RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shen ameutaka uongozi wa Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi kuwaangalia kwa karibu wafanyabiashara wanaokausha dagaa katika eneo la Kihinani, ili kuona wanafanya kazi zao katika mazingira bora na salama.
Dk. Shein amesema hayo Ikulu ndogo Kibweni mjini Zanzibar, alipokutana na uongozi wa Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi, ilipowasilisha taarifa ya Utekelezaji wa Mpango kazi wa Wizara hiyo kwa kipindi cha Julai 2018 hadi mwezi Machi, 2019.
Alisema wafanyabiishara hao waliojikusanya na kujiajiri wamekuwa wakifanya kazi kubwa ya uzalishaji wa dagaa na kuuuza hadi nchi za nje, hivyo kuna kila sababu ya kuwaunga mkono, kuwatia moyo na kuwasaidia ili kuhakikisha wanafanyakazi katika mazingira bora na kuondokana na hatari ya kukumbwa na maradhi ya mripuko, ikiwemo kipindupindu.
Aidha, aliutaka uongozi huo kujenga mashirikiano ya karibu na Kampuni ya Uvuvi Zanzibar (ZAFICO) kwa kuzingatia kuwa Shirika hilo ni mali ya serikali.
Alisema Shirika hilo lililoundwa kutokana an mtaji wa mashirika makuu matano ya serikali ni muhimu katika maendeleo ya Taifa na ustawi wa wananchi, hivyo kuna wajibu wa kulilea, sambamba na kufanikisha dhana ya Uchumi wa Bahari.
Dk. Shein aliukumbusha uongozi wa Wizara hiyo umuhimu wa kusimamia maazimio yaliofikiwa katika semina maalum kuhusiana na rasilimali ya mchanga iliyofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakil, akibainisha umuhimu wake katika uhifadhi wa rasilimali za Taifa.
Aliitaka Idara inayohusika na rasilimali ya mchanga kusimamia vyema pamoja na kuhakikisha taratibu zote za upatikanaji wa rasilimali hiyo zinafuatwa.
Aliutaka uongzi huo kukijengea mazingira mazuri Chuo cha Kilimo Kizimbani ili kukiweka katika nafasi nzuri kuelekea mpango wa Serikali wa kukiunganisha na Chuo Kikuu cha Taifa (SUZA).
Aidha, Dk. Shein aliupongeza uongozi na watendaji wa Wizara hiyo na ile ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji kwa kazi nzuri iliofanywa kufanikisha utekelezaji wa majukumu yao katika kipindi cha miezi tisa iliyopita.
Nae, Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi Mmanga Mjengo Mjawiri alisema katika kipindi hicho Wizara imepata mafanikio makubwa katika udhibiti wa matumizi ya mchanga kupitia Kamati ya Baraza la Mapinduzi.
Alisema utaratibu madhubuti uliowekwa umepelekea kuwepo matumizi sahihi ya mchanga kwa mujibu wa mahitaji, hivyo kuwa suluhisho la tatizo la kurundikana kwa mchanga.
Aidha, alisema Wizara hiyo ilishirikiana na Wizara ya Ardhi kuyatambuwa, kuyapima na kuyapatia Hati miliki maeneo ya kilimo ikiwa ni hatua ya kukabiliana na uvamizi wa maeneo ya misitu na kilimo kwa shughuli za makaazi ya watu na miradi mingine ya maendeleo.
Alisema Serikali kupitia Wizara hiyo ilitowa ruhusa ya kugawa mashamba ekari 732 yaliopo kisiwani Pemba ili yaendelezwe kupitia shughuli za kilimo na mifugo.
Vile vile, alise Wizara hiyo iliimarisha udhibiti wa matumizi ya raasilimali zisizorejesheka kwa kuandaa utaratibu maalum wa upatikanaji wa rasilimali hizo pamoja na kufanya doria shirikishi kwa kushirikiana na Vikosi vya SMZ .
Alisema katika kipindi hicho Serikali ilifanya kongamano la Sheria za Ardhi na hali halisi ya misitu na maliasili zisizorejesheka kwa lengo la kutoa elimu na kuihamasisha jamii juu ya umuhimu wa uhifadhi na matumizi endelevu ya rasilimali za Taifa.
Mjawiri alisema katika utekelezaji wa malengo yaliowekwa, pia Wizara hiyo ilikabiliana na changamoto za kuongezeka kwa bei ya pembejeo, matumizi mabaya ya misumeno, kuwepo kwa nzi wa matunda pamoja na kuwepo kwa mahitaji ya matumizi ya mchanga, huku maeneo ya uchimbaji yakipungua.
Alieleza azma ya kuziendeleza sekta zinazounda Wizara hiyo, kwa kuendeleza ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji maji, uchimbaji visima na mabwawa pamoja na mitaro ya Umwagiliaji maji kupitia mradi wa EXIM Bank wa Korea, utakaotumia hekta 500, sambamba na hekta 65 kupitia mradi wa ERPP
Aidha, alisema Wizara inalenga kuongeza uzalishaji wa zao la mpunga pamoja na kushajiisha matumizi ya pembejeo kwa kununua na kusambaza mbolea, dawa ya kuuliya magugu pamoja na mbegu ya mpunga.
Wakati huo huo, akiwasilisha taarifa ya mpango kazi kwa kipindi hicho, Waziri wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Sira Ubwa Mamboya, alisema Wizara hiyo imefanikiwa kukamilisha ujenzi wa kilomita 28 za barabara mbali mbali Unguja na Pemba kwa kiwango cha Lami, ikiwemo Bara ya Ole – Kengeja yenye urefu wa kilomita 14.
Aidha, alisema Wizara hiyo imefanikiwa kuendeleza ujenzi wa jengo jiipya la abiria katika Uwanja wa Ndege (terminal 111), kuendelea na ujenzi wa maegesho pamoja na msingi wa kupitisha maji katika eneo hilo.
Vile vile, alisema Wizara imekamilisha kazi ya upembuzi yakinifu kwa ajili ya uwanja wa ndege kisiwani Pemba.
Abdi Shamna, Ikulu Zanzibar