuhudiwa na kauli tukufu za Allah: “…ALLAH ANAKUTAKIENI YALIYO MEPESI WALA HAKUTAKIENI YALIYO MAZITO…” [2:185]

“…HAPENDI ALLAH KUKUTIENI KATIKA TAABU, BALI ANATAKA KUKUTAKASENI NA KUTIMIZA NEEMA YAKE JUU YENU ILI MPATE KUSHUKURU”. [5:6]

“ALLAH ANATAKA KUKUKHAFIFISHIENI MAANA MWANADAMU AMEUMBWA DHAIFU”. [4:28]

“ALLAH HAIKALIFISHI NAFSI YO YOTE ILA YALIYO SAWA NA UWEZA WAKE…” [2:286]

Na Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema: “Hakika dini hii ni nyepesi na hakuna ye yote atakayeitilia mikazo ila itamshinda tu…”

Allah Mtukufu kwa fadhila na huruma yake kwa waja wake amewahalalishia baadhi ya watu kula katika mwezi wa Ramadhani, kwa sababu zinazowalazimisha kutokufunga. Watu hawa wenye kibali cha Mola wao kinachowahalalishia kutokufunga wanagawika katika makundi kadhaa kama ifuatavyo:-

WALIOPEWA RUKHSA YA KULA NA KUWAJIBISHIWA KUKIDHI SIKU WALIZOKULA BAADA YA KUONDOKEWA NA UDHURU:

Kundi hili linawajumuisha:-

 • Wagonjwa wanaougua maradhi ambayo hutarajiwa kutibika na kupona baada ya kupata tiba. Na wanachelea swaumu itawazidishia maradhi au kuchelewesha kupona au itawapa taabu kubwa.
 • Wasafiri kwa sharti safari hiyo iwe ni ya
 • Halali,
 • Inaruhusiwa kupunguza swala ndani yake,
 • Ianze mchana.
 • Wanawake wajawazito na wale wanyonyeshao. Hawa wamehalalishiwa kula kwa ajili ya kuwaondoshea uzito.

WALIOPEWA RUKHSA YA KULA NA KUWAJIBISHIWA KUTOA FIDIA.

Walio chini ya kundi hili ni:-

Wagonjwa walio na maradhi ambayo hayatarajiwi kupona. Hawa ni kama vile wagonjwa wa saratani (cancer), kifua kikuu kilichopevuka (T.B.), kisukari (diabetes) na maradhi mengine kama haya.

Watu wazima vikongwe wenye umri mkubwa sana ambao wamekuwa kama watoto wadogo. Hawa wamehalalishiwa kula na kutoa fidia kwa kumlisha masikini chakula kwa kila siku au kumpa thamani ya chakula hicho. Na hiyo fidia ni kutoa kibaba kimoja cha chakula rasmi cha mahala pale, mithili ya mchele kwa ukanda huu wa pwani ya Afrika Mashariki. Na kibaba ni sawasawa na robo tatu ya kilo takriban.

C: WALIOWAJIBISHIWA KUKIDHI NA KUTOA KAFARA NA HEKIMA/FALSAFA YA KAFARA.

Kafara ni lile lifanywalo kwa ajili ya kufuta dhambi itokanayo na kukhalifu sheria. Ye yote atakayeikhalifu sheria kwa

 • Kumuingilia mkewe katika mchana wa Ramadhani.
 • Kula au kunywa kwa makusudi bila ya kuwa na udhuru unaozingatiwa kisheria.

Atalazimika kutoa kafara kwa mujibu wa sheria, mbali ya dhambi iandamiayo tendo hilo la mukhalafa wa sheria.

Na kafara ya huku kukhalifu sheria ni kutenda mojawapo ya mambo matatu haya:-

 • Kumuacha huru mtumwa muislamu, au
 • Kufunga miezi miwili mfululizo, au
 • Kuwalisha masikini sitini, kila mmoja kibaba kimoja cha chakula.

FALSAFA YA KAFARA.

Falsafa ya kuwekwa kafara hii ni kuilinda na kuihifadhi sheria dhidi ya kuchezewa na kuvunjwa hovyo kwa matashi ya mtu. Pia inamtwaharisha muislamu kutokana na dhambi ya kukhalifu sheria aliyoitenda bila ya udhuru.

HUKUMU YA ALIYEKUFA KABLA YA KUKIDHI SWAUMU YA RAMADHANI.

Mtu atakayekufa kabla ya kumakinika kukidhi siku alizokula ndani ya mwezi wa Ramadhani, kwa sababu ya udhuru unaozingatiwa kisheria. Walii wake miongoni mwa wenye haki ya kumrithi, au jamaa yake au ye yote anayehusiana na marehemu huyu, atamfungia. Na akimfungia pamoja na kumlishia chakula ni bora zaidi ikiwa anaweza kufanya hivyo. Imepokelewa kutoka kwa Ibn Abbas-Allah awawiye radhi-“Kwamba mtu mmoja alikuja kwa Mtume-Rehema na Amani zimshukie-akasema: Ewe Mtume wa Allah! Hakika mama yangu amekufa na ilhali anawiwa na swaumu ya mwezi (Ramadhani), basi je, nimkidhie? (Mtume) akamwambia: Lau mama yako angekuwa na deni ungemlipia? Akajibu: Naam, Mtume akamwambia: Basi deni la Allah linastahiki zaidi kulipwa”. Ahmad, Abuu Daawoud, Tirmidhiy, Ibn Maajah & wengineo.

SUNA ZA SWAUMU NA ADABU ZAKE.

Siku zote mtu mwenye akili huhangaika na kupupia kufikia ukamilifu katika utekelezaji wa ibada zake na baki ya mambo yake mengine. Na kila muislamu anatambua kwamba swaumu ni miongoni mwa ibada tukufu zenye daraja kubwa mbele za Allah. Kwa hiyo basi, inamuwajibikia kila muislamu kuitekeleza ibada hii kwa namna ambayo itakusanya kwa pamoja dhana ya uchaji-Mungu, unyenyekevu na kumuunganisha na Mola wake. Ili kuyafikia hayo, mfungaji anatakiwa kuyachunga na kuyatekeleza mambo haya yaliyosuniwa katika swaumu:-

KUHARAKIA KUFUTURU:

Ni suna kufanya haraka kufuturu baada ya kuwa na yakini kuwa jua limezama. Huku ni kuifanyia kazi kauli ya Bwana Mtume-rehema na Amani zimshukie: “Watu wataendelea kuwa katika kheri muda wa kuharakia kufuturu”. Bukhaariy & Muslim

KUFUTURU KWA TENDE:

Mara nyingi Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alikuwa akifuturu kwa kula tende au funda ya maji kama hakupata tende. Haya ni kwa mujibu wa riwaya iliyopokelewa kutoka kwa Bwana Mtume: “Atakapofuturu mmoja wenu, basi na afuturu kwa tende kwani hiyo ni baraka. Na asiyepata (tende), basi na afuturu kwa kunywa maji, kwani hayo ni twahara”. Abuu Daawoud & Tirmidhiy

Kufuturu huku kwa tende au maji au kitu cho chote chenye kufanana na hivyo kuwe ni kabla ya kuswali Magharibi. Kisha ndipo aswali na baada ya swala ndio aende kupata futari yake kamili, hivi ndivyo alivyofanya Bwana Mtume.

KUOMBA DUA:

Inatakikana kwa mfungaji kumuomba Allah mambo ya kheri wakati wa kufuturu bali katika kipindi chote cha swaumu. Imepokelewa kutoka kwa Ibn Umar-Allah awawiye radhi-amesema: “Mtume-Rehema na Amani zimshukie-alikuwa anapofuturu husema: DHAHABAD-DHWAMAU, WABTALLATIL-URUUQ, WATHABATAL-AJRU INSHAALLAH (Kimeondoka kiu, mishipa imerowa na ujira umethibiti apendapo Allah)”. Abuu Daawoud

KULA DAKU:

Ni suna mfungaji kula daku kwa mujibu wa kauli yake Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie: “Kuleni daku kwani mna baraka katika daku”. Bukhaariy & Muslim

Na imependelewa kuakhirisha kula daku kiasi ambacho mfungaji atakapomaliza kula daku iwe imebakia saa moja au chini yake kabla ya kuingia alfajiri. Imepokelewa kutoka kwa Zayd Ibn Thaabit-Allah amuwiye radhi-amesema: “Tulikula daku pamoja na Mtume-Rehema na Amani zimshukie-kisha akainuka kwenda kuswali (yaani swala ya alfajiri). Akauliza muulizaji: Kulikuwa na muda gani baina ya adhana (ya alfajiri) na daku? Akajibu: Kiasi cha (mtu) kusoma aya khamsini”. Bukhaariy & Muslim

KUJIEPUSHA NA MANENO YA FEDHULI NA VTENDO VYA KIPUUZI:

Miongoni mwa adabu ambazo mfungaji anatakiwa kujipamba nazo ni kuuzuia ulimi wake kutamka maneno ya kifedhuli na kipuuzi. Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema: “Asiyeacha maneno ya uwongo (uzushi) na kuyafanyia kazi, Allah hana haja na kuacha kwake chakula chake na kinywaji chake”. Bukhaariy

“Atakapopambazukiwa mmoja wenu siku moja ilhali amefunga, basi asitamke maneno machafu na wala asifanye upumbavu. Basi iwapo mtu atamtukana au kugombana naye na aseme: Hakika mimi nimefunga, hakika mimi nimefunga”. Bukhaariy & Muslim

KUJIPAMBA NA UKARIMU, KUKITHIRISHA KUSOMA QURAN, KUUPISHA TOBA, KUDUMISHA ISTIGHFAARI NA KUJITAHIDI KATIKA IBADA KHASA KHASA KATIKA KUMI LA MWISHO:

Haya ni katika jumla ya mambo mema mazuri ambayo mfungaji anapaswa kujipamba nayo ndani ya mwezi mtukufu wa Ramadhani. Na kuendelea kuishi nayo nje ya Ramadhani.

Imepokelewa kutoka kwa Ibn Abbas-Allah amuwiye radhi-amesema: “Alikuwa Mtume-Rehema na Amani zimshukie-mkarimu kushinda watu wote kwa kheri na alikuwa mkarimu mno katika Ramadhani kuliko katika miezi mingine…” Bukhaariy

Imepokelewa kutoka kwa Bibi Aysha-Allah amuwiye radhi-kwamba Mtume-Rehema na Amani zimshukie: “Alikuwa linapoingia kumi la mwisho uhuhisha usiku (hukesha kwa ibada) na huwaamsha wakeze (kufanya ibada) na hufunga kibwebwe” Bukhaariy & Muslim

Kwa ujumla mwezi wa Ramadhani ni mwezi wa kheri, subira, ukarimu na baraka. Kwa hivyo inatupasa tuitumie vema fursa ya mwezi huu ambayo hupatikana mara moja tu kila mwaka. Tuitumie fursa hii katika kuziadabisha na kuziadilisha roho zetu na kuzitwaharisha nyoyo na nafsi zetu. Na kuvizuilia viungo vyetu na kila ovu na kuiendea kwa upeo wa jitihada zetu zote kila ibada na mambo ya twaa. Ili tuwe kwa fadhila zake Allah miongoni mwa waja wake atakaowaridhia na wao kuyaridhia malipo na jazaa maridhawa atakazowapa.

MAMBO YENYE KABATISHA SWAUMU.

Mambo yenye kubatilisha swaumu ya mfungaji yanagawika katika makundi mawili haya:-

YENYE KUBATILISHA SWAUMU NA KUWAJIBISHA KADHAA (KULIPA).

Mambo yaliyo chini ya kundi hili ni pamoja na

Kula au kunywa kwa makusudi. Mfungaji akila au kunywa kwa kukusudia, pale pale swaumu yake itabatilika na atawajibika kuikidhi. Lakini iwapo alikula au kunywa kwa kusahau, basi hana kadhaa wala kafara. Haya ni kwa mujibu wa kauli yake Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie: “Atakayesahau na ilhali ana swaumu, akala au kunywa, basi na aitimize swaumu yake. Hakika si vinginevyo, Allah ndiye aliyemlisha na kumnywesha”. Tirmidhiy, Bukhaariy, Muslim & wengineo.

Kujitapikisha kwa makusudi pia kunaiharibu swaumu ya mfungaji na kumuwajibishia kadhaa. Lakini iwapo atatapika na si kujitapikisha, haitamuwajibikia kadhaa wala kafara. Imepokelewa kwamba Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema: “Yatakayemshinda matapishi (yakamtoka bila khiari), hakuna kadhaa juu yake. Na atakayejitapikisha kwa makusudi basi na akidhi”. Ahmad, Abuu Daawoud, Tirmidhiy, Ibn Maajah, Ibn Hibban & Al-Haakim.

Hedhi na nifasi hata kama imetoka katika kipindi kifupi tu kabla ya kuchwa (kuzama) kwa jua. Hili ni kwa mujibu wa IJMAA ya wanazuoni.

Kujitoa manii kwa kupiga punyeto, kumbusu au kumkumbatia mke, hili pia linabatilisha swaumu.

TANBIHI:

Ikiwa manii yatatoka mchana kwa sababu ya kuangalia tu, swaumu haitabatilika na hakitomuwajibikia cho chote zaidi ya kukoga janaba.

Hali kadhalika kutoka kwa madhii pia hakuiathiri swaumu kwa cho chote bila ya kujali kuwa ni mengi au machache.

v. Mfungaji kuingiza kitu katika uwazi wa ndani kwa

khiyari yake mwenyewe kupitia tundu zilizo wazi.

Mithili ya masikio, pua, tundu ya nyuma na

kadhalika. Kitu hicho kikawa ni chakula, kinywaji, dawa na mfano wa hivyo.

Na ni wajibu kwa mtu aliyeifisidi swaumu yake na kuwajibikiwa na kadhaa, kwa sababu ya kutenda mojawapo ya mambo madhukuru (tajwa) haya. Kufanya haraka kuzikidhi siku zote alizofungua, hii ni kwa sababu umri wake u mikononi mwa Allah.

YENYE KUBATILISHA SWAUMU NA KUWAJIBISHA KADHAA SAMBAMBA NA KAFARA.

Kundi hili linahodhi jambo moja tu, nalo ni kumuingilia mke katika mchana wa Ramadhani katika mazingira ya khiari. Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah-Allah amuwiye radhi-amesema: Alikuja mtu mmoja kwa Mtume-Rehema na Amani zimshukie-akasema: Nimehiliki ewe mtume wa Allah. (Mtume) akamuuliza: Ni lipi lililokuhilikisha? Akajibu: Nimemuingilia mke wangu katika (mchana wa) Ramadhani. (Mtume) akamuuliza: Je, una uwezo wa kumuacha huru mtumwa? Akajibu: Hapana sina. Akamuuliza (tena): Je, unaweza kufunga miezi miwili mfululizo? Akajibu: Hapana. Akasema (mpokezi): Kisha akakaa, Mtume-Rehema na Amani zimshukie-akaja na kapu la tende, akasema: Kalitoe hili sadaka. Akasema: Je, yuko fakiri zaidi kuliko sisi? Mtume-Rehema na Amani zimshukie-akacheka mpaka magego yake yakaonekana na akamwambia: Nenda ukawalishe watoto wako” Bukhariy, Muslim, Tirmidhiy & wengineo

——————————————————————————————————

IBADA YA ITIKAFU.

MAANA YA ITIKAFU:

Kilugha neno “Itikafu” lina maana kuu mbili, kama zifuatazo:

Kuzuia, na

Kukaa.

Kisheria “Itikafu” ni: Kitendo cha kukaa msikitini kwa mfumo maalumu uambatanao na nia ya kujikurubisha kwa Allah, kwa kutekeleza ibada mbali mbali.

HUKUMU YA ITIKAFU:

Itikafu ni ibada ya SUNAH katika wakati wo wote na imekokotezwa sana katika kumi la mwisho la mwezi wa Ramadhani. Na itikafu kwa upande mwingine inaweza kuchukua hukumu ya UWAJIBU, hii ni iwapo mtu atajiwajibishia mwenyewe. Mtu atakaposema nimenuia kukaa itikafu siku moja au mbili iwapo nitapata mtoto mathalan. Katika mazingira haya itikafu itakuwa imekwisha kuwa wajibu juu yake. Kwa sababu ya msingi usemao:(Kutekeleza nadhiri ni wajibu). Imepokelewa kwamba Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-amesema: “Mwenye kutia nadhiri ya kumtii Allah, basi na amtii”. Bukhaariy

DALILI YA ITIKAFU:

Ibada hii ya itikafu imethibiti ndani ya Qur-ani Tukufu, suna ya Mtume na Ijmaa ya wanazuoni. Allah Mtukufu anasema: “…WALA MSICHANGANYIKE NAO, NA HALI MNAKAA ITIKAFU MISIKITINI. HIYO NI MIPAKA YA ALLAH, BASI MSIIKARIBIE…” [2:187]

Yaani Allah Mtukufu anawaamrisha waja wake waumini kutokuwaingilia wake zao katika kipindi chote cha kukaa kwao itikafu msikitini. Na katika sunah, imepokewa kutoka kwa Bibi Aysha-Allah amuwiye radhi-amesema: “Mtume-Rehema na amani zimshukie-alikuwa akikaa itikafu katika kumi la mwisho la Ramadhani…” Bukhaariy & Muslim

SHARTI ZA KUSIHI ITIKAFU:

Ili itikafu ya mja isihi kisheria ni wajibu zipatikane sharti zifuatazo:-

Nia, kwa sababu amali zote hufungama na nia kama ilivyothibiti katika hadithi sahihi.

Twahara ya hadathi kubwa. Itikafu haisihi kwa mtu mwenye janaba, mwenye hedhi na mwenye nifasi.

Itikafu ifanyike msikitini kwa ushahidi wa kauli tukufu ya Allah: “…WALA MSICHANGANYIKE NAO, NA HALI MNAKAA ITIKAFU MSIKITINI…”

TANBIHI:

Mwanamke ana haki ya kukaa itikafu msikitini kama aliyo nayo mwanamume. Ila tu haki yake hii ni lazima ipate idhini ya mumewe akiwa ni mke wa mtu. Au walii wake kama si mwanandoa. Na sharti akae itikafu katika mahala palipotengwa kwa ajili ya wanawake msikitini humo. Hii ni kwa sababu wakeze Mtume-Allah awawiye radhi-walikuwa wakikaa itikafu msikitini na katika mahala palipotengwa kwa ajili yao.

YENYE KUBATILISHA ITIKAFU:

Ibada ya itikafu huwa ni batili mbele ya sheria, iwapo muhusika wa ibada hii atafanya mojawapo ya mambo haya:-

Kumuingilia mkewe.

Kutoka msikitini bila ya dharura ya msingi.

Kuondokewa na akili kwa kupatwa na wazimu, kulewa na baki ya mambo mengine.

Kupatwa na hedhi au nifasi.

TANBIHI:

Kutoka msikitini kwa ajili ya kwenda kukidhi haja ya kimaumbile kama kukidhi haja ndogo/kubwa. Kukoga na kununua mahitaji yake ya lazima mithili ya chakula, kinywaji na mengineyo. Haya yote hayabatilishi ibada ya itikafu, kwani imepokelewa kutoka kwa Bibi Aysha-Allah amuwiye radhi-amesema: “Mtume-Rehema na Amani zimshukie-alikuwa anapokaa itikafu haingii nyumbani ila kwa haja ya mwanadamu”. Bukhaairy & Muslim

YALIYOSUNIWA KUTENDWA NA MKAA ITIKAFU:

Mwenye kukaa itikafu ni suna kwake kukithirisha:-

Ibada mbali mbali za suna.

Kusoma Qur-ani Tukufu.

Kuleta nyiradi mbali mbali (kumdhukuru Allah kwa wingi)

Kuleta istighfaari (kumuomba Allah msamaha wa dhambi).

Kumswalia Bwana Mtume.

Kuomba dua.

Na baki ya mambo mengine ya twaa ambayo yanamkurubisha mja na kumuunga na Mola wake.

USIKU WA CHEO/MTUKUFU (LAYLATUL-QADRI).

Kama ambavyo Allah Mtukufu amemkirimu Mtume wake katika mwezi wa Rajabu kwa kumpeleka safari tukufu ya Israa na Miiraji. Na kama ambavyo amemkirimu katika mwezi wa Shaabani kwa kumbadilishia Qiblah kutoka msikiti wa Baytul-Maqdis kwenda msikiti mtukufu wa Makah. Ndivyo hivyo amemkirimu katika mwezi wa Ramadhani kwa kumpa usiku mtukufu. Uliotukuzwa na kupewa hishima ya kushushwa Qur-ani Tukufu ndani yake. Kuhusiana na hili Allah Mtukufu anasema: “ HAKIKA TUMEITEREMSHA (Qur-ani) KATIKA LAYLATUL-QADRI (usiku wenye hishima kubwa). NA JAMBO GANI LITAKALOKUJULISHA (hata ukaujua) NI NINI HUO USIKU WA LAYLATUL-QADRI? HUO USIKU WA HISHIMA (huo) NI BORA KULIKO MIEZI ELFU. HUTEREMKA MALAIKA NA ROHO MUAMINIFU (JibriIi) KATIKA (usiku) HUO KWA IDHINI YA MOLA WAO KWA KILA JAMBO. NI AMANI (usiku) HUO MPAKA MAPAMBAZUKO YA ALFAJIRI”. [97:1-5]

WAKATI WAKE:

Laylatul-Qadri inatarajiwa sana kuwa inapatikana katika kumi la mwisho la mwezi wa Ramadhani. Ni kwa ajili hii ndio kukasuniwa kukaa itikafu ndani ya kumi hili la mwisho ili kuuzengea usiku huu mtukufu. Usiku ambao ibada ifanywayo humo ni bora zaidi kiujira kuliko ibada ya miezi alfu moja isiyo na Laylatul-Qadri.

Imepokelewa kutoka kwa Bibi Aysha-Allah amuwiye radhi-amesema: “Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alikuwa akikaa itikafu katika kumi la mwisho la Ramadhani na akisema: “Izengeeni (itafuteni) Laylatul-Qadri katika kumi la mwisho la Ramadhani”.

Na katika riwaya yake nyingine, Bibi Aysha amesema: “Alikuwa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-linapoingia hilo kumi (la mwisho) uhuhisha usiku. Na akawaamsha wakeze na akajipinda na kujifunga kibwebwe (katika kufanya ibada) mpaka Allah alipomfisha. Kisha wakeze wakakaa itikafu baada yake”.

KUUHUHISHA USIKU HUU KWA IBADA:

Kuuhuhisha usiku huu kwa kufanya aina kwa aina za ibada ni suna. Kwa sababu hivyo ndivyo alivyofanya Bwana Mtume, wakeze na maswahaba wake. Na hekima ya kuuhuhisha usiku huu kwa ibada ni kuikumbuka neema ya Allah kwa waja wake. Neema ya kushushwa Qur-ani Tukufu ndani yake, muongozo wa watu uliosheheni kheri za ulimwengu na akhera yao. Ikiwa Allah Mtukufu ameutukuza usiku huu wa cheo hata akashusha sura nzima ndani ya Qur-ani kwa jina la usiku huu. Basi ni wajibu wetu sisi kama waislamu kuujua utukufu, cheo, hishima, umuhimu na thamani ya usiku huu kwetu. Tulionyeshe hili kwa kupupia kuuhuhisha usiku huu kwa kila aina za ibada na kujikurubisha kwa Allah. Muislamu mwenye akili, mkamilifu wa imani ni yule anayeuzengea usiku huu na kuuhuhisha kwa ibada.

Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema: “Atakayesimama (kufanya ibada) usiku wa Laylatul-Qadri kwa imani na kutaraji malipo ya Allah, atafutiwa dhambi zake zilizotangulia”. Bukhaariy & Muslim

ZAKAATUL-FITRI.

ZAKAATUL-FITRI NI NINI?

Zakaatul-fitri ni kile chakula au thamani ya chakula hicho anachokitoa mtu ndani ya mwezi wa Ramadhani na kuwapa mafakiri na wenye shida kabla ya Eidil-Fitri.

NINI HUKUMU YAKE?

Zakaatul-Fitri ni FARDHI mbele ya kundi kubwa la wanazuoni (jopo la wataalamu wa fani ya Fiq-hi). Ufaradhi huu unatokana na hadithi iliyopokelewa kutoka kwa Ibn Umar-Allah awawiye radhi-kwamba yeye amesema: “Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-AMEFARADHISHA Zakaatul-Fitri ya Ramadhani. Pishi ya tende au pishi ya shayiri, kwa mtumwa na muungwana, mwanamume na mwanamke, mtoto na mkubwa katika waislamu. Na ameamrisha itolewe kabla ya watu kutoka kwenda kuswali (yaani swala ya Eid)”. Bukhaariy & Muslim

Bwana Mtume ameifaradhisha Zakaatul-Fitri na kuamrisha itolewe katika mwaka ule ule uliofaradhishwa swaumu ya Ramadhani. Yaani katika mwezi wa Shaaban, mwaka wa pili wa Hijrah.

NINI FALSAFA/HEKIMA YAKE?

Zakaatul-Fitri imefaradhishwa kwa hekima nyingi, miongoni mwake ni:-

Kuwasaidia wenye shida katika siku ya sikukuu ili furaha ienee kwa watu wote.

Kuunga mapungufu na kuziba makosa yanayoweza kuwa yamemtokea mtu katika swaumu yake.

Haya tunayafahamu kupitia hadithi ya Ibn Abbas-Allah awawiye radhi-kwamba yeye amesema: “Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alifaradhisha Zakaatul-Fitri ili kumtwaharisha mfungaji kutokana na maneno na matendo machafu. Na ili iwe chakula kwa masikini, atakayeitoa kabla ya swala basi hiyo ndiyo zaka yenye kukubaliwa. Na atakayeitoa baada ya swala, basi hiyo ni sadaka kama sadaka nyinginezo”. Abuu Daawoud

INAMUWAJIBIKIA NANI?

Zakaatul-Fitri ni wajibu kwa kila muislamu, mwenye uwezo wa kutoa hata kama hamiliki kiwango cha zaka ya fardhi. Mwenye kumiliki chakula chake na familia yake cha siku ya Eid, kinachozidi hapo ni wajibu akitoe kama Zakaatul-Fitri. Atajitolea yeye mwenyewe na watu wote ambao chakula chao cha kila siku kinamuwajibikia yeye. Hawa ni pamoja na wanawe ambao bado wanamtegemea yeye, wazazi wake, mkewe na wale wote walio chini ya ulezi wake kwa njia ya wajibu na wala sio kwa njia ya ihsaani/ khiari.

NINI KITOLEWACHO?

Zimepokewa hadithi nyingi sahihi zinazoweka wazi alichowaamrisha Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-maswahaba wake kukitoa kwa ajili ya Zakaatul-Fitri. Miongoni mwa hadithi hizo ni ile iliyopokelewa kutoka kwa Abuu Saaid Al-khudriy-Allah amuwiye radhi-amesema: “Tulikuwa wakati alipokuwa miongoni mwetu Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-tukimtolea Zakaatul-Fitri kila mkubwa na mdogo. Kibaba cha chakula, au kibaba cha shayiri, au kibaba cha zabibu au kibaba cha maziwa ya unga”. Bukhaariy & Muslim

Na imepokelewa kutoka kwa Abdillah Ibn Tha’alabah-Allah amuwiye radhi-amesema: “Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alikhutubu siku moja au mbili kabla ya Eid akasema: Toeni kibaba cha ngano, au kibaba cha tende au cha shayiri. (Mtoleeni) kila muungwana au mtumwa, mkubwa au mtoto”. Abuu Daawoud

Mafaqihi wamesema mazingatio katika kutoa ni kuangalia chakula rasmi cha mahala husika, chakula kitumiwacho katika dhifa na shughuli zao mbali mbali. Na kibaba kwa kipimo cha kilogramu ni sawa na ¾ ya kilogramu moja. Hiki ndicho kipimo kinachopaswa kutolewa kwa kila kichwa kimoja.

ITOLEWE LINI?

Wakati bora kabisa wa kutoa Zakaatul-Fitri ni ule usiku wa kuamkia siku ya Eid. Na ni wajibu itolewe kabla ya kuswaliwa swala ya Eid. Na wajibu wa kutoa haupomoki/hauondoki kwa sababu ya kuchelewa kutoa. Bali itakuwa ni deni iliyo katika dhima ya aliyewajibikiwa kutoa. Na itamlazimu kulipa deni hilo hata mwishoni mwa umri wake, kwa sababu aliwajibikiwa na akafanya uzembe kutoa. Na haisihi kuchelewa kutoa bila ya dharura na ni haramu kisheria. Kwa sababu ucheleweshaji huu unapelekea kupotea kwa lengo la utoaji wake ambalo ni kuondosha uhitaji wa masikini katika siku ile ya furaha. Ambao Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-amelizungumzia suala lao kwa kusema: “Watosheeni na udhalili wa kuomba katika siku hii”. Yaani siku ya Edil-Fitri.

APEWE NANI?

Wanaopaswa kupewa Zakaatul-Fitri ni wale wale wenye sifa ya kupewa Zaka ya faradhi ambao wametajwa katika kauli yake Allah: “SADAKA HUPEWA (watu hawa): MAFAKIRI NA MASIKINI NA WANAOZITUMIKIA NA WANAOTIWA NGUVU NYOYO ZAO (juu ya Uislamu) NA KATIKA KUWAPA UUNGWANA WATUMWA NA KATIKA KUWASAIDIA WENYE DENI NA KATIKA (kutengeneza) MAMBO ALIYOAMRISHA ALLAH NA KATIKA (kupewa) WASAFIRI (walioharibikiwa) NI FARDHI INAYOTOKA KWA ALLAH, NA ALLAH NI MJUZI (na) MWENYE HEKIMA”. [9:60]

Lakini masikini na mafakiri ndio walengwa khasa wa Zaakatul-Fitri kuliko mafungu mengine yaliyotajwa.

———————————————————————————————

SOKO LA RAMADHANI HILOO LINAFUNGULIWA

Ndugu zangu Waislamu

Assalaam alaykum wa Rahmatullahi wa Barakatuh

Soko la Ramadhani ndiyo kwanza linafunguliwa na hiloo linakaribia kufungwa, kwani milango mine ishafungwa tayari na imebaki milango ishirini na tano tu.

Ndugu zangu Waislamu

Ramadhani ni Soko linalofunguliwa kila mwaka kisha likafungwa, hupata faida ndani yake mwenye kutaka kupata faida na hula hasara mwenye kutaka kula hasara.

Ramadhani ni soko tulilowekewa na Mola wetu Mtukufu Subhanahu wa Taala kwa ajili ya kuchuma ndani yake thawabu nyingi kiasi cha uwezo wa mtu. Soko liko wazi na milango yake iko wazi na idadi yake ni ishirini na tisa tu, na kila siku mlango mmoja unafungwa. Kwa hivyo anayetaka kuwahi na awahi.

Ndugu zangu Waislamu

Inatupasa kuukaribisha mwezi huu kwa furaha na tabasamu na kwa moyo mkunjufu, kwani ndani yake mna kheri nyingi sana, na baina yake na baina ya Ramadhani nyingine Mwenyezi Mungu husamehe madhambi mengi sana yakiepukwa yale makubwa.

Ndugu zangu Waislam

Kutokana na manufaa mengi yaliyomo ndani ya mwezi huu, Mtume wetu mtukufu (SAW) alikuwa akiusubiri kwa hamu kubwa sana.

Alikuwa tokea unapoanza kumalizika mwezi wa Rajab, akilia (SAW) huku akimuomba Mola wake amjaalie aufikie mwezi huu.

Alikuwa akiomba na kusema;

“Mola wetu tubarikie Rajabu yetu na Shaabani yetu, na utufikishe Ramadhani”.

Alikuwa akiomba asife kabla ya kuingia Ramdhani kwa sababu alikuwa akiujua utukufu wa neema zilizomo ndani yake .

Huyu ni Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) aliyekwisha samehewa madhambi yake yaliyotangulia na yale yanayofuatilia, Mtume aliyekabidhiwa funguo zote za hazina za ardhini. Alikuwa mara unapoingia mwezi huu akiikaza barabara nguo yake ya chini (saruni) na nyakati za usiku akiwaamsha watu wake ili wajishughulishe na ibada ndani yake, na hii ni kwa sababu alikuwa akiujua vizuri utukufu wa Mola wake na alikuwa akiitambua vizuri zawadi aliyowatayarishia waja wake wanaoshindana katika kufanya mema ndani ya mwezi huu.

Imepokelewa pia katika athar kuwa Masahaba (RAnhum) walikuwa wakimuomba Mola wao kabla ya Ramadhani kwa miezi sita ili awafikishe mwezi huu, na baada ya kumalizika mwezi wa Ramadhani walikuwa wakiendelea kumuomba Mwenyezi Mungu kwa muda wa miezi sita mingine ili azikubali amali zao njema walizofanya ndani yake na ili awaghufirie madhambi yao.

STAREHE YA DUNIA

Walikuwa wakifanya yote hayo kwa sababu walikuwa wakitambua vizuri  kuwa starehe za dunia ni haba sana.

Mwenyezi Mungu anasema;

“Sema starehe ya dunia ni kidogo”

Annisaa- 77

Starehe za dunia hakika ni ndogo sana, kwani tukichukulia mfano wa mwezi huu wa Ramadhani ambao ndani ya mchana wake utamuona mtu aliyefunga, akijishughulisha kukusanya kila aina ya vyakula. Sambusa, mikate ya chila maandazi nk. Lakini magharibi inapoingia akishakula tende na kunywa gilasi ya maji, na baada ya kusali Magharibi akarudi nyumbani na kunywa bakuli lake la uji, ile hamu ya kula vile alivyojikusanyia wakati wa mchana ishaondoka. Hana hamu tena ya kula hata kama chakula hicho ni kizuri namna gani, na iwapo atajilazimisha kula basi atakuwa anajitafutia mwenyewe matatizo katika tumbo lake.

Kwa ajili hii Mwenyezi Mungu akatujulisha kuwa starehe za dunia ni haba sana.

Ama starehe za huko Peponi ni kubwa, nyingi na hazichoshi.

Mwenyezi Mungu anasema;

“Hawatataka kuondoka humo”

Kwani huko hakuna kushiba wala kukinai, isipokuwa ni kufaidika na kutaladhadh kusikokuwa na mwisho.

Ladha ya chakula, ladha ya mandhari nzuri nzuri, ladha zote za huko hazikatiki wala hazichoshi.

Mtume(SAW) anasema;

“Al Firdous ni sehemu ya juu huko Peponi, ipo kati kati, na hiyo ndiyo sehemu iliyo bora kupita zote”.

Na katika Bukhari na Muslim, Mtume(SAW) amesema;

“Mnapomuomba Mwenyezi Mungu, basi muombeni Al Firdous, kwani hiyo ipo sehemu ya juu kabisa na kati kati ya Pepo, na hapo ndipo chemchem za mito ya Peponi inapoanzia”.

“Kwa ajili hiyo”, anasema Ibni Kathiyr;

“Mwenyezi Mungu anaposema;

“Hawatataka kuondoka humo”, maana yake ni kuwa hawatachoka kutizama mandhari zake na hawatopenda kuchagua mahali pengine badala yake, na hawatopenda kuhamishwa kutoka hapo”.

VYAKULA VYA PEPONI

Ama starehe ya vyakula vya huko inakhitalifiana na starehe ya vyakula vya hapa duniani, kwani huko hakuna kushiba wala kukinai, bali ni kustarehe na kutaladhadh tu.

Mtume(SAW) anasema;

“Watu wa Peponi wanakula na kunywa, hakuna kwenda haja ndogo huko wala haja kubwa wala kutema mate.”

Wakamuuliza;

“Vipi chakula (kitatokaje tumboni)?”

Mtume(SAW) akasema;

“Kinatoka kwa njia ya jasho lenye harufu ya Miski. Aliye katika daraja la chini kabisa Peponi, anahudumiwa na watumishi elfu kumi, kila mmoja kati yao anabeba sinia  mbili (za vyakula), moja ya dhahabu na moja ya fedha zenye rangi tofauti, ladha anayoipata katika chakula alichokula ndani ya sinia ya mwanzo ni ile ile anayoipata katika sinia ya mwisho.”

Ibni Abi Dunia – Attabarani na ameisahihisha Al Mendhiry katika kitabu chake cha Attarghiyb wa Tarhiyb.

Na Mwenyezi Mungu anasema;

“Na utakapoyaona huko utaona neema na ufalme mkubwa”

Ad Dahar – 20

QIYAMU RAMADHAN (TARAWEH)

UMUHIMU WA SALA

Tukiwa bado tumo ndani ya soko la Ramadhani leo tutalitembelea angalau kwa ziara fupi soko la Sala, soko ambalo ndani yake mna faida nyingi zaidi kupita biashara zote nyingine.

Sala ni nguzo ya pili ya Kiislamu baada ya Shahada mbili, na Sala ni ibada anayoipenda sana Mwenyezi Mungu Subhanahu wa taala, na daraja yake ni kubwa kupita ibada zote zilizobaki, nayo ni nguzo ambayo kwayo dini inasimama juu yake.

Mtume (SAW) amesema;

“Kichwa cha jambo ni Uislamu na nguzo yake ni Sala na kilele chake ni Jihadi”.

Na Sala ni amali  ya mwanzo atakayoulizwa mja siku ya Kiama. Ikikubaliwa, basi amali zote zilizobaki zitakubaliwa, ama ikikataliwa basi zilizobaki nazo pia zitakataliwa, kwani tofauti iliyopo baina yetu na baina ya makafiri ni Sala.

Mtume (SAW) aliendelea kuusia juu ya Sala katika maisha yake yote na hata pale alipokuwa akivuta pumzi zake za mwisho alikuwa akiusia huku akisema;

“Salaa salaa na kilichomilikiwa na kuume kwenu”.

SALA ZA SUNNAH

Mwenyezi Mungu ametuwekea sheria ya kusali Sala za Sunnah ili zipate kutusaidia katika kuinyanyua Sala ya Fardhi kutokana na makosa au upungufu wowote unaopatikana ndani yake kutoka kwetu.

Kutoka kwa Abu Huraira (RA) amesema kuwa Mtume (SAW) amesema;

“La mwanzo atakaloulizwa mja siku ya Kiama katika amali zake ni Sala. Mwenyezi Mungu atawaambia Malaika wake akiwa Yeye ni mwenye kujuwa zaidi:

“Tizameni katika Sala ya mja wangu. Ameitimiza au hakuitimiza”.

Ikiwa ameitimiza, basi ataandikiwa thawabu za Sala iliyotimia, ama ikiwa imepungua chochote ndani yake, basi Mwenyezi Mungu atasema;

“Tizameni ikiwa mja wangu amesali Sala za Sunnah”.

Ikiwa anazo Sala za Sunnah, atasema;

“Mtimizieni mja wangu fardhi yake kutoka katika Sunnah zake”. Kisha amali zilizobaki zitakubaliwa kwa njia hiyo”.

Abu Daud

Kutokana na hadithi zilizotangulia Mtume (SAW) akatuwekea sheria ya kusali Sala za Sunnah, na akaitilia nguvu sana katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani kwa kutuwekea sheria ya kusali Sala ya Qiyam Ramadhan (Taraweh).

Qiyam Ramadhan pia inajulikana kwa jina la ‘Taraweh’ (mapumziko), kwa sababu Masahaba wa Mtume (SAW) walikuwa wanaposali Sala hii wakipumzika baada kila raka-a nne, na Sala hii ni Sunnah kwa wanawake na wanaume.

Anasema Irfijah (RA) kuwa;

“Sayiduna Ali bin Abi Talib (RA) alikuwa akiamrisha watu kuisali jamaa Sala ya Qiyam Ramadhan (Taraweh), na alikuwa akimweka imamu mwanamume upande wa wanaume na imam mwanamke upande wa wanawake na mimi nilikuwa imam wa wanawake”.

Al Baihaqi – Kinz al aamal cha Al Muttaqi al Hindi na Fiqhi Ssunnah – Sayed Sabeq

Sala hii husaliwa baada ya Sala ya Ishaa na kabla ya Sala ya witri na husaliwa raka-a mbili mbili, na inaweza pia kucheleweshwa mpaka wakati wowote katika nyakati za usiku.

Imepokelewa na maimamu wa hadithi wa Ahli Ssunnah kutoka kwa Abu Huraira (RA) kuwa amesema;

“Mtume (SAW) alikuwa akipendekeza watu waisali Sala hii lakini bila kulazimisha. Alikuwa akisema;

“Atakayesali Qiyam Ramadhan kwa imani na kwa kutaraji thawabu, atasamehewa madhambi yake yaliyotangulia”.

Hii ni neema kubwa sana ambayo hatoiacha isipokuwa yule ambaye hana madhambi aliyotanguliza.

Na impokelewa na maimamu wote wa Ahli Ssunah isipokuwa Attirmidhy kutoka kwa Bibi Aisha (RA) kuwa amesema;

“Mtume (SAW) alisali msikitini, na watu wengi wakasali pamoja naye, kisha akasali tena siku ya pili yake na watu wakaongezeka, kisha wakakusanyika usiku wa tatu, lakini Mtume (SAW) hakuwatokea. Ulipoingia wakati wa asubuhi akasema;

“Nilikuoneni mlichofanya (kuningoja kwenu), na hakuna kilichonizuwia nisitoke nikasali pamoja nanyi isipokuwa nilihofia isije ikafaridhishwa juu yenu”. Na hii ilikuwa katika mwezi wa Ramadhani.

IDADI YA RAKA-A ZAKE

Imepokelewa kutoka kwa Bibi Aisha (RA) kuwa Mtume (SAW) hajapata kusali zaidi ya raka-a kumi na moja, iwe katika mwezi wa Ramadhani au mwezi mwingine wowote ule, ingawaje zipo baadhi ya riwaya ambazo Sheikh Al Albani anasema kuwa zina udhaifu ndani yake zinazosema kuwa Masahaba wengine (RA) walikuwa wakisali raka-a ishirini.

KUISALI JAMAA

Taraweh inaweza kusaliwa jamaa na pia anaweza mtu kuisali peke yake, isipokuwa maulamaa wengi wanaona kuwa kuisali jamaa msikitini ni bora zaidi, ingawaje wapo wanaoona kuwa kuisali nyumbani ni bora zaidi na kila mmoja anazo hoja zake.

Tulitangulia kueleza kuwa Mtume (SAW) aliisali jamaa Sala hii na akasema kuwa hakuna kilichomzuwia kuendelea kufanya hivyo isipokuwa kwa ajili ya kuwahofia ummati wake isije ikateremshwa amri ya kufaridhishwa, kisha Omar bin Khattab (RA) wakati wa ukhalifa wake akawakusanya watu wawe wanaisali jamaa nyuma ya imamu mmoja.

Anasema Abdul Rahman bin Abdul Qariy;

“Nilitoka usiku mmoja katika mwezi wa Ramadhani mimi na Omar bin Khattab kuelekea msikitini, tukawaona watu wamegawanyika na kufarikiana, kila mmoja anasali peke yake. Mtu anakuwa anasali peke yake kisha kundi lingine (linakuja na) linasali nyuma yake. Omar akasema;

Mimi naona ikiwa tutawakusanya wote wasali nyuma ya imamu mmoja itakuwa bora. Kisha akafanya hivyo na akamweka Ubay bin Kaab awasalishe watu. Kisha nikatoka naye usiku uliofuata na tukawaona watu wote wanasali nyuma ya imamu mmoja akasema;

‘Neemal bid ata hadhihi’ “Jitihada jema sana hii na ile wanayolala ikawapita ni bora zaidi kuliko wanayoisali”, akikusudia kuwa kuisali nyakati za mwisho za usiku ni bora zaidi.

Neno Bida-a alotumia Omar bin Khattab (RA) katika riwaya hii halina maana ya ‘Uzushi’, kwani Omar (RA) hawezi kuwa mzushi, bali Mtume (SAW) ametufundisha kuwa atakalotufundisha Omar au yeyote kati ya Makhalifa walioongoka (RA) (Khulafaa rashidiyn) ni katika Sunnah.

Kutoka kwa Al Irbadh bin Sariya (RA) amesema;

“Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) alitutolea mawaidha yaliyoingiza hofu nyoyoni na kututoa machozi machoni. Tukamuuliza; ‘ Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu kama kwamba mawaidha (haya ni) ya kutuaga?’

Akatuusia, akasema;

“Nakuusieni kumcha Mungu na kusikia na kutii hata akiwa amri wenu mtumwa, kwani atakayeishi kati yenu ataona khitilafu nyingi, kwa hivyo ni juu yenu kufuata Sunnah yangu na Sunnah za Makhalifa waadilifu walioongoka (katika riwaya nyingine amesema; “watakaokuja baada yangu) muzibane Sunnah zao kwa magego…”

Imepokelewa na Attirmidhiy na Abu Daud na Ibni Majah na wengineo.

Hii ni sawa na muadhini wa pili aloongeza Othman bin Affan (RA) wakati wa ukhalifa wake, muadhini ambao wakati wa Mtume (SAW) haukuwepo, lakini Ali bin Abi Talib (RA) aliyetawala ukhalifa baada yake aliuendeleza na wala hakuusimamisha, na hii ni kutokana na fahamu yao Makhalifa hawa juu ya hadithi iliyotangulia iliyosimuliwa na Al Irbadh bin Sariya (RA).

Kwa ajili hiyo neno Bida-a, alokusudu Omar (RA) hakukusudia Bidaa ya upotofu (kullu bidaatun dhalalah), bali alikusudia Bida-a ya kilugha na si ya kidini na maana yake ni ‘jitihada jema’ (Mubdi-u), kwani Omar (RA) ni mcha Mungu kuliko hao wanaojaribu kumkosoa na ni mtu wa mwisho kabisa kutegemewa kuleta uzushi katika dini.

Na Omar (RA) asingeruhusu watu waisali jamaa Sala hiyo angekuwa hakumuona Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) akiisali Sala hii jamaa pamoja na Masahaba wake (RA), yeye mwenyewe (SAW) akiwa imamu wao, na akaacha kuendelea kufanya hivyo kwa kuhofia wasije wakafaridhishiwa. Ama baada ya kufa kwa Mtume (SAW) ile hofu ya kufaridhishiwa ikaondoka kwa kukatika kwa Wahyi, na Masahaba (RA) walikuwa wakiisali jamaa Sala hiyo, isipokwa walikuwa wakisali kila kundi nyuma ya imamu yeyote yule, na jamaa zikawa nyingi msikitini wakati mmoja, na kwa ajili hiyo Omar akawakusanya ili waisali nyuma ya imamu mmoja.

Udhuru aloutoa Mtume (SAW) pale alipoacha kutoka na kusali nao ulikuwa;

“HAKUNA KILICHONIZUWIA NISITOKE NIKASALI PAMOJA NANYI ISIPOKUWA….”,  hii ikimaanisha kuwa Mtume (SAW) alikuwa akitamani kutoka na kusali pamoja nao, isipokuwa hofu yake ilikuwa ni moja tu, nayo ni kuwa Isije Ikafaridhishwa juu yao.

Anasema Imam Malik katika Muwata-a kuwa;

“Salatul Taraweh ni Sunnah iliyotiliwa nguvu, na kwa ajili hiyo makhalifa  wote waongofu (RA) waliitilia mkazo Sala hii wakiwemo Othman na Ali (Ranhum) na wakawa wanaipendekeza kusaliwa jamaa wanaume na wanawake pia.

“Ama kauli yake Mtume (SAW) aliposema;

“Nilihofia isije ikafaridhishwa juu yenu”, anaendela kusema Imam Malik;

“Anasema Al Kadhi Abubakar kuwa huenda ikawa Mtume (SAW) alifunuliwa kuwa akiendelea kuisali pamoja nao itakuja faridhishwa, au labda alidhania tu kuwa huenda ikafaridhishwa, au huenda akawa anahofia asije mmoja katika umati wake atakaposikia kuwa Mtume (SAW) alikuwa akiisali siku zote Sala hiyo katika jamaa akadhania kuwa ni fardhi kisha akawajulisha watu hiyvo kisha watu wakaionea uvivu”

(Mwisho wa maneno ya Imam Malik).

Imepokelwa pia kutoka kwa Abu Daud na An Nasai na Ibni Majah na Al Hakim na Attirmidhy, na lafdhi ya hadithi hii ni ya Imam Attirmidhy kama ilivyoandikwa katika sharhi ya Tuhfatul Ahawadhiy anasema;

“Kutoka kwa Abu Dhar amesema; ‘Tulifunga pamoja na Mtume (SAW) na hakusali pamoja na sisi (Sala ya Taraweh) mpaka zilipobaki siku saba kabla kumalizika mwezi (wa Ramadhani), akatusalisha Taraweh mpaka ilipomalizika thuluthi ya mwisho. Kisha usiku wa sita (kabla ya kumalizika kwa Ramadhani) hakutusalisha, akatusalisha usiku wa tano (kabla ya kumalizika Ramadhani) mpaka ulipomalizika nusu ya usiku.

Tukamwambia; ‘Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, si bora ungeendelea kutusalisha sehemu ya usiku iliyobaki?’

Mtume (SAW) akasema;

“Atakayesali na imamu mpaka atakapomaliza (imamu) Sala, ataandikiwa thawabu ya aliyesali usiku wote”.

Kisha Mtume (SAW) hakutusalisha mpaka zilipobaki siku tatu kabla ya kumalizika mwezi, akatusalisha na akawaita jamaa zake na wake zake na akatusalisha mpaka wakati wa kula daku ulipoingia.

Hadithi hii ina faida nyingi sana ndani yake, lakini ili nisiwachoshe wasomaji nitaelezea faida mbili tu nazo ni kuwa;

1- Mtume (SAW) aliwasalisha Sahaba zake (SAW) Sala yaTaraweh yeye akiwa imamu wao na akawaita watu wa nyumba yake pia.

2- Katika Soko hili la Taraweh, atakayesali nyuma ya imamu mpaka mwisho ataandikiwa thawabu ya aliyesali usiku kucha.

HITILAFU YA UBORA

Hata hivyo ipo khitilafu baina ya maulamaa kuhusu namna bora wa kuisali Sala ya Taraweh.

Anasema Imam Shafi na wengi katika wanafunzi wake, na pia Imam Abu Hanifa na Ahmed na baadhi ya wanavyuoni wa madhehebu ya Imam Malik na wengineo kuwa ni bora kuisali jamaa kama alivyofanya Omar na kama walivyofanya Makhalifa waongofu waliokuja baada yake na pia Masahaba na waliokuja baada yao, na ikaendelea katika hali hiyo mpaka wakati wetu huu sasa.

Ama Imam Malik na Abu Yusuf na baadhi ya wafuasi wa Imam Shafi wao ingawaje wanaona kuwa ni vizuri kuisali jamaa, lakini wanasema kuwa ni bora zaidi kuisali nyumbani mtu peke yake.

QURANI TUKUFU

Ndugu zangu Waislam

Assalaam alaykum wa Rahmatullahi wa Barakatuh

Ramadhani inaendelea kututoka na milango inaendelea kufungika, na biashara inaendelea kuchangamka. Kwani kila siku zinapokaribia kumalizika Mtume wenu Mtukufu (SAW) alikuwa akizidi kuikaza shuka yake na kukesha usiku wake na kuamsha watu wake.

Ndugu zangu Waislam

Mtume Muhammad (SAW) amesema;

“Hakika bidhaa ya Mwenyezi Mungu (mnayoinunua) ni yenye thamani sana, hakika bidhaa ya Mwenyezi Mungu ni Pepo”.

Atirmidhiy – Al Hakim – Al Baihaqy na wengineo

Anasema Ibnul Qayim;

“Ajabu mtu baada ya kutambua kuwa Mwenyezi Mungu ndiye mwenye bidhaa bora, kisha anakwenda kufanya biashara na mwengine mwenye bidhaa duni, na ajabu kubwa zaidi ni pale mtu anapotambua kuwa hana budi Naye Mola wake na kwamba hapana awezae kuondoa shida zake isipokuwa Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taala, kisha anajiweka mbali naye”.

Kwa ajili hiyo ndugu zangu Waislam, tuzidishe kufanya biashara na Mola wetu mtukufu katika mwezi huu wa Ramadhani huku tukitarajia bidhaa yake tukufu, bidhaa ghali kupita zote, Jannatul Firdaus.

BIASHARA YA KUSOMA QURANI

Mwenyezi Mungu anasema;

“Kwa yakini wale wanaosoma Kitabu cha Mwenyezi Mungu, na wakasimamisha Sala, na katika yale Tuliyowapa wakatoa, kwa siri na kwa dhahiri, hao wanatumai (faida ya) BIASHARA isiyododa (isiyobwaga)”.

Fatir – 29

Na akasema;

“Mwezi wa Ramadhani ambao imeteremshwa katika (mwezi) huo hii Qurani ili iwe uwongozi kwa watu, na hoja zilizo wazi wa uwongozi na upambanuzi (baina ya haki na batili)”.

Al Baqarah – 185

Katika aya hii Mwenyezi Mungu anausifia Mwezi huu mtukufu wa Ramadhani kuwa ni bora kuliko miezi yote kutokana na kuuchagua kwa kuiteremsha Qurani tukufu ndani yake, kitabu chenye uongofu, kilichopambanua baina ya haki na batili, ili kiwe hoja zilio wazi kwa kila mwenye kukisoma.

Maulamaa wanasema kuwa ili kufaidika na mafundisho yake, lazima kusoma huko kuwe kwa kutafakari na kuzingatia. Kwani yeyote anayetaka kufaidika na kitabu hiki kitukufu lazima awe anakisoma kwa moyo mkunjufu ulio hadhir na kwa kuzingatia aya zake huku akitambua kuwa yaliyomo ndani yake ni maneno anayohutubiwa yeye.

Mwenyezi Mungu anasema;

“Kwa yakini katika jambo hili mna ukumbusho kwa mwenye moyo au kwa ategaye sikio, naye mwenyewe awe hadhiri”.

Qaf – 37

Anasema Ibni Qutaybah katika kitabu chake kiitwacho ‘Tafsiyr ghariyb al Qur-an’;

“Aya hii inatufundisha kuwa ili mtu afaidike na mafundisho yaliyomo ndani ya Qurani tukufu lazima moyo wake uwe hadhiri pale anapiosoma au anapoisikiliza”.

Imetolewa na Addaylamiy kutoka kwa Ibni Abbas (RA) katika hadithi aloinyanyua moja kwa moja kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) kuwa;

“Mnapoisoma Qurani muisome vilivyo na muibainishe kwa ubainifu, muwe mnasimama (na kutafakiri) penye maajabu yake, na muusitue na kuuamsha moyo (muuharikishe) kwa hiyo Qurani, na isiwe hamu ya mtu ni kuimaliza sura tu.”

Ndugu zangu Waislam

Mwenyezi Mungu hutukuza na kuadhimisha anachotaka. Kama alivyowachagua baadhi ya Malaika wake akawafanya kuwa wajumbe, na kuwachagua miongoni mwa wanadamu na kuwafanya kuwa Mitume, akauchagua mwezi wa Ramadhani na miezi mitukufu kwa kuiadhimisha kuliko miezi mingine, Mwenyezi Mungu ameichagua pia Qurani tukufu ambayo ni maneno yake akayaadhimisha juu ya maneno yote mengine, kwa hivyo kuweni wenye kufahamu na wenye kutukuza yale aloyatukuza Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taala, kwa sababu hatukuzi yale aloyatukuza Mwenyezi Mungu isipokuwa mwenye kufahamu na mwenye akili.

Ndugu zangu Waislam

Mwezi wa Ramadhani ni mwezi wa Qurani, na Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) alikuwa akiisoma na kuiadhimisha Qurani tukufu zaidi katika mwezi huu kupita miezi mingine yote. Kwa hivyo na sisi tujitahidi kuuhitimisha msahafu ndani ya mwezi huu angalau mara moja, hii ni kwa uhaba kabisa, kwani mwezi huu ni mwezi wake, na ndani yake mna thawabu nyingi sana na manufaa mengi sana kwa ajili yetu.

Kutoka kwa Abdullahi ibni Masaud (RA) amesema kuwa Mtume (SAW) amesema:

“Atakayesoma herufi moja (tu) katika kitabu cha Mwenyezi Mungu atalipwa thawabu. Na kwa kila thawabu moja atalipwa kumi (nyingine). Si semi kuwa alif laam miym ni herufi moja, bali ‘aliyf’ ni herufi (moja), ‘laam’ ni herufi (moja) na ‘miym’ ni herufi (moja)”.

Yaani mtu anapotamka; ‘Aliyf laam miym’, anakuwa keshajipatia thawabu thelathini, na Mwenyezi Mungu humzidishia amtakae.

Huyu ndiye Mola wetu mkarimu, na bila shaka katika mwezi wake karimu malipo yake huongezeka maradufu.

Kutoka kwa Ibni Abbas (RA) amesema;

“Mtume (SAW) alikuwa mkarimu kupita wote katika mambo ya kheri, na alikuwa mkarimu zaidi katika mwezi wa Ramadhani wakati anapokutana na Jibril (AS), na alikuwa akikutana naye kila Ramadhani mpaka mwezi unapomalizika, na alikuwa akimsikiliza Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) Qurani yote, na kila anapokutana na Jibril, Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) alikuwa mwingi wa kheri mfano wa upepo uliopelekwa (kwa ajili ya kueneza kheri)”.

Bukhari na wengine

Ndugu zangu Waislam

Kila kitu kwa hesabu yake. Imepokelewa kutoka kwa Abdullah bin Amru bin Al Aas (RA) kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) amesema;

“Ataambiwa msomaji wa Qurani; ‘Soma upande daraja (za juu Peponi). Isome vilivyo kama ulivyokuwa ukiisoma duniani na daraja yako inaishia mwisho wa aya utakayoisoma”.

Abu Daud na Attirmidhiy na wengineo

Kwa hivyo ukisoma juzuu moja tu, basi daraja yako itaishia hapo, na hivi ndivyo ilivyo kila unapoisoma zaidi utapandishwa zaidi katika daraja za juu kabisa za huko Peponi

BAADHI YA HADITHI JUU YA FADHILA ZA QURANI TUKUFU

Kutoka kwa Abu Umamah (RA) amesema;

“Nilimsikia Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) akisema;

“Someni Qurani, kwa sababu itakuja siku ya Kiama kuwaombea shafaa wasomaji wake”.

Muslim

Kutoka kwa Al Nuwas bin Samaan (RA) amesema;

“Nilimsikia Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) akisema;

“Italetwa Qurani siku ya Kiama pamoja na wasomaji wake waliokuwa wakiifanyia kazi duniani ikitanguliwa na Suratul Baqarah na Aali Imran zikiwatetea wasomaji wake”.

Muslim

Kutoka kwa Othman bin  Affan (RA) amesema:

“Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) amesema;

“Mbora wenu ni yule atakayejifunza Qurani kisha akafundisha”.

Bukhari

Kutoka kwa Bibi Aisha (RA) amesema;

“Amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW):

“Mwenye kuisoma Qurani akiwa mahiri katika kuisoma, atakuwa pamoja na Malaika watiifu. Na mwenye kuisoma Qurani huku akihangaika katika kuyatamka maneno yake atalipwa ujira mara mbili”.

Bukhari na Muslim

Kutoka kwa Omar bin Khattab (RA) amesema kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) amesema:

“Mwenyezi Mungu kwa kitabu hiki atayanyanua makundi ya watu na atayaacha (makundi) mengine”.

Muslim

KUMI LA MWISHO

Hii ni tafsiri ya makala yaliyoandikwa na Al Hafidh Ibni Rajab Al Hanbaliy niliyobahatika kuyasoma na kufaidika nayo sana, nikaona bora kuyataf+siri katika lugha ya kiswahili ili na wenzangu wafaidike pia:

Bismillahi rrahmani rrahiym,

Shukrani zote ni za Mwenyezi Mungu peke yake na sala na salaam zimfikie yule ambaye hapana Mtume baada yake, Amma baad:

Kutoka kwa Bibi Aisha (RA) amesema;

“Alikuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) linapoingia kumi la mwisho akiikaza vizuri shuka yake, akikesha usiku wake na akiamsha watu wa nyumba yake”.

Bukhari na Muslim

AMALI ZA KUFANYA KATIKA KUMI LA MWISHO LA RAMADHANI

Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) alikuwa akilihusisha kumi la mwisho la mwezi wa Ramadhani kwa amali zifuatazo ambazo hakuwa akizifanya katika siku nyingine zisizokuwa hizo;

·        AKIKESHA;

Na maana ya kukesha inaweza kuwa alikuwa akifanya ibada usiku kucha, na hii inatokana na hadithi ya Bibi Aisha (RA) aliposema;

“Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) alikuwa katika siku ishirini za mwanzo za Ramadhani akichanganya baina ya Sala na kulala, lakini zinapobaki siku kumi (yaani za mwisho), alikuwa akipania na kuikaza barabara shuka yake”.

Ahmed bin Hanbal

Huenda pia ikawa na maana kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) alikuwa akikesha sehemu kubwa ya usiku na si usiku wote, na hii inatokana na hadithi nyingine ya Bibi Aisha (RA) katika Sahih Muslim isemayo;

“Sikumbuki kama aliwahi kusali usiku woote mpaka asubuhi”

·        AKIAMSHA WATU WAKE

Alikuwa akiamsha watu wake kwa ajili ya kusali katika usiku wa kumi la mwisho tofauti na usiku wa siku nyingine.

Anasema Sufyan Al Thauriy;

“Napenda linapoingia kumi la mwisho mtu awe anasali nyakati za usiku na ajitahidi sana ndani yake, na awaamshe watu wa nyumba yake pamoja na wanawe ikiwa wataweza kustahamili, kwani imesihi kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) alikuwa akimgongea mlango Bibi Fatima na Ali (RAnhum) huku akiwaambia;

“Hamuamki mkasali?”

Na imesihi pia kuwa akishamaliza kusali Tahajud katika nyakati za usiku na kabla ya kusali Witri alikuwa akimuamsha Bibi Aisha (RA), na imepokelewa pia kupendeza kwa mtu na mkewe kuamshana kwa ajili ya kusali tahajjud hata ikibidi kummichia maji mwenzake usoni.

Imetolewa na Imam Malik katika Muwata-a kuwa Omar bin Khattab (RA) alikuwa akishasali kiasi cha kusali katika nyakati za usiku, na inapoingia nusu ya pili ya usiku akiwaamsha watu wa nyumba yake kwa ajili ya kusali huku akiwasomea aya ifuatayo;

“Na waamrishe watu wako kusali, na uendelee mwenyewe kwa hayo”.

Ta-ha – 132

·        AKIIKAZA VIZURI SHUKA YAKE

Ama kuhusu ‘kuikaza vizuri shuka yake’, maulamaa wamekhitalifiana juu ya tafsiri yake. Wapo wanaosema kuwa hii ni kutujulisha juu ya jitahada kubwa anayofanya katika ibada ndani ya kumi la mwisho. Na wengine wakasema kuwa maana yake ni kuwa alikuwa akijiepusha kulala na wake zake, na zipo riwaya zinazotilia nguvu maana hii zinazoeleza kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) alikuwa hapandi kitandani mpaka imalizike Ramadhani. Na katika hadithi iliyosimuliwa na Anas (RA) anasema;

“Alikuwa akilikunja tandiko lake na kuwaepuka wake zake”.

·        KUAKHIRISHA FUTARI MPAKA WAKATI WA DAKU

Kutoka kwa Bibi Aisha (RA) na pia kutoka kwa Anas (RA) kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) alikuwa akiichelewesha futari yake na kuila wakati wa daku. Na hadithi yenyewe kama ilivyoelezwa na Bibi Aisha (RA) inasema;

“Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) alikuwa inapoingia Ramadhani akisali nyakati za usiku na akilala (pia), na linapoingia kumi la mwisho akiikaza shuka yake vizuri, na akijiepusha na wake zake (kulala nao), na alikuwa akikoga baina ya adhana mbili na alikuwa akiila futari yake wakati wa daku”.

Ibni Abi Asim

Na kutoka kwa Abu Saeed Al Khudhary (RA) kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) alisema;

“Msiiendeleze (saumu yenu), (lazima mule futari) na kama yeyote kati yenu anataka kuendelea na saumu (bila kula futari yake), basi aendelee mpaka wakati wa daku (tu)”.

Wakasema;

“Lakini wewe unaendeleza ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu”.

Akasema;

“Mimi nakhitilafiana na nyinyi, mimi nina mlishaji anayenilisha na mnywishaji anayeninywisha”.

Bukhari

Kutokana na haya, inaonesha kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) alikuwa anaendela na saumu yake usiku wote, na huenda ikawa alikuwa akifanya hivyo kwa sababu alikuwa akiona kuwa anakuwa mwepesi zaidi katika jitihada zake za kufanya ibada nyakati za usiku ndani ya kumi la mwisho la Ramadhani, na hakuwa akipata udhaifu wowote kwa sababu Mwenyezi Mungu alikuwa akimlisha na kumnywesha.

·        KUOGA BAINA YA ADHANA MBILI

Tulitangulia kueleza katika hadithi ya Bibi Aisha (RA) kuwa (Mtume (SAW)) ‘alikuwa akikoga baina ya adhana mbili’, na kusudi lake ni kuwa alikuwa akioga baina ya adhana ya Magharibi na adhana ya Ishaa.

Anasema Ibni Jariyr;

“Walikuwa wakipendelea kuoga kila usiku katika kumi la mwisho. Na Al Nakhaiy alikuwa akikoga katika kumi la mwisho kila usiku, na walikuwepo miongoni mwao waliokuwa wakipenda kuoga na kujipaka mafuta mazuri kila usiku wanaoutegemea kuwa Lailatul Qadar itakuwa ndani yake.

Kutokana na haya inatubainikia kuwa kila usiku unaotegemewa kuwa Lailatul Qadar utakuwa ndani yake inapendeza mtu kuoga na kuvaa nguo nzuri na kujipaka mafuta mazuri, na pia inapendeza kufanya hivyo kila Ijumaa na katika Sikukuu na inapendeza mtu kuvaa vizuri katika kila Sala.

Na kujipamba sehemu za nje ya mwili hakukamiliki pambo lake mpaka mtu ajipambe ndani ya nafsi yake pia kwa kujitakasa kutokana na madhambi yake kwa njia ya kutubu na kurudi kwa Mola wake. Kwani kujipamba mtu mwili wake wakati ndani yake kumeharibika hakutomsaidia kitu. Na haijuzu kumkabili Mfalme wa wafalme Mwenye kujuwa yaliyo dhahir na yaliyo siri na yaliyofichikana zaidi kuliko siri, ambaye hatizami nyuso zenu, bali anazitizama nyoyo zenu na matendo yenu bila ya mtu kujitakasa nje na ndani yake.

Kwa hivyo atakayesimama mbele Yake inampasa ajipambe nje yake kwa nguo safi na ndani yake kwa moyo msafi wenye kumcha Mungu.

ITIKAFU

Katika Bukhari na Muslim kutoka kwa Bibi Aisha (RA) amesema;

“Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) alikuwa akifanya itikafu katika kila kumi la mwisho la mwezi wa Ramadhani mpaka alipofariki dunia.

Na katika Sahih Bukhari, kutoka kwa Abu Hurairah (RA) amesema;

“Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) alikuwa akifanya itikafu katika kila Ramadhani siku kumi, ama katika mwaka alofariki ndani yake alifanya itikafu siku ishirini”.

Mtume (SAW) alikuwa akifanya itikafu katika siku kumi zile ambazo ndani yake unatarajiwa usiku wa Lailatul Qadar ili asijishughulishe na jingine gheri ya kumuomba na kumdhukuru Mola wake.

Hujitenga na kuacha shughuli zake zote kwa ajili ya kufanya itikafu kwa moyo wake wote ili apate kumtii Mola wake na kujikurubisha Kwake.

Kwa hivyo mwenye kufanya itikafu anakuwa amejitenga na kuacha shughuli zake zote kwa ajili ya kumtii Mola wake kwa moyo wake wote, na kwa ajili hiyo hapana kinachomshughulisha isipokuwa ta-a ya Mola wake na kufanya yale yanayomridhisha tu.

Na kila mja anapomjuwa zaidi Mola wake akampenda, basi huwa hastarehe  isipokuwa pale anapoacha shughuli zake zote kwa ajili ya kumuabudu.

LAILATUL QADRI

·        Mwenyezi Mungu anasema;

“Hakika Tumeiteremsha (Qurani) katika Laylatul Qadar (usiku wenye heshima kubwa).

Na jambo gani litakalokujulisha (hata ukajua) ni nini huo usiku wa Lailatul Qadar?

Huo usiku wa hishima ni bora kuliko miezi elfu”.

Suratul Qadar – 1- 3

Na kutoka kwa Abu Hurairah (RA) amesema kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) amesema juu ya mwezi wa Ramadhani;

“Ndani yake mna usiku ulio bora kuliko miezi elfu, na alonyimwa kheri zake, basi amenyimwa (amekula khasara)”.

Ahmed na Annasai

Ama kuhusu amali za mtu kufanya katika usiku wa Lailatul Qadar, imepokelewa hadithi sahihi ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) kuwa amesema;

“Atakayesimama usiku wa Lailatul Qadar kwa imani na kwa kutaraji thawabu, atasamehewa alotanguliza katika madhambi yake”.

Na maana ya neno ‘kusimama usiku wake’, ni kuuhuisha usiku huo kwa kusali Tahajud, na Mtume (SAW) alimtaka Bibi Aisha (RA) awe anaomba dua ndani yake.

Sufyan Al Thouriy amesema;

“Dua ndani yake usiku huo kwangu mimi ni bora kuliko Sala”.

Na kusudi lake ni kuwa kuomba dua kwa wingi ndani ya Sala katika usiku huo ni bora kuliko Sala isiyokuwa na dua ndani yake, na kama mtu atasoma Qurani na kuomba dua, hii itakuwa bora zaidi.

Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) alikuwa akisali ndani ya usiku wa Lailatul Qadar huku akisoma Qurani kwa utulivu, na kila anapoifikia aya inayozungumzia Rehma, alikuwa akimuomba Mwenyezi Mungu amrehemu, na anapoifikia aya inayozungumzia adhabu alikuwa akimuomba amuepushe nayo. Kwa hivyo katika Sala yake yalikuwa yakijumuika mambo mane; Sala, kusoma Qurani, kuomba dua na kutafakari, na hii ndiyo amali bora iliyokamilika kupita zote katika usiku wa kumi la mwisho na katika usiku mwengine pia.

Bibi Aisha (RA) alisema kumuuliza Mtume (SAW);

“Unaonaje ninapofanya ibada katika usiku wa Lailatul Qadar niwe nikisema nini?”

Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) akamwambia;

“Sema; “Allahumma innaka afuwun tuhibbu l afuwa, faafu anni.”

Na maana yake ni;

“Mola wangu wewe ni Mwingi wa kusamehe, unapenda kusamehe, kwa hivyo nisamehe”.

Na ‘Al Afuwwu’, ni katika majina ya Mwenyezi Mungu, na Yeye ni Mwingi wa kusamehe madhambi ya waja wake, Mwenye kuyafuta na kuyaondoa na Mwenye kuacha kumtia adabu anayestahiki.

Na kwa vile Yeye anapenda kusamehe, kwa hivyo bila shaka anapenda pia waja wake wawe wanasameheana wao kwa wao, na wakishasameheana wao kwa wao, na Yeye anawapitishia afuwa yake. Na Mwenyezi Mungu anapenda kusamehe kuliko kuadhibu. Na Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) alikuwa akisema;

“Najikinga kwa radhi Zako kutokana na ghadhabu Zako, na najikinga kwa kusamehe Kwako kutokana na adhabu Yako”.

Muslim

Na tumeamrishwa kuomba maghfira katika usiku wa Lailatul Qadar baada ya kujitahidi katika kufanya amali njema nyakati za usiku katika kumi la mwisho, na hii ni kwa sababu ‘wanaojuwa’, wanajitahidi katika kufanya amali njema huku wakiona kama kwamba hawakufanya lolote, kisha wanamuomba Mola wao awasamehe kama kwamba wamefanya madhambi au wamepunguza katika haki za Mola wao.

SABABU ZA MAGHFIRA KATIKA MWEZI WA RAMADHANI

Kutoka kwa Abu Huraira (RA) amesema kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) amesema;

“Atakayefunga Ramadhani kwa imani na kutaraji thawabu, atasamehewa yaliyotangulia katika madhambi yake, na atakayesimama (akasali) usiku wa Lailatul Qadar kwa imani na kwa kutaraji thawabu, atasamehewa yaliyotangulia katika madhambi yake”.

Na kutoka kwa Abu Hurairah (RA) pia kuwa amesema; ‘Mtume (SAW) amesema;

“Atakayesali usiku wa Ramadhani kwa imani na kwa kutaraji thawabu, atasamehewa madhambi aliyotanguliza”.

Bukhari na Muslim

·        Hadithi hizi zilizosimuliwa na Abu Hurairah (RA) zinatufundisha kuwa kila moja katika sababu tatu hizi zinasababisha kusamehewa mtu madhambi yake aliyotanguliza.

Na mambo yenyewe ni Saumu ya mwezi wa Ramadhani, kusali katika usiku wake (Taraweh), na kusali katika usiku wa Lailatul Qadar (Tahajjud).

Kusali katika usiku wa Lailatul Qadar peke yake kunatosheleza mtu kufutiwa madhambi yake, yote sawa ikiwa katika siku ya mwanzo ya kumi la mwisho au kati yake au mwisho wake, na yote sawa pia ikiwa ameihisi Lailatul Qadar au hakuihisi, na kufutiwa madhambi kunaendelea mpaka mwezi unapomalizika.

Ama katika kufunga mwezi wa Ramadhani na kusali usiku wake (Taraweh), ili mtu asamehewe madhambi yake, sharti awe amefunga na kusali mwezi mzima.

Akishaukamilisha mwezi, Muislamu anakuwa keshatimiza kufunga Ramadhani na kusali ndani ya usiku wake, na kwa ajili hiyo anastahiki kughufiriwa madhambi yake baada ya kutimiza masharti mawili hayo ya kufunga na kusali.

·        Kwa hivyo atakayeukamilisha mwezi wa Ramadhani kwa kufunga na kusali atakuwa keshakamilisha sharti alopewa, na kitakachobaki ni kupokea ujira wake kutoka kwa Mola wake na ujira huo ni kughufiriwa madhambi yake. Na Wasilamu wanapotoka kwenda kusali siku ya Idi wanagawiwa ujira wao huo na kwa ajili hiyo wanarudi majumbani mwao wakiwa washalipwa ujira wao kwa ukamilifu. Na atakayepunguza katika amali zake, na ujira wake pia utapunguzwa. Kila kitu kwa hesabu yake, na kwa ajili hiyo mtu asiilaumu isipokuwa nafsi yake.

Amesema Suleiman;

“Sala ni mezani, atakayekamilisha na Mwenyezi Mungu atamkamilishia, ama atakayepunguza, basi wenyewe mnajuwa nini Mwenyezi Mungu amesema juu ya wapunjao”

((Waylun lilmutaffifiyn (maangamizo yatawathubutikia wapunjao))

Sala na ibada zote hukmu zake ni kama hivyo, atakayekamilisha, huyo anakuwa kipenzi cha Mwenyezi Mungu, ama atakayepunja basi Waylun lilmutaffifiyn.

Basi haoni haya mtu, katika matamanio ya nafsi yake anafanya kwa ukamilifu, kisha anakwenda kupunja katika Saumu na Sala yake?

·        Watu wema waliotangulia walikuwa wakijitahidi kufanya amali zao kwa ukamilifu kisha wanajishughulisha kumuomba Mwenyezi Mungu azikubali amali zao hizo huku wakiogopa Mwenyezi Mungu asije akazikataa.

Hawa ndio wale ambao Mwenyezi Mungu amesema juu yao;

“Na hao ambao wanatoa waliyopewa, na hali nyoyo zao zinaogopa”.

Al Muuminun – 60

Imepokelewa kuwa Ali bin Abi Talib (RA) alikuwa akisema;

“Kuweni watu mnaojishughulisha sana na kukubaliwa kwa amali zenu kuliko mnavyojishughulisha na amali zenyewe, hamkumsuikia Mwenyezi Mungu aliposema;

“Mwenyezi Mungu huwapokelea wamchao tu”.?

Al Maidah – 27

Na kutoka kwa Al Hassan (RA) amesema;

“Hakika Mwenyezi Mungu ameujaalia Mwezi wa Ramadhani kuwa ni uwanja wa waja wake, wanashindana ndani yake katika kumtii na katika kutaka radhi Zake. Wengine wanashinda na kufuzu, na wegine wanabaki nyuma kisha wanajuta. Inastaajabisha kuona watu wanacheka na kucheza katika siku ambazo wafanyao mema wanafuzu na wafanyao maovu wanakula hasara”.

Na miongoni mwa sababu za mtu kusamehewa madhambi yake ni kumfuturisha aliyefunga, kumdhukuru Mwenyezi Mungu na kuomba maghfira. Dua ya aliyefunga inakubaliwa wakati anapokuwa amefunga na baada ya kufuturu, na pia Malaika wanawaombea maghfira waliofunga mpaka pale wanapofuturu.

Kwa vile sababu za mtu kusamehewa madhambi ndani ya mwezi huu ni nyingi sana, basi mtu anayenyimwa maghfira ndani yake huwa amekula hasara kikweli.

·        Basi lini anaweza kughufiriwa yule aliyekosa maghfira katika mwezi huu? Lini anaweza kusamehewa yule aliyekataliwa ombi lake katika usiku wa Lailatul Qadar? Atatengenea lini yule asotengenea ndani ya mwezi huu? Lini ataamka yule asiyeujua utukufu kisha akaghafilika katika mwezi wa Ramadhani? Kisichochumwa na kuvunwa kinapokuwa juu ya mti wakati wa mavuno, basi matokeo yake kitakatwa na kuchomwa moto, na atakayefanya mchezo asipande siku za kupanda, basi siku ya kuvuna hatovuna isipokuwa majuto na hasara.

RAMADHANI MWEZI WA KUEPUSHWA NA MOTO

Kwa vile katika kumi la mwisho la Ramadhani watu wengi wanaepushwa na Moto, na kwa vile kusamehewa kwa madhambi kunapatikana pia kwa njia ya kufunga na kusali, ndiyo maana Mwenyezi Mungu akatutaka pale mwezi unapomalizika tumtukuze na kumshukuru.

Mwenyezi Mungu anasema;

“Mtimize hesabu hiyo na kumtukuza Mwenyezi Mungu kwa kuwa amekuongozeni, ili mpate kumshukuru”.

Al Baqarah – 185

Kwa hivyo shukrani zote ni Zake yule aliyewaneemesha waja wake kwa kuwawezesha kufunga na kwa kuwaghufuria madhambi yao na kuwaepusha na Moto.

Ewe ambaye Mola wake amemuacha huru na Moto, usije ukarudia tena baada ya kuepushwa nao. Mola wako anakuepusha nao na wewe bado tu unendelea kuusogelea? Mola wako anakuepusha nao na wewe hutaki kuukimbia?

·        Kwa hivyo anayetaka kunusurika na Moto katika mwezi wa Ramadhani azitafute sababu zitakazomwezesha aachwe huru nao, na Mwenyezi Mungu amezieneza sababu hizo ndani ya mwezi huu.

Katika Sahih ya Ibni Khuzaimah imeandikwa;

“Zidisheni ndani yake mambo mane. Mambo mawili kwa ajili ya kumridhisha Mola wenu na mambo mawili hamwezi kuepukana nayo;

Ama mambo mawili mtakayomridhisha kwayo Mola wenu ni kutamka ‘Laa ilaaha illa Llah’, na kusema ‘Astaghfirullah’.

Ama mawili msiyoweza kuepukana nayo; Mumuombe Mola wenu akuingizeni Peponi na akuepusheni na Moto.

Sababu zote nne zilizotajwa katika hadithi hii zinamwezesha mtu aachwe huru na Moto na kupata maghfira, na hii ni kwa sababu tamko la ‘tawhiyd’; ‘Laa ilaaha illa Llah’, linaondoa madhambi na kuyafutilia mbali, na neno hili ni sawa na mtu kumuacha huru Mtumwa.

Ama neno ‘Astaghfirullah’, litasababisha kusamehewa mtu madhambi yake, na dua ya aliyefunga inakubaliwa pale anapokuwa amefunga na hata anapofuturu. Na Ishtighfar bora ni ile inayoambatanishwa na toba. Kwani anayeomba maghfira kwa ulimi wake wakati moyo wake umeazimia baada ya kumalizika mwezi kurudi tena katika maasi, huyo saumu yake inakataliwa na mlango wa toba anafungiwa.

Katika dua muhimu pia ni kumuomba Mwenyezi Mungu akuingize Peponi na akuepusha na Moto, kwani Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) aliwahi kusema juu yake;

“Hayo ndiyo lengo letu”.

Abu Daud na Ibni Majah

MUHAMMAD FARAJ SALEM AL SAIY

——————————————————————————————————-

VUNJA JUNGU NI MAASI
 
IMEANDIKWA NA: Ndugu zetu wa Kiislamu

BISMILLAHIR-RAHMAANIR-RAHIIM
Assalaamu Alaykum Warahmatullah!
Ni baada ya siku chache tu kwa msaada wake Allah Karim utakuwa unapumua na kuishi ndani ya mwezi mtukufu wa Ramadhani. Mwezi ambao huwapa waislamu fursa ya kuitekeleza mojawapo ya nguzo tano za Uislamu, swaumu ya Ramadhani. Katika kuuheshimu, kuutukuza na kuuenzi mwezi huu mtukufu.Naam, Ramadhani hiyo mlangoni mwako inabisha hodi. Wewe kama muislamu umejiandaje kuupokea mwezi wako huu mtukufu? Je, wewe ni mmoja wa wale wanaoupokea mwezi wa Ramadhani kwa kile kinachojulikana kama VUNJA JUNGU?

Hebu na tujiulize kwa pamoja, tulivunjao hilo jungu mwaka hata mwaka na wale tusiolivunja, vunja jungu ni nini khasa? Bila ya shaka mtakubaliana nasi kwamba vunja jungu kama litafsirikanavyo kutokana na matendo yatendwayo na wavunja jungu katika kulivunja kwao hilo jungu. Ni mkono wa kwaheri unaopungwa kwa maasi mbalimbali kwa ajili ya kuingia kwa mwezi mtukufu wa Ramadhani. Wavunja jungu huitumia fursa ya zile siku mbili tatu kabla ya kuandama kwa mwezi mwandamo unaoashiria kuanza kwa funga tukufu ya Ramadhani.

Kuogelea na kupiga mbizi maradufu katika maasi waliyokuwa wakiishi nayo katika kipindi cha ile miezi kumi na moja nje ya Ramadhani. Kwa hivyo basi, vunja jungu kwa mlevi ni kulewa sana kwani hataipata fursa hiyo tena ila baada ya kumalizika kwa mwezi wa Ramadhani.

Vunja jungu kwa mzinifu ni kuzini sana na kutengana na kimada wake kuipisha Ramadhani, kisha mchezo uendelee baada ya Ramadhani. Vunja jungu kwa mpenzi wa muziki ni kukesha katika kumbi za starehe akicheza na kunywa kufidia ile fursa atakayoikosa kwa sababu ya kuingia kwa mwezi mtukufu. Mbele za watu hawa Ramadhani ni mithili ya gereza/kifungo kinachowaondolea na kuwanyang`anya uhuru wa kuishi kama wapendavyo kwa kufuata matashi na matamanio ya nafsi zao.

Hawa wanasahau kwamba wanawajibika kuishi kwa mujibu wa muongozo wa Mola Muumba wao na sio kwa kuongozwa na matashi yao! Kwa ujumla vunja jungu ni kushindana katika aina mbalimbali za maasi kwa sababu ya kuingia kwa mwezi mtukufu wa Ramadhani ambao hautoi uwanja wa maasi hayo kwa mijibu wa fikra zao potofu. Kwa nini tunasema kwa mujibu wa fikra zao potofu, hilo linatokana na ukweli kwamba hakuna kibali wala uhalali wa kufanya maasi na mtu kuishi kama apendavyo nje ya Ramadhani.

Ikiwa vunja jungu linaashiria jambo, basi jambo hilo halitakuwa jingine zaidi ya kuonyesha kufilisika kiimani kwa huyo mvunja jungu. Kwani muumini wa kweli hawezi kuvunja jungu, kwa kuwa anatambua kwamba kufanya hivyo ni kumuasi Allah Mola Muumba wake. Kwa muumini wa kweli kujiepusha na maasi na kumtii Mola wake ni zoezi linaloyatawala maisha yake yote. Bila ya kuangalia kuwa huu ni mwezi wa Ramadhani au ni nje ya Ramadhani. Kuagana na maasi eti kwa sababu tu ya kuingia kwa mwezi mtukufu wa Ramadhani, kisha kuyarejea tena baada ya kumalizika kwake.

Huo tukubali au tukatae ni UDHAIFU WA IMANI na si vinginevyo. Kwani huyo Mola wa Ramadhani unayeacha maasi ndani yake kwa ajili yake, ndiye Mola wa hiyo miezi mingine unayojihalalishia maasi ndani yake. Amri ya kumtii Mola wako kwa kuyatekeleza yote aliyokuamrisha na kuyaacha yote aliyokukataza inauhusu mwezi wa Ramadhani na baki ya miezi mingine isiyo Ramadhani.

Kumuabudu Mola wako ndani ya Ramadhani tu ni kujiuundia utaratibu wa ibada kinyume na ule aliokupangia Allah Mola Muumba wako. Elewa kufanya kwako hivi ni sawa na kusema kuwa utaratibu wa ibada aliokuwekea Mola wako aliye mjuzi wa manufaa na maslahi yako ama haufai au umepitwa na wakati. Na kwamba wewe kama kiumbe unaweza kujiundia utaratibu utakaokudhaminia manufaa na mafanikio katika ulimwengu wako huu na ule ujao. Elewa kwa mtindo na mtaji wako huo siku ya kiyama Allah atakuambia ujilipe wewe mwenyewe kwa kuwa yeye hakukuamrisha kufanya ibada kwa utaratibu huu unaokwenda nao sasa.

Ewe ndugu mpenzi wee! Elewa na ufahamu fika kwamba Ramadhani ipokelewayo na kukaribishwa na vunja jungu haitakuwa na athari yo yote kwako wewe ambaye ndiwe mlengwa wa Ramadhani na wala sio Mola wako. Kwako Ramadhani haitakuwa ila mithili ya kujenga nyumba angani bila ya kuwa na msingi imara uliokita ardhini.

Ewe ndugu mpenzi mvunja jungu, utaendelea kulivunja hilo jungu na kumuasi Mola wako mpaka lini?! Hebu jiulize, nini utakuwa mwisho wa huku kuvunja jungu kwako?! Tangu umeanza kuvunja jungu na bila shaka ni jungu la maasi umepata na kuvuna nini?! Ndugu mpenzi hebu ihurumie nafsi yako kwa kuitegea sikio la usikivu kauli hii tukufu ya Mola wako: “ANAYEFANYA MEMA ANAJIFANYIA (mwenyewe) NAFSI YAKE, NA MWENYE KUTENDA UBAYA NI JUU (ya nafsi) YAKE (vile vile)…” [41:46]

Aya inakuongoza kutambua kwamba unapovunja jungu, hufanyi hivyo ila ni kwa hilaki na maangamivu ya nafsi yako wewe mwenyewe leo hapa duniani na kesho kule akhera. Ambapo utapewa daftari la amali zako uikute na vunja jungu yako, hapo ndipo utasema: “…OLE WETU! NAMNA GANI MADAFTARI HAYA! HAYALIACHI DOGO WALA KUBWA ILA YAMELIDHIBITI (yameliandika)! NA WATAKUTA YOTE YALE WALIYOYAFANYA YAMEHUDHURIA HAPO; NA MOLA WAKO HAMDHULUMU YO YOTE”. [18:49]

Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-anasema: “Jibril alinijia na akaniambia: Ewe Muhammad! Ishi utakavyoishi, hakika wewe ni mwenye kufa. Na penda ukipendacho hakika utatengana nacho, na tenda ulitakalo hakika utalipwa kwalo…” Al-Baihaqiy Elewa ewe ndugu mpenzi ukiwa mwana kuelewa, elewa kwamba kwa mujibu wa hadithi hii:-
Vunja jungu yako ina mwisho wake ambao ni kufa kunakoashiria mwanzo wa safari ngumu ya kuhudhurishwa mbele ya Mola wako. Hii ndiyo siku anayoitaja Mola wako kwa kauli yake tukufu: “NA IOGOPENI SIKU AMBAYO MTARUDISHWA KWA ALLAH, KISHA VIUMBE WOTE WATALIPWA KWA UKAMILIFU YOTE WALIYOYACHUMA; NAO HAWATADHULUMIWA”. [2:281]

Lewa sana kwani pesa ni zako,zini sana na endelea kuvunja jungu, lakini tambua kuwa iko siku moja utalipwa kwa yote uliyoyatenda hapa duniani: “BASI ANAYEFANYA WEMA (hata) WA KIASI CHA UZITO WA MDUDU CHUNGU ATAONA JAZAA YAKE. NA ANAYEFANYA UOVU (hata) WA KIASI CHA UZITO WA MDUDU CHUNGU ATAONA JAZAA YAKE”. [99:7-8]

Ewe mvunja jungu wee! Hebu waidhika na sehemu hii ya kauli ya swahaba wa Mtume;Sayyidna Abdullah Ibn Abbas-Allah amuwiye radhi: “Ewe mtenda dhambi wee! Usijiaminishe na matokeo ya dhambi yako na tambua kwamba kiifuatiacho dhambi hiyo ni kikubwa kuliko dhambi yenyewe.

Kwani kule kutokuwaonea kwako haya malaika walioko kuliani na kushotoni kwako wakati unapofanya dhambi, hakupungui kuwa ni dhambi. Na kicheko chako wakati unatenda dhambi na ilhali hujui Allah atakufanya nini, ni kikubwa zaidi kuliko hiyo dhambi uitendayo.

Na kuichelea kwako dhambi unapofanikiwa kuitenda, ni kukubwa zaidi kuliko hiyo dhambi yenyewe. Na kuihuzunikia kwako dhambi kwa kushindwa kuitenda, ni kukubwa zaidi kuliko dhambi husika. Haya mpenzi mvunja jungu, ikiwa mpaka hapa bado hujawaaidhika na ukaacha kulivunja hilo jungu, hebu zidi kutega sikio:

Mtu mmoja alimwambia Sufyaan Thauriy-Allah amuwiye radhi-nipe nasaha ambazo nikizifanyia kazi sitathubutu kumuasi Allah. Sufyaan akamwambia: Yakumbuke mambo matano:
Je, inastahiki kwako kumuasi Allah na ilhali yeye ndiye anayekuruzuku?
Je, unadhani kuwa wewe unamuasi Allah na ilhali yeye anakuona?
Je, unaweza kumuasi Allah nje ya ufalme/milki yake?
Je, unaweza kuyaakhirisha mauti yakikujia?
Je, siku ya kiyama utakuwa una uwezo wa kujiondoshea adhabu?
Yule mtu akajibu: Siwezi lo lote katika hayo. Sufyaan akamwambia: Basi vipi unathubutu kumuasi yule anayekuruzuku, anakuona, nawe uko katika milki yake, akakuandikia mauti na wala huwezi kuizuia adhabu yake isikufike? Akasema mtu yule: Wallah sitamuasi muda wa uhai wangu.

Hebu nawe mvunja jungu, jiulize maswali matano hayo halafu ndio uamue ama kulivunja jungu au kutokulivunja. Kumbuka ewe ndugu muislamu kwamba:-
Kuvunja jungu ni kumuasi Allah na Mtume wake: “NA ANAYEMUASI ALLAH NA MTUME WAKE, NA KUIRUKA MIPAKA YAKE (Allah) ATAMUINGIZA MOTONI. HUMO ATAKAA MILELE NA ATAPATA ADHABU ZIFEDHEHESHAZO”. [4:14]

Kuvunja jungu ni kuudhihaki mwezi mtukufu wa Ramadhani. Na kuudhihaki mwezi huu hakumaanishi kingine zaidi ya kuidhihaki Qur-ani Tukufu. Nako huku kuidhihaki Qur-ani, hakika si vinginevyo ila ni kumdhihaki aliyeshushiwa Qur-ani Mtume. Na hakuna anayethubutu kupinga kwamba kumdhihaki Bwana Mtume ni kumdhihaki Allah akiyemtuma. Na huko kumdhihaki Allah ni ukafiri tu na si vinginevyo: “AMA WALE WALIOKUFURU, NITAWAADHIBU ADHABU KALI KATIKA DUNIA NA AKHERA, WALA HAWATAPATA WASAIDIZI WA KUWASAIDIA”. [3:56] Vunja jungu ni khadaa na ghururi za dunia. Uovu basi si huko kukhadaika, bali ni kushikilia kukhadaika baada ya kutanabahishwa. Wasalaamu Alaykum Warahmatullah

————————————————————————————————–
HOTUBA YA MTUME KATIKA KUUKARIBISHA MWEZI MTUKUFU WA RAMADHAN:
Jueni na eleweni enyi ndugu zanguni Waislamu kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu amejaalia mafanikio ya duniani ni ya muda mfupi, yenye kwisha na kuondoka, na mafanikio ya akhera ndiyo yenye kusalia/kubakia milele. Haya mafanikio ya kudumu, hayapatikani ila kwa kupitia barabara ngumu ya “TAQ-WA” kumcha Mwenyezi Mungu na kumtii na kumfuata Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie-. Katika jumla ya nguzo kuu za Taqwa ni kuufunga huu mwezi mtukufu wa Ramadhani ambao Allah ameujaalia kuwa ni REHMA kwa viumbe. Nao kama mjuavyo ndio mwezi ambao imeteremshwa ndani yake Qur-ani Tukufu ikiwa ni muongozo kwa watu wote. Muongozo uliosheheni hoja wazi za uongofu na upambanuzi baina ya haki na batili. Ramadhani pia ni mwezi ambao hufunguliwa ndani yake milango ya pepo na kufungwa milango ya moto. Ni kwa kuuzingatia umuhimu na nafasi ya mwezi wa Ramadhani, ndipo Bwana Mtume akaitoa Khutba yake tukufu, khutba ya kihistoria, khutba kongwe katika kuupokea na kuukaribisha mwezi mtukufu wa Ramadhani.Imepokelewa na Salmaan Alfaarisy – Allah amuwie Radhi – amesema : Alitukhutubia Mtume wa Mwenyezi Mungu – Rehema na Amani zimshukie – katika siku ya mwisho ya mwezi wa Shaabani, akasema : “Enyi watu, umekufikieni mwezi mtukufu wenye baraka. Ndani ya mwezi huu umo usiku wa LAYLATIL QADRI usiku ambao ni bora kuliko miezi alfu moja. Mwenyezi Mungu amejaalia funga ya mwezi huu kuwa ni FARADHI na kisimamo (cha ibada) cha usiku wake kuwa ni SUNA. Atakayejikurubisha (kwa Mola wake) ndani ya mwezi huu kwa (kutenda) jambo lolote la kheri, (malipo, jazaa yake) itakuwa ni kama mtu aliyetekeleza fardhi katika miezi mingine. Na atakayetekeleza fardhi katika mwezi huu, atakuwa ni kama mtu aliyetekeleza fardhi sabini katika miezi mingine. Na mwezi huu ni mwezi wa SUBIRA, nao ni mwezi ambao mwanzo wake ni REHEMA na katikati yake ni MAGHFIRA/MSAMAHA WA ALLAH na mwisho wake ni KUACHWA HURU NA ADHABU YA MOTO. Yeyote atakayemfuturisha mfungaji ndani ya mwezi huu, (ujira wa futari hiyo) utakuwa ni maghfira ya madhambi yake (mfuturishaji) na kuachwa huru na adhabu ya moto na atapata ujira kama aupatao mfungaji bila ya kupungua chochote katika ujira/thawabu zake (mfungaji)”. Tukasema : Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, sio sote tunaweza kupata (kitu) cha kumfuturisha huyo mfungaji. (Mtume) akawajibu : “Mwenyezi Mungu humpa thawabu hizi yule atakayemfuturisha mfungaji ndani ya mwezi huu kwa onjo/funda ya maziwa au (kokwa ya) tende au funda ya maji. Na atakayemshibisha ndani ya mwezi huu mfungaji, itakuwa ujira (wa shibe hiyo) ni maghufira ya madhambi yake (mshibishaji) na Mola wake atamnywesha katika hodhi (birika) langu funda moja ambayo hatopata kiu baada yake kabisa. Na atakuwa na ujira kama aupatao mfungaji bila ya kupungua chochote katika ujira wake (mfungaji). Na atakayempunguzia kazi mtumishi/mfanyakazi wake ndani ya mwezi huu, Mwenyezi Mungu atamghufiria madhambi yake na kumuacha huru na adhabu ya moto. Basi kithirisheni sana ndani ya mwezi huu mambo manne. Mtamridhisha Mola wenu kwa kutenda mambo mawili kati ya manne hayo; na mambo mawili hamjikwasii (hamna budi) nayo. Ama hayo mambo mawili mtakayoridhisha nayo Mola wenu ni shahada (kushuhudia kwamba hapana Mola apasaye kuabudiwa kwa haki ila ALLAH) na mumtake maghfira. Na ama yale mambo mawili msiyojikwasia nayo ni mumuombe Mola wenu pepo na mjilinde/mjikinge kwake na (adhabu) ya moto”. Ibn Khuzaymah katika sahihi yake.

MAELEZO : Ikiwa tunafuatana pamoja, tunaweza tukaigawa hadithi hii tukufu ambayo ni khutba kongwe iliyo hai hadi leo na itaendelea kuwa hai mpaka mwisho wa dunia. Khutba hii iliyotolewa na Khatibu mahiri, Bwana Mtume katika kuukaribisha mwezi mtukufu wa Ramadhani, inagawanyika katika sehemu kuu tatu au tuseme ina vipengele vikuu vitatu. Ukiizingatia hadithi utakuta mwanzo wa khutba yake, Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie – anawafahamisha maswahaba na umma mzima juu ya utukufu, ubora, cheo na nafasi ya mwezi wa Ramadhani. Kuna hekima/falsafa gani ndani ya maelezo haya ? Mtume anauelezea mwezi wa Ramadhani ni mwezi wa namna gani ili muislamu aujue, kwani waswahili husema asiyekujua hakuthamini. Akishaujua atauthamini na kuupa hadhi yake unayostahili. Kuuthamini na kuupa heshima mwezi wa Ramdhani ni kuzidisha sana TWAA kwa Mwenyezi Mungu kwa kufanya namna mbali mbali za ibada na mambo mengine ya kheri.

Sehemu ya pili ya hadithi, Bwana Mtume anataja fadhila/faida na ubora wa mwezi wa mtukufu wa Ramadhani na kuwa ibada yeyote inayofanywa ndani ya mwezi huu hailingani kithawabu/kiujira na ile ibada inayofanywa katika miezi mingine. Kwa hiyo basi, Ramadhani ni ndio musimu wako wa ibada. Kadhalika Bwana Mtume anatuelezea malipo na thawabu adhimu anazozipata mja mwenye kumfuturisha nduguye muislamu katika mwezi huu wa Ramadhani. Hapa Bwana Mtume anaashiria moyo wa ukarimu na upendo utakiwao waislamu wajipambe na kuwa nao. Kwani waislamu wakipendana watakuwa ni wamoja na mshikamano, na wakishikamana watautawala ulimwengu na hapatakuwa na nguvu ya kuwashinda, si magharibi wala mashariki.

Kisha ndipo Bwana Mtume akaikhitimisha khutuba yake kwa kutoa wito muhimu kwa waislamu. Akawataka wakithithirishe sana kumpwekesha Mola wao kwa kuleta kalima ya shahada na wamtake sana maghfira. Hali kadhalika akawataka waislamu wakithirishe mno kumuomba Mola wao pepo na wamuombe awakinge na moto wa jahanamu. Ili kuutekeleza wito huu ndipo wanazuoni wetu wema -Allah awarehemu- wakatuwekea uradi uletwao msikitini ndani ya mwezi wa Ramadhani. Chimbuko la uradi huu ni ile sehemu ya mwisho ya hadithi. Uradi wenyewe ni huu :

ASH-HADU AN LAA ILAHA ILLA-LLAHU NASTAGHFIRULLAH, NAS-ALUKAL-JANNATA WANA’UDHU BIKA MINAN-NAAR ALLAHUMMA INNAKA AFUWWUN, TUHIBBUL-AFWA FA’FU ‘ANNAA YAA KARIIM

Tunashuhudia kuwa hapana Mola apasaye kuabudiwa kwa haki ila Allah, Tunakuomba maghfira (msamaha wa madhambi) Ewe Allah, Tunakuomba pepo na tunajikinga kwako na moto, Ewe Allah, wewe mimi ni msamehevu na unapenda msamaha, basi tusamehe Ewe KARIMU.

Haya shime ndugu zanguni waislamu, tukithirishe kuuleta uradi huu ndani ya mwezi wa mavuno; mwezi mtukufu wa Ramadhani. Kwa kufanya hivyo tutakuwa tumeuitikia wito wa Bwana Mtume kwa maslahi na faida yetu wenyewe.

TUNDA LA RAMADHANI :

Karibu ndugu yangu muislamu katika bustani ya Bwana Mtume -Rehema na Amani zimshukie – uchume utakavyo na kula kiasi chako matunda matamu, mazuri yasiyokwisha hamu; matunda ya Ramadhani. Ili ufaidike na kunufaika na matunda haya unatakiwa uingie ndani ya bustani hii tukufu kwa unyenyekevu, utulivu, adabu, heshima na usikivu.

TUNDA LA KWANZA – DUA YA KUFUTURU

Amepokea Ibn Majah kutokana na hadithi ya Abdillah Ibn Amri (amesema Mtume) : YUNA MFUNGAJI WAKATI WA KUFUTURU KWAKE DUA ISIYOREJESHWA (yenye kujibiwa bila ya kipingamizi)”. Ni kwa sababu hiyo ndiyo Mtume alikuwa akisema (wakati wa kufuturu) :

[ALLAHUMMA INNIY LAKA SWUMTU WA’ALAA RIZQIKA AFTWARTU FAGH-FIRLIY MAA QADDAMTU WA MAA AKHARTU DHAHABAD-DHWAMAU WABTALLIT-‘URUQU WATHABATAL AJRU IN-SHAALLAHU TAALA]

Maana yake : “Ewe Mola wa haki ni kwa ajili yako tu nimefunga na nimefuturu kwa riziki yako. Basi (nakuomba) unisamehe dhambi zangu zilizotangulia na zijazo. Kiu kimeondoka na mishipa imelowana na ujira umethibiti pindipo atakapo Mwenyezi Mungu Mtukufu”

Haya shime ndugu zanguni waislamu, tumuige Mtume wetu katika hili na mengineyo ili tutengenekewe duniani na akhera. Usikubali kuipoteza fursa hii adimu ya kukubaliwa duao, omba na Mola Karimu atakupa.

TUNDA LA PILI : FADHILA ZA KUHARAKIA KUFUTURU :

Imepokelewa hadithi kutoka kwa Abuu Hurayrah – Allah amuwie Radhi – amesema, Amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu – Rehema na Amani zimshukie- “AMESEMA MWENYEZI MUNGU : HAKIKA WAJA WANGU WAPENDEZAO SANA KWANGU NI WALE WAHARIKIAO KUFUTURU” Ahmad na Tirmidhi.

MAELEZO : Ni vema mtu akafanya haraka kufuturu, maadam ana uhakika wa kutua/kuzama kwa jua. Ikiwa hana uhakika, basi ni vema akasubiri adhana ili asije akafuturu kabla ya muda. Haya zingatia upendwe na Mola wako.
_________________
Jazaakumullah

email to: alnoor@alnoorcet.co.uk

——————————————————————————————-
FAID ZA KUFUNGA MWEZI MTUKUFU WA RAMADHAN


Waislamu duniani kote katika wiki hii wameanza kufunga Mfungo Mtukufu wa mwezi wa Ramadhan ikiwa ni kutekeleza moja ya nguzo za Kiislamu.Pamoja na kufunga mwezi mzima, wapo baadhi ya watu wasiofahamu faida zake na hasara zake bali hujikuta wakifunga kwa jinsi wanavyotaka huku wengine wakiacha bila kufunga.Kwa mujibu wa mafundisho ya dini ya Kiislamu, kufunga mwezi wa Ramadhan ni lazima kwa kila Muislamu mwenye afya njema na aliyekwisha balehe kama kwenye Qur aan surat Baqara aya 183 inavyosema “Enyi ambao mlioamini mmefaradhishiwa kufunga kama walivyofaradhishiwa wale ambao waliopita kabla yenu ili muwe wacha Mungu”.

Hata hivyo watu walioruhusiwa kutofunga ni pamoja na mtoto mdogo asiyefikia balehe, mgonjwa ambaye akifunga anaweza kuzidiwa, mwanamke aliye kwenye siku zake za mwezi (hedhi) au baada ya kujifungua (nifasi) pamoja na mzee asiyeweza ambaye hutakiwa kumpa masikini kibaba cha chakula kwa kila siku asiyofunga.

Kwa Tanzania kibaba cha chakula hufaa kuwa unga wa sembe au mchele kwani ndio huliwa na watu wengi zaidi.Mtume Muhammad (S.A.W) anasema kuwa kwa watakaofunga wataweza kuingia katika mlango wa Alrayaan ambao upo katika pepo na siku hiyo ya Kiyama patasemwa “Wako wapi wenye kufunga? Hataingia katika mlango huu mtu yeyote asiyekuwa wao”.

Kufunga huko ni kujizuia kula , kunywa, kutofanya tendo la ndoa pamoja na kuacha mambo yote mabaya yanayokatazwa ikiwamo kutukana matusi au kutembea uchi na badala yake ni kufanya mambo mema kwa kadiri ya uwezo wako. Kufunga huko huanza alfajiri mpaka Magharibi baada ya jua kuzama.

Mbali na ulazima wa kufunga kwa kila Muislamu, kuna mambo yanayoweza kuharibu funga ya mtu na kulazimika kuilipa swaumu hiyo iliyoharibika. Mambo hayo ni pamoja na kutoka katika Uislamu kuhamia dini nyingine, kujitapisha kwa makusudi, kufuturu kabla ya kuzama jua, kuingiza kitu tumboni, kujitoa manii na kufanya tendo la ndoa mchana.

Mtume Muhammad (S.A.W) anasema, kwa wanaodharau kufunga ikiwa ni kuiacha nguzo ya nne ya Uislamu ni kafiri na wanafaa kuuliwa na mali zao kuchukuliwa na pia mali yake anayotoa kwa ajili ya dini pamoja na shahada yake haikubaliwi.

Na kwa wale wanaoacha kufunga Ramadhan bure bila kuwa na sababu ya msingi inayokubalika kidini, hata akija kuilipa haiwezi kukubalika maishani mwake.Licha ya kila Muislamu kulazimishwa kufunga, pia hupata malipo mazuri kutoka kwa Mwenyezi Mungu ambayo ni pamoja na kuyeyuka kwa nyama ya haramu iliyoko mwilini mwa mfungaji, kupata rehema za Mungu na kupewa amali zilizo bora.

Mfungaji huyo pia hatashikwa na kiu siku ya Kiyama, kuondolewa adhabu za kaburi pindi atakapofariki dunia, hupewa karama kubwa siku ya Kiyama pamoja na huepushwa na njaa siku ya Kiyama.Wakati wa Ramadhan inaelezwa ni wakati mzuri zaidi wa kuomba dua na kwa anayeomba akiwa kwenye swaumu, dua yake hukubaliwa kwa haraka.

Hadithi iliyopokelewa na Bukhari na Muslim inasema kuwa Mtume Muhammad (S.A.W) anasema utakapokuja mwezi wa Ramadhan hufunguliwa mlango wa peponi na hufungwa mlango wa motoni na yanafungwa mashetani hivyo ni kipindi kizuri kwa Waislamu na hasa kufanya toba.

Mwezi wa Ramadhan ndipo kulipoteremshwa Quraan na usiku wa mwezi huo unaelezwa ni bora kuliko miezi 1,000 ambapo malaika huteremka katika usiku kwa amri ya Mola wao kwa kila jambo hivyo wakati huo huwa mzuri kwa ajili ya maombi.

Wakati wa Ramadhan kuna mambo ambayo Muislamu akiyafanya huweza kumfanya apate thawabu kama kuwahi kufuturu, kuchelewa kula daku, kuwafuturisha Waislamu wenzake, kusoma Qur-an na kuzungumza maneno mazuri.

Wanaotoa sadaka za Ibada wakati wa Ramadhan wanapata thawabu gani?
Kwa anayefunga siku moja katika Ramadhan kwa ajili ya Mwenyezi Mungu atamuepusha uso wake na moto umbali wa baina ya mbingu na ardhi na humpa thawabu za mashahidi 300.

Kwa mwenye kuswali rakaa moja katika Mfungo huo, malipo yake ni sawa na mtu aliyesali rakaa 70,000 isiyokuwa Ramadhan na kwa atakayemsalia Mtume rakaa moja ni sawa na kumsalia rakaa 100,000 katika miezi mingine ya kawaida.

Mtu atakayemfuturisha mtu akashiba au wakala pamoja ni kama mtu aliyetoa sadaka ya dhahabu iliyojaa katika ardhi huku kwa atakayempa sadaka mcha Mungu ni kama katoa sadaka vituo vyote vinavyopata mwangaza wa jua.

Mafundisho ya dini yanaeleza kuwa kwa mtu atakayempa nguo moja mtu asiyekuwa na nguo katika mwezi wa Ramadhan basi Mungu atampa mtoaji nguo 70 peponi katika nguo watakazovaa mashahidi. Pia atakayemtembelea Muislamu katika mwezi huu hulipwa thawabu mfano wa mtu aliyemtembelea Nabii Muhammad(S.A.W).

Wafungaji wa mwezi huu wa Ramadhan, wanaelezwa kuwa siku ya Kiyama watakapotoka kwenye makaburi yao watajulikana kwa harufu nzuri kuliko manukato kutoka kwenye vinywa vyao.

Watapelekewa sinia nyingi za vyakula vya aina mbalimbali na wataambiwa na malaika “Kuleni kwani mlikaa na njaa wakati watu walipokuwa na shibe, tena kunyweni kwani mlikuwa na kiu wenzenu walipokuwa roho zao zimeburudika, pumzikeni kwani mlikuwa katika taabu na hali watu walikuwa ndani ya starehe”.

————————————————————————————-

KARIBU RAMADHAN:

“Enyi mlioamini! Mmeandikiwa saumu, kama walivyoandikiwa waliokuwa kabla yenu ili mpate kumcha Mungu, Siku maalum za kuhesabika , na atakaye kuwa miongoni mwenu Mgonjwa au yumo safarini atimize hisabu katika siku nyengine, na wale wasioweza watoe fidia kwa kumlisha maskini, na atakayefanya wema kwa kujitolea basi ni bora kwake na mkifunga ni bora kwenu kama mnajua”

Hizo ni ayya mbili tukufu zinazolingania saumu yaani ya mwezi mtukufu wa Ramadhani utakaoanza kesho penye majaliwa. Imepita miezi kumi na moja, nani kati yetu alitubia mwaka jana mwezi wa Ramadhani na nani aliusindikiza akadhani hautarudi tena ?. Nani alitenda maovu huku akijua na nani alijibabaisha na kusema bahati mbaya bilisi kanizidi badala ya kumzidi yeye!!.

Basi kwa Mola ipo hesabu, lakini tuukaribishe mwezi huu mtukufu kwa dua na sala na kutenda mema. Mwezi huu ni zaidi kwani muda wote wa umri wa mtu ni ibada hivyo fadhila za wema katika Ramadhan ni kulipwa wema maradufu. Ramadhan kwa waumini wa kiislamu ina siri kubwa kwani nyoyo hurejea kwa walioteleza na neema hushukia wanaadamu kwa kujikubalisha kutii mengi ambayo aliyasahau au kuyapuuza mja, hivyo wale wanaonyooka kupitia mwezio huo mtukufu wana fursa nzuri ya kuunganisha fadhila iliyowatakasa hadi miezi mengine kumi na moja.

Lakini ni wangapi wenye kuifanyia stihizai Ramadhani katika kuikaribisha. Huikaribisha vyema ? au huzidisha dozi ya maovu ijulikanayo kama vunja jungu kwa kumuasi M/mungu. Wema wenye kuikurubia saumu hii ya Ramadhan, huwa wanapanga mambo tofauti, kwa wale walio na kazi za ajira wao huzitenga saa zao vyema kabisa na huwa wamejiandalia misikiti na darasa mbali mbali na kama wanauwezo basi tayari hugawa mafungu ya kutoa sadaka zao. Wao na familia zao huzidisha ucha Mungu, kama walikuwa wazito siku zilizopita basi hutafuta walimu wa kuwaendeleza kukifahamu na kukisoma kitabu hicho.

Wanaotafuta vibarua nao hawagomei kazi ya Mungu kwa maana bado hawajabarikiwa na waliomba siku nyingi na kuhangaika bali huzidisha zaidi na kuiacha kazi ya rizki iamuliwe na Mola mwenyewe, hawavunjiki moyo au kukata tamaa.

Matajiri mwezi kama huu wana mtihani wa pekee kwa kujiandaa kutumia neema walioneemeshwa kwa kutoa sadaka zao kuimarishia misikiti, kuwalisha wanaohitaji, na kuwatibu wanaougua kwa gharama mbali mbali, bali wakijiwa na wenye kutafuta elimu katika vyuo vya juu basi hawawapi kisogo bali huwaongezea palipopungua au kubeba gharama kwani wanawekeza vyema mbele ya Mola.

Mfanya biashara huu simwezi wa mavuno ya kidunia na ni hatari kuumiza nyoyo za wahitaji wa huduma kwa kutafuta nafuu maana watu wanahitaji zaidi, ni wewe mfanya biashara utakayempa moyo wa furaha mfungaji mwenzio, kwa kumuuzia kihalali wala usile viapo vya bei kujihalalishia biashara yako, sema kweli tuu akufahamu. Ukitaka akuamini kwa kula yamini basi Uumini wenu mnautia dosari maana WALLAHI Ilitoka kwa kutokuaminiana waumini nanyi mmo katika saumu.

Hapana sababu hata moja mkulima kuzuia bidhaa na matunda kuleta mjini wakati huu wakuikaribisha ramadhani , maana msimu wa kupata umekaribia. Huu ni msimu wakuvuna thawabu, Usimpe dalali wa sokoni sababu, top ikawa top kweli mkakisahau kitabu.

Hiki sikipindi cha watu kunyanyasana kwa mambo yapitayo mambo ya Ulimwengu, kupigana au kutiana ngeu, kusema yasiyoridhisha kama matusi, kuvaa visivyo na kuzisahau nyakati za ibada kwa utashi wa kidunia . Tuombeane kheri , tustahamiliane na tutendeane yenye kweli na uadilifu.

Tunaikaribisha Ramadhani tujihadhari sana tena sana kwani mwezi huo una malipo makubwa anaeuendea kinyume huyo anadai vita vinavyoiandama nafsi yake. Basi mhurumie Muumini mwenzio, Usimghasi,Usimuuzi, Usimsengenye, Usimuumize wake, Usimzulie mambo na jitahidi usimchukulie chake au kumwaga damu yake. Haya tunayakumbusha na kukumbushana maana tuna mtihani mbele yetu na M/Mungu atuvushe Salama.

YARABBI

Tupe amani nchini mwetu, Utupe huruma baina yetu.

Utupe neema ya mazao na elimu kati yetu.

Uwabariki masheikhe na Maimamu zetu.

watupe darsa na kutuongoza katika sala zetu.

Zikubali ibada na Dua zetu.Tuhidie Wana wetu.

Zidhibiti na kuziongoza ndoa zetu.Wape moyo wakutoa Matajiri wetu.

Wape moyo wasubira mafukara na maskini miongoni mwetu.

Ramadhani yote iwe ya salama

Amiin Yarabbi Amiin .

Kijana Wenu Mtifu

Al Udii (Sauti Ya Nasaha).

———————————————————————————————–

Njia 10 Za Kuukaribisha Vizuri Mwezi Mtukufu Wa Ramadhaan-

Inatupasa tumshukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) kwa kutupa umri tukiwa katika Uislamu na Iymaan hadi kutufikisha tena kukaribia Mwezi Mtukufu wa Ramadhaan. Na hii ni fursa nyingine Anayotupa Allaah Ta’aala katika maisha yetu kushuhudia mwezi huu na kupata fadhila zake.

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala):

((يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ كُتِبَ عَلَيْكُمُ الصِّيَامُ كَمَا كُتِبَ عَلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِكُمْ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ))  (( أَيَّامًا مَّعْدُودَاتٍ …

((Enyi mlioamini! Mmefaradhishiwa Swawm, kama waliyofaradhishiwa waliokuwa kabla yenu ili mpate kumcha Allaah)) (([Mfunge] siku maalumu za kuhisabika….  [Al-Baqarah: 183-184]

Hii ni neema ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala)Ambaye Ametujaalia kuwa na miezi iliyo bora kuliko miezi mingine au siku bora au masaa bora kuliko mengine, ambazo thawabu zake za mema yanayotendeka humo huwa ni zaidi ya nyakati nyingine. Mfano wake ni kama kunapokuwa na mauzo yaliyopunguzwa bei dukani (sale), ambayo kawaida yake huwekwa kwa muda mdogo tu maalum.  Na muda huu mtu huweza kununua vitu vingi kwa malipo kidogo tu. Hali kadhalika Ramadhaan, ni mwezi mmoja tu, lakini malipo yake huwa ni mengi kuliko hata malipo ya miezi yote mingine.  Ikiwa mtu atatimiza Swawm yake inavyopaswa na kufanya mema mengi, na akawa katika Twa’a (utiifu) kamili na kuomba maghfira, basi hutoka katika mwezi huu akiwa ameghufuriwa madhambi yake.

Amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

(( من صام رمضان إيماناً واحتساباً ، غفر له ما تقدم من ذنبه )) أخرجه البخاري ومسلم

((Atakayefunga Ramadhaan kwa iymaan na kutaraji malipo, ataghufuriwa madhambi yake yaliyotangulia)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

Ramadhaan ni mwezi ambao tunatimiza Fardhi mojawapo ya Kiislamu. Ni mwezi uliojaa baraka, kheri na Rahma za Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala). Kila Muislamu inampasa aukaribishe mwezi huu kwa furaha na matumaini kamili.

Zifuatazo ni njia kumi za kujitayarisha kuukaribisha mwezi wa Ramadhaan na kupata manufaa makubwa pindi utakapotimiza:

1-Du’aa

Anza kwa kuomba Du’aa kwamba mwezi huu ukufikie wakati umo katika hali ya siha nzuri na usalama hata uweze kufunga na kufanya ibada zako kwa hamu kubwa na wepesi.

2-Mazoezi katika mwezi wa Sha’abaan

Funga Sunnah nyingi katika mwezi wa Sha’abaan, soma Qur-aan Juzuu moja kila siku au chini yake, amka usiku uswali japo Raka’ah mbili, kisha zidisha kidogo kidogo hadi inapoingia Ramadhaan uwe tayari umeshapata mazoezi mazuri.

3-Shukurani Na Furaha:

Mshukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Kukupa uhai na siha hata uifikie Ramadhaan nyingine.  Imaam An-Nawawy alisema, kwamba shukurani inapasa kwa kila jambo jema unalojaaliwa kubwa au dogo na vile vile shukurani inapasa kwa kila jambo baya Analokuepusha nalo Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala). Kwa hivyo fanya ‘Sajdatush-Shukr’ [Sajda ya kumshukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala)] kwa neema hii tukufu.

Furahia kukufikia mwezi wa Ramadhaan kama unavyomfurahikia mgeni mpenzi anapokuja kwako na kumuandalia mazuri yote.  Maswahaba (Radhiya Allaahu ‘anhum), walikuwa wakiamkiana unapoingia mwezi wa Ramadhaan na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akisema hivi anapowapa habari nzuri za mwezi wa Ramadhaan:

((جاءكم شهر مبارك افترض عليكمصيامه تفتح فيه أبواب الجنة وتغلق فيه أبواب  الجحيم وتغل فيه الشياطين فيهليلة خير من ألف شهر من حرم خيرها فقد حرم)) رواه أحمد

 

((Umekujieni mwezi wa Ramadhaan, ni mwezi wa Baraka.  Imefanywa Swawm kwenu kuwa ni Fardh, milango ya Pepo hufunguliwa na milango ya moto hufungwa na mashaytaan hufungwa. Umo katika mwezi huu usiku ulio bora kuliko miezi alfu.  Atakayenyimwa kheri zake hakika kanyimwa [yote ya kheri] )) [Ahmad]

4-Jipangie wakati na weka maazimio

Ni jambo la kusikitisha kuona watu wengi wanafurahia kuingia mwezi wa Ramadhaan kwa kujiandaa kupanga mambo ya kidunia badala ya mambo ya Akhera.  Wengi hukimbilia kwenda sokoni kununua nguo za ‘Iyd, na kufurahikia vipindi vya Ramadhaan katika televisheni ambavyo sio vya dini kama ‘misalsal‘ (maonyesho ya sinema yanayoendelea [series]), na pia kuanza kukusanya video za filamu, mipira, na mambo ya kupotezea muda usiku wa Ramadhaan. Pia wengine kunua karata, dhumna, meza ya mchezo wa keram kwa maandalizi ya vipumbazo na vipoteza muda katika mchana wa Ramadhaan ili wasiihisi Swawm au kuupeleka muda haraka kama wanavyoamini wao. Badala ya kufanya maandalizi ya kununua misahafu ya ziada, kanda za mawaidha, Qur-aan, kukusanya video za mawaidha na mafunzo mbalimbali ya Dini, vitabu vya Dini kwa lugha wanayoifahamu kwa wepesi na kadhalika.

Huu ni mwezi wa kufanya ibada na fursa ya kujichumia mema mengi yamfaayo mtu Akhera. Kwa hiyo ndugu Waislamu, tujitahidi kuutumia wakati wetu wote bila ya kupoteza hata dakika moja, na muhimu sana kujipangia mapema wakati wako kama ifuatavyo:

 • Ni bora kujipangia nyakati zote za mwezi mzima vipi utatumia muda wako wa mchana na usiku. Weka maazimio ya dhati kuchukua fursa kamili ya wakati wote wa mwezi huu.
 • Weka mpango maalum wa kazi zako hata uweze kuswali kwa wakati kila kipindi, kusoma Qur-aan, kula daku na mengineyo kama tutakavyotaja hapa chini.
 • Kama ni mwanafunzi na kama unakuwa ukisoma usiku, lala mapema, kisha uamke uswali Qiyaamul-Llayl na usome masomo yako baada ya hapo.
 • Anza mpango wako kwa siku chache na kama unahitaji kurekebisha kuboresha nidhaam yako fanya hivyo uweze kujua nidhaam ipi itakayowafikiana na hali yako.

Nasaha kwa kina Mama na kina Dada:

Fanyeni maandalizi mapema ya kununua vyakula vya mwezi wa Ramadhaan na kuviandaa vyenye kuandalika mapema kabla Ramadhaan haijaanza, kama vile; sambusa, madonge ya chapati, maandazi, maji ya matunda n.k. na kuweka kwenye mashine ya kugandisha barafu (freezer) au jokofu ili ikifika Ramadhaan muwe na kazi chache za jikoni na muweze kupata nafasi kubwa ya kushughulika na Ibaadah mbalimbali kama kusoma Qur-aan, kusikiliza mawaidha na hata kuhudhuria Darsa za Dini.

5-Tawbah na Maghfirah

Omba Tawbatun-Nasuuha kwa Mola wako na waombe msamaha wale uliowakosea. Kufanya hivi kutanufaisha zaidi Swawm na Swalah zako na  pia kukupa imani kuwa huna haki ya mtu.

6-Jifunze Fiqhi ya Swawm

Jifunze elimu ya mambo yanayohusu Swawm (Fiqhi ya funga), hiyo ni muhimu ili usije kufanya jambo la kuharibu Swawm yako.  Jifunze Swawm kama aliyokuwa akifunga Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)  ndio mfano bora kabisa wa kuufuata.

Swawm haifunguliwi kwa kula na kunywa tu, bali pia ni kujiepusha na maneno mabaya na kufanya mambo mabaya kama kusengenya, kutukana, kugombana. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)    amesema:

((من لم يدع قول الزور والعمل به والجهل فليس لله حاجة في أن يدع  طعامه وشرابه))البخاري

((Yeyote asiyeacha kusema maneno mabaya? Na vitendo vibaya basi hana haja kuacha chakula chake na maji)) [Al-Bukhaariy]

7-Jitayarishe kuchuma mema mengi

 • Mwezi wa Ramadhaan ni mwezi wa ukarimu, huruma, rahma na mapenzi.
 • Panga kabisa na kuweka kiwango fulani cha kutoa Sadaka na kutoa kwa maskini, anzia kwanza kwa ndugu na jamaa.
 • Kama inakupasa kutoa Zakah, na umependa iwe katika mwezi wa Ramadhaan fanya hima uitimize Fardhi hii pia.
 • Weka ‘azma ya kufuturisha kwa kualika ndugu, jamaa, jirani na marafiki kwani kumfuturisha mtu ni thawabu.

((قال صلى الله عليه وسلم :  من فطر صائماً كان له مثل أجره غير أنه لا ينقص من  أجر الصائم شيء)) أخرجه أحمد والنسائي وصححه الألباني

Amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alahyi wa aalihi wa sallam) ((Atakayemfutarisha aliyefunga, atapata ujira kama ujira wake bila ya kupungua chochote katika ujira wa yule aliyefunga)) [Ahmad, An-Nasaaiy na kasahihisha Imaam Al-Albaaniy]

 • Kama unaye jirani asiye Muislamu, mjulishe kuhusu Ramadhaan, faida na Fadhila zake. Hii ni njia na fursa mojawapo ya kufanya da’awah kwa jirani yako.

8-Hitimisha Qur-aan, Hifadhi na jifunzeTarjama

Jipangie wakati uweze kuhitimisha Qur-aan kwani Ramadhaan ndio mwezi ulioteremshwa Qur-aan na hii ni Sunnah aliyokuwa akifanya Jibriyl (‘alayhis-salaam)  kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)  kusoma naye Qur-aan yote:

عن ابن عباس رضي الله عنهما قال: “كان رسولالله صلى الله عليه وسلم أجود الناس،وكان أجود ما يكونفي رمضان حين يلقاهجبريل، وكان يلقاه في كل ليلة من رمضانفيدارسه القرآن؛ رواه البخاري

Kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (Radhiya-Allaahu ‘anhumaa)  kwamba: Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa alihi wa sallam) alikuwa ni mbora (mwenye matendo mema) wa watu, lakini alikuwa mbora  zaidi katika Ramadhaan kwa sababu Jibriyl alikuwa akimjia kila usiku wa Ramadhaan akimfundisha Qur-aan))  [Al-Bukhaariy]

Hadiyth hii inatufundisha yafuatayo:

 • Kusoma Qur-aan katika Ramadhaan;
 • Kukutana kwa ajili hiyo;
 • Kupima hifdh yako ya Qur-aan kwa kukaa na Mwalimu au mwenye elimu nzuri ya Qur-aan kwa kukusikiliza au kukufundisha;
 • Kuongeza juhudi za kusoma Qur-aan zaidi katika mwezi wa Ramadhaan:

Katika muda wa masaa 24 weka saa moja au mbili khaswa iwe ya Qur-aan kusoma na kujifunza maana ya maneno ya Mola wako uonje ladha ya Qur-aan. AlhamduliLLaahi Alhidaaya imewaandalia ‘Tarjama Ya Qur-aan Tukufu Neno Kwa Neno’, humo faida na thawabu nyingi zitapatikana pindi Muislamu atakapojifunza apate kuelewa maneno ya Mola Wake Mtukufu. Vile vile jitahidi kujiwekea wakati wa kuhifadhi japo sura ndogo ili ukitoka katika Ramadhaan uwe una surah zaidi za kusoma katika Swalah zako.

9-Mdhukuru (Mkumbuke) Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Kila Mara

 

Usiache ulimi wako na moyo wako kuwa mtupu bila ya kumdhukuru Mola Mtukufu kila wakati kila mahali. Huku unafanya kazi zako za jikoni, fanya Adkhaar za Tasbiyh (Subhaana Allaah), Tahliyl (Laa ilaaha illa-Allaah), Tahmiyd (AlhamduliLLaah), Takbiyr (Allaahu Akbar). Kufanya hivi utajichumia thawabu maradufu, kwa kutimiza wajib wako na kuongezea kumdhukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) na juu ya hivyo kuongeza baraka katika kazi zako:

 

10-Darsa

Hudhuria Darsa katika mwezi huu au soma vitabu vya dini, au sikiliza mawaidha.  Jambo hili ni muhimu sana kwani kusikiliza mawaidha ni njia muhimu na bora kabisa katika kuzidisha imani yako.  Kwa hakika unahitaji saa tu kuweza kutimiza jambo hili muhimu kila siku.  Kama huwezi kuhudhuria msikitini, Alhamdulillah, ALHIDAAYA imejaa  mawaidha mengi ya kusikiliza.  Tumia muda wako hata wakati unafanya kazi zako za nyumba na za jikoni huku unasikiliza mawaidha. Kwa hiyo badala ya kutazama televisheni na kusikiliza muziki jambo ambalo ni haramu ni bora utazame na kusikiliza mawaidha ujipatie manufaa, thawabu na kuongeza elimu yako. Kumbuka kwamba kama vile mwili unavyohitajia chakula, hali kadhalika Moyo na Nafsi zinahitaji chakula chake nacho ni kumkumbuka Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) kwa kila aina ya ukumbusho, na mawaidha na darsa za dini ni mojawapo ya chakula kizuri kabisa cha kutakasa Moyo na Nafsi kwa kuzijaza iymaan na mapenzi ya Mola Wako Mtukufu.

Kwa kumalizia, tunasema:

Fungua ‘Swafha‘ (Ukurasa) mpya katika maisha yako

Baada ya kuweza kuyatimiza hayo yote, bila ya shaka hali yako ya iymaan imekuwa bora kabisa na utakuwa umejibadilisha na kuwa mtu tofauti na ulivyo.  Kwa hivyo weka maazimio ya kuendelea hata baada ya Ramadhaan kuwa katika twa’a na ibada, na kuendeleza Qiyaamul-Layl (Swalah za usiku), kusoma Qur-aan japo kidogo KILA SIKU, na iwe umefungua UKURASA MPYA wa maisha yako na kumuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala)  Akuendeleze katika hali hii.

Tunachukua Fursa hii ya kuwaombeeni Ramadhaan yenye baraka na kheri nyingi, tutoke katika mwezi huu tukiwa tumesafishwa madhambi yetu yote, na wenye kubeba thawabu nyingi ziwe nzito katika Miyzaan ya Hasanaat (mizani ya amali njema) Siku ya Qiyaamah.

اللَّهُمَّ تَقَبَّلْ مِنّأ وَ مِنْكُم صَالح الأّعْماَل

Allaahumma Taqabbal Minnaa wa Minkum Swaalih al-A’amaal.  Aamiyn
————————————————————————–

Nini Baada Ya Ramadhaan?

 

Ummu Iyyaad

بسم الله الرحمن الرحيم  الحمد لله رب العالمينوالصلاة و السلام على سيدنا محمد وعلى آله وأصحابه أجمعين وبعد

Tumeshauga mwezi wa Ramadhaan Mtukufu, mwezi wa Baraka na Rahma, tumeziaga siku zake za  mchana tukiwa katika subira ya Swawm, na siku zake za usiku zenye ladha ya ‘Ibaadah.  Tumeuaga mwezi wa Qur-aan, mwezi wa Taqwa, mwezi wa Jihaad, mwezi wa Maghfirah, Mwezi wa Du’aa kutakabaliwa,  na mwezi wa kuepushwa na moto.   Amefaulu aliyetimizia Swawm ilivyopaswa akachuma mema mengi na akajitahidi kufanya ‘Ibaadah zaidi na amekhasirika aliyepuuza Swawm na sheria zake na asichume mengi, na akafanya uvivu asiyejitahidi kufanya ‘Ibaadah zaidi.

Kama Alivyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) katika Aayah zilizotufaridhisha kufunga Ramadhaan kuwa lengo la Swawm ni kuingia katika Taqwaaa.

((يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ كُتِبَ عَلَيْكُمُ الصِّيَامُ كَمَا كُتِبَ عَلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِكُمْ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ))

((Enyi mlioamini! Mmeandikiwa Swawm, kama waliyoandikiwa waliokuwa kabla yenu ili mpate kumcha Mungu)) [Al-Baqarah: 183]

Kwa hiyo kila Muislamu aliyeingia katika mwezi wa Ramadhaan atakuwa ameingia katika madrasa ya Taqwa. Na mtu anapoingia katika madrasa yoyote hutoka humo akiwa amepata shahada yake ya lile somo alilolisoma, na baada ya hapo huitumia ile elimu aliyoisoma aidha kuifanyia kazi au kumsaidia katika kuendesha maisha yake yamuongoze katika uhusiano wa tabia yake pamoja na familia yake, mujtamaa wake na watu wote kwa ujumla.

Na huendelea kuitumia hiyo elimu katika maisha yake yote hadi kufa kwake. Na ni hivyo hivyo ndivyo shahada ya Taqwa inayopatikana katika mwezi huu, elimu yake humuongoza Muislamu katika uhusiano wake pamoja na Mola wake, familia yake na watu wote kwa ujumla. Kwa hiyo inampasa Muislamu aendelee kuitumia elimu hii ya Taqwa hadi atakapoonana na Mola wake kama Alivyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala):

(( وَاعْبُدْ رَبَّكَ حَتَّى يَأْتِيَكَ الْيَقِينُ))

((Na muabudu Mola wako Mlezi mpaka ikufikie Yakini[Maana yake hadi yakufukie mauti])) [Al-Hijr: 99]

Na hii ndio maana ya Istiqaamah (kunyooka au kuendelea kuthibiti) kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala):

((فَاسْتَقِمْ كَمَا أُمِرْتَ وَمَن تَابَ مَعَكَ وَلاَ تَطْغَوْاْ إِنَّهُ بِمَا تَعْمَلُونَ بَصِيرٌ))

((Basi, simama sawa sawa kama ulivyoamrishwa, wewe na wale wanaoelekea kwa Allaah pamoja nawe; wala msikiuke mipaka. Hakika Yeye anayaona yote myatendayo)) [Huud: 112]

((فَاسْتَقِيمُوا إِلَيْهِ وَاسْتَغْفِرُوهُ))

((Basi nyookeni sawa kumwendea Yeye, na mumtake msamaha)) [Fusswilat: 6]

Kunyooka katika ‘Ibaadah vile vile ametufundisha Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika Hadiyth ifuatayo:

عن أبي عَمْرو، وَقِيلَ: أبي عَمْرَةَ، سُفْيَانَ بْنِ عَبْدِ اللهِ الثّقَفيِّ رَضيَ اللهُ عَنْهُ قَال: قُلْتُ: يا رَسُولَ الله، قُلْ لي في الإِسْلاَمِ قَوْلاً، لاَ أَسْأَلُ عَنْهُ أَحَداً غَيْرَكَ. قَال: ((“قُلْ: آمَنْتُ باللهِ ثُمَّ اسْتَقِمْ”)).

Kutoka kwa Abu ‘Amr, vile vile (anajulikana kama) Abu ‘Amra Sufyaan bin Abdillaah (Radhiya Allaahu ‘anhu) ambaye amesema: Nilisema: Ewe Mjumbe wa Mwenyeezi Mungu, niambie kitu kuhusu Uislamu ambacho siwezi kumuuliza mtu yeyote ila wewe.  Akasema (Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): ((Sema; Namuamini Allaah, kisha kuwa mwenye kunyooka. (kwa kuendelea kufanya ibada na kuwa na msimamo madhubuti katika dini)) [Imesimuliwa na Muslim]

Kuthibitika katika  ‘ibaadah ya Ramadhaan au msimu wowote wa ‘ibaadah ni alama ya kukubaliwa vitendo vya ‘ibaadah alivyovifanya Muislamu humo na kupotoka na kuingia katika maasi baada ya kutoka kwenye Taqwa ni alama ya kuviharibu vitendo vyake vyema. Na inampasa Muislamu anapotoka katika mwezi wa Ramadhaan, hali yake ya twa’a na Mola wake iwe bora zaidi kuliko ilivyokuwa kabla. Na kuhakikisha hali hii, jiulize na ujibu maswali haya:

1.       Je, Umekufikia mchana mmoja kama mchana wa Ramadhaan ukiwa katika Swawm?

2.       Je, Umekufikia usiku mmoja kama usiku wa Ramadhaan ukiwa katika Qiyaamul-Layl?

3.       Je, Umeburudika na kusoma Qur-aan kama ulivyoburudika katika Ramadhaan?

4.       Je, Umeuburudisha moyo wako kwa dhikr, istighfaar, du’aa kama ilivyokuwa hali yako katika Ramadhaan?

5.       Je umetokwa na machozi kwa kukumbuka madhambi yako na kumkumbuka Mola Mtukufu na adhabu Zake?

Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anapenda vitendo vya mwanaadamu anavyoviendeleza japokuwa kama ni kidogo vipi, kuliko vitendo vingi kisha asiviendeleze:

قال رسول الله صلى الله عليه وسلم : (( أحب الأعمال إلى الله أدومها وإن قل)) متفق عليه

Amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ((Vitendo Anavyovipenda Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) zaidi (kuliko vyote) ni vile vinavyodumishwa japokuwa ni vidogo)). [Al-Bukhaariy na Muslim]

Kwa hiyo nyooka ewe ndugu Muislamu kwa kujiendeleza kufanya vitendo vyema na ibada katika miezi mingine yote kama ulivyokuwa ukifanya katika mwezi wa Ramadhaan nazo ni:

Swawm:

Funga siku sita za mwezi wa Shawwaal ili ujipatie thawabu za kufunga mwaka mzima kama alivyosema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

((من صام رمضان ثم أتبعه ستاً من شوال كان كصيام الدهر))رواه مسلم و الترمذي وابن ماجه, أبو داود و أحمد

((Yeyote atakayefunga mwezi wa Ramadhaan, kisha akafuatia kwa kufunga siku sita za mwezi wa Shawwaal, basi atapata ujira wa aliyefunga mwaka mzima)). [Imepokewa na Maimaam Muslim, At-Tirmidhy, Ibn Maajah, Abu Dawuud na Ahmad]

Vile vile kuna Swawm za Jumatatu na Alkhamiys, siku tatu katika mwezi, (Ayaamul-Biydh), Swawm ya Arafat, Swawm ya ‘Ashuraa na zote zimetajwa fadhila zake katika mada inayopatikana katika AL HIDAAYA kwenye kiungo hiki kifuatacho:

Swawm Baada Ya Ramadhaan

Qiyaamul-Layl (kisimamo cha kuswali usiku)

Ni Swalah ya Sunnah iliyo bora kabisa baada ya Swalah ya Fardh kama ilivyo katika Hadiyth ifuatayo:

((أفضل الصلاة بعد الفريضة صلاة الليل))رواه مسلم.

((Swalah iliyo bora kabisa baada ya Fardh ni Swalah ya usiku)) [Muslim]

Na fadhila zake zimetajwa nyingi sana, ingia katika vitengo vifuatavyo utambue fadhila zake:

Fadhila Za Qiyaamul-Layl – 1 (Kusimama Kuswali Usiku)

Faida za Qiyaamul-Layl -2 (Kusimama Kuswali Usiku)

Sadaka:

Ikiwa ulikuwa ukitoa sadaqa katika Ramadhaan kwa wingi, basi endelea kutoa sadaka japo kidogo kidogo miezi mingine katika milango mingi ya Jihaad fiy Sabiyli-LLaah (Jihaad katika njia ya Allaah). Sadaka ni kinga kubwa ya kumuepusha Muislamu na maovu mengi, kama uhasidi, huwa ni kinga hata kwa adui zake, na pia ni kumtoharisha mtu moyo wake na kuuweka uwe safi kutokana na maradhi ya moyo kama uhasidi, chuki, ufidhuli n.k.  Na juu ya hivyo humzidisha kheri na baraka nyingi katika mali yake, umri wake, humpa mtu siha nzuri, na ni kumuepusha na moto pia.

Kulisha Masikini:

Ni jambo Analolipenda Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) na Amelisisitiza katika Qur-aan na kuwasifu wenye kulisha maskini na wengineo kwamba ni waja wema na jaza yao ni Pepo:

((إِنَّ الْأَبْرَارَ يَشْرَبُونَ مِن كَأْسٍ كَانَ مِزَاجُهَا كَافُورًا   ((عَيْنًا يَشْرَبُ بِهَا عِبَادُ اللَّهِ يُفَجِّرُونَهَا تَفْجِيرًا ))

(( يُوفُونَ بِالنَّذْرِ وَيَخَافُونَ يَوْمًا كَانَ شَرُّهُ مُسْتَطِيرًا))    ((وَيُطْعِمُونَ الطَّعَامَ عَلَى حُبِّهِ مِسْكِينًا وَيَتِيمًا وَأَسِيرًا))

(( إِنَّمَا نُطْعِمُكُمْ لِوَجْهِ اللَّهِ لَا نُرِيدُ مِنكُمْ جَزَاء وَلَا شُكُورًا ))  (( إِنَّا نَخَافُ مِن رَّبِّنَا يَوْمًا عَبُوسًا قَمْطَرِيرًا ))

(( فَوَقَاهُمُ اللَّهُ شَرَّ ذَلِكَ الْيَوْمِ وَلَقَّاهُمْ نَضْرَةً وَسُرُورًا ))  (( وَجَزَاهُم بِمَا صَبَرُوا جَنَّةً وَحَرِيرًا ))

5. Hakika watu wema watakunywa katika vinywaji vilivyochanganyika na kafuri,

6. Ni chemchem watakaoinywa waja wa Allaah wakiifanya imiminike kwa wingi.

7. Wanatimiza ahadi, na wanaiogopa siku ambayo shari yake inaenea sana,

8. Na huwalisha chakula, juu ya kukipenda kwake, masikini, na yatima, na wafungwa.

9. Hakika sisi tunakulisheni kwa wajihi wa Allaah. Hatutaki kwenu malipo wala shukrani.

10. Hakika sisi tunaiogopa kwa Mola wetu Mlezi hiyo siku yenye shida na taabu.

11. Basi Allaah Atawalinda na shari ya siku hiyo, na atawakutanisha na raha na furaha.

12. Na atawajazi Bustani za Peponi na maguo ya hariri kwa vile walivyosubiri. [Al-Insaan: 5-12]

 

Kutenda Wema Na Ukarimu:

Ikiwa Ramadhaan ilikubadilisha tabia yako ukawa unatenda wema kwa wazazi, ndugu, jamaa, jirani na marafiki, basi kutenda wema huko kuendelee miezi yote mingine.

Na vitendo vingi vyenginevyo inampasa Muislamu aendelee navyo siku zote wakati wote.

Tunatoa Nasiha za dhati kwa ndugu Waislamu waliofunga Ramadhaan ipasavyo, kuendelea kuthibiti katika Taqwa na kumshukuru na kumuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Akusaidie kuwa katika hali hiyo bila ya kurudi nyuma.  Wala usiwe kama yule aliyeshona nguo yake akaipenda sana kisha akaiharibu kwa kuivuta uzi bila ya sababu kama mfano wa mwanamke mmoja aliyekuwa Makkah ambaye alikuwa akifuma uzi na kuufanya madhubuti kisha kila ukiwa madhubuti huufumua, naye Amemtaja Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala):

((وَلاَ تَكُونُواْ كَالَّتِي نَقَضَتْ غَزْلَهَا مِن بَعْدِ قُوَّةٍ أَنكَاثًا))

((Wala msiwe kama mwanamke anayeuzongoa uzi wake baada ya kwisha usokota ukawa mgumu)) [An-Nahl: 92]

Hii ni kama hali ya mwenye kurudia katika maasi baada ya kutoka katika Ramadhaan na akaacha kuwa na twa’a na kufanya mema, akawa badala ya kuitumia neema ya kuwasiliana na Mola wake na kuwa karibu Naye, akarudi katika madhambi. Waovu walioje watu wanaomtambua Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) katika Ramadhaan pekee.

Alipofariki Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), Maswahaba walikuwa katika vilio  na huzuni kubwa za ajabu hadi wengine walipigwa  na bumbuwazi, na ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) alifika hadi kusema “Atakayesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amefariki nitamuua. Walivunjikwa moyo sana hadi hali ikawa sio ya kupendeza, ndipo Abu Bakar (Radhiya Allaahu ‘anhu) akawaambia:

“من كان يعبد محمد فمحمد قد ماتومن كانيعبد الله فان الله باقي حي لا يموت”

“Yeyote aliyekuwa anamuabudu Muhammad, basi Muhammad amefariki na yeyote aliyekuwa anamuabudu Allaah, basi Allaah Anabakia, Yu hai Hafi”

Hali kadhalika tunasema ‘aliyekuwa anaabudu Ramadhaan, basi Ramadhaan inapita na aliyekuwa anamuabudu Allaah, basi Allaah Anabakia, Yu hai Hapiti kuondoka (Hafi)”

Kutokuwa katika istiqaamah baada ya Ramadhaan kunadhihirika kwa njia kama zifuatazo:

Kupuuza Swalah:

Kutokuswali Swalah za Fardhi, au kutokuziswali kwa wakati wake au kutokuziswali kwa kwa utulivu kama ipasavyo.

Kuacha Kuswali Jamaa’h Misikitini:

Swalah ya Jama’ah ni jambo liliosisitizwa sana na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) sio Ramadhaan tu, bali siku zote za kawaida. Lakini utaona misikiti inajaa watu siku za Ramadhaan khaswa katika Swalah ya Tarawiyh ambayo ni Sunnah, wakati Swalah za fardhi ndizo muhimu zaidi. Na fadhila nyingi zimetajwa katika Sunnah anazozipata Muislamu kuswali Jama’ah.

Kuacha Kusoma Qur-aan Na Kujua Maana Yake:

Wengine  huijua Qur-aan katika Ramadhaan tu, ikimalizika Ramadhaan, misahafu inarudishwa katika kabati ijae vumbi hadi Ramadhaan nyingine, wakati Qur-aan ni uongofu kamili wetu, na ina manufaa makubwa sana katika maisha yetu kwa kila upande kwani imekusanya neema zote humo zenye manufaa kwetu kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala):

((يَا أَيُّهَا النَّاسُ قَدْ جَاءتْكُم مَّوْعِظَةٌ مِّن رَّبِّكُمْ وَشِفَاء لِّمَا فِي الصُّدُورِ وَهُدًى وَرَحْمَةٌ لِّلْمُؤْمِنِينَ))

((قُلْ بِفَضْلِ اللّهِ وَبِرَحْمَتِهِ فَبِذَلِكَ فَلْيَفْرَحُواْ هُوَ خَيْرٌ مِّمَّا يَجْمَعُونَ))

((Enyi watu! Yamekujieni mawaidha kutoka kwa Mola wenu Mlezi, na poza kuponyesha yaliyomo vifuani, na uongofu, na Rehma kwa Waumini))

((Sema: Kwa fadhila ya Allaah na Rehma Yake! Basi nawafurahi kwa hayo. Haya ni bora kuliko hayo wanayoyakusanya) [Yuunus: 57-58]

Vile vile ni muhimu sana Muislamu ajue maana ya maneno ya Mola wake ili atambue maamrisho na makatazo yake, sheria zake anazozihitaji katika maisha yake, na vile vile Qur-aan ni kipumbazo cha moyo kwani humo kuna visa vya Mitume na watu wa kale ambavyo vina mafundisho mazito kwetu na masimulizi ya kuburudisha nyoyo.

Kurudia Katika Mambo Ya Upuuzi:

Inampasa Muislamu aendelee kujiepusha na mambo ya upuuzi kama kutazama michezo ya televisheni, kusikiliza nyimbo, kukaa barazani kupiga soga, kusengenya katika simu, kusoma vitabu visivyo vya elimu na haswa elimu ya dini ya Kiislamu na kadhalika, na badala yake anatakiwa ajitahidi autumie wakati wa thamani katika kutafuta elimu ya dini yake tukufu na kuutumia wakati wake wote katika yale yenye kumridhisha Mola wake tu. Kujiepusha na mambo ya upuuzi ni moja wa sababu ya kumrithisisha Muislamu Pepo ya Firdaws kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) katika Aayah ifuatayo:

((وَالَّذِينَ هُمْ عَنِ اللَّغْوِ مُعْرِضُونَ))

((Na ambao hujiepusha na mambo ya upuuzi))  [Al-Muuminuun: 3]

Ndugu Muislamu, endelea kunyooka katika Taqwa siku zote, wakati wote, kwani hujui lini Malaika wa kuchukua roho atakuwa mgeni wako. Jihadhari kukutana naye wakati uko katika maasi na jitayarishe uwe katika wale ambao wanapofikiwa na Malaika wa roho uambiwe:

((يَا أَيَّتُهَا النَّفْسُ الْمُطْمَئِنَّةُ)) ((ارْجِعِي إِلَى رَبِّكِ رَاضِيَةً مَّرْضِيَّةً)) ((فَادْخُلِي فِي عِبَادِي)) ((وَاد ْخُلِي جَنَّتِي))

((Ewe nafsi iliyotua))  ((Rejea kwa Mola wako Mlezi umeridhika, na umemridhisha))  ((Basi ingia miongoni mwa waja wangu))  ((Na ingia katika Pepo yangu)) [Al-Fajr: 27- 30]

Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Atutakabalie amali zetu zote tulizozifanya katika Ramadhaan na Atuhidi kutuendeleza kunyooka katika Taqwa na wenye kuzidisha kufanya vitendo vyema siku zote, wakati wote hadi tutakapokutana Naye Mola wetu Mtukufu tuwe miongoni mwa wale walioamini na Atuingize Peponi kama Alivyotuahidi katika kitabu chake Kitukufu:

((إِنَّ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ أُوْلَئِكَ هُمْ خَيْرُ الْبَرِيَّةِ))

((جَزَاؤُهُمْ عِندَ رَبِّهِمْ جَنَّاتُ عَدْنٍ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا أَبَدًا رَّضِيَ اللَّهُ عَنْهُمْ وَرَضُوا عَنْهُ ذَلِكَ لِمَنْ خَشِيَ رَبَّهُ))

((Hakika walioamini na wakatenda mema, hao ndio bora wa viumbe))

((Malipo yao kwa Mola Wao Mlezi ni Bustani za daima, zipitazo mito kati yake. Wakae humo milele. Allaah Yu radhi nao, na wao waradhi Naye. Hayo ni kwa anaye mwogopa Mola wake Mlezi)) [Al-Bayyinah: 7-8]

Du’aa ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ya kututhibitisha nyoyo zetu katika Dini yetu tukufu.

اَللَّهُمَّ يَا مُقَلِّبَ الْقُلُوبِ ثَبِّتْ قَلْبِي عَلَى دِينِك

Allaahuuma Yaa Muqallibal-Quluub Thabbit Qalbiy ‘Alaa Diynik

(Allaahuumma, Ewe Mgeuza nyoyo, thibitisha  moyo wangu katika Dini Yako(

اّللَّهُمَّ ياَ مُصَرِّفَ الْقُلُوب صَرِّف  قُلُوبَناَ عَلَى طَاعَتِك

Allaahuumma Ya Muswarrifal-quluub Swarrif Quluubana ‘Alaa Twaa’atik

(Allaahumma, Ewe Muelekezaji wa nyoyo, Elekeza nyoyo zetu katika Twa’aa Yako)

Na Allaah Anajua Zaidi
—————————————————————————————-

Nasiha 40 Za Ramadhaan – Zitekeleze Ufaidike na Mwezi Mtukufu

www.alhidaaya.com

1-Anza kwa kuzingatia mwezi huu mtukufu uwe wa kujihesabu, kutenda amali nyingi na kujirekebisha hali yako na uhusiano wako na Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) uwe bora zaidi:

2- Kumbuka kwamba huu mwezi ni mgeni ambaye amekutembelea kisha ataondoka, hivyo mpokee mgeni wako na mkirimu kwa mazuri yote anayostahiki.

3-Tahadhari na kutokufunga bila ya sababu au udhuru wowote, kwani kufanya hivyo, Swawm yako haitolipika hata ukifunga mwaka mzima.

4-Swali kwa wakati wake, usiache Swalah ikakupita. Na jua kuwa ukiwa huswali Ramadhaan huna Swawm kwa mujibu wa fatw za Maulamaa wengi.

5-Soma sana Qur-aan kadiri uwezavyo kwani ni mwezi ulioteremshwa Qur-aan. Kamilisha msahafu mzima japo mara moja, ukishindwa basi hata nusu yake, robo yake.

6-Zidisha ibada za Sunnah, kama Sunnah zilizo Muakkadah (zilizosisitizwa) na zile Ghayri Muakkadah (zisizosisitizwa). Tazama ratiba katika kiungo kifuatacho:

Ratiba Ya Swalah Za Sunnah Zilizosisitizwa Na Zisizosisitizwa

7-Chukua fursa kuomba du’aa sana kila mara nyakati za kukubaliwa du’aa, khaswa ukiwa bado katika Swawm. Tumia wakati wa baina ya adhana na iqaamah kuomba du’aa na haja zako kwani ni wakati wa kukubaliwa du’aa. Vile vile nyakati za thuluthi ya mwisho ya usiku.

8-Iborishe Swalah yako kwa kuiswali ipasavyo na kuzidisha khushuu (unyenyekevu).

9-Usiache kuswali Taarawiyh pamoja na jama‘ah, usiondoke hadi Imaam amalize upate thawabu za Qiyaamul-Layl.

10-Tahadhari na kufanya israaf ya mali, chakula na neema nyinginezo, kwani israaf ni mbaya na itakuondoshea neema ulizojaaliwa.

11- Tumia wakati wako vizuri na zingatia kwamba umri wako unazidi kupunguka.

12-Mwezi huu ni wa ibada na sio kula, kulala na kufanya ya upuuzi.

13-Zoesha ulimi wako uwe umerutubika kwa kumtaja Mola wako, usiwe miongoni mwa wasiomkumbuka Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) ila kidogo tu.

14-Chukua fursa kufanya da‘awah. Amrisha mema na kataza maovu, kwani yule unayemuongoza atakapotekeleza mema, utazibeba nawe thawabu zake pia. Tuma ujumbe wa dini kwa wenzako. Chapisha idadi nyingi ya makala zenye mafunzo ya dini, chapisha du’aa ugawe misikitini, vyuoni, majumbani. Unaweza kupata makala na du’aa mbali mbali katika www.alhidaya.com.  Pia kama una uwezo zaidi rekodi mawaidha yaliyomo ndani ya tovuti na wagawie wenzako upate ujira zaidi. Gawa bure na usiuze, kwani si ya kuuzwa.

15-Fanya kila aina ya wema uwezavyo, patanisha waliokhasimiana, msaidie mwenye haja na muokoe mwenye shida.

16-Wakumbuke wazazi, ndugu, jamaa na marafiki katika du’aa zako kwani kuwaombea wao bila ya wao kujua Malaika hukuombea na wewe vile vile.

17-Wasiliana na ndugu, jamaa kwani ni jambo lililosisitizwa sana na lenye kukuongeza umri, kheri na baraka nyingi. Walio mbali na wewe wasiliana nao kwa simu.

18-Unapohisi njaa, wafikirie masikini wasio na uwezo wa kula, na utambue kuwa uko katika neema ya Mola wako.

19-Muombe msamaha uliyemdhulumu kabla hajalipwa mema yako.

20-Mfuturishe aliyefunga upate thawabu zake juu ya thawabu zako.

21-Omba maghfirah na msamaha kwa Mola wako, kwani tambua kwamba Yeye ni Mwingi wa Msamaha na Mwingi wa Rahma.

22-Ikiwa umetenda maasi kisha Akakusitiri Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala), tambua kuwa hiyo ni onyo utubie na weka azma kutokurudia tena.

23- elimu ya dini yako kwa kujifunza tafsiyr ya Qur-aan, Hadiyth, Fiqhi n.k. upate kuongeza taqwa.

24-Sikiiza mawaidha japo moja kwa siku kwani kusikiliza kunaleta taathira kubwa ya kuongeza Iymaan na Ucha Mungu.

25-Jiepushe na marafiki waovu na vikao vyao na ungamana na marafiki wema na vikao vya kheri.

26-Usipoteze muda wako kutazama televisheni vipindi visivyokupa faida na dini yako, bali tumia wakati wako kwa yatakayokuongezea elimu na ucha Mungu.

27-Usiharibu Swawm yako kwa kunena ya upuuzi, au Ghiybah (kusengenya), au kubishana au kupandisha sauti. Jizuie unapokuwa na hamaki.

28-Fika msikitini mapema zaidi, kwani hivyo ni dalili ya hamu na mapenzi ya ibada na kuwa karibu na Mola wako.

29-Waamrishe na kuwafunza mema ya dini yao walio katika majukumu yako; mke, mume, watoto, ndugu, jamaa n.k. kwani wako karibu yako zaidi na kukutii.

30-Usijaze tumbo sana katika suhuur (daku) kwani itakufanya uwe mvivu na ushindwe kukaa macho nyakati za asubuhi na mchana na ushindwe kufanya ibada vizuri na kusoma sana Qur-aan.

31-Usijaze tumbo sana katika iftwaar (kufuturu) kwani itakushinda kusimama Qiyaamul-Layl au kuzingatia Aayah za Qur-aan zinaposomwa na Imaam.

32-Punguza kwenda madukani/sokoni khaswa kumi la mwisho kwani utakosa kheri na thawabu nyingi zilizomo katika masiku hayo ya thamani kubwa.

33-Tilia hima kubwa kuswali Qiyaamul-Layl kumi la mwisho upate Laylatul-Qadr, usiku ambao ibada yake ni bora kuliko miezi elfu.

34-Jitahidi ufanye I’tikaaf msikitini katika kumi la mwisho japo siku chache, upate fadhila zake na uchume mema mengi pamoja na kupata Laylatul-Qadr.

35-Tambua kwamba siku ya ‘Iyd ni siku ya kumshukuru Mola wako na sio siku ya kutenda yale uliyojizuia ya maovu katika Ramadhaan.

36-Siku ya ‘Iyd , wafanyie wema wazazi, watembelee ndugu, jamaa na marafiki kuboresha uhusiano wako nao.

37-Usiache kutoa Zakatul-Fitwr – wakumbuke maskini, yatima na wanaohitaji na wasaidie na kuwagawia chochote wabakie katika furaha.

38-Tamka Takbiyrah siku ya ‘Iyd kwa sauti unapokwenda msikitini ili kuwakumbusha wengine wanaokwenda au kufuatana nawe ili nawe waweze kupiga Takbiyrah hizo.

39-Weka azma baada ya Ramadhaan kujiendeleza katika hali ya ibada uliyokuwa nayo katika Ramadhaan, ukifanya hivyo itakuwa ni dalili ya kukubaliwa Swawm yako.

40- Funga Sita Shawwaal upate thawabu za Swawm ya mwaka mzima.

———————————————————————————–

Sifa Za Mtu Wa Peponi

 

 

‘Abdun-Naaswir Hikmany

Je, umeamka na Swawm leo?

Je, umehudhuria mazishi leo?

Je, umemlisha masikini leo?

Je, umemtembelea mgonjwa leo?

Tuchukulie kila suala hapo juu lina alama 25 na jumla yake ni 100. Hivyo kama umejibu yote ‘ndio’ basi unazo alama 100 kamili. Na hizo ndio sifa za mtu wa Peponi.

Bila ya shaka wapo wengine watashangaa kwa kuiona pepo ni nyepesi kwa kuyafanya hayo tu. Bal, Laa! Sivyo hivyo. Yatakikana vitendo hivyo kufungamana na kupata radhi za Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala). Vitendo hivyo viwe huru na shirki na riyaa. Vifuatane na kuziweka kifuani nguzo za imani pamoja na kutekeleza nguzo za Uislamu bila ya upungufu wowote.

Matendo hayo manne ni mwenendo uliokuwa umeyapamba maisha ya Sayyidna Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘Anhu). Ambaye hakika alikuwa ni Swahaabah aliyebashiriwa pepo kabla ya kifo chake.

Huyu ndiye Sayyidna Abu Bakr aliyeitwa ‘Mkweli Muaminifu’ hakuacha kusadiki yale yote asemayo Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hata kama yakiwa ni yenye kustaajabisha.

Alikuwa ni Swahiba wake wa mwanzo kuamini Utume wa Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Hakusita alipopatiwa da’awah na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ya kuingia kwenye Uislamu, mara moja alikubali bila ya kudadisi. Huyu ndiye wakala wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwenye shughuli zake nyingi azifanyazo. Abu Bakr alikuwa kifua mbele kuisadikisha ziara ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ya Israa na Mi’iraaj na ndiye aliyehama pamoja na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwenda Madiynah.

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesimulia ya kwamba hayakutani mambo haya manne isipokuwa Muislam huyo atakuwa na sifa ya mtu wa Peponi:

Siku moja Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliuliza:

“Yupi kati yenu asubuhi ya leo amefunga?”

Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘Anhu) akasema: “Mimi”.

Kisha akauliza tena:

“Yupi kati yenu aliyehudhuria mazishi siku ya leo?”

Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘Anhu) akasema: “Mimi.”

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akauliza tena:

“Yupi kati yenu aliyemlisha masikini siku ya leo?”

Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘Anhu) akasema: “Mimi.”

Akauliza tena:

“Yupi katika yenu aliyemtembelea mgonjwa?”

Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘Anhu) akasema: “Mimi.”

Kisha Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema:

“Hayajumuiki yote haya kwa mtu, isipokuwa ataingia Peponi.”

[Imepokewa na Muslim]

Sifa ya mtu kufaulu masomo yake ni kuonekana akiwa na juhudi ya kusoma na bidii ya hali ya juu. Sifa ya kafiri ni kuacha Swalah na kuikana kalimah ya Uislamu. Na kwa hakika sifa za watu wa motoni ni kuwa waovu, makafiri au wanafiki. Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Atuepushe na adhabu Zake. Na hizi sifa nne zilizotajwa kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ndizo sifa za mtu wa Peponi. Nazo ni:

1) Kufunga Swawm

2) Kuhudhuria mazishi

3) Kulisha masikini na

4) Kutembelea mgonjwa

Kama tutazichunguza kwa makini sifa hizo nne tutagundua kwamba ni la mwanzo tu lenye kufungamana na faida ya Muislam mwenyewe binafsi. Yaliyobaki yote ni ya kuitumikia jamii inayotuzunguka, bila ya kujali dini, rangi, umri, jinsia wala kabila.  Hivyo, asilimia 75% ya maisha ya Muislam ni katika kuitumikia jamii inayomzunguka na sio kujifunga kwenye ibada tu peke yake.

Ni kusema kwamba, Muislam anaposhikamana na sifa hizi, basi atakuwa ni mwenye kuisaidia mno jamii yake inayomzunguka. Ni tabia inayojijenga kidogo kidogo kwa uzuri kabisa kujizoesha sifa hizi hadi kujikutia ukimtumikia mgonjwa badala tu ya kumzuru ukaondoka.

Sifa hizi zinatudhihirishia kwamba Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) sio tu Anatoa malipo kwa zile ibada zinazofanywa kumuabudia Yeye tu kama Swalah na Swawmu, lakini pia Anatilia mkazo mno katika kuihudumia jamii. Lakini Waislam hivi leo wanaonekana kuwa ni wageni mno kwenye nyanja ya kuihudumia jamii inayotambulika kana kwamba ni sekta maalum inayohitaji kuhudumiwa na makafiri kutoka Magharibi.

Haya ni mambo ambayo kila Muislam yatakiwa kujipamba nayo iwapo anahitaji kidhati kuwa na sifa za mtu wa Peponi. Wapi utampata masikini au mgonjwa na wapi utahudhuria mazishi hilo ni suala lako kulifanyia uchunguzi kwa kina. Kwani Sayyidna Abu Bakr hakuambiwa ya kwamba kulikuwa na mazishi au mtu yule ni masikini anayehitaji kusaidiwa. Hakuombwa wala kunyenyekewa kutoa msaada wake kwenye masuala haya. Alitoa kwa ridhaa yake bila ya kinyongo na moyo wake ukiwa na lengo moja tu: kupata radhi za Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala).

Sifa hizi zinaturudisha kwenye Hadiyth ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) inayosema:

((Chukua faida ya mambo matano (5) kabla ya matano (5): ujana wako kabla ya uzee wako, afya yako kabla ya maradhi yako, mali yako kabla ya ufukara wako, faragha yako kabla ya wakati utakaoshughulishwa na mambo mbali mbali, na maisha yako kabla ya kifo chako.))[Al-Haakim]

Ukweli unadhihiri kutokana na Hadiyth hiyo hapo juu kwamba, yatakiwa Muislam kujipamba na sifa hizi za mtu wa Peponi kwa kutumia afya yake kutembelea wagonjwa, kutoa mali yake kwa kulisha masikini, kutumia faragha yake kwa kufunga Swawm na kuhudhuria mazishi kabla ya kifo chake.

 

Baada ya kupata utangulizi kwa muhtasari kuhusu sifa hizi. Sasa ni vyema tukaanza kuchambua athari ya sifa moja baada ya nyengine ili Atakapopenda Allaah tushajiike kuyafanyia kazi.

1-Athari Ya Swawm

Swawm sio tu siku za Ramadhaan, bali ni vizuri zaidi Muislam akawa ni mwenye kuwa na Swawm za Sunnah nje ya Ramadhaan pia. Muislam anayeelewa lengo la kuumbwa kwake haachi kuhimizwa mara mbili. Ni yule anayefahamu fadhila za kumtumikia Mola ndio hujihimiza mwenyewe kufunga kwa kutaka radhi za Allaah tu.

Kabla ya yote, tuelewe kwamba lengo la Swawm, iwe ni ya faradhi au Sunnah ni kuwa mcha Mungu. Ni kumukhofu Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) pekee ndio azma inayotakiwa kuwemo ndani ya moyo wa mwenye Swawm.

Hapa ndipo Muislam anapopata kujitakasa mbele ya Muumba wake. Siku yake nzima huitanguliza kwa ajili Yake Yeye Pekee tu. Muislam anapofunga huwa hatamanishwi na lahwa za dunia hii, zilizokuwa mfano wa plastiki linapounguzwa huyeyuka mara moja tu. Plastiki ambalo linageuzwa kila umbo mwanaadamu analohitaji kutengeneza.

Swawm inampatia Muislam mafungamano baina yake na Muumba wake. Hakuna ajuaye ukweli wa Swawm ya Muislam isipokuwa nafsi yake na Muumba wake. Ni wakati huu ambao Muislam huzungumza na Mola wake akiomba radhi Zake na kughufuriwa dhambi zake zote. Halikadhalika, du’aah ya mwenye Swawm ni yenye kupokewa na Allaah.

Swawm humtakasa Muislam kwa kujizuia na maovu makubwa na madogo yake. Kupitia Swawm, huweza kuacha kuzungumza uongo na usengenyaji. Ndio wakati huu ambao huwa karibu na Qur-aan pamoja na kutekeleza amri zitokanazo humo.

Pia, Swawm huweka ulinganifu baina ya masikini na tajiri. Waislam wanapokuwa kwenye Swawm huwa kitu kimoja, kwani huacha kula na kunywa. Hahitaji chakula chake kitamu aliye tajiri na wala sahani iliyo tupu kwa masikini. Hapa ndio tajiri anapata kuwaza na kuwafikiria masikini na ndipo anapojitahidi kutekeleza ile sifa ya nne ya mtu wa Peponi kwa kumlisha masikini.

Swawm inafanana na mtu kukaa njaa siku nzima. Na kama njaa hii itaendelea kwenye mazingira ya dhiki na shida husababisha watu kukosa kula na kutumbukia kwenye janga la maradhi tofauti. Hapa ndipo ugonjwa unaposababishwa, na kuibuka mahitaji ya mgonjwa kuliwazwa na kuangaliwa kwa karibu mno.

Moja miongoni mwa faida kubwa za kiafya za Swawm ni kwamba, Swawm ni njia nzuri ya watu kuacha kula ovyo na kujiepusha na mambo ya upuuzi. Swawm inajulikana kuwa ina athari nzuri kwa baadhi ya maradhi kama saratani na kifafa.

Kuacha matamanio yako ili kwamba yaweze kutimizwa katika wakati unaofuata ni njia muhimu ya kuudhibiti mwili mzima. Inaufanya mwili pamoja na akili kuweza kupanga mambo vizuri kwa siku zinazokuja.

Hivyo, badala ya matendo yetu kutupangia, ni miili yetu inayotupangia. Swawm ipo ndani ya bongo zetu, na ni bongo hizi zinazotufanya kuwa ni binaadamu; wenye kubadilika na kuweza kupata mafanikio kwa kudhibiti mazingira yetu.

Bila ya shaka, maradhi makuu ambayo yanashauriwa kupatiwa matibabu ya Swawm ni kula kupita mpaka. Matatizo ya kula sana yapo zaidi nchi za Magharibi, ambayo yanasababisha maradhi ya moyo, sukari, saratani na mengineyo. Swawm ni njia bora ya kudhibiti maradhi haya, na muhimu zaidi ni njia ya kuzuia hayo maradhi.

2- Athari Ya Kuhudhuria Mazishi

Tumpwekeshe Mwenyezi Mungu Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Pekee na tujihadhari na kusahau mauti. Kusahau kwetu mauti ndio kunapelekea kutenda maovu chungu nzima. Ndipo hata Muislam anapofanana na kafiri kwa kuacha kwake kuswali. Yote hayo yanafanyika kwa sababu ya kujidai kusahau mauti.

Naye Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametuhimiza kujitahidi kukumbuka mauti;

((Zidisheni katika kukumbukamauti)) [Imepokewa na At-Tirmidhy, Ahmad na Ibn Maajah]

Njia iliyo nzuri zaidi ya kukumbuka mauti ni kuhudhuria mazishi. Muislam anapofariki ni vyema kukumbuka mema yake na kumuombea du’aa na kumtakia maghfira katika wakati wa Swalah ya Jeneza. Hivyo ni muhimu kuhudhuria mazishi, kwani kila mmoja wetu atapita njia hii. Na hakuna asiyehitajia du’aah njema kutoka kwa ndugu yake.

Sifa hii ina ugumu wake kuitekeleza kuliko sifa zote tatu. Kwani yahitaji kujitolea na kupania kisawasawa. Yawezekana ukatimiza sifa zote tatu, likabakia hili na kujikutia unalala bila ya kulitekeleza. Usikate tamaa kwani ‘kwenye nia pana njia’. Na Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Atakufunulia njia Atakapopenda.

Labda tutoe kisa cha kweli ambacho kimemkuta kijana Muislam:

Aliamka siku ya mwanzo ya Ramadhaan akiwa na shauku kubwa ya kutekeleza sifa zote hizo nne. Hivyo, alikuwa kwenye sifa moja ambayo ni Swawm. Alihitaji nyengine tatu. Siku ya nyuma yake alipokea maagizo kutoka kwa mzee wake akimtaka kwenda eneo fulani kwa ajili ya kutoa sadaka ya vitabu kwenye Madrasah moja. Wakati akielekea huko nyakati za saa sita mchana alipita eneo la msikiti na kukutia dalili ya mazishi. Hakurudi nyuma aligeuza na kuingia msikitini kuhudhuria mazishi.

Alipotoka mazikoni, alikwenda kutimiza sifa mbili zilizobaki. Ambazo ni kutembelea mgonjwa na kumlisha masikini. Hivyo, aliulaza mgongo wake kwenye kitanda akiwa ametekeleza yote manne ‘Alhamduli Llaah’.

Sio hilo tu. Wapo ndugu wengine ndani ya jamii zetu wanafungua redio kwa ajili ya kusikiliza matangazo ya vifo ili kuisaka sifa hii tu basi. Na anapoikamata haiwachi hadi aitekeleze.

Ni kweli kwamba maeneo ya ughaibuni ni ngumu kulitekeleza hili kwani hakuna matangazo ya vifo na maeneo ni mbali mbali mno. Lakini kama tulivyosema ‘penye nia pana njia’. Insha Allaah, Mwenyeezi Mungu Atakuongoza kama kweli unahitajia sifa hii.

 

Sio vyema kusubiri hadi rafiki au jamaa wako wa karibu afariki ndio uhudhurie mazishi. Kwani kila mmoja wetu atapita kwenye njia hii ya mawt, lililo bora ni kumswalia Muislam mwenzio hata kama humuelewi.

 

Kumswalia maiti kunamfutia maiti madhambi yake na huwenda kwayo ikapatikana nafuu insha Allaah.

 

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Hakuna mtu Muislam aliyekufa, basi wakasimama (wakamswalia) katika jeneza lake watu arobaini, wasiomshirikisha Mwenyezi Mungu na kitu chochote, isipokuwa Atampatia (maiti) msamaha ndani yake” [Imesimuliwa na Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘Anhu) na kupokewa na Muslim]

Pia amesema:

“Mnapomswalia maiti fanyeni wingi wa kumuwombea du’aa” [Imesimuliwa na Abi Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘Anhu) na kupokewa na Abu Daawud]

Malipo hayapo tu katika kumuombea dua’ah maiti, bali pia kwa anayehudhuria mazishi:

“Mwenye kulifuata jeneza la Muislam kwa iymaan na kutaraji thawabu, na akawa nalo (jeneza) hadi akamswalia na kuingizwa ndani ya kaburi, basi hurudi na qiyraatun mbili, kila qiyraatun ni mfano wa mlima Uhud” [Imesimuliwa na Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘Anhu) na kupokewa na Al-Bukhaariy]

3-Athari Ya Kumlisha Masikini

Hapa ndipo panapopatikana ladha ya kuona na kuhisi ile hali ya umasikini kwa ndugu yako. Hali hii yaweza pia kumkumba yeyote miongoni mwa matajiri. Kwani hakuna anayejua mwisho wake mtu.

Kulisha masikini kwa anayetaka Pepo ni muhimu kwa kila Muislamu mwenye uwezo. Dhahiri iliyopo ni kuwa Waislam wengi wasingependa kuona amali zao za khayr ni chache mbele ya Muumba Siku ya Hesabu kwa sababu tu ya kuacha sifa hii ambayo ni sehemu ndogo tu ya mali yao:

{{Wala wasidhani wale ambao wanafanya ubakhili katika Aliyo wapa Mwenyezi Mungu katika fadhila zake kuwa ni kheri yao. Bali hiyo ni shari kwao.}} [Suratul-Imraan: 180]

Kuna bishara njema ya malipo makubwa atayopata Muislamu anayemlisha masikini. Uislamu unatueleza kwamba anayelisha masikini:

§         Atapata malipo makubwa;

§         Atapata khayr;

§         Atakuwa amefanya wema;

§         Atapata ujira;

§         Hatakuwa na hofu;

§         Hatahuzunika;

§         Atakuwa amesafisha mali yake na

§         Kujenga uhusiano mwema na watu wengine.

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amehimiza kuwalisha masikini mpaka kwenye shughuli zetu. Na amekemea mno kwa waliymah kuacha kuwapatia nafasi masikini:

((Chakula kiovu kibaya kabisa ni chakula cha karamu ya harusi ambayo wamealikwa matajiri na kutengwa kando masikini.)) [Muslim na Al-Bayhaqiy]

Bila ya shaka, uwezo wetu wa kupanga kutokana na mafunzo ya Swawm ndio unatuwezesha kuwa ni wingi wa kutoa ndani ya maisha haya kwa lengo la kufanikiwa zaidi maisha ya baadaye ya Qiyaamah. Hivyo, kumlisha masikini kwa ajili ya kupata radhi za Allaah ni funzo bora la kwamba ni ‘amali njema.

Kuna mgongano wa mawazo ndani ya nafsi ya mwanaadamu baina ya kumlisha na kutomlisha masikini. Hivyo, kuweza kuimiliki nafsi yako ni njia muwafaka ya kujiweka huru na utumwa wa nafsi.

4-Athari Ya Kutembelea Mgonjwa

Mwanaadamu ameumbwa na hali mbili kuu; uzima dhidi ya ugonjwa. Ni hali zinazoenda sambamba ndani ya maisha ya mwanaadamu. Hakuna shaka yoyote ya kwamba hakuna kiumbe kilicho kosa sifa ya kuugua.

Anayemukhofu Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) daima huwa anawaza baina ya hali hizi mbili na khofu yake inakuwa kwenye uzima na uhai. Kwani kila neema ni mtihani na utaulizwa kwayo na ni neema hiyo ndio huweza kumpoteza mja katika njia iliyonyooka. Anayemukhofu Muumba huwa daima yuwaza namna alivyo tofauti na ndugu yake mgonjwa; anayetaabika, kuteseka na kudhoofika kutokana na maradhi.

Dhiki ya mgonjwa inatulizwa kwa kiwango kikubwa pale anapotembelewa. Sio tabibu pekee anayeshiriki kumpatia huduma mgonjwa. Na ndio maana yakawekwa masaa maalum ya kutembela wagonjwa. Wakuu wa hospitali wamechunguza na kuelewa umuhimu wa wasio wagonjwa kuwatembelea walio wagonjwa. Na aliye mkuu wa matabibu hawa ni Mtume wetu Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliyeamrisha kutembelewa wagonjwa miaka 1400 iliyopita!

Wangapi wapo vitandani wakiugua miaka nenda miaka rudi? Leo una uzima wako unashindwa kumtembelea hata jirani yako unayefahamu fika ya kwamba anaugua. Kunahitajika kuwepo mahusiano ya karibu baina ya mzima na mgonjwa.

Walipita watu maarufu ambao sasa wamekwishafariki. Hao hawakuwa tu Waislam peke yao, bali hata wasio kuwa Waislam walishikilia kamba barabara ya kufuata mwenendo wa Sayyidna Abu Bakr (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa kutembelea wagonjwa. Hawakwenda kuzuru tu wagonjwa, bali pia kuwahudumia. Hii ni hali inayokuja wenyewe (automatic) wakati wa kumtembelea mgonjwa. Muhali waondoka wenyewe, na unaanza mwenyewe kusukuma kiti cha maringi cha mgonjwa kumpeleka kwenye kitanda chake na mara wachukua kikombe kwa ajili ya kumsuuzia ili apate kunywa uji wake.

Haifai kuiga sifa za wanasiasa ambao wanatembelea maeneo haya ya wagonjwa vipindi vya uchaguzi au wakati wa maafa makubwa makubwa tu. Wanafanya hili ili kupata ridhaa ya macho ya wananchi wao ambao hawatosheki hata wakipatiwa milima ya dhahabu.

Hitimisho

Uislamu wetu ni njia bora ya kupata mafanikio hapa duniani na kesho Qiyaamah. Matendo ya Muislam yahitaji kufanywa kwa ikhlaasw bila ya kumshirikisha Mola Mlezi. Anayepokea amali hizi njema ni Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) na yastahiki tuzitekeleze kwa ajili Yake tu.

Hayo mambo manne ni mepesi kabisa kama Muislam atajihimiza nayo, haswa ndani ya kipindi hichi cha Ramadhaan. Si vyema kuanza kupaka rangi vibaraza visivyo na khayr wakati wagonjwa wapo nyuma ya mgongo wako. Kuna mengi ya kufanya ndugu zangu wa Kiislamu, haya ni manne tu, bado hujasoma Qur-aan, bado hujaswali Sunnah na hata bado hujahudhuria darsa. Huo muda wenzangu munaupata wapi wa kukaa kuangalia TV au kuketi vibarazani kufanya yaliyokatazwa na Uislamu? Tumukhofu Allaah wala tusilinganishe ghadhabu na adhabu Zake dhidi ya mtu yeyote

Advertisements