Archive for March, 2011

MAALIM SEIF AREJEA NCHINI

Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar, Malim Seif Shariff Hamad anatarajiwa kurejea nchini Ijumaa ijayo akitokea nchini India alikokuwa akipatiwa matibabu baada ya kufanyiwa upasuwaji wa goti.

Malim Seif kabla ya kufanyiwa upasuwaji huo alitokea nchi za Uholanzi, Umoja wa Falme za kiarabu na Oman kwa ziara ya kiserikali.

Kwa mujibu wa habari iliyotolewa na idara ya habari ya maelezo Zanzibar, mara baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Zanzibar malim Seif atafanya mazungumzo na wanandishi wa habari kuelezea mafanikio ya ziara hiyo.

WASANII 13 WAFARIKI DUNIA KATIKA AJALI YA GARI MOROGORO YAUWA

Basi dogo lilibeba wasanii na kupata ajali

Wasanii 13 wa kundi la taarab la Five Star Modern Taarab wamefariki dunia katika  ajali ya gari Mikumi mkoani Morogoro usiku wa kuamkia leo.

Kwa mujibu wa mkuu wa kikosi cha usalama barabarani mkoani Morogoro Ibrahim Mwamakula amewataja marehemu hao kuwa pamoja na Issa Kijoti, Nasoro Madenge, Mapande, Fembe Juma, Omary Hashim, Tizo , Omari Tall, Ngeleza Hasan, Hamisa Omari, Maimuna, Haji Msaniwa na mcheza show wa kundi la Kitu Tigo Ilala.

Ajali hiyo mbaya iliyohusisha gari tatu, ambapo waliokufa wote ni kutoka kwenye basi dogo la wasanii wa kikundi cha Five Stars na kusababisha majeruhu tisa kulazwa katika Hospitali ya Mkoa wa
Morogoro.

Majeruhi hao ni pamoja na Mwanahawaa Ally( 55) kutoka Kundi la East African Melody, Susana Benedict (32), Zena Mohamed
(27), Samira Rajab (22)na Mwanahawa Hamisi (36).

Kwa mujibu wa Kamanda huyo wa Kikosi cha Usalama Barabarani aliwataja wasanii wengine waliolazwa katika Hospitali hiyo ni pamoja na Ally Juma (25), Rajabu Kondo ( 25), Issa Hamis , Shaaban Hamis (41) na Msafiri Musa (22).

WANDISHI WA HABARI WACHARUKIA MDAHALO WA KATIBA MPYA

Wandishi wa habari Zanzibar wamesema midahalo inayoendelea ya kutoa maoni juu ya katiba mpya ya jamhuri ya muungano Tanzania haitaleta matunda mazuri kutokana na wananchi kutoifahamu katiba ya sasa

Wakizungumza katika warasha ya siku moja juu ya upatikani wa elimu ya uraia vijijini huko hoteli ya Zanzibar Ocean View wamesema wananchi wengi wanaochangia midahalo hiyo hawana upeo wa kutosha juu ya katiba inayoendelea kutumika.

Hivyo wamesema kuna uwezekano wa michango wanayotolewa katika midahalo hiyo isiguse vipengele vya msingi vinayohitajika kufanyiwa marekebisho ili kuleta maslahi kwa pende zote mbili za muungano.

Wandishi hao wameshauri kutolewa kwa kopi za katiba ya sasa ili wananchi wangalie mapungufu yaliomo na hatimae kutoa mapendekezo yao

Hata hivyo baadhi ya wandishi wengine wamepinga  madai hayo

Warsha hiyo ya siku moja iliyowashirikisha wandishi wa habari wa vyombo vya radio na Televisheni za serikali na watu binafsi imeandaliwa na Tume ya utangazaji Zanzibar na kufadhiliwa na shirika la umoja wa mataifa UNDP.

KERO ZA MUUNGANO ZITATULIWE KABLA YA KUANDIKWA KATIBA MPYA-MASHEIKH

Jumuiya za dini ya kiislamu nchini zimetaka kutatuliwa kero za muungano wakati huu wazanzibari wakitoa maoni yao juu kuandikwa kwa katiba mpya ya jamhuri ya muungano katika midaho inayoendelea.

Wakizungumza katika mdahalo wa kujadili katiba mpya huko Michenzani mjini hapa wawakilishi wa taasisi hizo wamesema hatu  hiyo  ni  muhimu  katia  kufikia mustakbali  wa  katiba mpya.

Hata hivyo taasisi hizo zimesema zinaunga mkono mawazo ya kuandaliwa katiba mpya na kushirikishwa wazanzibari kutoa maoni  yao  kwa uwazi  juu ya mabadiliko ya katiba hiyo.

Sheikh Farid Hadi amewaomba waumini wa kislamu kuacha tofauti zao na kuwa kitu kimoja katika kutoa maoni yao yanayozingatia maslahi ya dini ya kislamu.

 

TASISI ZINAZOPATA MISAADA KUTOKA LIBYA ZITAUMIA

Mufti Issa Shaaban bin Simba

Taasisi za dini ya Kislamu nchini Tanzania zinazopata msaada kutoka Libya zinaweza kuathirika kutokana na mashambulizi ya anga yanayofanywa na majeshi ya nchi za magharibi nchini humo.

Akizungumza na BBC sheikh mkuu wa Tanzania Issa Shaaban Simba amesema taasisi nyingi za dini ya kislamu duniani zinaweza kuathirika kutokana na nchi ya Libya kutoa misaada mingi kwa taasisi hizo.

Hivyo ameyaomba mataifa hayo kutafuta njia nyingine kama vile kumuwekea vikwazo kiongozi huyo badala ya kuishambuilia kijeshi nchi yake.

Nae waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa Benerd Membe amesema suala hilo linashughulikiwa kupitia umoja wa Afrika AU.

10 WANAOSADIKIWA MAJAMBAZI WAKAMATWA NUNGWI

Eneo la bandari ya Nungwi

Watu kumi wanashikiliwa na jeshi la polisi katika mkoa wa Kaskazini Unguja kwa tuhuma za kuiba katika hoteli moja ya kitalii.

Kaimu kamanda wa polisi mkoani humo Henry Mwaibambe amesema tukio hilo limetokea majira ya saa 8 usiku wa kuamkia leo wakati watu hao walivamia hoteli ya My Blue ilioko Nungwi.

Amesema watuhumiwa mmoja wao alivaa sare ya jeshi la polisi aliwaamuru walinzi wa kimasai katika hoteli hiyo wakusanyike kwa kuwakagua.

Wakati walipokusanyika mtuhumiwa huyo alitoa panga na kumtaka mguu wa kulia mlinzi mmoja ambapo walipiga kelele za kuomba msaada.

Watuhumiwa hao walikamatwa wakiwa kwenye gari yenya usajili Z 490 AV Super Custome wakati wakijaribu kutoroka baada kutofanikiwa kuiba kwenye hoteli hiyo.

Kaimu kamanda huyo amewataja watuhumiwa hao ni Khamis Msoma Masanja miaka 31 mkaazi wa Welezo, Khamis Kombo Juma miaka 34 mkaazi wa Tomondo, Jeremiah Joseph Maico miaka 31 mkaazi wa Dodoma.

Wengine ni Msafiri Ali Mengi miaka 25 mkaazi wa Jang’ombe skuli, Hendry Hendry Yussuf miaka 24 mkaazi wa Kigamboni vijibweni Dar es salaam na  Salum Yoso miaka 30 mkaazi wa Manzese.

Abdulla Nassib Makota miaka 33 mkaazi wa kiembe samaki kisima mbaazi, Faki Makame Faki miaka 40 mkaazi Kariakoo Dar es salaam na Miraji Mohammed Rashid miaka 36 mkaazi wa Magomeni Zanzibar.

Hata hivyo kaimu kamanda Mwaibabe amesema awali watuhumiwa hao walidanganya majina yao na sasa wanahojiwa napolisi

SMZ PIGA MARUFUKU SALOON ZA WANAUME ZINAZOTOA HUDUMA KWA WANAWAKE-MASHEIKH

WAUMINI WA DINI YA KIISLAM WAKIIOMBEA DUWA YA NCHI KUEPUKA NA MABALAA UWANJA WA MAISARA (PICHA NA MAPARA)

Serikali ya Mapinduzi Zanziar imeshauriwa kupiga marufuku Saloon za wanaume zinazowahudumia wanawake wa kislamu.

Akisoma risala ya jumuiya za kislamu Zanzibar katika dua ya kuliombea taifa amani iliyofanyika Maisara mjini hapa, Sheikh Ali Basaleh amesema watu wanaondesha Saloon hizo wanawavunjia heshima waislamu na kuilekeza jamii mahala pabaya.

Amesema taasisi za dini zinaheshimu sheria, lakini inapotokezea kuumiza kwa kuona maovu na machafu yamekithiri mwenyezi mungu ametoa muongozo wa kuondoa hadi kuchukia.

Aidha Sheikh Basaleh ameiomba serikali kuondoa madanguro, baa za chochoroni na kuwataka waislamu waliokodisha nyumba zao zinazofanywa vitendo hivyo kusitisha mikataba yao.

Jumuiya hizo za kislamu pia zimeishauri serikali kudhibiti ungiaji wa watoto katika nyumba za starehe hasa kwenye disco kwa vile zinachangia vitendo vya ubakaji, ukahaba na utumiaji wa dawa za kulevya.

Nae mwongozaji katika dua hiyo Hassan Issa amesema waislamu wanalazimika kuiombea dua nchi yao akidai wapo baadhi ya watu wasiotakia meme Zanzibar.

Amesema Zanzibar imepita katika mitikisiko kadhaa hasa nyakati za uchaguzi mkuu kulikotishia amani ya nchi, hivyo ni vyema kwa waislam kukusanyika na kuiombea amani nchi yao

Dua hiyo iliyohudhuriwa na waziri wa elimu Ramadhan Abdalla Shaaba aliemuwakilisha makamo wa pili wa rais balozi Seif Ali Idd inafuatiwa dua ya mwanzo ya kuiombea amani Zanzibar iliandaliwa na jumuia za kiislamu kabla ya uchaguzi mkuu mwaka jana.

 

 

DR. SHEIN AFUNGUA MSIKITI DIMANI

WAISLAMU nchini wametakiwa kuifanya misikiti iwe kwa dhamira za kuendeshea ibada na kuendeleza manufaa ya elimu ya dini  na mambo mengine ya kheri ikiwa ni pamoja na kusomeshea darasa za dini na kuwasomesha watoto.

Hayo yameelezwa leo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi , Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein mara baada ya ufunguzi wa msikiti wa Masjid Taqwa uliopo Dimani Bondeni, Mkoa wa Mjini Magharibi.

Katika maelezo yake Alhaj  Dk. Shein amewasisitiza Waislamu wa eneo hilo la Dimani wasikubali kwa hali yotote kubaguana katika hayo na kama walivyoshirikiana katika kuujenga msikiti huo basi wasikubali kugawanywa katika uendeshaji na usimamizi wake.

Alielezaa kuwa MwenyeziMungu na Mtume wake Mohammad (S.A.W), hawakuelekeza Waislamu kugombana  kwa ajili ya kugombania uongozi wa msikiti bali viongozi huchaguliwa na watu ambao ndio wenyewe waumini wa dini ya Kislamu.

Alhaj Dk. Shein alisema kuwa ujenzi wa misikiti ni kielelezo thabiti cha imani ya Waislam kwa Mola wao na dini yao kwa ujumla na kusisitiza kuwa Mwenyezi Mungu amewasifu wanaojenga na kuimarisha misikiti kuwa ni waumini wa kweli na Mtume Muhammad (S.A.W), amethibitisha malipo mema juu yao.

Akinukuu aya ya 18 ya Suratul Jinni, Alhaj Dk. Shein alisema kuwa ‘Na hakika Misikiti ni ya MwenyeziMungu basi msimuabudu yeyote pamoja na MwenyeziMungu”. Pia alinukuu kauli ya Bwana Mtume Muhammad (S.A.W) kuwa “Anaejenga msikiti kwa ajili ya MwenyeziMungu basi MwenyeziMungu atamjengea nyumba peponi”.

Aidha, Dk. Shein alitoa wito kwa Waislamu kuwa wasikubali kugawanywa katika dhana zisizo njema kuwa  kuna ubora wa misiki na kusihi kuwa misikiti yoye  ni ya MwenyeziMungu na yote ni mitukufu  hivyo haifai kudharauliwa.

 

Alisema kuwa Misikiti iliyotajwa kwa utukufu, ubora zaidi ni Msikiti Mtukufu wa Makka (Masjid Haram), Msikiti Mtukufu wa Mtume Madina (Masjid Nabawi) na Msikiti Mtukufu wa Al Quds uliopo Jerusalem.

 

Alhaja Dk. Shein alisisitiza suala la kusomeshwa Qur-an na kuwataka wale wote wenye elimu hiyo  kuwasaidia wenzao ambao hawana elimu hiyo ili Zanzibar iendeleze historia yake juu ya elimu ya Qur-an. “Hakuna mbadala wa Qur-an  kwani ni uongofu wetu”,alisisitiza Alhaj Dk. Shein

 

Pamoja na hayo, Dk. Shein alitoa shukurani kwa wafadhili wote waliofadhili, waliosaidia ujenzi wa msikiti huo na kuwatakia kila la kheri kwa MwenyeziMungu Waislamu wote wa kijiji cha Dimani na wengineo waliotumia nguvu zao na mali zao na hata mawazo na busara katika kufanikisha azma ya kuhakikisha wanashirikiana vyema na wafadhili katika kuukamilisha msikiti huo.

 

Akisoma taarifa fupi ya ujenzi wa msikiti huo, Maalim Juma Wakili alisema kuwa ujenzi wa msikiti huo ulianza Agosti 2010 mpaka kumalizika umegharimu jumla ya Shilingi Milioni 75 za Kitanzania.

 

Alieleza kuwa kabla ya hapo msikiti uliokuwepo ulikuwa mdogo na usiokuwa na mazingira mazuri na kwa vile kijiji kina kuwa siku hadi siku pia wana malengo ya kusali sala ya Ijumaa na sala ya Idd hapo baadae katika msikiti wao huo mpya sanjari na kutoopata nafasi kwa ajili ya kuendesha darsa kwa watu wazima na vijana wadogo ndani ya msikiti.

 

Pia, Maalim Juma alieleza kuwa  hivi sasa vijana wengi wa Kizanzibari  wanamomonyoka kimaadili kwa kujiingiza katika mambo mbali mbali yasiofaa hiyo ni kutokana na kukosa elimu ya dini yao ya Kiislamu.

 

Alitoa wito kwa wazazi na Waislamu wote kwa ujula kushirikiana na kuweka mikakati madhubuti ili kuwanusuru vijana wa Kizanzibari na Taifa kwa jumla.

 

Aidha, Waislamu hao wa kijiji cha Dimani waliunga mkono juhudi za serikali katika kupambana na madawa ya kulevya na kuomba juhudi hizo ziendelee ili kuondosha na maovu mengine yote.

 

Akimkaribisha mgeni rasmi Naibu Kadhi Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Khamis Haji alitoa shukurani kwa wafadhali wa msikiti huo, waumini wa dini ya Kiislamu  pamoja na viongozi wa Jimbo hilo la Dimani kwa kushirikiana pamoja katika ujenzi wa msikiti huo na kutoa shukurani kwa Alhaj Dk. Shein kwa kushirikiana nao pamoja.

 

Mapema Katibu wa Mufti Sheikh Fadhil Soraga akitoa hutuba ya sala ya Ijumaa, alitoa wito kwa Waislamu kuwa misikiti iwe kitovu cha mafundisho ya Uislamu na kuitaka Kamati ya msikiti huo kuwa madhubuti kutokana na matukio mbali mbali yanayojitokeza katika misikiti hapa nchini juu ya suala zima la kugombania uongozi wa misikitini.

 

Viongozi mbali mbali wa dini, vyama na serikali pamoja na wananchi wa Dimani walihudhuria katika ufunguzi huo wa msikiti huo.

 

WANANCHI WA NUNGWI WATISHIA KUANDAMANA KUPINGA BAA

Wananchi wa kijiji cha Nungwi mkoa wa Kaskazinu Unguja wametishia kuandamana endapo agizo la makamo wa kwanza wa rais wa Zanzibar la kufungwa baa zilizokuwa hazifuati utaratibu halitatekelezwa.

Wakizungumza na Zenji Fm Radio kituoni hapa wananchi hao wamesema endapo baa hizo hazitafungwa wataandamana kutoka Nungwi hadi ikulu ya makamo wa kwanza kwa rais   kuwasilisha malalamiko yao hayo.

Akizungumza kwa niaba ya wananchi hao mwalimu wa Madrasa Juma Haji Nguti ameishauri serikali kukaa pamoja na wananchi hao kufanya mashauriano ili kuzuwia vitendo vinavyokwenda kinyume na utamaduni wa kijiji hicho.

Amefahamisha kuwa vitendo hivyo ni ukahaba, utumiaji wa dawa za kulevya, wizi na upigaji wa ngoma ovyo

Nae mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Kaskazini ‘A’ Machano Fadhil Machano amekiri kuwepo kwa agizo hilo, lakini amesema halmashauri haitowi vibali vya kufanya biashara ya vileo isipokuwa ni kutoa lesini kwa wale waliopata vibali kutoka bodi ya vileo.

Hivyo amesema halmashauri haina uwezo wa kuwafungia wafanyabiashara hao, hata hivyo amesema halmashauri inaweza kukaa pamoja na wananchi kuzungumzia hali hiyo

BENKI YA DUNIA KUFADHILI UJENZI WA BARABARA ZA MJI WA ZANZIBAR

Kiasi cha Dola za Kimarekani milioni 1.399 zinatarajia kutumika katika kuzifanyia tathmini Barabara zote katika manispaa ya mji wa Zanzibar.

Utiaji saini mkataba wa tathmini hiyo umefanywa kati ya Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano Zanzibar na kampuni za M/s International consultants na M/s Apex Engineering ya India huko Malindi.

Akizungumza katika ghafla hiyo Waziri wa wizara hiyo Hamad Masoud Hamad amezitaja barabara zitakazofanyiwa tathmini  ni Bububu – Mtoni Kinazini na Malindi zenye urefu wa kilomita tisa, Creek road – Mkunazini, Mnazi mmoja  yenye urefu wa kilomita 1.2.

Barabara nyengine ni Fuoni – Magomeni, Kariakoo, Mkunazini zenye kilomita 8.3, Welezo – Amani, Ngambo, Kariakoo kilomita 3.5, Amani –Mtoni, Kiembe samaki kilomita 8.5.

Nyengine ni Uwanja wa Ndege, Kiembe Samaki, Mnazimmoja yenye urefu wa kilomita saba na Bububu – Mahonda, Mkokotoni yenye urefu wa kilomita 40.

Tathmini ya Barabara zote hizo inatarajiwa kukamilika baada ya mwaka mmoja ambapo mradi huo umefadhiliwa na Benki ya Dunia