RAIS MAGUFULI AWATAKA WAKIMBIZI KUTOKA BURUNDI WAJIANDAE KUREJEA KWAO


Rais John Magufuli amewataka wanachi wenye asili ya urundi waliopo nchini Tanzania wafanye wawezavyo kwa hiari yao warudi kwao wakaijenge nchi wasisingizie kuna vita kwa kuwa Rais wao Pierre Nkurunziza ameshawahakikishia kuwa kuna amani ya kutosha.

Rais Magufuli ametoa kauli hiyo wakati akihutubia wakazi wa wilaya ya Ngara mkoani Kagera katika mkutano wa hadhara uliyofanyika katika viwanja vya Posta baada ya kupokea ugeni kutoka nchini Burundi wa rais huyo pamoja na baraza lake la mawaziri mchana wa leo uliyokuja kwa mazungumzo ya kiuchumi.

“Ndugu zangu warundi mmesikia taarifa iliyotolewa na Rais Nkurunziza anawaomba mrudi kwenye nchi yenu, mkajenge nchi yenu, mkajitafutie maisha. Ni kama wanaotoka Afrika kwenda Itali lakini kuna wakimbizi wamezoea kukimbia tu, sasa kwa sababu Rais ameshawaambia murudi nyumbani sasa mchukue hatua za kurudi nyumbani kwa hiyari wala sisi hatuwafukuzi. 

“Ninafahamu wapo baadhi ya watu ambao hufanya biashara na wakimbizi kwa sababu ndipo wanaotoa vyakula, wanaomba misaada kule nje ya kusema kuna wakimbizi sana na saa zingine wanaelezea hali ambayo haipo”, amesema Rais Magufuli.

Pamoja na hayo Rais Magufuli ameendelea kwa kusema “Nimesikia wakimbizi wengine wameahidiwa kwamba mtakuwa mnapewa  elfu kumi kumi wabaki sasa nasema wakawapeni hizo hela mkiwa Burundi.

“Nataka tuelezane ukweli kwasababu tunawajibu wa kulinda amani katika nchi zetu na Mhe. Rais ameshazungumza hapa lakini nchini Tanzania tumekuwa na uzalendo mzuri kwamba wakimbizi wanapokuja muda mwingine tunawapa uraia. Sasa kama wapo watu wanakimbia kule kwa sababu waje tuwape uraia waziri wa mambo ya ndani simamisha zoezi la kuwapa uraia wanaokuja huko”.

Aidha, Rais Magufuli ameunga mkono ombi la Rais wa Burundi aliyowataka wananchi wake warundi kwao wakaijege kwa pamoja nchi hiyo kwa kuwa hakuna shida ya aina yoyote katika kipindi hiki.

“Na mimi niwaombe nitoe wito kwa ndugu zangu wa Burundi kwa hiyari yao mimi siwafukuzi ila kwa hiari yao warudi nyumbani na niwapongeze wale laki moja na hamsini elfu waliorudi kwa hiari yao pia niyaombe Mashirika yanayoshughulikia wakimbizi waache kuwahubiri wakimbizi kwamba Burundi kuna matatizo, waanze kuhubiri amani ya kweli kwamba wanao uwezo hawa wakimbizi kwenda Burundi”, amesisitiza Rais Magufuli.

Kwa upande mwingine, Rais Magufuli amemthibitishia Rais Nkurunziza kuwa Tanzania itaendelea kutoa ushirikiano mkubwa kwa majirani zake wote waliopo ndani ya Afrika Mashariki ndani ya SADC pamoja na nchi ya Burundi.

ZSSF KUTOA MIKOPO YA KIJIENDELEZA KIELIMU KWA WANACHAMA WAKE

 

Exif_JPEG_420

Mkurugenzi mtendaji Benki ya Posta Tanzania TPB Sabasaba Mushingi (kushoto) akibadilishana hati za makabidhiano ya mikopo na Kaim Mkurugenzi Mtendaji wa ZSSF Makame Mwalimu Silima kwenye ofisi za ZSSF mjini Zanzibar_JPEG_420

Mfuko wa hifadhi ya jamii Zanzibar ZSSF kwa kushirikiana na Benki ya Posta TanzaniaTPB zinatarajia kutoa mikopo ya kujiendeleza kielimu na kuanzia maisha kwa wanachama wa mfuko huo.

Akizungumza katika utiaji saini hati ya makabidhiano ya mikopo hiyo Mkurugenzi mtendaji Benki ya Posta Tanzania TPB Sabasaba Mushingi amesema hatua hiyo imefikiwa baada ya kuona wafanyakazi wanakosa fursa za kujiendeleza kielimu kutokana na kushindwa kumudu gharama masomo

Nae Kaimu Mkurugenzi wa ZSSF Makame Mwalimu Silima amesema mikopo yenye masharti nafuu ni miongoni mwa malengo ya mfuko huo kutaka kuwaendeleza wanachama wake kiuchumi

Mfuko wa ZSSF kwa kushirikiana na Benki ya Posta Tanzania TPB umeshatoa mkopo kwa wastaafu na wanachama wa mfuko huo kiasi ya shilingi bilioni 5 kuanzia mwaka 2014.

 

SMZ YALITAKA JESHI LA POLISI KUCHUNGUZA VIFO VYA WATOTO WANNE

 

 

 

ISLAM-WATOTO

Watoto hao ndio waliofariki dunia ndani ya gar

akamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amezitaka Familia za Watoto Wanne waliofariki Dunia baada ya kukutwa kwenye Gari mapema wiki hii katika Mtaa wa Kidongo Chekundu Mjini Zanzibar kuendelea kuwa na moyo wa subra katika kipindi hichi kigumu cha msiba.

Alisema Jamii kupotelewa na watoto Wanne ni jambo zito linalotia huzuni lakini jamii hiyo hiyo inalazimika kuelewa kwamba Allah amewapenda zaidi Watoto hao Malaika za Mungu.

Balozi Seif Ali Iddi alitoa nasaha hizo wakati alipofanya ziara fupi ya kutoa mkono wa pole pamoja na kuzipa faraja familia za Watoto hao hapo katika Mtaa wa Kidongo chekundu Mkoa Mjini Magharibi.

Alisema tukio hilo la kusikitisha lililopokelewa kwa huzuni ya Serikali Kuu litaendelea kubakia Historia ndani ya nyoyo za Wananchi walio wengi katika Maeneo mbali mbali Nchini.

Kufuatia tukio hilo la maafa, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameliagiza Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi wa kina wa tukio hilo ili Serikali ipate kujiridhisha  baada ya kupokea taarifa zenye mchanganyiko wa maelezo kutokana na mazingira ya vifo vya Watoto hao.

Balozi Seif ameendelea kuwasisitiza Wananchi na Wazazi  wote Nchini kuwafuatilia Watoto wao katika mazingira yao ya kila siku ili kuwaepusha watoto kukumbwa na vitendo viovu pamoja na majanga yanayoweza kuepukika.

Mapema Sheha wa Shehia ya Jang’ombe Bwana Khamis Ahmada alisema Wazazi na Wananchi wa Mtaa huo walikusanyika pamoja baada ya kubaini utoekaji wa Watoto hao mapema asubuhi.

Sheha Ahmada alimueleza Balozi Seif kwamba Timu hiyo ilianza harakati za kuwatafuta Watoto hao kuanzia majira ya saa Tano za Asubuhi na hatimae kufanikiwa kuwagundua ndani ya gari wakiwa tayari wameshafariki Dunia.

Bwana Khamis Ahmada kwa niaba ya Wananchi wa Shehia hiyo na Vitongoji vyake ameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa imani ya Viongozi wake wa ngazi mbali mbali kujitokeza kwa wingi katika kutoa faraja na mkono wa pole kwa familia ya Watoto hao.

Bwana Ahmada alisema kitendo hicho cha kiutu na cha kiungwana kwa kiasi kikubwa kimeleta faraja, upendo pamoja na kupunguza machungu kwa wananchi waliopatwa na mtihani huo.

 

 

Othman  Khamis Ame

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

Rais Pierre Nkurunziza afanya ziara nje ya nchi kwa mara ya kwanza tangu 2015

mediaRais wa Burundi Piere Nkurunziza alivyokaribishwa na rais wa Tanzania John Magufuli Julai 20 2017 wilayani NgaraIkiriho

Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza ameondoka nchini mwake kwa mara ya kwanza kwa kipindi cha miaka miwili, tangu kutofanikiwa katika  jaribio la kumwondoa madarakani mwaka 2015.

Nkurunziza amezuru nchini Tanzania katika Wilaya ya Ngara, kukutana na mwenyeji wake rais John Magufuli.

Ziara hii imekuja wakati huu Tanzania ikiendelea kutoa hifadhi kwa zaidi ya wakimbizi 200,000 waliokimbia nchi yao kwa sababu za kiusalama.

Rais Nkurunziza ameandamana na idadi kubwa ya Mawaziri wake katika ziara hiyo ya kwanza ambayo ilitangazwa katika dakika za lala salama.

Jaribio la kumpindua Nkurunziza lilifanyika wakati akihudhuria mkutano wa wakuu wa nchi kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Akiwahotubia wananchi, rais Nkurunziza amewaambia wakimbizi wanaoishi nchini Tanzania kurejea nyumbani ili kuijenga nchi yao.

“Tunawaomba raia wa Burundi wanaoishi hapa nchini Tanzania, kurudi nyumbani ili tuijenge nchi yetu,” alisema.

Aidha, ameishukuru Tanzania kwa kuwa jirani mwema na kuwapa hifadhi raia wa Burundi waliokimbia nchi yao.

Rais Magufuli amesisitiza ujumbe wa rais Nkurunziza na kuwataka wakimbizi hao kuchukua hatua za kurudi nyumbani kwa hiari.

“Rudini nyumbani kwa hiari, sisi hatutawafukuza,” alisema rais Magufuli.

Mamia ya watu wamepoteza maisha na wengine kutoweka kwa mujibu wa Mashirika ya Kimataifa ya kutetea haki za Binadamu kama Human Rights Watch.

Rais wa zamani wa Tanzania Benjamin Mkapa ni mratibu wa mazugumzo ya kisiasa nchini humo, ambaye ameendelea kujaribu kuwaleta wapinzani wa kisiasa nchini humo kujaribu kuleta mwafaka wa kisiasa nchini humo.

Hata hivyo, kumekuwa na changamoto ya kuwakutanisha wanasiasa wa upinzani na viongozi wa serikali.

Rais Kabila wa DRC na familia yake wana utajiri wa mamilioni ya dola

Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na familia yake wanamiliki hisa katika mashirika 80 nchini humo na maeneo mengine ya dunia na utajiri wake unakadiriwa kuwa makumi ya mamilioni ya dola.

Ripoti iliyotolelwa Alhamisi na Kituo cha Utafiti wa Kongo katika Chuo Kikuu cha New York, Marekani imesema uchunguzi wake kuhusu utajiri wa Kabila umetegemea tu taarifa zilizo wazi kwa umma kama vile hati miliki za ardhi na nyaraka za uanzishaji mashirika. Hadi sasa  ripoti hiyo ndio kamilifu zaidi kuhusu utajiri wa Kabila na familia yake baada ya miongo miwili ya kuwa rais wa nchi hiyo tajiri kwa madini.

Msemaji wa serikali ya Kongo Kinshasa Lambert Membe amesema, kwa mujibu wa katiba ya nchi hiyo rais hakatazwi kuwa na hisa au kuwekeza katika mashirika mbali mbali.

Kabla ya baba yake Kabila, Laure-Desire, kuingia madakrani mwaka 1997, alikuwa akiishi na familia yake uhamishoni Tanzani ambako taarifa zinasema hali yao ya kifedha haikuwa nzuri. Lakini hivi sasa familia ya Kabila ina karibu hekari 70,000 za mashamba ya kilimo, idadi kubwa ya hisa katika shirika kubwa zaidi la simu za mkononi DRC pamoja na leseni zaidi ya 100 za kuchimba dhaharbu na almasi.

Wakimbizi wa ndani ya nchi DRC

Uchunguzi unaonyesha kuwa mashirika hayo yamekuwa na mapatano ya mamilioni ya dola tokea mwaka 2003 huku mali za Kabila na familia yake zikiwa na thamani ya makumi ya mamilioni ya dola. Ripoti hiyo haijaashiria akaunti za Kabila na familia yake katika benki mbali mbali nchini humo na maeneo mengine duniani.

SOURCE- RADIO IRAN IDHAA YA KISWAHILI

Polepole: Lowassa Sio Tishio kwa CCM……Amechuja na Akigombea Tena 2020 Tutamshinda

Siku moja baada ya mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Edward Lowassa kusema atagombea tena urais katika uchaguzi ujao, CCM imesema inamsubiri na ina uhakika itamshinda tena kwa kuwa tayari ameshachuja na wala sio tishio.

Lowassa aliweka rekodi ya kuwa mgombea wa upinzani aliyepata kura nyingi baada ya kugombea kwa tiketi ya Chadema na kuungwa mkono na vyama vingine vitatu vya upinzani katika Uchaguzi Mkuu uliopita.
Alipata kura milioni 6.07, takriban mara tatu ya kura ambazo wapinzani wamekuwa wakipata katika chaguzinne za awali. Mshindi alikuwa John Magufuli wa CCM aliyepata kura milioni 8.8.
Waziri huyo mkuu wa zamani ametangaza nia ya kusimama tena kugombea urais wakati alipofanya mahojiano na waandishi wa Nation Media Group jijini Nairobi, Kenya ambako alikwenda kuhudhuria mazishi ya aliyekuwa waziri wa mambo ya ndani, lakini CCM imesema asitarajie ushindi.
Alipoulizwa kuhusu tamko la Lowassa, katibu wa itikadi na uenezi wa CCM, Humphrey Polepole alisema mbunge huyo wa zamani wa Monduli si tishio na hayuko katika fikra za chama hicho.
“Katika orodha ya vitu muhimu, Lowassa hatumfikirii kabisa na si tishio hata kidogo,” alisema Polepole ambaye katika uchaguzi uliopita aliapa kuzunguka nchi nzima kumpinga Lowassa.
Polepole alisema kwa sasa chama hicho kimejikita kutekeleza Ilani yake inayotokana na ahadi za wananchi, kama kushughulikia changamoto za uadilifu kwa viongozi ndani ya CCM na Serikali.
“Tunatimiza wajibu wetu vizuri tuliotumwa na Watanzania na kazi inaonekana. Nje ya hapo tunasubiri Watanzania watupatie haki yetu katika uchaguzi ujao, na tumeshajipangia kupata ushindi wa zaidi ya asilimia 70, kwa hiyo hatumfikirii kabisa,” alisema Polepole.
Hata hivyo, jina la Lowassa limekuwa gumzo katika vikao vya chama hicho tawala na alisababisha wajumbe watatu wa Kamati Kuu ya CCM kuchukuliwa hatua, wenyeviti wanne wa mikoa kuvuliwa uongozi na uanachama na wengine kadhaa kuadhibiwa kwa njia tofauti.
Hiyo ilitokana na baadhi kuendelea kumuunga mkono baada ya kujivua uanachama wa CCM na kujiunga upinzani, akiwa Waziri Mkuu wa kwanza kufanya hivyo tangu siasa za ushindani zirejeshwe mwaka 1992.
SOURCE: MPEKUZI

Polisi Akatwa Mkono Katika Ugomvi wa Kugombea Mwanamke

Jeshi la Polisi katika Mkoa wa Kipolisi wa Tarime-Rorya, linawashikilia watu wawili wakazi wa Mtaa wa Nkende mjini Tarime wakidaiwa kumkata mkono Mkaguzi wa Polisi wa Kituo cha Ngamba Tana-River cha nchini Kenya, James Mnuve (50), wakati wakimgombania mwanamke.

Kamanda wa Polisi Tarime Rorya, SACP Henry Mwaibambe, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo la kukatwa mkono Mkaguzi huyo wa Polisi wa nchini Kenya.

Mwaibambe alidai kuwa tukio hilo lilitokea Julai 13 mchana katika mtaa wa Nkende mjini Tarime ambapo vijana hao walitenda kosa hilo.

Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Michael Omahe, anayedaiwa kumtorosha mwanamke huyo, Anne Njeri, kutoka Kenya na kumleta Tanzania kisha kuishi naye kinyumba huku akisaidiana na rafiki yake, Daniel Onchiri.
“Mwanamke huyo (Njeri) anadaiwa alikuwa na uhusiano wa kimapenzi pia na askari James Mnuve na walikuwa wakiishi huko Tana River nchini Kenya, baada ya kuondoka, Julai 13 mchana askari huyo alimfuatilia kutoka Kenya hadi Mtaa wa Nkende, Tarime alipokuwa anaishi na kijana aliyemtorosha (Michael Omahe),” alisema Kamanda.
Akaongeza, “Alipofika Mtaa wa Nkende alimkuta Michael, pamoja na rafiki yake huyo wakiwa na mwanamke huyo na hapo ndipo ugomvi ulipoanza kwani askari James alitaka kuondoka na mwanamke huyo na zikazuka vurugu kubwa na kusababisha Mnuve kukatwa kwa kutumia panga.”
Aidha Kamanada huyo alisema kuwa, “Jeshi la Polisi tulifika kwenye eneo la tukio mapema na kuweza kuwakamata watuhumiwa wote watatu; Marandi, Ochiri na mwanamke huyo na kisha tukawahoji kabla ya kuwafikisha mahakamani huku majeruhi akiwa amepelekwa katika Hospitali ya Wilaya ya Tarime kwa matibabu.” 
Majeruhi James anadai kuwa yeye ni Inspekta wa Polisi wa Kituo cha Ngamba Tana River nchini Kenya na mwanamke huyo, Njeri Wanjoi, ni mke wake.